Deni – Uamuzi wa Kila Siku

(Kumbukumbu la Torati 15, Mithali 17, 2 Wafalme)
Swahili
Year: 
2018
Quarter: 
1
Lesson Number: 
11

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Jarida la Forbes linataarifu kuwa kutumia fedha kipumbavu ndio chanzo cha kwanza kabisa cha wanandoa kutalikiana. Wakati watu wengine wanahoji kiwango cha uhusiano kati ya fedha na talaka, mtazamo wa kawaida ni kwamba matatizo ya kifedha yana kawaida ya kupenya hadi kwenye maeneo mengine ya maisha ya kifamilia na kusababisha msuguano. Ubashiri wangu ni kwamba wanandoa hawagombani juu ya namna ya kutumia fedha za ziada, bali wanagombana kutokana na madeni yanayotokana na matumizi ya kijinga ya fedha. Je, unafahamu kuwa Biblia inatupatia ushauri kuhusu madeni? Hebu tuchimbue somo letu la Biblia na tuone kile tunachoweza kujifunza kuhusu mtazamo wa Mungu juu ya madeni!

 

  1.    Kanuni za Agano la Kale Kuhusu Deni

 

    1.    Soma Kumbukumbu la Torati 15:6. Tumejadili mara kadhaa ahadi za Mungu kutubariki kifedha ikiwa tutakuwa wakarimu kwake kwenye matumizi ya fedha na talanta zetu. Kifungu hiki kinashiria nini kuhusu baraka za Mungu kwetu na deni? (Hii inatuambia kuwa baraka za Mungu zitatufanya tuwe wakopeshaji, na kutuepusha kuwa wakopaji.)

 

      1.    Kifungu hiki kinalinganisha ukopaji wa fedha na kitu gani? (Unatawaliwa na wale wanaokudai fedha.)

 

      1.    Je, kifungu hiki kinasema kuwa kukopa fedha ni makosa? (Hapana. Lakini, hakiweki kitendo cha kukopa kwenye hali chanya. Kinasema kuwa katika suala la kukopesha na kukopa, Mungu anatutaka tuwe wakopeshaji!)

 

    1.    Soma Kumbukumbu la Torati 15:1-3. Jambo gani lilitokea kila baada ya miaka saba katika mfumo wa ukopaji na ukopeshaji miongoni mwa Waisraeli? (Madeni yalifutwa!)

 

      1.    Fikiria jinsi mfumo wa Mungu kwa watu wake unavyolinganishwa na mfumo wa kisasa wa benki. Je, benki zinataka kukupatia “credit cards” ili uweze kuingia kwenye madeni? (Naam.)

 

        1.    Tabia za benki zitabadilikaje ikiwa madeni yangekuwa yanafutwa kila baada ya miaka saba? (Leo, benki zinataka kutushawishi kuingia kwenye madeni kwa sababu zinatoza riba kubwa sana. Lakini, hii inaonesha kuwa chini ya mfumo wa Mungu, kiuhalisia wakopeshaji walikabiliana na ukomo mdogo sana wa ukopeshaji.)

 

      1.    Vipi kuhusu kuwakopesha wageni? (Hiyo ilikuwa tofauti.)

 

    1.    Soma Kumbukumbu la Torati 15:7-9. Naam, naam! Hii inaelezea ukomo wa dhahiri kwenye mfumo wa ufutaji madeni kila baada ya miaka saba. Mungu anaiita jina gani ikiwa hutaki kukopesha fedha mwaka wa saba unapokaribia? (Dhambi!)

 

    1.    Soma Kumbukumbu la Torati 15:10-11. Kifungu kinapozungumzia “katika nchi yako” na “nduguyo,” hii inazungumzia nini kuhusu sera ya Mungu? Tafsiri ya NIV inaandika kuwa “kwa nduguzo na kwa maskini na wahitaji.” Hata hivyo, hivyo sivyo tafsiri nyingine za Biblia nilizozisoma zinavyoshughulika na jambo hili. Tafsiri nyingine za Biblia zinawazungumzia maskini na wahitaji miongoni mwa nduguzo. Hii inaonekana kujikita kwenye sera ya waumini wenzako.)

 

    1.    Soma Mithali 3:28. Kifungu hiki kinaunga mkono kanuni gani? (Ulipaji wa madeni kwa wakati.)

 

    1.    Soma Kumbukumbu la Torati 28:12-14. Unapotafakari vifungu hivi pamoja na mambo tuliyojifunza kutoka katika Kumbukumbu la Torati 15, Mungu anaunganisha dhana zipi? (Mafundisho yanayohusu uhusiano kati ya utii na baraka, kanuni za ukopedhaji na jinsi tunavyowajali maskini.)

 

      1.    Kwa nini dhana hizi zinaunganishwa? (Lengo la Mungu ni kutubariki ili tusiwe na hitaji la kukopa. Lakini, kuwakopesha maskini (na kuwasamehe madeni yao), ni sehemu ya kuwa wakarimu kwa Mungu.)

 

      1.    Ikiwa kuwa watiifu kwa Mungu kutatuepusha kuwa na madeni, je, kanuni hizo ni zipi? Hebu tuchimbue zaidi katika sehemu inayofuata!

 

  1.   Kudhamini Mikopo

 

    1.    Soma Mithali 17:18 na Mithali 22:26. Inamaanisha nini “kudhamini?” (Hili ni hakikisho la ulipaji wa deni. Biblia inatuonya kuhusu kutoa ahadi ya kulipa deni la mtu mwingine ikitokea mtu huyo ameshindwa kulilipa.)

 

      1.    Kimsingi kwa nini hii ni tofauti na kumkopesha huyo mtu mwingine?

 

    1.    Soma Mithali 22:27. Hii inaashiria kuwa tatizo halisi ni lipi kwa kitendo cha kuwa mdhamini wa deni? (Tatizo halisi ni kushindwa kulipa deni. Kama kweli ungekuwa na fedha, basi ungechukua deni wewe mwenyewe. Lakini, tatizo linatokea pale unapotaka kuwa wa msaada (au kuonekana tajiri) wakati huna fedha.)

 

  1. Kukopa Vitu

 

    1.    Soma 2 Wafalme 6:4-7. Mtu ambaye kwa isivyo bahati alipoteza chuma cha shoka angekuwa na wajibu gani endapo Elisha asingekuwepo mahali pale kutenda muujiza? (Soma Kutoka 22:14-15. Unatakiwa kulipa. Hii sivyo ikiwa ulilipa ili kuazima shoka au kama mmiliki wa shoka alikuwa akifanya kazi pamoja nawe.)

 

    1.    Wazazi wa mke wangu walikuwa wakulima maskini. Anasimulia kisa cha baba yake kuazima mashine ya kutobolea kwa jirani yake. Mashine iliungua kwa umeme baba yake alipokuwa anaitumia, na matokeo yake ni kwamba walimlipa jirani yao mashine mpya na hawakuwa na chochote cha kujivunia. Je, njia bora ingekuwa ipi? (Kununua mashine mpya kwa ajili yako.)

 

  1.   Akili ya Kawaida

 

    1.    Soma Luka 14:28-30 na Mithali 21:5. Hii inaashiria nini kuhusu matumizi ya fedha? (Tumia akili! Panga kwa umakini. Andaa bajeti. Hakikisha una fedha za kutosha kwa mradi wowote unaotaka kuutekeleza.)

 

    1.    Soma Mithali 22:1. Kwa nini watu wanataka kuishi kuliko vipato vyao? Kwa nini ukope fedha ili uonekane una mali nyingi? (Unadhani kuwa kwa kufanya hivyo kutakutukuza zaidi. Watu wengine watakufikiria vizuri zaidi.)

 

      1.    Kifungu hiki kinasema kuwa jambo gani ni bora zaidi kuliko kuonekana tajiri? (Kuwa na jina jema. Habari njema ni kwamba jina jema halikugharimu chochote zaidi ya kukufanya uyasimamie maneno yako na kumtii Mungu.)

 

      1.    Tukiyaweka pamoja maelekezo ya Luka 14 ya kutumia akili na Mithali 22, je, kukopa fedha ili kuonekana tajiri kunaishia kuwa na matokeo unayoyataka? (Hapana. Unaishia kuwa maskini zaidi. Sio tu kwamba utatakiwa kulipa deni, bali pia wakopeshaji wanachukua sehemu ya fedha zako kwenye riba.)

 

    1.    Soma 1 Timotheo 6:6-8. Hapa tunaona tiba gani kwenye matamanio yetu ya kukopa fedha ili kununua vitu vipya? (Kuwa na kiasi (kuridhika).)

 

    1.    Soma Mithali 13:11. Ikiwa una tamaa (lengo) ya kuwa na vitu vizuri, kifungu hiki kinasema kuwa tunapaswa kutimizaje lengo hilo? (Kwa kuweka akiba sehemu ya fedha zetu.)

 

    1.    Soma 1 Timotheo 6:9-10. Je, kukopa fedha usizozihitaji ni “tamaa ya kipumbavu yenye kudhuru?” (Ikiwa unakopa ili “kuonekana tajiri,” basi tamaa hii ni “mtego.”)

 

    1.    Soma tena Luka 14:28 na utumie dhana hii kwenye magari tunayoyaendesha. Ninakumbuka nilipokuwa mdogo, nilikuwa na magari mawili na nilikuwa ninabadilisha mojawapo ya magari hayo kwa kununua gari jipya takribani kila baada ya miaka miwili. Kimsingi nilikopa fedha ili kununua magari yangu. Siku moja, niliangalia nyumba yangu ndogo yakiwepo magari yangu mawili “mapya” yakiwa yameegeshwa nje (nyumba yangu haikuwa na gereji ya kuegeshea magari). Utabadili nini kutokana na taswira hii? (Nilitambua kwamba fedha zangu zilikuwa mahali pasipostahili. Magari yanachakaa, kwa kawaida nyumba zinaongezeka thamani. Nilinunua nyumba kubwa zaidi (yenye gereji) na kuendesha magari ya mtumba kwa miaka ishirini iliyofuatia.)

 

      1.    Je, kununua magari yasiyo ya gharama sana ya mtumba itakufanya ujisikie kama vile uko kwenye utaratibu maalumu wa chakula (aghalabu kwa mtu anayetaka kupunguza uzito/unene)? Kwamba unafahamu ni jambo jema kufanya hivyo, lakini unachukia mchakato wote wa utekelezaji? (Angalia jinsi Mungu alivyobariki mpango wangu wa “gari langu la mtumba.” Wakati fulani nilikuwa na magari mawili mazuri kwenye gereji yangu: gari jekundu aina ya Corvette na gari la Mercedes. Nje ya gereji yangu palikuwepo na gari la bluu iliyokolea aina ya Mercedes S Class nililolitumia kuendea kazini kila siku na gari aina ya Dodge Grand Caravan ambalo nililitumia kubebea vitu. Magari yote haya yaligharimu dola za Marekani 16,000. Najua hii inaonekana kuwa jambo lisilowezekana, lakini ni ukweli.)

 

    1.    Tumekuwa tukijadili juu ya ukopaji wa fedha kwa mambo tusiyoyahitaji. Vipi kama tunahitaji kukopa fedha ili tuweze kuishi? Soma Mathayo 6:28-33. Mungu anatoa mbadala gani dhidi ya kukopa fedha kwa ajili ya kuishi?

 

      1.    Inaonekanaje “kuutafuta kwanza ufalme wake na haki yake?” (Kuwa mkarimu kwa Mungu hutuletea baraka, kama tulivyojadili kwenye masomo yetu yaliyotangulia kwenye mfulilizo wa masomo haya. Pili, kuwa na vipaumbele sahihi itatusaidia kuwa na malengo mazuri kibajeti.)

 

      1.    Ungependa kuishije maisha yasiyo na wasiwasi kuhusu masuala ya fedha?

 

    1.    Rafiki, maisha yako yatakuwa bora zaidi pasipokuwa na deni. Kwa nini usidhamirie, sasa hivi, kwamba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, utadhamiria na kujitahidi kuwa mkopeshaji badala ya mkopaji?

 

  1.    Juma lijalo: Tabia za Wakili.