Worship in the Psalms

(Psalms 19, 49 & 73)
Swahili
Year: 
2011
Quarter: 
3
Lesson Number: 
7

 

Utangulizi: Je, umegundua kuwa masomo yetu ya sasa kuhusu ibada yanalenga kwenye sababu zetu binafsi za kumwabudu Mungu? Tunamwabudu kwa sababu ya kile alichoturendea! Hizi sababu binafsi za kuabudu zinaleta machozi ya furaha na shukrani machoni mwangu. Lakini, je, hizi sababu binafsi za kuabudu ni za “kibinafsi?” Ukizingatia kuwa, Shetani alimwambia Mungu kuwa ibada ya Ayubu ilikuwa ni kwa sababu zake binafsi. (Ayubu 1:9-10.) Vipi kama unaamini kwamba Mungu amekuangusha? Vipi kama maisha hayajaenda vizuri, ingawaje unadhani kwamba umekuwa mwaminifu? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tuweze kutafiti na kuchunguza kuhusu ibada isiyoweza kuelezeka kutokana na fikra zetu binafsi!

I.       Mwovu na Ibada

A.  Soma Zaburi 73:1-3. Kwa nini huyu mfuasi wa Mungu karibia apoteze imani yake? (Wivu kwa waovu.)

B.  Soma Zaburi 73:4-6. Je, unawafahamu watu kama hawa? Wanaishi vizuri, wanajivunia kuhusu maendeleo yao, na hawamruhusu mtu yeyote awaingilie!

C.  Soma Zaburi 73:9-11. Je, mahusiano ya hawa watu wajivuni na Mungu ni yapi? (Wanaleta madai ya kiroho ya namna fulani. Wao ni watu maarufu na wenye mafanikio. Watu “wanakunywa” kile wanachotakiwa kukiuza. Marekani tunasema “watu wanaodanganywa na kiongozi.”)

1.  Je, wanywaji wanasema nini kuhusu Mungu? (Kama watu wajivuni na wenye mafanikio wanadai njia ya kiroho, kwa nini wafikiri kuwa Mungu ana busara yoyote au maarifa?)

2.  Je, unaona kwamba huu ni ukweli hivi leo? (Hali ya kiroho ya “watu maarufu” ni kwamba kila mtazamo wa maisha (isipokuwa Wakristo walio makini) una hadhi sawa.)

D.  Soma Zaburi 73:13-14. Je, umekuwa ukimfuata Mungu na kudhani kuwa hakukunufaishi kwa jambo lolote zuri? Kusema kweli, kumfuata Mungu kumeyafanya maisha yako kuwa mabaya zaidi? Je, huwa “unaadhibiwa kila asubuhi” kwa kumfuata Mungu?

E.  Je, hisia za aina hii zinaingilianaje na ibada? (Hutajisikia kuwa na shukrani kwa Mungu.)

II.     Kulitafakari

A.  Soma zaburi 73:15. Je, nini kinachomzuia rafiki yetu mwenye mashaka asielezee haya mawazo hadharani? (Ana wasiwasi kwamba atawafanya watu wengine waende mbali (wamwache) na Mungu.)

1.  Je, yu sahihi kunyamaza kuhusiana na mashaka yake?

B.  Soma Zaburi 73:16-17. Je, jibu limekuja kiurahisi? (Hapana. “Alikandamizwa” na tatizo. Kwa hakika, alipambana nalo nafsini.)

 

1.  Hivi karibuni tulijifunza kuhusu patakatifu. Je, panatusaidiaje kutatua tatizo? (Kumbuka kuwa patakatifu ni taswira/picha ya Mungu ya mpango wa wokovu. Mwanakondoo anakufa kwa ajili ya dhambi ya mwanadamu. Yesu, Mwana Kondoo wa Mungu, alikufa ili kutupatia uwezekano wa uzima wa milele.)

C.  Hebu tuendeleze huu mtizamo wa fikra katika Zaburi 49:10-11. Je, hatima/majaaliwa ya kawaida ya werevu na wapumbavu ni yapi? (Wanakufa.)

D.  Soma Zaburu 49:16-20. Je, hili ndilo jibu? Tunapokuwa na wivu kwa waovu wanaoishi vizuri sana, tunapaswa kusema, “Utakufa kama mbwa na hutakuwa na chochote mautini.”

1.  Je, huo ni mtazamo wa aina gani?

E.  Soma Zaburi 49:14-15. Maelezo ya kawaida ni “Nitalala nitakapokuwa nimekufa.” Je, hii ni “Nitatawala nitakapokuwa nimekufa?”

1.  Je, ni kwa namna gani unaweza kuelezea hili katika mtazamo chanya kwa kadri iwezekanavyo? (Maisha haya ni kile chote ambacho wanapewa waovu. Wenye haki wanakombolewa na Mungu kuingia kwenye uzima wa milele.)

F.  Soma Zaburi 73:21-22. Je, sisi ni Wakristo wa namna gani kama tunamtilia Mungu mashaka na kushindwa kujifunza neno lake ili kuyaelewa mapenzi yake? (Wanyama katili: wasiokuwa na akili na wajinga.)

G.  Soma Zaburi 73:23-24. Je, Mungu anatupatia nini zaidi ya uzima wa milele? (Fungu hili lipo ukutani ofisini kwangu. Kama tunajifunza ili kuyaelewa mapenzi ya Mungu, atatulinda na mafundisho yake hapa duniani, na baadaye “atatuchukua na kutupeleka kwenye utukufu wake.”)

H.  Soma Zaburi 73:25-26. Je, ni kwa namna gani nyingine tunapaswa kuthibitisha usitawi wa waovu? (Raha za duniani zina ukomo. Matamanio ya kweli ya mioyo yetu yanapaswa kuwa Mungu. Yeye ni nguvu yetu na utajiri wetu.)

III.    Tamko

A.  Hebu tubadili gia kidogo. Hadi hivi sasa tumejifunza kwamba mfuasi wa Mungu anaweza kuona kwamba mtu mwovu anakusanya mali zaidi (utajiri) na utukufu zaidi hapa duniani, lakini Mkristo anapata ushauri/mawaidha na urafiki (kuwa pamoja na) wa Mungu sasa, na uzima wa milele baadaye. Je, tunawezaje kujua kuwa haya mambo ni ya kweli? Soma Zaburi 19:1. Unadhani ni kitu gani mbingu zinakitangaza kuhusu Mungu?

1.  Fikiria kwamba meli kubwa ajabu inatia nanga kwenye mji wako. Haina kiungo/ufa (kati ya mbao), haina vifaa (vya dhahiri) vinavyotumika kukazia vitu. Imetengenezwa kwa vifaa ambavyo kamwe hatujawahi kuviona, sehemu yake ni angavu kama gilasi/kioo. Inatembea kwa uwezo mkubwa, lakini haina kelele. Je, unasema nini kuhusu watu walioitengeneza? (Wana teknolojia ya hali ya juu na ya kisasa kuliko sisi.)

2.  Fungu letu linasema kwamba anga ni “kazi” ya mikono ya Mungu. Je, tunapaswa kuhitimisha nini kutokana na hilo? (Ya kwamba Mungu alilifanya.)

 

3.  Ili kupata dhana nzuri zaidi kuhusiana na tunachokiongelea, unapaswa kuangalia kwenye You Tube kwenye intaneti na kuangalia video za Louie Giglio zinazoelezea ukubwa na maajabu ya mbingu.

4.  Katika mwaka mfupi, umbali ambao mwanga unasafiri katika kipindi cha mwaka mmoja, ni maili trilioni sita au kilometa trilioni 10. Louie Giglio anazungumzia kuhusu Kundi la Nyota la Whirlpool ambalo lipo umbali wa miaka mifupi milioni 31 kutoka kwetu. Lina nyota bilioni 300. Kwa hiyo, hebu fikiria kuhusu hili: Mungu aliumba kitu ambacho kipo umbali wa miaka mifupi milioni 31 na kina nyota bilioni 300. Kama unaabudu mungu (miungu), je, utakuwa  ni ule uliotengenezwa kwa mikono yako? Au, je, utamwabudu Yule aliyeumba Kundi la Nyota la Whirlpool?

a.  Tukizungumzia kuhusu mikono yetu, kama nikikutaka utengeneze kundi la nyota lililopo umbali wa miaka mifupi milioni 31, je, utaanzaje?

B.  Soma Zaburi 19:2-4. Tumejadili kile ambacho tungehitimisha kuhusu watu waliotengeneza meli kubwa ajabu ya kufikirika. Je, watu wanasikia nini kutoka ulimwenguni hivi leo?

1.  Je, umegundua kuwa kwa kadri watu wengi wanapokuwa wanaishi mahali fulani, basi ndivyo kwa hali ya chini kabisa mbingu zinatokea kwa uwazi?

2.  Fungu letu linasema kuwa mbingu “hutolea maarifa.” Je, ni kwa jinsi gani hiyo ni kweli? (Hazionyeshi uwezo wa kufikiri na mpangilio tu, bali pia zinaonyesha uwezo mkubwa na rasilimali zilizo nje ya uwezo/mpaka wetu wa kufiriki.)

3.  Je, ni nani asiye na uwezo wa kusikiliza huu ujumbe mbalimbali kumhusu Mungu? (Hakuna hata mmoja. Unasikika katika kila lugha na kabila na kila sehemu ya dunia.)

a.  Je, unadhani kwamba hiyo ndio sababu Mungu aliziumba mbingu?

C.  Soma Zaburi 19:5-6. Je, ni kwa jinsi gani jua linafanana na bwana harusi? (Kwenye ndoa tunamwangalia bwana harusi na bibi harusi. Bibi harusi anaweka matumaini yake katika mafanikio ya bwana harusi. Dunia yetu inategemea katika joto la kila siku na mwanga wa jua.)

IV.     Uhusiano Kati ya Mbingu na Sheria

A.  Soma Zaburi 19:7-8. Je, kwa nini Daudi anabadili mada kutoka kwenye mbingu kwenda kwenye sheria? Au, je, Daudi anabaki kwenye mada ile ile? (Anabadilika kutoka kwenye elimu ya sayari hadi kwenye teolojia (elimu ya dini), kutoka kwenye nyota hadi kwenye Amri Kumi. Lakini, vyote viwili vinafanya kazi kutokana na sheria zilizowekwa.)

B.  Hebu tuhusishe hili na mjadala wetu wa awali. Je, ni tatizo gani linalowakabili waovu? (Hawaifuati sheria ya Mungu. Wanakosa mawaidha na urafiki (ukaribu) hapa duniani, na maisha ya duniani ndio pekee “wanayoyafurahia.”)

1.  Je, tunawezaje kujua kwamba kile tunachoamini kuhusu Mungu na sheria Yake ni cha kweli? (Kama Mungu ana uwezo wa kutosha kuweza kuweka kanuni zinazoongoza mbingu, tunaweza kuwa na imani na kanuni Zake zinazoongoza maisha yetu.)

 

2.  Baini kile ambacho Daudi anakisema kuhusu sheria – kwamba ni kamilifu. Je, sheria zinazoongoza mbingu ni kamilifu? (Hili ni jambo la kushangaza. Watu wanaoamini kususu suala la uibukaji (mageuko/mabadiliko) wanaelewa kwamba mbingu zinafuata sheria ambazo zinaweza kuelezewa kimahesabu. Tunaweza kubashiri mahali ambapo sayari na nyota zitakuwa siku zijazo, na kuelezea mahali zilipokuwa karne zilizopita. Matokeo yake, wale wanaoshadadia/wanaotetea suala la bahati na uchaguzi wa kiasili katika suala zima la uumbani wa ulimwengu na kila kilichomo, pia wanaelewa kwamba ulimwengu unaongozwa na sheria za kuaminika. Haina mantiki.)

C.  Rafiki, Daudi anasema kwamba sheria inamfanya mtu “wa kawaida” kuwa mtu “mwenye busara.” Je, ungependa kuwa na busara? Kama wewe tayari una akili nyingi sana, fikiria vile ambavyo sheria ya Mungu itakutendea! Mungu anakiri kwamba baadhi ya watu wanaomkataa wanaendelea vizuri. Lakini, kama tuna busara vya kutosha kuweza kuona taswira/picha kubwa, tutaona kwamba watu waovu ni kundi lisilo na furaha. Kundi hilo halina mawaidha ya Mungu na urafiki (ukaribu) na Mungu sasa na milele. Rafiki, je, utachagua hivi leo kuwa miongoni mwa wale wanaotafuta kutembea na Mungu?

V.       Juma Lijalo: Kukubaliana, Mwafaka na Hatari Katika Ibada.