Kristo Kama Bwana wa Sabato
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Unalichukuliaje Agano la Kale? Je, limejaa sheria kali? Je, unalichukulia Agano Jipya kuwa limejikita zaidi kwenye upendo badala ya sheria? Hivi karibuni, mzozano uliopo kuhusu haki za ndoa za jinsia moja ulinifanya nisome na kujadili mtazamo wa Biblia juu ya ndoa. Je, umechukulia kwamba Agano Jipya limetilia mkazo sheria za ndoa ikilinganishwa na torati ya Musa ya Agano la Kale? Angalia Mathayo 19:3-9. Agano Jipya pia linaonekana kukazia (Mathayo 5:27-28) sheria zinazohusu uzinzi. Endapo ni makosa kudhani kwamba Agano Jipya lilibadilishana (replaced) sheria kali na upendo, vipi kuhusu Sabato? Je, sheria zinazohusu Sabato zimekazwa zaidi au zimepunguzwa makali katika Agano Jipya? Je, inawezekana kwamba suala zima linalohusu utekelezaji wa sheria limepoteza maana fulani? Huenda Yesu anarejesha tu matumizi halisi ya sheria. Hebu tuchimbue somo letu la Luka ili tujifunze zaidi!
- Mavuno Siku ya Sabato
- Soma Luka 6:1-2. Kwa nini Mafarisayo waliashiria kwamba kitendo hiki kilikuwa ni kinyume na utaratibu?
- Soma Kumbukumbu la Torati 23:25. Je, walikuwa wakiiba tena? (Hapana. Walichokuwa wakikifanya kilikuwa ni halali kabisa katika siku nyingine yoyote ile isipokuwa siku ya Sabato. Picha za Maneno zilizopo kwenye kitabu cha Agano Jipya la Robertson zinatuambia kwamba “kwa mujibu wa mawazo ya Kirabi,” matendo ya wanafunzi “yalikuwa ni kuvuna, kupura, kupepeta/kupembua, na kuandaa chakula, vyote hivyo kwa wakati mmoja” – jambo ambalo halipaswi kufanyika siku ya Sabato.)
- Je, Yesu pia alijihusisha kwenye kitendo hiki? (Hapana, angalao haijaandikwa kwamba alihusika.)
- Soma Luka 6:3-4. Ikiwa Yesu hakuhusika, kwa nini anatoa jibu? (Ama Yesu alilichukulia kama jambo la muhimu kiteolojia, au alijisikia kuwajibika kwa matendo ya wanafunzi wake.)
- Unalichukuliaje jibu la Yesu? Je, ungeridhika endapo mmojawapo wa watoto wako angekujibu, “Marafiki zangu pia wanafanya vivyo hivyo?”
- Au, je, Yesu anazungumzia jambo jingine kabisa?
- Unalichukuliaje jibu la Yesu? Je, ungeridhika endapo mmojawapo wa watoto wako angekujibu, “Marafiki zangu pia wanafanya vivyo hivyo?”
- Soma tena Luka 6:4. Swali langu la awali kuhusu “watu wengine pia wanafanya vivyo hivyo,” lilichukulia kwamba matendo ya Daudi si halali. Yesu pia anaonekana kuchukulia kwamba si ya halali. Je, hayakuwa halali?
- Kwa kuzingatia kwamba tunajadili mada inayohusu tabia zisizo halali, kwa nini Yesu hakusema tu kwamba “Wanafunzi wangu hawafanyi kazi.” Hakuna jambo baya linaloendelea hapa!
- Soma Luka 6:5. Hapa Yesu anazungumzia nini? Anachokisema kinahusianaje na jibu lake la awali “watu wengine pia wanafanya vivyo hivyo?” (Katika hali ya kawaida, kauli hii inaonekana kutokuwa na uhusiano wowote hata kidogo. Lakini, hebu itafakari. Yesu anasema kuwa yeye ndiye bosi (“Bwana wa Sabato”). Kitendo cha Daudi kuomba mikate ya hekaluni (1 Samweli 21) kilikuwa cha pekee (jambo ambalo halikuwahi kutokea). Hata hivyo, kilisaidia kutangaza lengo kuu la Mungu kumweka Daudi kuwa Mfalme. Je, kuna kisingizio kwa ajili ya “Mfalme/Bwana?”
- Soma Hosea 6:6. Je, hii inaongezea nini katika mjadala wetu kuhusu Yesu kuwa Bwana wa Sabato na utunzaji sahihi wa Sabato? (Tunatakiwa kujikita kwenye jambo la msingi – ambalo ni kukiri mamlaka ya Mungu. Yesu alikuwa Bwana wa Sabato na alikuwa na haki ya kubainisha kipi ni halali kufanyika siku ya Sabato.)
- Tunatakiwa kuangalia taarifa ya ziada iliyopo kwenye kitabu cha Mathayo. Soma Mathayo 12:5-8. Utagundua kwamba Yesu ananukuu Hosea 6:6. Unaelewaje kile anachokifundisha Yesu? (Kwanza, Yesu anasema kuwa yupo katikati ya jambo hili, yeye ni Mungu, na wanafunzi wake wanamtumikia. Yesu anasema kwamba “rehema” ndio dhana ya msingi ya Sabato.)
- Yesu anamaanisha nini anapokataa “sadaka” ili apate rehema ya Sabato?
- Je, utunzaji wa Sabato uliozoeleka unahusu sadaka – yale mambo tusiyoyatenda, mambo tunayoyaacha?
- Hebu turejee kwenye swali nililoliuliza hapo awali: kwa nini Yesu hakusema tu kwamba, “hii si kazi?” (Yesu anaelekeza umakini na usikivu wetu kwenye jambo la muhimu zaidi la rehema. Hebu tuangalie kisa kinachofuata ili tuweze kuelewa wazo hili vizuri zaidi.)
- Soma Luka 6:1-2. Kwa nini Mafarisayo waliashiria kwamba kitendo hiki kilikuwa ni kinyume na utaratibu?
- Uponyaji Siku ya Sabato
- Soma Luka 6:6-7. Kwa nini Mafarisayo walidhani kwamba Yesu anaweza kufanya uponyaji siku ya Sabato? (Walikuwa na uelewa wa kutosha kuweza kufahamu kwamba hili ni jambo analoweza kulifanya!)
- Soma Luka 6:8-9. Kwa nini Yesu anamwambia mtu aliyepooza mkono kusimama kabla hajauliza swali lake? (Yesu anaashiria kwamba hili ni jambo la muhimu. Sasa tuna uhakika kwa nini Yesu aliwajibia wanafunzi wake kwenye kile kisa cha “mavuno” tulichokijadili hivi punde.)
- Angalia swali la Yesu. Endapo ungekuwa Mfarisayo mwerevu, ungelijibuje? (Kwa dhahiri, kutenda mema, na si kutenda mambo mabaya ndilo jibu sahihi. Lakini, nani anayeuhoji uovu?)
- Soma Luka 6:10-11. Je, kuna yeyote anayeuhoji uovu? (Hii inaonesha kwamba Mafarisayo walikuwa wanapanga njama jinsi ya kumdhuru Yesu siku ya Sabato.)
- Soma Yohana 7:21-24. Watoto wachanga walipashwa kutahiriwa siku ya nane baada ya kuzaliwa (Mwanzo 17:12). Hivyo, wanateolojia wa Kiyahudi walikuwa na mgongano wakati siku ya nane ilipoangukia kwenye siku ya Sabato. Je, Yesu alikabiliana na mgongano alipofanya uponyaji siku ya Sabato? (Hakulazimika kufanya uponyaji siku ya Sabato. Angeweza kufanya hivyo katika siku nyingine yoyote ile.)
- Kwa hiyo je, Yesu anazungumzia jambo gani? Hana utetezi wa mgongano, kweli au si kweli? (Yohana 7:24 inatuambia kwamba Yesu anaona mgongano kati ya mtazamo uliozoeleka juu ya Sabato na mtazamo wake. Mtazamo wake ni kwamba Sabato ni kwa ajili ya kutenda mambo mema. Ni siku ya kuonesha rehema na sio sadaka.)
- Hebu tutafakari visa hivi viwili na kile vinachotufundisha kuhusu Sabato. Soma Kutoka 20:8-11. Fundisho kuu kuhusu kuikumbuka siku ya Sabato na kuitakasa ni lipi? (Usifanye kazi siku ya Sabato. Sheria hiyo hiyo inahusika kwa watumwa wako au wanyama wako – usiwafanyishe kazi.)
- Je, Yesu amepanua wigo kwenye fundisho la Agano la Kale kuhusu Sabato?
- Je, Yesu ameifanya kuwa na mkazo zaidi au mkazo kidogo? (Kama ilivyo kwenye fundisho la ndoa na uzinzi, nadhani anaiangalia upya ili kutusaidia kuelewa maana halisi iliyodhamiriwa. Anatuambia kwamba kupumzika kijuujuu sio lengo kuu la Sabato. Lengo kuu la Sabato ni kuonesha rehema.)
- Je, pumziko la Sabato ni kitendo cha rehema? (Ndiyo! Baada ya siku sita za uumbaji, Mungu aliitoa siku ya saba kwa wanadamu kama tendo la upendo na rehema. Lakini, rehema inajumuisha mambo mengi zaidi ya kutokufanya kazi tu. Baadhi ya kazi zifanywazo siku ya Sabato (Mathayo 12:5) ni kitendo cha kuonesha rehema.)
- Kutenda kwa Usahihi
- Soma Luka 4:16. Hapa Yesu anafundisha nini kuhusu Sabato? (Ilikuwa ni kawaida yake. Visa hivi kuihusu Sabato vinaonesha kwamba Yesu hakuwa kwenye mchakato na kuachana na hizo habari na matukio siku ya Sabato. Umuhimu endelevu wa Sabato unaoneshwa, kama ilivyo kwa ndoa, na matamanio ya Yesu kwamba wanadamu waielewe sheria ya Mungu kwa usahihi.)
- Soma Marko 2:27-28. Nani anayepaswa kuwa mnufaika wa Sabato? (Wanadamu! Mungu aliifanya Sabato kwa manufaa yetu. Sio sheria ya kidhalimu (isiyo na mantiki) ya kuwapima wanadamu kama wanaendana nayo.)
- Soma Luka 13:10-13. Nani anayetukuzwa katika jambo hili? (Alimtukuza Mungu!)
- Nani anayenufaika na tukio hili? (Huyu mwanamke maskini.)
- Soma Luka 13:14. Ujumbe huu unaelekezwa kwa nani? (Kwa wale waliokuwa hekaluni wakiabudu na kutaka kuponywa.)
- Soma Luka 13:15-17. Ni muhimu kiasi gani kuwa upande sahihi wa fundisho kuhusu Sabato? (Yesu anawaita “wanafiki” na “anawaaibisha.” Kujikita kwenye rehema ni muhimu sana. Hatupashwi kusema, “mitazamo yote kuhusu Sabato ina uhalali sawia.” Badala yake, Yesu anasema kuwa kuikuza sadaka kuwa juu ya rehema ni makosa, na sio fundisho linalokubalika.)
- Hebu turejee kwenye kisa cha Daudi na mkate. Sasa unadhani kuwa Yesu anamaanisha nini kuhusu “watu wengine wanafanya vivyo hivyo?” (Rehema ni jambo la kifani. Hii ilikuwa ni kuonesha rehema kwa Daudi na watu wake.)
- Unadhani katika nyakati za sasa jambo gani linaweza kufanana/kulingana na tukio la kumnywesha maji ng’ombe au punda siku ya Sabato?
- Ninapotafakari tukio la uumbaji na Sabato lililobainishwa kwenye kitabu cha Mwanzo, fikra yangu ya kwanza ni kwamba Sabato inamsheherekea Mungu Muumbaji wetu. Hii inaendanaje na wazo la rehema ya Sabato dhidi ya wanadamu? (Alituumba! Kilele cha juma la uumbaji ni uumbwaji wa wanadamu. Utakumbuka kwamba baada ya mateso ya Yesu alipumzika siku ya Sabato. Hiki ni kitendo kingine cha kustaajabisha cha rehema kwetu.)
- Rafiki, je, una mtazamo sahihi kuhusu Sabato? Yesu anadhani kwamba kuielewa Sabato kwa usahihi ni jambo la muhimu sana. Matamanio yake ni kuwa na pumziko linalojikita kwenye rehema – rehema ambayo inawanufaisha wanadamu. Je, utadhamiria leo kuitunza Sabato kwa usahihi?
- Juma lijalo: Wanawake Katika Utume wa Yesu.