Haki na Rehema Katika Agano la Kale: Sehemu ya 1

(Kutoka 23, Amosi 8, Mambo ya Walawi 25)
Swahili
Year: 
2016
Quarter: 
3
Lesson Number: 
3

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Umewahi kuuchukulia “utawala wa sheria” kama programu ya kuwanufaisha maskini? Ili kuyaweka mawazo yako sawa, kauli ya “utawala wa sheria” inamaanisha kuwa watu wanaishi chini ya sheria zilizotungwa, na sio chini ya usununu (tabia ya mtu kubadilika-badilika) na amri za mtawala zinazobadilika mara kwa mara. Hivi karibuni niliangalia makala (documentary) iliyokuwa na ujumbe kwamba njia bora ya kuwasaidia masikini waliopo katika nchi zinazoendelea (nchi zenye maendeleo duni) sio kwa kuwapelekea misaada ya mara kwa mara, bali kuwasaidia zana za kuwafanya waweze kujitafutia maisha bora. Zana hizi zinajumuisha kuishi chini ya utawala wa sheria, ambazo zinawatendea kwa usawa maskini na matajiri, yaani pasiwepo na mtu aliye juu ya sheria kati ya makundi haya mawili. Hebu tuzame kwenye somo letu ili tuone kile Biblia inachotufundisha katika hii mada!

 

1)      Haki

 

a)       Soma Kutoka 23:2. Kwa nini Biblia inaonya mkutano wa watu katika kuandamana kupotosha haki? (Makala niliyoiangalia juma hili ilionesha kuwa udanganyifu huongezeka mara dufu inapotokea kwamba watu wengine pia wanafanya udanganyifu huo.)

 

b)      Soma Kutoka 23:3. Kwa nini usimpendelee mtu mnyonge katika neno lake? (Kama nilivyobainisha kwenye utangulizi, makala nyingine niliyoiangalia juma hili ilijenga hoja kuwa misaada mingi ya kigeni haikutolewa kwa busara kwa sababu ilichukulia kwamba watu waliopokea msaada hawakuwa na msaada. Kumpendelea mtu maskini sio kitendo cha haki, na kitendo hicho kinachukulia kwamba maskini huyo anahitaji kipimo chake kifanyiwe upendeleo kwa kuwa yeye ni wa hali ya chini.)

 

i)        Je, hapo kabla umekuwa ukichukulia kwamba kuwapendelea maskini ni kuonesha ubaguzi dhidi yao? Hiyo inaonekana kuwa kinyume na matarajio!

 

ii)      Angalia muktadha: “katika neno lake.” Je, hiyo inaleta utofauti kwenye katazo la kuwapendelea maskini? (Nadhani. Huu ni mjadala mahsusi unaotakiwa kujadiliwa na kufikiwa mwafaka, na bila kujali kama wewe ni maskini au si maskini haina maana yoyote kwenye ustahili.)

 

c)       Soma Kutoka 23:4-5. Mtazamo gani mwingine uwezao kuathiri maamuzi yetu vibaya? (Kulipiza kisasi. Kwa kuwa hatuwapendi watu fulani basi hatuwapi msaada ambao katika hali ya kawaida tungewapatia.)

 

d)      Soma Kutoka 23:6. Sasa tunaambiwa tusiipotoe haki ya maskini! Kwa nini tufanya hivyo? (Kwa kuwa hawawezi kutusaidia. Namna ya kushughulika na maskini inatakiwa ishughulikiwe kwa usawa. Si kuwapendelea wala kutowapendelea katika masuala ya kisheria.)

 

e)       Soma Kutoka 23:7. Hili ni tatizo kubwa kiasi gani? (Mungu anasema hatatuachilia! Hii inaonekana kama vile tunaukosa uzima wa milele.)

 

 

f)       Soma Kutoka 23:8. Ikiwa ungeniuliza kuwa mtu mwenye haki anapokea rushwa, ningejibu kuwa, “hapana.” Fungu hili linaashiria nini? (Linaashiria kuwa wanachukua rushwa, na kitendo hiki kinaathiri maamuzi yao.)

 

g)      Soma Kutoka 23:9. Nchi za magharibi zinajaa wageni. Wajibu wa Mkristo kwa wageni hawa ni upi? (Fungu hili linaonekana kuwa na upungufu – usiwakandamize.)

 

i)        Tafakari rejea ya kihistoria katika fungu hili. Wamisri waliwatendeaje watu wa Mungu? (Waliwafanya kuwa watumwa.)

 

2)      Sabato na Haki

 

a)       Soma Kutoka 23:10-11. Je, huu ni upendeleo kwa maskini? (Sio kwa kiasi kikubwa. Kupumzisha ardhi kila mwaka wa saba kuliifanya izalishe mazao bora zaidi katika miaka mingine. Hilo ndilo lililokuwa lengo – kuifanya ardhi ya mkulima iweze kuzalisha zaidi. Mazao yaliyosalia baada ya mavuno yalikuwa ni kwa ajili ya msaada kwa maskini. Hata kama mkulima hakufanya kazi yoyote kwenye ardhi yake, baadhi ya mazao yaliota na kukua yenyewe.)

 

i)        Je, huu ni mkono wa heri (wa msaada) kwa maskini? (Maskini walitakiwa kuvuna wenyewe. Hata hivyo, waliweza kunufaika kutokana na ardhi ya mkulima.)

 

ii)      Unadhani mkulima alilinda ardhi yake ili kuhakikisha kuwa maskini pekee ndio waliokusanya chakula? (Inaonekana watu waliwachagua watu waliostahili.)

 

b)      Soma Kutoka 23:12. Lengo la Sabato ni lipi kwa mujibu wa hili fungu? (Kuwapumzisha na kuwaburudisha wanyama wetu na wasaidizi wetu.)

 

i)        Je, unaichukulia Sabato kama siku ya kupata pumziko?

 

c)       Soma Amosi 8:4-5. Watu hawa wanaonekana kutenda jambo gani kwa usahihi? (Angalao wanaitunza Sabato kwa juujuu. Lakini, matarajio yao ni kwamba iishe mapema ili waweze kurejea kwenye kazi zao.)

 

i)        Je, watu hawa wanaburudishwa na Sabato?

 

ii)      Watu hawa wanafanya nini ambacho si kitendo cha haki kwa maskini? (Wanafanya udanganyifu. Wanawapimia masikini kipimo kidogo kuliko kile wanacholipwa.)

 

iii)    Kwa nini kwa pamoja tunapata rejea za Sabato na kuwafanyia udanganyifu masikini? (Mungu anatutaka tuuone unafiki wetu. Tunadhani kwamba tunaitunza Sabato, lakini kiuhalisia maisha yetu yamepotoka.)

 

d)      Soma Amosi 8:6. Ni kwa namna gani nyingine tunaweza kuwatendea isivyo haki maskini? (Amosi 8:5 inarejea “kuongeza shekeli” na fungu hili linaonekana kurejea kuwalipa masikini kiasi kidogo sana cha fedha kwa kazi wanazozifanya. Tunapaswa kuwalipa maskini kile wanachostahili kulipwa.)

 

e)       Soma Isaya 1:13. Kwa mara nyingine tena tunaona rejea ya Sabato na ibada. Mungu anawezaje kuyaita matoleo kuwa ni ya “ubatili (hazina maana)?” Ibada yetu inawezaje kuwa ya “chukizo” kwa Mungu? (Soma Isaya 1:16-17. Kumwabudu Mungu si mbadala wa kuwatendea haki maskini na wanyonge. Isaya 1:13 inasema kuwa matoleo na uvumba ni “machukizo.” Mungu hataki tumtolee kile tulichokiiba kutoka kwa maskini.)

 

 

f)       Hivi karibuni, nilikuwa kwenye vikao na kusoma makala zinazohusu suala la haki kwa maskini katika mahakama za Marekani. Tatizo kubwa ni kwamba maskini hawezi kumudu kumlipa wakili, na mara kwa mara mahakamani huwa wanashitakiana na matajiri ambao wanaweza kumudu gharama za mawakili. Biblia inapendekeza kuwa tutatueje tatizo hili? (Mafungu tuliyoyasoma yanasema kuwa hakimu anapaswa kumtendea masikini na tajiri kwa usawa. Maskini hapaswi kupendelewa au kutopendelewa.)

 

i)        Vipi kuhusu kuwapatia maskini mwanasheria?

 

(1)    Ikiwa utamlipa mwanasheria kwa ajili ya kumhudumia maskini, lakini hufanyi hivyo kwa tajiri, je, huko ni kumpendelea maskini?

 

ii)      Ikiwa hakimu hatakiwi kumpendelea maskini, je, lugha ya (Isaya 1:17) “wasaidieni walioonewa, mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane” inarejea jambo gani? (Hii inawapa wajibu mawakili na wale wanaowafadhili (wanaowalipa) mawakili.)

 

(1)    Tulijadili dhana potofu kuhusu maskini. Je, Biblia inaashiria kwamba wajane na wanaoonewa hawana msaada? (Ndiyo. Utagundua kwamba jamii inayohusika ni kigezo kikubwa. Wajane walipungukiwa haki za kisheria.)

 

g)      Soma Mambo ya Walawi 25:8-12. Hii ni “Sabato Kuu na ya pekee kabisa! Kila baada ya miaka 49 inafuatiwa na “Yubile” katika mwaka wa 50. Kila mtu anatakiwa kurudi nyumbani. Wanakulaje wote? (Soma Mambo ya Walawi 25:20-22. Hawatakiwi kujihusisha na upandaji wa wazao na uvunaji kama ilivyo ada. Badala yake, Mungu anawabariki mavuno mengi kabisa katika mwaka wa sita.)

 

h)      Soma Mambo ya Walawi 25:25-28. Jambo gani jingine linatokea katika mwaka wa Yubile? (Kila mtu anarejeshewa mali yake. Hii inaelezea jinsi kila mtu anavyoweza kurejea nyumbani.)

 

i)        Je, hii inaendana na utawala wa sheria? (Ndiyo, kwa sababu wote wanafahamu sheria.)

 

ii)      Soma Mambo ya Walawi 25:23-24. Msingi wa hii sheria ni upi? (Mungu anamiliki mali zote, na kwa kuwa sisi ni wapangaji/wageni tu, tunafuata kanuni/sheria yake.)

 

iii)    Je, hii sheria ya “urejeshaji wa mali” inawapendelea maskini? (Sidhani. Kwa kuwa sheria inafahamika, watu watalipa thamani ya kukodi ardhi (au mali nyingine) kwa muda wa miaka 49 pekee.)

 

i)        Soma Mambo ya Walawi 25:29-30. Kwa nini sheria hii ni tofauti? (Ardhi italimwa, hivyo urejeshaji wakati wa Yubile uliwaruhusu watu kuwa na uwezo wa kufanya kazi na kujipatia chakula. Kimantiki nyumba zilizozungushiwa uzio ni jambo tofauti kabisa.)

 

j)        Soma Mambo ya Walawi 25:39-43. Jambo gani jingine linatokea katika mwaka wa Yubile? (Deni la kibinadamu linasamehewa. Hii inawapatia watu nafasi nyingine.)

 

k)      Soma Mambo ya Walawi 25:35-37. Je, kitendo hiki kinawapendelea maskini? (Ndiyo, kwa maana ya kwamba hawalipi riba na wanapata chakula kwa kukilipia na kwa gharama nafuu.)

 

i)        Soma tena Mambo ya Walawi 25:35. Kuna kigezo gani kwenye msaada wa aina hii? (Mtu “hawezi kujisaidia mwenyewe.” Wale wasioweza kufanya kazi wanatakiwa kusaidiwa, lakini hii haiashirii kuwasaidia kifedha, chakula au mavazi. Inaashiria msaada.

 

 

l)        Kile tulichokisoma kuhusu Sabato ni jambo ambalo tunaweza kulitenda kwa urahisi sasa hivi. Lakini je, tunawezaje kutumia sheria za Yubile? (Ingawa huu ni mfumo tofauti kabisa wa sheria dhidi ya zile tulizonazo nchini Marekani, hakika tuna dhana zinazofanana. Kwa mfano, watu wanawekwa huru dhidi ya deni kwa njia ya ufilisi. Ingawa hawarejeshewi ardhi yao, sheria za “makazi” kwa kiasi fulani zinalinda mashamba ya familia.)

 

m)    Rafiki, angalia jinsi kanuni za utoaji haki za Agano la Kale zinavyoweza kuhusika maishani mwako. Unaweza kufanya jambo gani ili kuakisi dhana ya Mungu ya haki na rehema?

 

3)      Juma lijalo: Haki na Rehema Katika Agano la Kale: Sehemu ya 2