Somo la 12: Kuushinda Uovu kwa Wema

Swahili
(Warumi 12 - 13)
Year: 
2017
Quarter: 
4
Lesson Number: 
12

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Unakumbuka juma lililopita Paulo alikuwa anajiuliza sana kuhusu Wayahudi wenzake? Alitaka wote waokolewe, lakini kushindwa kwao kuyafuata mapenzi ya Mungu kulikuwa na upande chanya: kulifanya ujumbe maalum wa Paulo uwafikie Mataifa. Paulo aliandika kuwa Mataifa wanapaswa kuwa na shukrani kutokana na fursa hii ya pekee “kupandikizwa” ndani ya wale walioteuliwa kupeleka injili. Juma hili Paulo anaendelea na fikra hii kwa kutuambia kuwa shukrani yetu kwa kile alichotutendea Mungu kinapaswa kuyabadili maisha yetu. Hebu tuendelee na somo letu la Warumi kwa kuzama kwenye Warumi 12 na 13!

 

 1. Dhabihu Iliyo Hai

 

  1. Soma Warumi 12:1. Unadhani kwa nini Paulo anatuambia kuwa tunapaswa kuwa “dhabihu iliyo hai?” Hiyo inaashiria nini kuhusu namna tunavyoishi maisha yetu? (Wokovu wetu kwa njia ya imani pekee ni matokeo ya kafara ya Yesu kwa ajili yetu. Hiyo inapaswa kutufanya kujitoa dhabihu ili kuutangaza ufalme wa Mungu. Dhabihu inamaanisha kujitoa kwa ajili ya jambo kubwa. Tunapaswa kuziacha tamaa zetu zilizojaa ubinafsi kwa ajili ya mambo makubwa zaidi ya kumpa Mungu utukufu.)

 

  1. Soma Warumi 12:2. Tunawezaje kuyajua mapenzi ya Mungu? Je, Paulo anatuambia tujifunze Amri Kumi kwa makini sana? (Paulo anatuambia kuwa mawazo yetu yanatakiwa kufanywa upya. Tunatakiwa kuyazingatia mapenzi ya Mungu.)

 

   1. Soma Mathayo 5:27-28. Yesu anasema nini kuhusu dhambi ya uzinzi? (Anasema kuwa sio tu suala la kusaga meno yetu na kutokufanya uzinzi. Ikiwa hatuyaelewi mapenzi yake, tunaonekana kuwa chini sana. Mungu anazitaka nia zetu, sio miili yetu tu, ili kuwa mbali na suala la uzinzi. Hiki ndicho Paulo anachokiandika katika Warumi 12:2 anaposema kuwa nia zetu zinatakiwa kufanywa upya ili tuwe wafuasi kamili wa Yesu.)

 

   1. Unapendekeza kuwa ufanye nini kuhusu kuifanya upya nia yako ili kuyaeleza mapenzi ya Mungu vizuri zaidi?

 

 1. Kuziweka Kazini Nia Zilizofanywa Upya

 

  1. Soma Warumi 12:3. Matokeo ya kwanza ya kuzifanya upya nia zetu ni yapi? (Tunatakiwa kuepuka kiburi. Badala ya kutafakari, kwa mujibu wa matendo yetu, kwamba sisi ni bora kuliko watu wengine, tunatakiwa kuzingatia viwango vyetu vya imani.)

 

   1. Je, umewahi kujaribu kujifanyia tathmini katika suala la kumtumaini Mungu? Nini matokeo ya tathmini yako juu ya imani yako kwa utulivu kabisa?

 

 

  1. Soma Warumi 12:4-5. Kwa nini kujiangalia nafsi yako kama kiungo kimoja tu cha mwili inakusaidia kuwa na mtazamo wenye mantiki zaidi wa thamani yako binafsi? (Mwili hauwezi kufanya kazi kwa kiungo kimoja pekee. Mkono si chochote pasipo mwili uliosalia. Hivyo, kuelewa kwamba wajibu wetu katika Ufalme wa Mungu ni sawa na kiungo kimoja cha mwili inatusaidia kuwa wanyenyekevu.)

 

  1. Soma Warumi 12:6-8. Je, unatakiwa kuamua kuwa ungependelea kuchagua wajibu fulani kanisani? (Paulo anatuambia kuwa, kwa neema, sisi ni karama zilizotolewa. Unapaswa kugundua karama yako na kisha kutimiza wajibu wako kanisani.)

 

   1. Rejea ya Paulo kwenye ukweli kwamba tunapewa hizi karama kwa neema inatufanyia nini katika juhudi zetu za kuepuka kuwa na kiburi? (Si kosa lako ikiwa umepewa karama unayodhani kuwa inakufaa zaidi. Hupaswi kudhani kuwa wewe ni bora zaidi kutokana na karama yako.)

 

  1. Soma Warumi 12:9-13. Kauli hii inayohusu jinsi tunavyopaswa kuishi kwa namna ya kumpendeza Mungu inatofautianaje na Amri Kumi? Je, ungependa kushtakiwa kutokana na kuzishika Amri Kumi au kutenda kinachosemwa hapa? (Hii ndio sababu wale wanaojenga hoja kuhusu Amri Kumi wanachanganyikiwa sana. Kuzishika Amri Kumi sio kiwango cha juu kabisa, ni kiwango cha chini. Anachokiandika Paulo hapa kinaakisi kwa usahihi kabisa kile alichotufundisha Yesu kuhusu uzinzi – sio tu kuepuka kitendo cha kufanya uzinzi, bali kuwa na mtazamo sahihi.)

 

   1. Unaelezeaje kile ambacho Paulo anatuhamasisha kwenye hivi vifungu? Je, hivi ni vitendo au mitazamo? (Hii ni mitazamo: upendo, ibada, ari, tumaini, subira, uaminifu, ukarimu.)

 

   1. Nikikwambia kuanza kupenda au kuanza kuwa na bidii, utafanya nini? Kwa dhahiri haya sio mambo ambayo “unayafanya” (au unajizuia kuyafanya) kama mojawapo ya Amri Kumi. Mambo hayo ni usiibe, usiue, nk. Haya ni mabadiliko mawazoni mwako, mabadiliko ya mtazamo wako.)

 

   1. Soma tena Warumi 12:2. Je, sasa ni dhahiri kwamba ni muhimu sana kwa nia zetu kufanywa upya na kubadilishwa? Hii pia inapaswa kuwa dhahiri kwamba jambo hili haliwezi kupatikana kwa kufuata orodha ya amri. Badala yake, linapatikana kwa Roho Mtakatifu kuzibadili nia yetu. Kwa mara nyingine, hii ni neema tu. Unatakiwa kufanya uchaguzi. Unatakiwa kumwomba Roho Mtakatifu kubadili nia yako.)

 

 1. “Mind to Hand”

 

  1. Soma Warumi 12:17-21. Je, haya ni matendo tunayoweza kuyatenda? (Ndiyo, kwa ujumla hii ni orodha ya matendo kinyume na mitazamo. Lakini, ni matendo magumu sana kuyatenda bila kuwepo kwa badiliko la mtazamo.)

 

  1. Soma Warumi 13:1-2. Tunatakiwa kuwa na mtazamo gani dhidi ya serikali? (Hatupaswi kuwa waasi.)

 

 

   1. Ungetekelezaje jambo hili kivitendo endapo ungekuwa mmojawapo wa wateja wangu? Wateja wangu wanaambiwa na waajiri wao (mara nyingi huwa ni serikali) kwamba wanapaswa kutegemeza chama cha wafanyakazi. Wateja hawataki kulipa fedha kwenye chama kwa sababu wanaamini kuwa kinajihusisha na mambo maovu. Je, ni uasi kupinga kukilipa chama? (Inategemeana na aina ya serikali. Mfumo wa mahakama nchini kwangu ni sehemu ya hatua za serikali kutatua migogoro. Kwenda mahakamani kuepuka kushiriki kwenye jambo unaloamini kuwa Mungu amelikataza si uasi, ni kutumia zana zinazotolewa na serikali kuepuka migogoro.)

 

  1. Soma Warumi 13:3. Je, hiki ndicho ulichokigundua?

 

  1. Soma Warumi 13:4-5. Paulo anatuambia kuwa inaleta mantiki kabisa kuitii serikali. Kwa kutii utaepuka adhabu. Paulo anatoa sababu gani ya pili ya kuitii serikali? (Dhamiri yetu. Hicho ndicho anachokitaka Mungu kutoka kwetu.)

 

   1. Kwa nini dhamiri zenu zihusike kwenye huu uamuzi? (Wazo la mamlaka limetolewa na Mungu. Maisha yanakuwa bora zaidi kuishi chini ya utawala wa sheria.)

 

   1. Vipi kama serikali yako ni ovu? Vipi kama inawaua wanyonge na wasio na msaada? (Kwa kuwa Paulo anatuambia kuwa dhamiri ndio sababu ya utii, inaleta mantiki kuhitimisha kwamba ikiwa serikali inajihusisha na uovu – au kibaya zaidi, serikali inakutaka ujihusishe na uovu – basi dhamiri ndio itakayokuwa sababu ya kutokutii.)

 

  1. Soma Warumi 13:6-7. Nchini kwangu, kodi zangu zinakwenda kusaidia kuua watoto ambao bado hawajazaliwa. Je, ninapaswa kuliangalia jambo hili kama suala ovu – na kukataa kulipa sehemu ya kodi zangu? Watu wengine wanaweza kutafakari kuacha kulipa kodi zao kutokana na vita isiyo ya haki. Je, hayo ni makosa? (Kwa mujibu wa kodi, Paulo anasema lipa kile unachostahili. Wale wanaoongoza wanawajibika kwa Mungu kwa uovu wanaojihusisha nao kwa fedha ya kodi. Ndio maana Rumi ilijihusisha na uovu wa aina yote kwa kodi iliyokusanya.)

 

  1. Soma Warumi 13:8. Paulo anasema nini kuhusu upendo na sheria?

 

   1. Tafakari jambo hili kidogo. Je, unaona kwamba kuwapenda watu wengine ndio msingi wa Amri Kumi? Je, unaona kwamba kuwa mbinafsi ndio msingi wa dhambi? (Soma Warumi 13:9-10. Upendo humaanisha kwamba hatumdhuru jirani!)

 

  1. Soma Warumi 13:11-13. Tumerejea kujadili matendo. Je, mtazamo wa upendo kwa watu wengine ndio kiini cha kuepuka hizi dhambi mahsusi pia?

 

  1. Soma Warumi 13:14. Tunamvaaje Yesu Kristo? (Alitupenda upeo kiasi cha kutufilia. Jivike mtazamo huo unapochangamana na watu wanaokuzunguka. Hii ndio kazi ya muhimu ya Roho Mtakatifu – kutuvika na mtazamo wa kimungu.)

 

 

  1. Rafiki, kiasi gani cha maisha yako kinageukia katika kuzingatia kwamba unatendewa vyema na kupewa haki yako inayokustahili? Kiasi gani cha maisha yako kinazingatia kuhakikisha kwamba mahitaji yako yanapatikana? Ikiwa somo hili linakuchochea kuutafakari upya mtazamo wako, kujumuisha mtazamo usio na ubinafsi, kwa nini usimwombe Roho Mtakatifu, sasa hivi, akujie na kukubadilisha?

 

 1. Juma lijalo: Kuishi Kikristo