(Luka 15 & 16)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Katika mjadala unaohusu utandaaji, mtu mmoja aliniambia kuwa kanisani kwake “tunahubiri injili bila kupindapinda.” Nilielewa kwamba wanahubiri mafundisho ya kanisa bila madoido na kwamba watu wa nje wanapaswa kuvutiwa na ujumbe wa kweli. Nikamuuliza, “Mnapata mafanikio gani kwa kutumia njia hiyo?” Alishusha kichwa chake chini na kukiri kwamba walifanikiwa kumpata mshiriki mmoja mpya katika kipindi cha miaka kumi iliyopita. Luka anaandika mkakati wa kufurahisha wa Yesu kuhusu utandaaji. Hebu tuzame kwenye somo letu ili tujifunze zaidi!
- Vitu Vilivyopotea
- Soma Luka 15:1-4. Endapo Yesu angekuuliza swali hilo, ungemjibuje? (Mimi si mchungaji, lakini kama kondoo tisini na kenda walikuwa “nyikani” ningemwacha huyo mmoja apotee na kuwalinda waliosalia.)
- Kwa nini jibu langu si sahihi? (Yesu anauliza swali kana kwamba jibu ni la dhahiri, hivyo lazima jibu lake lilikuwa la moja kwa moja la wasikilizaji wake.)
- Soma Luka 15:5-7. Sijaribu kupingana na jambo hili, lakini ikiwa mnyama wako kipenzi atakufanya umtafute baada ya kupotea, utajisikiaje? (Nitafurahi kumpata mnyama wangu kipenzi, lakini nitasikitika kumtafuta.)
- Linganisha mwitikio wangu (na mwitikio wako?) na ule wa Mungu. Je, hii inatufundisha nini kumhusu Yesu? (Anapenda kutufuatilia. Anafurahia tunapotubu na kumgeukia yeye. Sisi tunapendwa.)
- Soma Luka 15:8. Utakumbuka kwamba nilisikitika kutokana na kondoo aliyepotea. Kisa hiki kina utofauti gani? (Sarafu haiwajibiki kutokana na kupotea kwake. Mimi ndiye nina makosa kwa kupoteza fedha yangu.)
- Soma Luka 15:9-10. Kwa nini tu kisielezewe kisa cha kondoo? Kondoo mmoja bubu anakimbia. Huo unaonekana kuwa mlingano sahihi kwangu ninapomkimabia Mungu. Kwa nini kuongezea kisa cha sarafu? (Sababu ya dhahiri kabisa ni kwamba Mungu anatutaka tufahamu kwamba tatizo la “upotevu” linamhusisha yeye. Nadhani kisa chetu kinachofuatia kinaweka wazi zaidi kuhusu ukweli huo.)
- Katika kisa cha kondoo na sarafu, mitazamo gani ya Mungu inaonekana? (Anaweka madai ya kutumiliki sisi. Anawalenga waliopotea. Anaweka bidii kubwa kuwarejesha waliopotea. Anafurahia pale waliopotea wanaporejea kwake. Wewe, “mdhambi mmoja,” ni wa muhimu kwa Mungu na kwa malaika.)
- Soma Luka 15:1-4. Endapo Yesu angekuuliza swali hilo, ungemjibuje? (Mimi si mchungaji, lakini kama kondoo tisini na kenda walikuwa “nyikani” ningemwacha huyo mmoja apotee na kuwalinda waliosalia.)
- Mwana Mpotevu
- Soma Luka 15:11-12. Je, kuna chochote chenye haki kwenye hili ombi?
- Kila ukifikiriacho si cha haki? (Kwa kawaida, mwana huwa anapata urithi wake baada ya baba kufariki. Kwa sasa, mwana anamsaidia baba, kwa kuwa mwana huyu alikuwa mdogo, alipata nusu ya urithi ya ule wa kijana mkubwa. Baba anapoteza theluthi moja ya mali yake na manufaa ya kazi ya mwana (pale anapomsaidia).)
- Soma Luka 15:13. Unadhani baba alikuwa ana ufahamu wa kutosha kuhusu azma ya mwanaye ya siku zijazo?
- Ikiwa ndivyo, kwa nini baba alikubali?
- Je, utamwambia mwana wako “Hapana. Hilo si wazo zuri, mwisho wake si mzuri,” huku ukiwa na matumaini kwamba hadi mauti yanakukuta, mwana atakuwa mkomavu zaidi?
- Soma Luka 15:14-17. Fedha zote zimekwisha. Je, kuna mema yoyote yaliyotokana na fedha hizo? (Akili zilimrudia. Lilikuwa ni fundisho kubwa sana maishani.)
- Ninawasikia wazazi wanaojaribu kutumia juhudi kubwa kuwaepusha watoto wao wasiwe na tabia mbaya. Je, kisa hiki kinaashiria nini juu ya jambo hilo?
- Angalia upande mmoja katika mifano yote hii mitatu. Mungu haonekani kutia juhudi kubwa kufanya kondoo/sarafu/mwana “wasipotee.” Bali, anatumia nguvu kubwa sana kupata na kurejesha kilichopotea. Kwa nini?
- Soma Luka 15:18-19. Matamanio ya mwana ni kuwa kama “mtumishi.” Hapo awali, hakuwa ameridhika kuwa mwana. Mtazamo wake umebadilikaje kabisa?
- Je, mtazamo wake ungebadilika endapo baba angekataa kumruhusu kuondoka? (Hii inabainisha suala la badiliko litokalo ndani, si litokalo nje.)
- Soma Luka 15:20-24. Mawazo ya mwana juu ya hadhi yake sahihi ni yapi? (“Sistahili tena kuitwa mwanao.”)
- Maoni ya baba juu ya hadhi ya mwana ni yapi? (“Huyu mwanangu … amefufuka.”)
- Baba amenufaika nini? (Alimpata mwana ambaye hakutaka kuwa mwana wake. Yeye alitaka fedha tu. Sasa ana mwana anayetaka kuwa naye.)
- Au, je, ninamhurumia mwana kupita kiasi? Je, amerejea tu ili apate chakula? (Alirejea ili apate chakula, lakini upendo wa ajabu sana wa baba bila mashaka yoyote uliubadilisha moyo wake.)
- Wazazi, tafakarini kilichotokea hapa ikiwa una mwana mpotevu anayetaka kurejea nyumbani ili apate chakula (na kazi).
- Soma Luka 15:25-28. Je, hivi ndivyo ambavyo uneenenda endapo ungekuwa mwana mkubwa? (Ningekuwa na wasiwasi kwamba sasa mwana mdogo anatishia urithi wangu kwa kuwa alifanya chaguzi zisizo sahihi.)
- Soma Luka 15:29-30. Je, kaka mkubwa ni mwana wa kweli? (Anachukulia huduma yake kwa baba yake kama “utumwa” usio na fursa ya kufurahia.)
- Wazazi, jiwekeni kwenye nafasi ya huyu baba. Mwana mdogo anataka tu fedha zako. Mwana mkubwa anadhani anakutumikia wewe. Je, una watoto wa namna gani?
- Soma Luka 15:11-12. Je, kuna chochote chenye haki kwenye hili ombi?
- Soma tena Luka 15:28 kisha soma Luka 15:31-32. Je, baba anamfukuzia mwana mkubwa? (Ndiyo! “Alimsihi,” na anamwambia mwana kuwa anamiliki “kila kitu.”)
- Je, umewahi kufikiria kwamba inaweza kuwa jambo jema kuja kwa Mungu kabla tu hujafariki ili kwamba uweze kufanya kile unachokitaka na bado ukaipata mbingu?
- Kama ndivyo, tatizo ni lipi? (Tatizo moja ni kwamba unakuwa umekosa “Mungu pamoja nami” – Luka 15:31. Unakuwa umekosa utajiri wa Mungu sasa hivi. Kimsingi kile unachokiona kama “utumwa” ni umiliki wa mibaraka ya Mungu.)
- Nani mwenye huruma zaidi hapa? (Baba! Vijana wake wanamtenda vibaya sana. Yeye anawatendea vizuri mno. Ndama aliyechinjwa kwa ajili ya mwana mdogo ni mali ya baba, si ya mwana mkubwa. Baba aliacha haki zake ili kuwafanya wanawe wapate “haki.”)
- Je, umewahi kufikiria kwamba inaweza kuwa jambo jema kuja kwa Mungu kabla tu hujafariki ili kwamba uweze kufanya kile unachokitaka na bado ukaipata mbingu?
- Wakili Laghai
- Soma Luka 16:1-2. Tatizo ni lipi? (Wakili “anatapanya” fedha za mwajiri wake.)
- Soma Luka 16:3-7. Tatizo la wakili ni lipi? (Wakili atapata shida kubwa kuyakabili maisha kwa kuwa amefilisika na ana majivuno.)
- Suluhisho la tatizo ni lipi? (Kumdanganya mwajiri wake! Atajinufaisha kwa mgongo wa mwajiri wake.)
- Mimi ni mwanasheria, je, ungependa wakili wako akufanyie hivi – akufanyie udanganyifu ili ajinufaishe? (Kitendo hiki kinamfanya mwanasheria aachishwe uwakili na kufungwa jela.)
- Soma Luka 16:8. Je, utamsifia wakili wako (au mwajiriwa) kwa kukutendea hivi?
- Soma Luka 16:9. Nani anayezungumza hapa? (Yesu!)
- Je, umewahi kuwasikia viongozi wa dini wakisema, “Hatutumii mbinu za ulimwengu kuwaleta washiriki wapya kanisani!” Unauchukuliaje mtazamo huu? (Hauendani kabisa na huu mfano na kauli ya Yesu!)
- Hebu turudi nyuma kidogo. Tumesoma mifano minne: kondoo aliyepotea, sarafu iliyopotea, mwana mpotevu, na wakili asiye mwaminifu. Yesu anajaribu kutufundisha nini? (Anataka kurudisha kilichopotea kwa kuwa anawapenda bila ubinafsi, na anatutaka tutumie juhudi za kisasa, tuwe waangalifu na werevu katika kuwatafuta waliopotea.)
- Soma Luka 16:10-12. Je, Yesu anatufundisha kutokuwa waaminifu? (Hapana.) Anatufundisha nini? (Tunao “utajiri wa kidunia” na anatutarajia tuutumie kuuendeleza Ufalme wa Mungu.)
- “Utajiri wa kidunia” ni upi? Soma Luka 16:9 kwa umakini. (Dunia ina thamani gani? Akili, uzuri, talanta, na fedha. Ikiwa tutakabidhiwa chochote kati ya hivi, tunao wajibu wa kuvitumia kwa “busara” (Luka 16:8) ili kusaidia kuwatafuta waliopotea. Ikiwa hatutafanya hivyo, hatutakabidhiwa “mali ya kweli” (Luka 16:11). Hilo ni wazo la busara.
- Rafiki, kanisa lako linatumia busara kiasi gani katika kuwatafuta waliopotea? Je, utajitoa leo kutumia mkakati wako bora kabisa pamoja na talanta kuwatafuta waliopotea?
- Juma lijalo: Yesu, Mwalimu Mkuu.