Pambano Kuu na Kanisa la Awali

(Matenso 1, 2, 4, 7 & 10)
Swahili
Year: 
2016
Quarter: 
1
Lesson Number: 
9

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Majuma mawili yaliyopita tulijifunza kuwa msingi mkuu wa maisha yetu ya Kikristo ni kuielewa asili ya Mungu. Anatujali kuliko wazazi wenye upendo wanavyowajali watoto wao. Kuelewa suala hilo kwa usahihi ni jambo la msingi sana. Ukweli mwingine wa muhimu ni namna ya kuelewa na kuyafuata mapenzi ya Mungu. Somo letu juma hili linauzungumzia umuhimu huo. Hebu tuchimbue ili tuone kile Biblia inachokizungumzia kutuhusu sisi!

 1. Vichwa Maji (Wapumbavu)
  1. Soma Matendo 1:6. Ninapenda sana kuzungumzia kifungu hiki kwa sababu kinafurahisha sana. Yesu anapaa angani kurudi mbinguni, na hili swali la mwisho linamhabarisha kwamba kundi hili litafikishaje ujumbe ulimwenguni? (Swali hili linampa Yesu uelewa kwamba watu hawa hawana uelewa! Walidhani kwamba Yesu alikuwa anawashinda Warumi, anaanzisha ufalme hapa duniani, na kuwasimika kuwa viongozi.)
   1. Je, hawakuwa wamekosea zaidi ya hapo?
  2. Hebu tusome muktadha wa hili swali la kipumbavu. Soma Matendo 1:1-5 na Matendo 1:7-8. Tiba ya huu mkanganyiko wa kutisha ni ipi? (Ubatizo wa Roho Mtakatifu.)
   1. Hitaji kubwa la wale wanaotaka kuelewa na kuyatenda mapenzi ya Mungu ni lipi? (Ubatizo wa Roho Mtakatifu.)
  3. Soma Matendo 2:1-4. Tafakari jinsi ilivyokuwa kwa mtu kuwemo ndani ya kile chumba. Unadhani wanafunzi walikuwa na mashaka yoyote kwamba walikuwa wamejazwa Roho Mtakatifu?
   1. Je, tunapaswa kutarajia jambo kama hili au la?
   2. Ufahamu wetu wa kwamba Mungu wetu anakaa ndani yetu ni mojawapo ya mafundisho ya pekee ya Kikristo. Ikiwa Mungu hakai ndani yako, angalia kama una imani za “kipumbavu” ambazo hazijarekebishwa?
  4. Soma Matendo 2:5-11. Weka kando huu muujiza, unadhani lengo la Roho Mtakatifu katika hili tukio ni lipi? (Kuleta uelewa kwa wale ambao yumkini walikuwa na ugumu kuelewa lugha iliyozungumzwa na Wagalilaya. Roho Mtakatifu anavuta usikivu wao, na kisha anawasaidia kuelewa. Utagundua kwamba hiki ndicho ambacho Roho Mtakatifu alikuwa anakifanya kwa wanafunzi – kuwasaidia kuelewa.)
 2. Mtafaruku
  1. Soma Matendo 4:1-4. Kuna tatizo gani kwa mahubiri ya Petro na Yohana? (Ikiwa Yesu alikuwa amefufuka, fundisho hilo linakinzana na mtazamo wa Masadukayo kwamba “hakuna maisha baada ya kifo.” Pia mafundisho hayo yalikuwa yanahusika sana kuzungumzia faida za kumwua Yesu.)
  2. Soma Matendo 4:5-8. Roho Mtakatifu anawajibikaje hapa? (Anauongoza ujumbe wa Petro kwa viongozi wakuu wa nchi.)
   1. Je, Roho Mtakatifu atatuepusha na mtafaruku? (Kwa dhahiri, lengo sio kutuondoa kutoka kwenye mtafaruku.)
  3. Soma Matendo 4:9-14. Tafakari hotuba ya Petro. Roho Mtakatifu anamwongozaje? (Kwanza, Roho Mtakatifu alimponya “kiwete,” na kiwete huyu anaifanya hoja ya Petro ikingiwe kifua (kama “kizuizi cha risasi”). Pili, Roho Mtakatifu anampatia Petro uwezo wa kuzungumza kwa nguvu na maneno yenye mantiki.)
   1. Je, umewahi kupitia uzoefu huu – kwamba Roho Mtakatifu anatenda kazi pamoja nawe na kuzifanya juhudi zako kuwa kubwa ajabu?
   2. Angalia kile ambacho Roho Mtakatifu anakitimiza. Ananyoosha (anabainisha) mawazoni mwa wanafunzi, uelewa wao kuhusu maneno ya Yesu. Analeta ukomavu na uwazi kwenye ujumbe wa wanafunzi. Anawasaidia watu kuuelewa ujumbe. Analeta mguso kwa wasikilizaji – ambao unawafanya kuukubali au kukaa kimya.)
  4. Mmojawapo wa viongozi wa Kanisa, Stefano, anakamatwa kwa kusambaza injili. Ananukuu historia ya kuasi kwa watu wa Mungu. Soma Matendo 7:54-60. Kuna fundisho gani la ziada tunalojifunza kuhusu kujazwa na Roho Mtakatifu? (Ujumbe wako uliojazwa Roho Mtakatifu unaweza kuwakasirisha sana watu kiasi cha kuwa radhi kukuua.)
   1. Hebu tuchunguze sehemu moja nyuma ya pazia kuhusu kifo cha Stefano. Soma Matendo 6:8-11 na Matendo 6:13-15. Tuna mashahidi wa namna gani hapa? (Mashahidi wa uomgo “walioshawishiwa” kusema uongo.)
   2. Soma tena Matendo 7:57-59. Watu gani wanavua nguo zao ili waweze kufanya kazi njema ya kumpiga Stefano kwa mawe? (Kumbukumbu la Torati 17:6-7 inaashiria kuwa hawa mashahidi wa uongo ndio waliokuwa wa kwanza kutupa mawe ya kwanza ili kumwua Stefano.)
    1. Je, Roho Mtakatifu atatulinda dhidi ya vitendo vyote visivyo vya haki? (Roho Mtakatifu alimpa Stefano mtazamo wa kusamehe. Matendo 7:60. Lakini, hakumwepusha Stefano dhidi ya kifo hapa duniani mikononi mwa watu waovu.)
 3. Sahihisho la Ubaguzi
  1. Soma Matendo 10:1-2. Kornelio ana imani gani za kidini? Je, yeye ni muumini mpya wa dini ya Kiyahudi? Je, yeye ni Mkristo? (Yeye si mwabudu sanamu. Anamwabudu Mungu wa kweli. Matendo 10:36 inaashiria kuwa alikuwa na ufahamu wa maisha na mafundisho ya Yesu.)
   1. Inamaanisha nini kusema kwamba alikuwa “mcha Mungu?” (Alitaka kuyatenda mapenzi ya Mungu.)
  2. Soma Matendo 10: 3-6. Mungu amegundua jambo gani kumhusu Kornelio? (Matendo yake mema!)
   1. Je, Mungu anaweza kugundua mambo haya kwako?
  3. Soma Matendo 10:9-14. Jambo gani linajenga msingi wa Petro kusita kupata chakula kizuri? (Mambo ya Walawi 11 inaelezea wanyama wanaokubalika kwa ajili ya chakula na wale wasiokubalika kwa sababu ni “najisi.” Petro anaiambia sauti inayosikika kwenye maono kwamba “kwa hakika hatakula” wanyama wasio safi.)
  4. Soma Matendo 10:15-16. Unadhani kwa nini jambo hili lilitokea mara tatu?
   1. Je, Petro anapingana na maelekezo ya Mungu ya dhahiri kabisa mara tatu?
  5. Soma Matendo 10:17. Kwa nini Petro anaona shaka wakati sauti kutoka mbinguni iko wazi kabisa? (Anaona ukinzani kati ya neno la Mungu lililoandikwa, na kile kinachosemwa kwake kwenye hii sauti kutoka mbinguni. Petro anaona shaka kwa sababu anaamini kuwa Biblia na sauti kutoka mbinguni havipaswi kuhitilafiana.)
  6. Soma Matendo 10:18-20. Sasa Roho Mtakatifu anamwambia Petro asione “tashwishi kwenda” na watu waliotumwa na Kornelio. Kwa nini Petro anasita?
  7. Petro anakwenda na watu hawa kumwona Kornelio. Soma Matendo 10:25-29. Tunapata jibu gani kutokana na kusita kwa Petro? (Anasema kuwa ni kinyume na “sheria yetu.”)
   1. Ni sheria gani hiyo? (Taswira iliyopo kwenye Agano Jipya la tafsiri ya Robertson inabainisha kuwa kuwatembelea watu wa Mataifa haikuwa kinyume na jambo lolote katika Agano la Kale. Hili lilikuwa tu ni fundisho la kirabi (sheria za Kiyahudi) ambalo lilikuwa kama desturi.)
   2. Sasa petro anaelewa nini kuhusu wanyama wasio safi na sauti iliyokuwepo kwenye maono? (Kwamba Mungu hawazungumzii wanyama, bali anawazungumzia wanadamu.)
    1. Kwa nini haoneshi chombo kikishushwa kikiwa na Warumi ndani yake? Kwa nini anaufanya ujumbe kuwa mgumu? (Alitaka Petro apambanue suala hilo. Hiyo ingesaidia somo hilo likae ndani yake.)
  8. Soma Matendo 10:30-33. Hii inatufundisha nini kuhusu uelewa mpya? (Inaonesha kuwa Mungu atathibitisha maelekezo yake tunapokubali kumfuata Mungu kwa njia mpya ambayo inaweza isiwe ya kustarehesha.)
 4. Soma Matendo 10:34-38. Angalia jinsi Petro anavyosema kuwa tayari “mnayajua” maisha ya Yesu pamoja na injili. Ikiwa tayari wanafahamu, kwa nini wanataka Petro azungumze nao? (Kuna mambo mawili. Kwanza, wanataka kujifunza zaidi. Pili, hii pia ni kwa manufaa ya Petro. Sasa Petro anafahamu kuwa Ukristo sio tu dini ya “Kiyahudi,” bali ni imani inayotakiwa kupokewa kwa moyo (kukumbatiwa) na ulimwengu wote.)
  1. Soma Matendo 10:39-40. Kuna jambo gani linalokosekana kwenye elimu ya hawa watu wa mataifa? (Hawaufahamu ufufuo – suluhisho la dhambi na tumaini la uzima wa milele!)
  2. Rafiki, je, unayaona matendo yasiyo ya kawaida (yanayotendwa kwa nguvu zisizo za kawaida) katika kanisa la awali? Roho Mtakatifu anabainisha wazi, anatugusa na kutufunulia ukweli na anatenda miujiza. Mungu anazungumza na Petro ili kumsaidia kuelewa upana wa injili. Je, unamtafuta Roho Mtakatifu ali akujaze na kukuongoza? Je, unatafuta kuingia ubia na nguvu isiyo ya kawaida ili kutangaza neno la Mungu? Kwa nini usimwombe Mungu, sasa hivi, akujaze Roho wake?
 5. Juma lijalo: Paulo na Uasi.