Ukombozi

Swahili
(Ufunuo 20-22)
Year: 
2016
Quarter: 
1
Lesson Number: 
13

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Hili ni somo letu la mwisho katika mfululizo wa masomo juu ya Uasi na Ukombozi. Habari njema ni kwamba tunamalizia kwa habari njema zinazohuzu ukombozi wetu na makao yetu ya milele. Hebu tuzame kwenye somo letu ili tupate kuhamasishwa!

 

I.                              Kufungwa

 

A.                         Soma Ufunuo 20:1-3. Unajisikiaje pale “adui” wako anapokuwa hana nafasi tena maishani mwako?

 

1.                           Unapotafakari jambo baya kabisa ambalo mwanadamu amemfanyia mwanadamu mwenzake, Shetani ndiye aliyehamasisha huo uovu. Ni habari njema kiasi gani kwamba Shetani atafungwa mnyororo na kutupwa kuzimu na kufungiwa na kutiwa muhuri juu yake?

 

2.                           Jambo gani linakupa ahueni katika hii habari? (Kwamba Shetani atafunguliwa baada ya miaka 1,000. Lakini, tunaambiwa kuwa atakuwa huru kwa muda mchache.)

 

II.                           Kuokolewa

 

A.                         Soma Ufunuo 20:4-5. Jambo gani linaendelea katika hicho kipindi cha miaka elfu moja ambacho Shetani amefungwa? (Kundi la watu ambao wamefufuliwa wanakaa na kutawala pamoja na Yesu.)

 

1.                           Inamaanisha nini fungu linaposema kuwa baadhi wakapewa “mamlaka ya kuhukumu?” (Hili kundi la kwanza, kundi la watu wenye haki, kwa namna Fulani hivi nao wanatoa hukumu.)

 

2.                           Je, hawa ndio watu pekee waliokatwa vichwa? (Tunaambiwa kuwa wafia dini hawa ni sehemu ya kundi hilo, lakini kwa namna fungu hili lilivyoandikwa wanaonekana tu kuwa sehemu ya kundi kubwa ambalo halikuwaabudu watu wabaya ama kwa njia ya kukubaliana nao (kwa kutia chapa kwenye vipaji vya nyuso zao) au kwa kulazimishwa kukubali kutiwa chapa (kwenye mikono yao).)

 

B.                         Soma Ufunuo 20:6. Lengo lako ni lipi unaposoma habari hii? (Kuwa sehemu ya kundi la ufufuo wa kwanza kwa sababu “mauti ya pili haina nguvu juu yao.”)

 

1.                           Kuna habari gani mbaya hapa? (Wapo pamoja na Yesu kwa muda wa miaka 1,000 – kipindi ambacho Shetani amefungwa. Kuwa na Yesu ni jambo zuri sana na la kufurahisha, lakini ningependa kuwa naye milele.)

 

C.                         Soma Ufunuo 20:7-9. Hebu subiri kidogo, watu hawa wanatoka wapi? (Kwa dhahiri huu ni ufufuo wa pili. Shetani anafunguliwa, waovu waliokufa wanafufuliwa, na wanaunda jeshi kubwa kumshambulia Yesu, Yerusalemu Mpya na watakatifu waliofufuliwa katika ufufuo wa kwanza.)

 

 

D.                         Hebu turuke mafungu kadhaa. Soma Ufunuo 21:1-3. Je, “Mji Mtakatifu, Yerusalemu Mpya” unatoka wapi? (Unashuka kutoka mbinguni.)

 

1.                           Angalia tena Ufunuo 20:9. Kitu gani kinazungukwa? (Inaonekana kwamba Yerusalemu mpya ndio inayozungukwa.)

 

2.                           Kitabu cha Ufunuo hakitupatii taarifa iliyopangiliwa kwa utaratibu wa miaka na matukio. Unawezaje kuunganisha mikanganyiko hii ili kuelezea kisa chenye mantiki? (Kuna ufufuo wa kwanza wa watu wenye haki. Wanakwenda mbinguni na Shetani anakwenda kuzimu. Kule mbinguni, wanatawala pamoja na Yesu kwa muda wa miaka elfu moja na kwa namna fulani hivi kujihusisha na utoaji wa hukumu. Katika kipindi cha miaka elfu moja waovu wote wanakuwa wamekufa – kitendo ambacho kwa sehemu fulani kinaweza kuelezea jinsi Shetani “alivyofungwa.” Baada ya miaka elfu moja Yerusalemu Mpya inashuka kutoka mbinguni ikiwa pamoja na wenye haki, waovu wanafufuliwa katika ufufuo wa pili na Shetani anafunguliwa. Chini ya uongozi wa Shetani wanaishambulia Yerusalemu Mpya.)

 

E.                          Sasa hebu turejee nyuma. Soma Ufunuo 20:9-10. Shambulio hili la Yerusalemu Mpya linakwishaje? (Shambulio linashindwa kwa sababu waovu “wanateketezwa” kwa moto na Shetani na washirika wake wakuu wanatupwa kwenye ziwa la moto.)

 

F.                           Soma Ufunuo 20:11-15. Nini kinawatokea wale ambao majina yao hayakuandikwa kwenye kitabu cha uzima? (Wanatupwa kwenye ziwa la moto.)

 

1.                           Angalia fungu lenye maneno yasemayo “ziwa la moto ndiyo mauti ya pili.” Tulijifunza nini katika Ufunuo 20:6? (Wale ambao ni sehemu ya ufufuo wa kwanza hawapitii uzoefu wa haya “mauti ya pili.” Hii inabainisha wazi kuwa ufufuo wa kwanza ni kwa ajili ya wenye haki wote, na ufufuo wa pili ni kwa ajili ya waovu wote wanaoishambulia Yerusalemu Mpya na kisha wanapitia uzoefu wa “mauti ya pili.”)

 

2.                           Akina nani ni “wafu, wakubwa kwa wadogo” ambao wanahukumiwa kwa mujibu wa vitabu vinavyofunguliwa? (Hili ni kundi la “mauti ya pili,” waovu wanahukumiwa kutokana na matendo yao.)

 

3.                           Kitabu kingine ni kipi, je, ni “kitabu cha uzima?” (Ikiwa jina lako limeandikwa kwenye kitabu cha uzima, hauhukumiwi kwenye hukumu ya waovu.)

 

a.                            Jambo hili inatufundisha nini kuhusu neema? (Tunapompokea Yesu, maisha, kifo na ufufuo wake kwa ajili yetu, majina yetu yanaandikwa kwenye kitabu cha uzima, na hatuhukumiwi kwa matendo yetu maovu.)

 

b.                           Kwenye Ufunuo 20:4 tulijifunza kuwa wenye haki waliopo mbinguni kwa muda wa miaka elfu moja wana mamlaka ya kutoa hukumu. Je, habari hii inaingiaje kwenye kisa chetu? (Miaka elfu moja ni mingi sana! Mantiki iliyopo ni kwamba wenye haki wanaangalia jinsi Mungu anavyotoa hukumu zake kwa waovu. Inawezekana wanamuuliza Mungu kwa nini mambo fulani yaliwatokea maishani mwao. Wanaalikwa kujiridhisha wenyewe kwamba Mungu ametenda haki katika hukuzu yake.)

 

 

(1)                        Je, kuna jambo jingine lolote ambalo ungependa kulifanya katika kipindi cha miaka elfu moja? (Ningependa kujifunza habari zote kuhusu ndugu zangu waliookolewa. Itapendeza sana kuzungumza na mashujaa wa Biblia. Katika kipindi hiki cha miaka elfu moja tunakuwa jumuiya imara tukipendana baina yetu tukiwa na Bwana wetu.)

 

III.                        Ushindi

 

A.                         Soma tena Ufunuo 21:1-3. Unakumbuka tulivyochukulia habari ya kukaa na Yesu mbinguni kwa muda wa miaka elfu moja tu? Je, habari hii inazungumzia nini kuhusu makao mapya ya Yesu? (Sasa hivi Yesu anakaa duniani. Anakaa pamoja nasi milele!)

 

B.                         Soma Ufunuo 21:4. Bila shaka umesoma fungu hili mara nyingi sana hapo kabla. Jiulize sababu za vilio, maumivu na maombolezo? Hayo yote yamepita. Yamekuwa sehemu ya “mambo ya kale!”

 

C.                         Soma Ufunuo 21:5. Je, ahadi hizi hazina uhakika? (Mungu ndiye aliyeelekeza ahadi hizi “zenye kuaminika na za kweli” na akaagiza kuwa ziandikwe ili tuweze kuzifahamu na kuziamini.)

 

D.                         Soma Ufunuo 21:6-7. Tutafurahia uhusiano wa aina gani na Mungu katika nchi itakayofanywa upya? (Tutakuwa na uhusiano kama wa mzazi na mtoto. Na, tutakuwa na mzazi mzuri sana!)

 

E.                          Soma Ufunuo 21:8. Hili ni fungu la muhimu sana, na kwa mara ya kwanza linaonekana kuwa la ajabu. Hebu niambie, kwa nini dhambi inayoorodheshwa kwanza (badala ya kuwa yenye kutia aibu au mauaji) ni “uoga?” Ujasiri unahusianaje na wokovu?

 

1.                           Angalia orodha ya dhambi inayofuata. Kwa mara nyingine, dhambi ya kutoamini inaorodheshwa kabla ya dhambi ya mauaji! Kwa nini jambo hili ni la muhimu sana? (Kuutanguliza uoga na kutoamini kwenye hii orodha kunatuelekeza kwenye neema na imani. Mungu anatutaka tumtumaini na kumwamini yeye.)

 

2.                           Nina uhakika kuwa si wengi wasomao somo hili ni wauaji. Hata hivyo, je, umeshindwa kumtumaini Mungu? Je, umeteseka kutokana na uoga kwa sababu umeshindwa kumtumaini kwamba Mungu atayafanya mambo kuwa barabara?

 

F.                           Soma Ufunuo 22:1-5. Je, ungependa kuishi mahali hapo?

 

G.                         Soma Ufunuo 22:6. Tuna dhamana ya aina gani? (Mungu alimwambia malaika wake kutuhakikishia kuwa mambo haya ni ya kweli.)

 

H.                         Soma Ufunuo 22:7. Inamaanisha nini “kuyashika” maneno ya unabii huu? (Nadhani hii inakwenda mbali hadi kwenye suala la kuwa mwoga na asiyeamini. Mungu anatutaka tumwamini na kumtumaini yeye pamoja na ahadi zake.)

 

I.                              Rafiki, mustakabali huu wenye utukufu mwingi unaweza kuwa wako. Kwa nini usitubu dhambi zako sasa hivi, kwa imani umpokee na kumkiri Yesu kama Mwokozi wako, na kuishi maisha yanayoongozwa na Roho Mtakatifu ambapo unaweza kuachana kabisa na woga?

 

IV.                      Juma lijalo: Tutaanza somo jipya kutoka katika kitabu cha Mathayo!