Imani Katika Agano la Kale

Swahili
(Wagalatia 3:1-14)
Year: 
2017
Quarter: 
3
Lesson Number: 
5

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Nilipokuwa mdogo, kulikuwa na programu kwenye televisheni iliyokuwa inaitwa “Kurogwa.” Katika somo letu juma hili, Paulo anawaambia Wagalatia kwamba “wamerogwa.” Tunafahamu kwamba Wagalatia wasingekuwa wanatazama televisheni kupita kiasi! Je, Paulo anazungumzia juu ya kupagawa pepo? Nimeangalia tafsiri ya “Strong” juu ya neno la Kiyunani na linamaanisha “kupumbaza (kwa kutumia mbinu za uongo).” Tusingependa kupotoshwa juu ya injili, hivyo hebu tuzame kwenye somo letu la barua kwa Wagalatia ili tuubaini ukweli!

 

 1. Kurogwa

 

  1. Soma Wagalatia 3:1. Kwa nini ufahamu wa mateso ya Yesu ni muhimu ili “kutokurogwa?” (Soma Wagalatia 2:21. Tulimalizia somo la juma lililopita kwa ujumbe huu – ikiwa tunadhani kuwa tunaweza kuokolewa kwa matendo yetu, tunakidhihaki kifo cha Yesu kwa ajili yetu. Kudhihaki kile ambacho Yesu ametutendea ni kosa kubwa sana.)

 

  1. Soma Wagalatia 3:2. Ni muhimu kiasi gani “kumpokea Roho?” (Kwa namna Paulo anavyoandika jambo hili, ni uthibitisho wa muhimu sana kwamba maisha yako ya Kikristo yapo kwenye msitari sahihi. Paulo anawakumbusha kwamba Roho Mtakatifu hakuwaendea kutokana na wao kutii matendo ya sheria.)

 

   1. Je, umegundua jambo ambalo Paulo analizungumzia? Makanisa yanayoonekana kujikita kwenye sheria yamekauka kama mifupa. Hawana (wanapungukiwa) Roho Mtakatifu. Kwa upande mwingine, makanisa yaliyojaa watu wanaofurahia kukubaliwa kwao kwa imani wanaonekana kujawa Roho. Je, haya ndio maoni yako?

 

  1. Soma Wagalatia 3:3-4. Wagalatia wametesekea nini bure? Mateso hayo ni yapi na jambo gani ni bure? (Kubadili imani yako ya dini kutakufarakanisha na marafiki na wanafamilia. Kwa kuwa kila dini, isipokuwa Ukristo, imejengwa juu ya matendo kwa namna fulani, Paulo anasema kwamba baada ya kuteseka kutokana na uamuzi wako wa kubadilika, sasa unarejea kwenye matendo yako. Hivyo, kubadilika kwako kulikuwa bure.)

 

  1. Soma Wagalatia 3:5. Paulo anahusianisha nini na kuwa na Roho Mtakatifu kanisani? (Miujiza.)

 

   1. Ikiwa hatuna miujiza, na katika eneo la dunia hii ninakoishi ninadhani kwamba tunapungukiwa/hatuna miujiza ya “hakuna anayeweza kuwaamulia,” je, hiyo inamaanisha kuwa hatuna Roho Mtakatifu? (Ninaamini kuwa mjukuu wangu wa kike aliponywa kimiujiza baada ya kuzaliwa. Lakini, naweza kufikiria jinsi baadhi ya watu wanavyoweza kusema juu ya jambo hili. Ubashiri wangu ni kwamba wewe pia unao uzoefu wa kufanyiwa/kuona miujiza, lakini miujiza hiyo si sawa na ile miujiza mbalimbali ya Mathayo 12:22-23 – kila mtu anashangazwa nayo. Kutokuwepo kwa miujiza ya namna hii katika eneo langu leo hunitaabisha.)

 

 

   1. Je, miujiza inaweza kutokana na kuishika sheria? (Hapana! Ninachokiona kuwa ni sababu ya kutokuwepo miujiza ni kwamba tunajikita zaidi kwenye sheria kuliko neema na Roho Mtakatifu. Panaweza kuwepo sababu nyingine, kwa mfano, kwamba hatuna udhibiti juu ya kazi ya Mungu, lakini hili ni jambo la kulichukulia kwa umakini.)

 

 1. Ibrahimu

 

  1. Soma Wagalatia 3:6. Je, kuhesabiwa haki kwa njia ya imani ni fundisho la Agano la Kale? (Ndiyo! Fikiria mfumo wa patakatifu. Ulimchinja mnyama na damu yake ilifanya upatanisho wa dhambi zako. Huo si wokovu kwa njia ya matendo, huo ni wokovu kwa njia ya kifo cha mnyama. Naam, tunajua kwamba jambo hilo lilikuwa linazungumzia kifo cha Yesu katika siku zijazo.)

 

  1. Hebu tusome utangulizi wa kauli ya Paulo juu ya Ibrahimu. Soma Mwanzo 15:4-6. Ibrahimu anaamini nini? (Kwamba atampata mwana na uzao mkubwa.)

 

   1. Kwa nini imani huleta haki? Kwa nini tusisema kuwa imani huleta “watoto?” (Hii inaonesha kwamba jambo halisi na la msingi ni kumtumaini Mungu. Je, tunaamini anachokisema Mungu na kile alichokitenda na atakachotutendea?)

 

  1. Soma Wagalatia 3:7-9. Kwa nini kusema kwamba injili ilitangazwa “mapema kabla” kwa Ibrahimu? Je, injili (kuhesabiwa haki kwa njia ya imani) haikutolewa tangu kipindi hicho? (Hii ilikuwa ni kabla ya kutolewa kwa Amri Kumi pamoja na sheria nyingine zilizotangazwa na Musa. Dhana iliyopo ni kwamba kila kilichofuatia, fundisho la msingi lilikuwa ni kuhesabiwa haki kwa njia ya imani.)

 

 1. Laana

 

  1. Soma Wagalatia 3:10. Hivi karibuni, nilikuwa ninatafakari jinsi ninavyoweza kushiriki injili na mtu aliyekuwa anakaribia kufariki, na alikuwa anaichukia dini kwa kiasi fulani. Nina uhakika mtu huyu anadhani kwamba “mimi ni mtu mwema sana, sina hitaji la kitu kingine chochote kile.” Je, huu ni mtazamo unaoleta laana? (Ndiyo. Mtu anaposema, “mimi ni mwema na ni mtu bora zaidi kuliko watu wengine wengi tu ninaowafahamu,” mtu huyo anadhani kuwa wokovu wake unatokana na matendo yake. Tatizo la njia hiyo ni kwamba haitoshi kuwa bora zaidi ya watu wengine. Unatakiwa kuwa mkamilifu, unatakiwa “kuendelea kutenda kila jambo lililoandikwa kwenye Kitabu cha Sheria.”)

 

  1. Soma Wagalatia 3:11-12. Je, unapata wakati mgumu kutafakari wazo la kwamba mtu anayejtahidi sana kuishika sheria anaweza kulaaniwa? Huyu ni “mtu mwema.” (Kuyatii mapenzi ya Mungu ni jambo jema. Tatizo ni kuutegemea utiifu huo kwa ajili ya wokovu wako.)

 

   1. Watu wangapi wanayategemea matendo yao kwa ajili ya wokovu na hawajui kuwa wanayategemea? (Utaona kwamba Paulo anawazungumzia wale wanaoishika sheria: “Mtu atendaye mambo haya ataishi kwa imani.” Hii inatoa taswira ya mtu mtiifu, na anayeamini kuwa jambo hili huleta stahili ya kukubaliwa na Mungu.)

 

  1. Soma Wagalatia 3:13. Je, adhabu, laana ya sheria ilitundikwa juu ya nani? (Yesu. Alilipa adhabu kwa ajili ya dhambi zetu. Alilaaniwa ili kutukomboa kutoka kwenye laana.)

 

 

   1. Ikiwa tunayategemea matendo yetu kwa ajili ya wokovu, je, tunaichukua laana? (Ndiyo!)

 

  1. Siku za hivi karibuni, nimekuwa nikipambana na dhambi mahsusi. Sina chembe ya shaka mawazoni mwangu kwamba Mungu anatamani tuwe watiifu, kwa ajili ya manufaa yetu na kwa ajili ya utukufu wake. Tatizo ni kwamba ninaposhindwa, ninadhani kuwa kitendo hiki kinaathiri kwa kiasi kikubwa sana uhusiano wangu na Mungu. Wakati huo huo naamini kuwa kitendo hiki kinakiuka maelekezo ya Paulo kwamba hatupaswi “kutegemea” ushikaji wa sheria. Una maoni gani?

 

   1. Je, itakuwa sahihi kuamini kwamba kila (wewe na mimi) tunapoielekea haki, anguko lolote linaathiri maisha yetu ya hapa duniani, haliathiri uhusiano wetu na Mungu?

 

   1. Soma Warumi 7:4-6. Hapa Paulo anatuambia kuwa tunapaswa kuishi kwa mujibu wa maelekezo ya Roho Mtakatifu. Hii inaashiria kwamba ikiwa “tunadhibitiwa” na asili ya dhambi, kimsingi tunakuwa na tatizo la kiuhusiano na Roho Mtakatifu. Unawezaje kuelezea kwa ufupi ukweli juu ya mapambano dhidi ya dhambi? (Hiki ndicho ninachokifikiria: Roho Mtakatifu akaaye ndani yetu anasimama mahali pa sheria katika kuyaelekeza matendo yetu. Tunapopambana na dhambi, ni Roho Mtakatifu ndiye anayetenda kazi pamoja nasi. Tusichoweza kukifanya ni kumpuuzia Roho Mtakatifu. Katika mapambano haya, bado tunaokolewa kwa neema. Kazi ya Roho Mtakatifu ni kuyapatanisha zaidi maisha yetu na mapenzi ya Mungu.)

 

  1. Soma Wagalatia 3:14. “Ahadi aliyopewa Ibrahimu” ni ipi? Watoto wengi? (Soma tena Wagalatia 3:6. Mbaraka unaozungumziwa hapa ni kuhesabiwa haki. Fursa hii sasa imeongezwa kwetu sisi tusio Wayahudi.)

 

   1. Ni jambo gani tunalolipokea kwa imani? (Ahadi ya Roho Mtakatifu.)

 

    1. Hii inaongezea msisitizo wa Roho Mtakatifu. Nilidhani lengo lilikuwa ni kuhesabiwa haki kwa njia ya imani, badala ya karama ya Roho Mtakatifu. Kwa nini Paulo anabainisha karama ya Roho Mtakatifu kama matokeo ya imani yetu? Hii inaturejesha kwenye Warumi 7:6. Mbadala wa kuzishika Amri Kumi sio kuishi kwa namna yoyote ile unayoichagu Mbadala ni kwamba “tupate kutumika katika hali mpya ya Roho.”)

 

  1. Rafiki, ikiwa unaamini (kama nilivyokuwa ninaamini wakati fulani), kwamba kuzishika Amri Kumi ni muhimu sana kwa ajili ya wokovu, unaweza kuona jinsi kitendo hicho kinavyoweza kukutumbukiza kwenye kulaaniwa? Kwa kuwa ni hakika kwamba utashindwa katika juhudi zako za kuishika sheria yote, utapungukiwa (utaukosa) ukamilifu, na hivyo utaukosa wokovu. Yesu anatupatia kitu kingine. Anatupatia fursa, kwa njia ya ubatizo, kushiriki kifo chake kwa ajili ya dhambi zetu, na ufufuo wake kwa ajili ya uzima wa milele. Anatupatia uchaguzi wa kuishi maisha yanayoongozwa na Roho Mtakatifu. Je, utakubali, sasa hivi, “ofa” ya Yesu?

 

Juma lijalo: Kipaumbele cha Ahadi.