Somo la 7: Njia ya Kuiendea Imani

Swahili
(Wagalatia 3:21-25)
Year: 
2017
Quarter: 
3
Lesson Number: 
7

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Hebu tufanye mapitio kidogo. Juma lililopita tulijifunza kwamba mkataba wa awali (asili) kati ya Mungu na Ibrahimu ulibainisha kuwa Ibrahimu atamwamini Mungu (kumtumaini Munu) na Mungu atamtunuku Ibrahimu haki. Hizi zilikuwa ni ahadi kati ya Ibrahimu na Mungu. Mkataba huu ulikuwa unatekelezeka hata kama Ibrahimu alikuwa mdhambi. Pia tulijifunza kwamba tulirithi upande wa Ibrahimu wa haya makubaliano ya kimkataba kati ya Mungu na Ibrahimu. Baada ya mkataba wa awali, Mungu aliwapatia wanadamu Ahadi Kumi (pamoja na sheria nyingine), na baada ya hapo, Yesu alikuja ili kuboresha mkataba kati ya Ibrahimu na Mungu. Kwa muktadha huo, je, hii inaiweka sheria katika mazingira gani? Je, ni kumbukumbu ya zamani? Ikiwa ndivyo, kwa nini ilitolewa baada ya mkataba wa awali? Ikiwa sio kumbukumbu, je, inao wajibu gani katika maisha yetu ya kila siku? Hebu tupitie somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi!

 

 1. Sheria Dhidi ya Ahadi?

 

  1. Soma Wagalatia 3:21. Unadhani hasa Paulo anawaambia Wagalatia wafanye nini? Kwa kuangalia kauli hiyo, Paulo anaonekana kuuliza endapo kwa namna fulani hivi sheria inabatilisha upande wa Mungu wa mkataba. Je, hiyo ni sahihi?

 

  1. Angalia tena Wagalatia 3:21. Paulo anatoa jibu gani? Jibu hili linatuambia nini juu ya swali ambalo Paulo alikuwa analiuliza? (Kimsingi Paulo anasema, “Jambo gani litawafanya wanadamu wawe wenye haki? Je, sheria inaweza kuwezesha jambo hilo? Hapana!” kwa kuwa sheria haiwezi kutufanya tuwe na haki, Paulo anatuambia kuwa sheria haiwezi “kupingwa,” au kuwa mbadala, kwenye makubaliano yetu ya kimkataba tuliourithi.)

 

  1. Soma Wagalatia 3:22. Uhusiano wako na dhambi ukoje? (Kama wewe ni sehemu ya ulimwengu, basi wewe ni “mtumwa wa dhambi.”)

 

   1. Paulo ana mamlaka gani kusema kwamba “ulimwengu wote ni mfungwa wa dhambi?” (Paulo anatuambia kuwa “Andiko linasema.” Biblia inatuambia kuwa sisi ni wafungwa.)

 

   1. Mantiki inakuambia nini? Kama tulivyojadili tulipojifunza Wagalatia 2, Paulo anajenga hoja kwamba kwa asili tunafahamu kuwa tuna tatizo endelevu la dhambi – tatizo ambalo sheria haiwezi kulitibu.)

 

  1. Angalia tena sehemu ya mwisho ya Wagalatia 3:22. Tiba ya tatizo letu endelevu la dhambi ni ipi? (Ahadi ya Mungu ni kwamba ikiwa tunamtumainia yeye, ikimaanisha kumwamini (kumtumaini) kwa kile ambacho Yesu amekitenda kwa ajili (niaba) yetu ili kutupatia haki, basi tutakuwa wenye haki.)

 

 1. Sheria

 

 

  1. Soma Wagalatia 3:23. Hebu subiri kidogo! Paulo amekuwa akitujengea hoja kwamba ahadi (ahadi ya haki ya kimkataba) ilikuja kabla ya sheria. Anawezaje kuandika sasa kwamba sheria “imetufunga mpaka ije ile imani itakayofunuliwa?” (Utimilifu wa upande wa Mungu wa ahadi ulikuwa ni Yesu kuja duniani, kuishi maisha makamilifu, na kufa kwa ajili (niaba) yetu ili kulipa adhabu kwa ajili ya dhambi zetu. Kabla ya hapo tulikuwa “tumefungwa” kwenye mauti ya milele kwa sababu ya dhambi zetu.)

 

  1. Soma Wagalatia 3:24. Paulo anaelezea lengo la sheria. Ni lengo gani hilo? (“Kutuleta kwa Kristo.”)

 

   1. Sheria inatupelekaje kwa Kristo? Nilidhani hapo awali Paulo alituambia (katika Warumi 7:7-12) kwamba mwitiko wetu wa kidhambi kwenye sheria ulitufanya tutende mambo yale yale ambayo hatupaswi kuyatenda. Kama ilivyo kwenye ishara za “usiguse” kwenye makumbusho ya magari zinavyokufanya utake kuyagusa magari! Hili linatuletaje kwa Yesu? (Tunatambua kwamba hatuwezi kuishika sheria. Sheria ni kipimo, na njia pekee tunayoweza kufikia kipimo chake kikamilifu ni kwa njia ya kile ambacho Yesu amekitenda kwa ajili (niaba) yetu.)

 

   1. Badala ya “kutuleta kwa Kristo,” tafsiri ya Biblia ya Mfalme Yakobo (KJV) inatafsiri Wagalatia 3:24 kwamba “sheria ilikuwa mkuu wetu wa shule.” Tafsiri hiyo inatoa umaizi (ufahamu) gani mwingine wa ziada? (Ukiangalia jinsi tafsiri tofauti tofauti zinavyotafsiri lugha ya asili ya Biblia, ni sawa na kuangalia kito kutokea kwenye kona mbalimbali. Tunajifunza jambo tunapojikuta tunakiuka sheria ya Mungu. Tunajifunza kuwa sheria yake iko sahihi, na tunajifunza kwamba tu wabaya sana katika kuishika. Hiyo inatufundisha kwamba sheria ni nzuri na sisi si wema. Tunatakiwa kudai mbadala kamili wa Yesu kwa ajili yetu.)

 

  1. Soma Wagalatia 3:25. Inamaanisha nini kwamba hatupo tena “chini ya uongozi wa sheria?” Kwamba sheria haina tena chochote cha kutufundisha? Hilo linawezekanaje?

 

   1. Je, kuna tofauti kati ya mwalimu na msimamizi? Je, kuna tofauti kati ya mwalimu wa shule na afisa wa polisi? (Hii itaonesha tofauti kubwa kutokana na jinsi kifungu hiki kinavyotafsiriwa kwenda kwenye lugha ya Kiingereza. Lakini, nilipoangalia jambo hili katika tafsiri ya Strong, neno lile lile la Kiyunani linatumika katikia kifungu cha 24 (mwalimu) kama ambavyo linatumika katika kifungu cha 25 (msimamizi).)

 

   1. Hii inatuweka kwenye kasha la mantiki. Wagalatia 3:24 inatuambia kuwa sheria inatuleta kwa Yesu. Wagalatia 3:25 inasema kuwa hatuhitaji tena uongozi wa sheria. Unaweza kuelezea jambo hili?

 

  1. Soma tena Wagalatia 3:24-25. Ikiwa wajibu wa sheria umebadilika kati ya hivi vifungu viwili, je, kuna jambo jingine lolote lile kati ya hivi vifungu viwili? (Kifungu cha 24 kinasema sheria “inatuleta kwa Kristo.” Kifungu cha 25 kinasema, “iwapo imani imekuja.” Kwa kuangalia jambo hili, ningeweza kudhani kwamba “kuja kwa imani” kulimaanisha “kuja kwa Yesu.” Lakini, ikiwa unasoma “kuja kwa imani” kama imani yako kwa Yesu inavyokua, basi tunaweza kuona tofauti yenye mantiki. Sheria ilituongoza (ilitufundisha) juu ya hitaji letu la Yesu. Yesu alipokuja na tukaamini yeye ndio mbadala wetu kamilifu, basi Roho Mtakatifu anakuwa mwalimu wetu wa msingi, sio sheria.)

 

 

  1. Ikiwa una mashaka juu ya maelezo haya, hebu tupitie anachokisema Paulo kuhusu sheria katika kitabu cha Warumi. Soma Warumi 8:1-2. Paulo anasema kuwa jambo gani limebadilika hapa? (Anasema kuwa “sheria ya Roho wa uzima” imetuweka huru mbali na “sheria ya dhambi na mauti.” Hii inaonekana kama maisha yanayoongozwa na Roho Mtakatifu yametuweka huru mbali na maisha yanayoongozwa na Amri Kumi.)

 

  1. Soma Warumi 8:3-4. Hii inatuambia kuwa sheria haina uwezo wa kutenda jambo gani? (Haiwezi kutuokoa kwa sababu sisi ni “mtu [mwili] mwenye dhambi.” Hata hivyo, kupitia kwa Yesu, “matakwa ya kisheria ya haki yanaweza kufikiwa na kutekelezeka.”)

 

   1. Hapa masharti ni yapi? (Kwamba tuishi “kwa mujibu wa Roho.”)

 

   1. Je, sasa jambo hili linaleta mantiki kwako? Kabla Yesu hajaja, sheria ilitufundisha habari za Mungu na ikatufundisha hali yetu ya kutokuwa na uwezo wa kuishi maisha makamilifu. Kwa kuwa Yesu alikuja, alitimiza wajibu wetu kwenye sheria (tukiikubali na kuipokea kafara yake kwa ajili ya maisha yetu ya dhambi), lakini Yesu ametenda zaidi ya jambo hilo. Yesu ametupatia Roho Mtakatifu ili awe kiongozi wa maisha yetu.)

 

  1. Soma Yohana 16:5-7. Nani anayekuja baada ya Yesu kuondoka kurejea mbinguni? (Roho Mtakatifu.)

 

  1. Soma Yohana 16:8-11. Majukumu ya Roho Mtakatifu ni yapi? (Kama anavyotuambia Paulo! Kama ambavyo sheria ilitufunulia upungufu wetu, Roho Mtakatifu anatugusa na kututia hatiani. Anatugusa kwenye “dhambi na haki na hukumu.”)

 

   1. Unadhani Roho Mtakatifu ana kipimo tofauti kwa ajili ma maisha yetu kama kile kilichowekwa kwenye Amri Kumi? (Soma Warumi 3:3 Hakuna ubaya wowote kwenye sheria, kuna jambo lisilo sahihi kwetu! Ndio maana tunahitaji neema. Roho Mtakatifu ni Mungu. Haileti mantiki kwa kiwango cha juu kabisa kudhani kwamba Roho Mtakatifu atatuongoza kutenda mambo ambayo sheria inayabainisha kuwa ni dhambi.)

 

  1. Soma Warumi 8:5-8. Paulo anasema kuwa jambo gani lina uhusiano kati ya uongozi wa Roho Mtakatifu na sheria? (Ikiwa “nia ya dhambi ya mwili” “haitii sheria ya Mungu,” hii inaashiria kwamba kimsingi mawazo “yaliyojikita kwenye kile ambacho Roho anachokitamania” yanatii sheria ya Mungu.)

 

   1. Je, “kujitoa” ni sawa na “kutii?” (Tukiweka mwanya hapa na kuishia kusema kwamba tunalazimika kuitii sheria ili tuweze kuokolewa, basi tunafanana na Wagalatia “waliorogwa” (angalia somo la juma lililopita)! Kama Wagalatia 3:3 inavyoonya, hatutakiwi kuanza na Roho kisha turudi kujaribu kujipatia haki kwa juhudi zetu za kibinadamu.)

 

  1. Soma Waebrania 8:10. Inamaanisha nini sheria ya Mungu kuandikwa mioyoni mwetu? (Hapa ndipo mahali tunapotaka kuwepo. Roho Mtakatifu anakaa ndani yetu na kutufikisha kwenye hatua ya kutaka kuyatenda mapenzi ya Mungu. Sisi si waasi tena, bali wafusi wa Mungu wenye shukrani.)

 

  1. Rafiki, je, ungependa sheria ya Mungu iandikwe moyoni mwako? Je, unataka kuwa na uhusiano na Mungu maishani mwako, na si kuwa na uhusiano na mabaki ya binadamu (utii wa mwanadamu wa sheria)? Kwa nini usimwombe Roho Mtakatifu kila siku ili ayaongoze maisha yako?

 

 

 1. Juma lijalo: Kutoka Kuwa Watumwa Hadi Kuwa Warithi.