Filipo Kama Mmisionari

(Matendo 8)
Swahili
Year: 
2015
Quarter: 
3
Lesson Number: 
10

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Je, utasema nini ikiwa hutapewa chakula cha kutosha? Baadhi ya watu watasema kwamba wanataka kupunguza uzito wa mwili, lakini katika kanisa la awali, kitendo hiki kiliitwa kwamba ni ubaguzi wa rangi. Kwa mujibu wa Matendo 6:1-2, yalitolewa malalamiko kwamba wajane wa rangi (kabila) moja walikuwa hawapewi chakula kwa usawa katika programu ya kanisa ya kugawa chakula. Kanisa likaamua kuwachagua mashemasi saba ili kushughulikia hili tatizo la “kusubiria muda mrefu mezani ili kupata chakula”. Mashemasi hawa, kwa mujibu wa Matendo 6:3-4, walitakiwa kuwa watu “wenye kujawa na Roho, na hekima.” Stefano na Filipo walichaguliwa. Hata hivyo, muda mfupi baadaye Stefano aliuawa na viongozi wa Kiyahudi mjini Yerusalemu kwa kueneza injili. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tuendelee na kisa cha Filipo!

  1. Mateso
    1. Soma Matendo 7:59-Matendo 8:1. Je, utawaombea msamaha watu wanaokutesa na kukuua kwa kukupiga mawe?
      1. Unadhani kwa nini kifo cha Stefano kwa kupigwa mawe kilisababisha mateso makubwa? (Huenda ilikuwa ni aina fulani hivi ya tamaa ya damu iliyohamasishwa na Shetani.)
    2. Soma Matendo 8:2-4. Je, haya ni maafa kamili kwa kanisa? (Yaliifanya injili ienee.)
  2. Samaria
    1. Soma Matendo 8:5-8. Matokeo ya kifo cha Stefano na mateso yaliyofuatia ni kusambaa kwa mashemasi saba. Filipo alikwenda kwenye mji uliopo Samaria. Tulijifunza nini kuhusu Wayahudi na Wasamaria majuma kadhaa yaliyopita Yesu alipokutana na mwanamke kisimani? (Hawakuwa wakipendana kwa sababu Wayahudi walikuwa wanawadharau Wasamaria. Licha ya hayo, Yesu alianza kuwaongoa Wasamaria.)
      1. Filipo anapokelewaje katika mji huu uliopo Samaria? (Anapokelewa vizuri sana! Analeta furaha katika mji.)
    2. Soma Matendo 8:9-11. Maisha ya Simoni yakoje? (Watu wanamwita “Mwenye Uweza Mkuu” na wanamchukulia kama ana “uweza wa Mungu.”)
      1. Chanzo cha uwezo wa Simoni ni kipi? (Shetani. Simoni alikuwa anafanya vitendo vya kichawi.)
    3. Soma Matendo 8:12-13. Unadhani Shetani anamchukuliaje Filipo? (Filipo hatoi tu pepo wachafu wa Shetani kutoka kwa watu (Matendo 8:7), bali sasa pia anamwongoa yule anayeonekana kuwa mwakilishi mkuu wa Shetani katika nchi ile.)
  3. Roho Mtakatifu
    1. Soma Matendo 8:14-17. Je, Filipo alikuwa akibatiza kwa jina la Roho Mtakatifu? (La hasha.)
      1. Unawezaje kuelezea jambo hili kwa kuwa Filipo alichaguliwa kuwa shemasi kwa sababu alijulikana “kujawa Roho” (Matendo 6:3), na Roho Mtakatifu alikuwa akitenda miujiza mikubwa kupitia kwake?
      2. Kwa nini Petro na Yohana wanatakiwa kumgawa Roho Mtakatifu?
    2. Soma Matendo 8:18-23. Hatuna uhakika jinsi uwezo wa Roho Mtakatifu unavyoweza kupelekwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine. Kwa mfano, kwa nini Filipo hakupeleka/hakumgawa Roho Mtakatifu kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine, lakini Petro na Yohana waliweza. Lakini, tunafahamu jinsi asivyopelekwa. Kosa ni lipi? (Kwa kutaka kuununua.)
      1. Kuna ubaya gani kwa hilo? Ikiwa watu wanaupata uwezo huo bure, kwa nini isiwezekane kulipa fedha na kuupata uwezo huo? (Roho Mtakatifu ni Mungu! Je, Mungu anauzwa? Kimsingi, hapana.)
      2. Tumesoma kwamba Simoni amebatizwa hivi punde. Hali yake ya kiroho ikoje? (Moyo wake umejaa “uchungu na mateka wa dhambi.”)
        1. Je, ni sahihi kuwabatiza watu kama hao?
        2. Muktadha unaashiria kwa uthabiti kwamba Filipo alimbatiza Simoni. Kwa kuwa Roho Mtakatifu alikuwa anamtumia Filipo kwa nguvu sana, na kwa kuwa mojawapo ya sababu iliyomfanya achaguliwe kuwa shemasi ni hekima yake, je, alifanya kosa kumbatiza Simoni?
    3. Soma Matendo 8:24. Je, sasa moyo wa Simoni umeongoka? (Anaonekana kujali sana kuhusu kuepuka matokeo mabaya.)
    4. Tunajifunza nini leo kuhusu Roho Mtakatifu? Je, ugawaji wa karama unadhibitiwa na wanadamu? Kwa mfano, Petro na Yohana wanaweza kugawa uwezo wa Roho Mtakatifu, lakini Filipo hawezi? Anawezaje mtu, kama Filipo, kujawa Roho Mtakatifu lakini asiwezi kumgawa kwa mtu mwingine? (Ingawa naamini kwamba Mungu hadhibitiwi na wanadamu, ninaamini kwamba Mungu anaturuhusu kufanya uchaguzi. Angalia tena Matendo 8:16. Inaonekana kwamba kushindwa kwa Filipo kubatiza “kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu” (Mathayo 28:19) ndio chanzo cha tatizo. Kwa mjadala zaidi, angalia Matendo 2:28.)
  4. Mkushi
    1. Soma Matendo 8:26. Angalia maisha ya Filipo. Malaika anampa maelekezo majira ya asubuhi kwa ajili ya safari yake ya siku! Je, umewahi kufikiria kumwomba Mungu amruhusu malaika wako akupe maelekezo maishani?
    2. Soma Matendo 8:27-29. Nani mwingine anayempa Filipo maelekezo? (Roho Mtakatifu!)
      1. Tumejifunza nini kuhusu huyu towashi Mkushi? (Yeye ni mkuu wa hazina ya taifa (benki) la Ethiopia. Lazima alikuwa Myahudi kwa sababu aliabudu Yerusalemu. Ana shauku ya kujifunza zaidi habari za Mungu kwa sababu anasoma Biblia yake.)
    3. Soma Matendo 8:30. Je, huyu Mkushi (Muethiopia) ni kiongozi mzuri? (Anasoma kwa nguvu. Jambo hili si la kawaida kabisa kutendeka leo.)
    4. Soma Matendo 8:31-33. Kuna ugumu gani kuhusu kuelewa sehemu hii?
    5. Pitia kwa haraka haraka Isaya 53. Chukulia kwamba wewe ndiye Mkushi unayerejea kutoka Yerusalemu kutoa sadaka kwa ajili ya dhambi zako. Niambie kilichopo katika Isaya 53? (Maneno haya yanashangaza. Yanamzungumzia mtu, lakini yanamrejea kana kwamba ni kondoo anayetolewa kafara. Lazima hii imkumbushe Mkushi juu ya kile kinachotendeka hekaluni mjini Yerusalemu.)
    6. Soma Matendo 8:34-35. Mkushi anasoma nini? (Anasoma unabii kumhusu Yesu. Yesu anatimiza mfumo wa kafara ambao Mkushi ameona uzoefu wake hivi punde. Fundisho kuhusu kazi ya Yesu li dhahiri pale Filipo anapolielezea.)
      1. Ndugu wasomaji: kuna masuala yanayohusu kiwango ambacho Mkushi anaweza kushiriki huduma za hekaluni. Angalia Kumbukumbu la Torati 23:1.
    7. Soma Matendo 8:36-38. Unadhani tukio hili litakuwa na athari gani kwa Mkushi? (Injili itasambazwa na afisa wa ngazi za juu!)
      1. Je, Filipo alitakiwa kujibu kuwa, “sifahamu, unahitaji kujifunza zaidi mafundisho mbalimbali ya kanisa kabla ya ubatizo?” (Tunafahamu Filipo hahitaji masomo kwa sababu alimbatiza Simoni Mchawi.)
    8. Niambie mambo yote yaliyowakutanisha Filipo na Mkushi? (Uongozi wa malaika, maelekezo ya Roho Mtakatifu, utayari wa Filipo kuitikia, safari ya kimataifa ya Mkushi, na uvuvio wa Roho Mtakatifu kusoma huu unabii mahsusi kumhusu Yesu.)
      1. Je, unaamini katika upatanifu linapokuja suala la kueneza injili?
      2. Je, unamwomba Roho Mtakatifu akuongoze ili ushiriki injili na msikilizaji aliye na utayari?
    9. Soma Matendo 8:39-40. Filipo anatumia usafiri wa aina gani? (Roho Mtakatifu anamsafirisha!)
      1. Filipo alianza kwa miadi ya kufanya kazi iliyohitaji umakini mkubwa. Hekima na kujawa Roho Mtakatifu ndivyo vilivyokuwa vigezo, hivyo inaonekana kwamba lazima Filipo ni mtu mwenye kufuata utaratibu. Je, hilo linaendanaje na matukio ya kushangaza katika siku hii? (Utaratibu na mipango ipo nje ya mlango! Malaika anatoa maelekezo, Roho Mtakatifu anamwambia nini cha kufanya na kisha anamsafirisha kwenda kwenye mji mwingine. Hii ni kuishi kila mara kwa imani.)
    10. Je, haya ndio maisha ambayo ungependa kuyaishi? Huna mipango bali ile ambayo Mungu anakupatia kila siku kwa njia ya Roho Mtakatifu au malaika. Kamwe hujui mahali utakapokuwa au jinsi utakapofika mahali hapo. Ushuhuda ni halisi kabisa kila siku!
    11. Soma Matendo 21:7-9. Angalia taarifa hii ya ziada kumhusu Filipo. Ana nyumba, huenda na mke, na mabinti wanne. Je, hii inaendana na maisha yanayobadilika kila siku? (Nimekuwa nikifikiri kwamba Filipo alikuwa akiishi maisha haya halisi ya kupendeza, huku Roho Mtakatifu akimsafirisha kwa kumrusha kwenye fursa tofauti tofauti za kiinjilisti. Lakini, hii inaashiria kwamba Filipo ni sawa na wewe na mimi. Anaishi maisha ya kawaida, akiwa na nyumba na familia, lakini kazi yake ya msingi ni ile ya uinjilisti. Mara nyingine Mungu anamtendea mambo ya kushangaza.)
    12. Rafiki, je, ungependa Roho Mtakatifu awe hai zaidi maishani mwako? Kwa nini usiombe sasa hivi ili Roho Mtakatifu akuongoze kwa watu wanaotaka kuyaelewa mapenzi ya Mungu vizuri zaidi?
  5. Juma lijalo: Paulo: Asili na Wito.