Roho Mtakatifu na Kanisa

(Waefeso 1, 1 Wakorintho 12)
Swahili
Year: 
2017
Quarter: 
1
Lesson Number: 
9

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Je, kuna ushahidi kwamba Roho Mtakatifu yu hai kanisani kwako? Je, kuna ushahidi kuwa anaongoza kazi za kanisa lako? Haya ni maswali mazito yanayojikita kwenye kiini cha usitawi wa kusanyiko lenu. Kilichomo akilini mwangu ni kwamba madhehebu yangu, pamoja na madhehebu mengine, yanaye Roho Mtakatifu kwa “kiwango cha chini sana kuliko itakiwavyo.” Ama kwa hakika, baadhi ya madhehebu yanaonekana kuwa na uhasama wa namna fulani dhidi ya makanisa ya “kikarismatiki.” Je, “kutokuwa karismatiki” ni sawa na “kutoongozwa na Roho Mtakatifu?” Uhusiano kati ya usitawi wa kanisa na kazi ya Roho Mtakatifu unaibua maswali mazito ambayo yanajibiwa na somo letu juma hili. Hebu tuzame kwenye somo letu juma hili ili tuone kile tunachoweza kujifunza kuhusu kanisa na Roho Mtakatifu!

 

  1. Mfumo wa Kanisa na Yesu

 

    1. Soma Waefeso 1:17-21. Nani aliye wa muhimu katika kumfahamu Mungu vizuri zaidi? (Roho Mtakatifu.)

 

      1. Waefeso 1:19 inazungumzia “na ubora wa ukuu wa uweza ndani yetu tuaminio,” je, inarejea jambo gani? (Hii inamzungumzia Roho Mtakatifu. Yeye ndiye nguvu ya Mungu hapa duniani. Angalia hususani, uwezo wake “ulimfufua [Yesu] katika wafu.”)

 

        1. Je, unakubaliana kwamba uwezo wa kumfufua Yesu katika wafu ni “uwezo mkuu usio wa kawaida?” (Fikiria kwamba wewe unao uwezo huo!)

 

    1. Soma Waefeso 1:22-23. Nani aliye mkuu wa mambo yote kwa ajili ya kanisa? (Vifungu hivi vinazungumzia sehemu zote tatu za Utatu Mtakatifu, lakini hapa vinamzungumzia Yesu! Yesu ndiye anayelisimamia kanisa lake.)

 

      1. Mwili wa Yesu ni kitu gani? (Kanisa ndilo “mwili” wa Yesu.)

 

        1. Kwa nini Biblia inatumia analojia ya kanisa kuuelezea mwili, hususani mwili wa Yesu? (Hebu tugeukie jambo hilo katika sehemu inayofuat)

 

  1. Mfumo wa Kanisa na Roho Mtakatifu

 

    1. Soma 1 Wakorintho 12:12-13. Paulo anatumia “mwili” gani kutufundisha mambo yanayohusu mwili wa kanisa? (Mwili wa mwanadamu. Ni sawa na kanisa kwa namna mlivyojipanga (na natumaini mmejipanga) chini ya Yesu.)

 

      1. Jambo gani lililo la muhimu katika umoja wa mwili wako wa kibinadamu? (Ulizaliwa kwa jinsi hiyo. Haukuwa na uchaguzi.)

 

 

      1. Jambo gani lililo la muhimu katika umoja wa kanisa? (Roho Mtakatifu! “Hatubatizwi tu kwa Roho mmoja katika mwili mmoja,” bali sote “tunapewa Roho mmoja kwa ajili ya kumnywa.)

 

        1. Mwili wako utajisikiaje pasipokuwepo na kitu cha kunywa? (Utakufa haraka san)

 

        1. Je, hilo pia ni kweli katika mwili wa kanisa? Je, kanisa litakufa lisipokunywa kutoka kwa Roho Mtakatifu? (Hiyo ndio analojia, na ninaamini ni kweli.)

 

        1. Je, kuna makanisa ambayo ni “madubwana” (zombie) ambayo yamekufa kutokana na kutokuwa na Roho Mtakatifu, lakini bado yanatembea na yako hai?

 

        1. Umewahi kusikia kwamba mtu anaweza kunywa maji mengi kupita kiasi? Kama jibu ni hapana, je, unaweza kumnywa Roho Mtakatifu kupita kiasi? Je, unaweza kuwa karismatiki kupita kiasi?

 

    1. Soma 1 Wakorintho 12:14-20. Unajifunza nini kuhusu “mwili” wa kanisa kutoka kwenye mfululizo huu wa kauli hizi na maswali haya? (Kwamba kanisa linasimamiwa na Mungu. Kila mtu anayo sehemu, na tunatakiwa kuipa thawabu sehemu yetu. Jambo la muhimu kabisa katika mafanikio ya jumla ya “mwili” ni umoja – uratibu wa sehemu mbalimbali za mwili.)

 

    1. Soma 1 Wakorintho 12:21-24. Umewahi kuwa kwenye kanisa ambapo mtu anayetimiza wajibu fulani anamwambia mtu mwingine mwenye wajibu tofauti, “Hatukuhitaji?”

 

      1. Mshiriki wa kanisa anawezaje kufikisha wazo ambalo mtu mwingine hahitajiki bila kulisema kwa uwazi? (Tunaweza kulisema kwa mtazamo wetu. Je, kuna nafasi ambazo hudhani kuwa ni za muhimu?)

 

        1. Paulo anasema kuwa jambo gani ni la muhimu kwenye hizi sehemu zisizo na heshima kubwa? (Anasema kuwa tunazitendea sehemu zisizo za heshima sana za miili yetu kwa “heshima ya pekee,” wakati sehemu zingine hazihitaji “huduma ya pekee.”)

 

        1. Unawezaje kutumia dhana hii kanisani kwako? (Nadhani kila mtu anahitaji kutiwa moyo. Tunashindwa kufuata ushauri wa Paulo tunapompa sifa nyingi zaidi mhubiri kuliko tunavyowasifia wale wanaopanga viti, au wanaoshughulikia mitambo ya sauti.)

 

          1. Unaweza kufanya nini ili kutatua tatizo hili kanisani kwako, tukichukulia kwamba hilo ni tatizo?

 

    1. Soma 1 Wakorintho 12:25-26. Kama mguu wako umeumia, si utagundua? (Naam!)

 

      1. Uliubaini mguu wako kabla haujaanza kukughasi?

 

      1. Paulo anamaamisha nini? (Linapokuja suala la miili yetu wenyewe, tunagundua mara moja pale sehemu ya mwili inapokuwa na tatizo. tunahitaji umoja wa namna hiyo kanisani kwetu. Tunahitaji kuzifahamu sehemu zote za miili yetu na kuhakikisha kwamba zote zinaheshimiwa.)

 

      1. Dhana ya kumheshimu mwanadamu inakinzana na dhana ya Biblia? (Si kwa mujibu wa Paulo!)

 

 

  1. Mfumo wa Kanisa na Karama za Roho

 

    1. Soma 1 Wakorintho 12:27-28. Hatuzungumzii tena sehemu halisi za miili kama vile mikono na miguu, bali tunazungumzia wajibu tofauti tofauti kanisani. Je, majukumu haya yanatakiwa kufanya kazi kama sehemu za mwili? (Hilo ndilo hitimisho lenye mantiki kwa hoja ya Paulo.)

 

      1. Utaona kwamba Paulo anasema “wa kwanza… mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu.” Je, Paulo anapanga madaraja ya majukumu kanisani? Ikiwa ndivyo, kwa nini anafanya hivyo? (Anaweka madaraja. Ukiangalia mbele katika 1 Wakorintho 12:31 anazungumzia “karama zilizo kuu.” Alipochukulia analojia ya mwili, alizungumzia “heshima” ya miili inayohusika. Ujumbe tunaouona ni kwamba karama zote ni za muhimu, lakini karama zingine ni “kuu.”)

 

      1. Kwa nini karama ya “maongozi” imewekwa nafasi ya pili kutoka mwisho? Katika makanisa mengi, viongozi wanaonekana kuwa kwenye nafasi ya juu kabisa.

 

        1. Kwa nini karama ya kuwa “mtume,” ambayo ni ya kwanza kwenye orodha, ni tofauti na kuwa kiongozi? (Katika Mathayo 10:2-3 tunawaona wanafunzi kumi na wawili wakizungumziwa kama mitume. Warumi 1:1 ni sehemu mojawapo (kati ya sehemu nyingi) ambapo Paulo anaeleza kwamba yeye ni mtume, hata kama hakuwa sehemu ya mitume kumi na wawili wa awali. Katika Warumi 16:7 tunawaona “Androniko na Yunia” wakiorodheshwa kama mitume. Wajibu wa “mtume” unaonekana kuwa kama mabalozi viongozi wa Yesu. Unaweza kuona jinsi jambo hilo linavyoweza kutofautiana na kuwa kiongozi?)

 

    1. Soma 1 Wakorintho 12:29-30. Paulo anamaanisha nini kwa kuuliza maswali haya? (Jibu ni la dhahiri, “Hapana.” Sote tunayo sehemu katika mwili (1 Wakorintho 12:27), lakini sehemu yetu ni tofauti.)

 

      1. Je, tunaweza kujongea mbele? Je, tunaweza kufurahia jukumu kubwa? (Soma 1 Wakorintho 12:3 Jibu ni, “Ndiyo.”)

 

    1. Soma 1 Wakorintho 13:1-3. Baadhi ya karama za roho zimeorodheshwa hapa. Unadhani kwa nini Paulo anaandika mambo haya mara baada ya kuandika namna karama kadhaa zinavyofanya kazi pamoja kanisani? (Karama zetu, bila kujali ukubwa wake, hazitusaidii chochote ikiwa hatuna upendo. Karama hazihusiani na umuhimu binafsi, zinahusiana na kuwasaidia watu wengine.)

 

    1. Soma Wagalatia 5:22. Upendo ndilo tunda la kwanza la Roho Mtakatifu linalobainishwa. Kwa dhahiri matunda ya Roho Mtakatifu ni tofauti na karama za Roho Mtakatifu. Vinafanyaje kazi pamoja? (Tulijifunza matunda ya Roho Mtakatifu majuma mawili yaliyopita, na tulijifunza karama za Roho Mtakatifu juma lililopita. Matunda yanahusiana na kila mmoja wetu binafsi. Karama zinahusiana na wajibu wetu kanisani. Mguu uliovunjika, ni sawa na kuwa na jambo bovu kwenye “tunda” lako. Sio tu kwamba mguu unahitaji tiba, lakini haisaidii sana katika kuusaidia mwili.)

 

 

    1. Rafiki, tulianza kwa kuuliza, “Roho Mtakatifu ni wa muhimu kiasi gani kwa usitawi wa kanisa?” Vifungu tulivyojifunza juma hili vinatuambia kuwa Roho Mtakatifu anawasimamia na kuwafanya washiriki wa kanisa wawe kwenye mwili mmoja chini ya uongozi wa Yesu. Roho Mtakatifu ni wa muhimu kwa usitawi wa kanisa. Kuwa na Roho Mtakatifu kwa wingi ni bora kuliko kuwa naye kwa uchache! Je, utaomba kwamba Roho Mtakatifu akujaze kwa nguvu wewe pamoja na kanisa lako?

 

  1. Juma lijalo: Roho Mtakatifu, Neno, na Maombi.