Kristo Katika Patakatifu pa Mbinguni

Error message

  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
  • Deprecated function: unserialize(): Passing null to parameter #1 ($data) of type string is deprecated in css_injector_init() (line 53 of /home/krwester/gobibletranslations.org/sites/all/modules/css_injector/css_injector.module).
(Waebrania 7-10)
Swahili
Year: 
2018
Quarter: 
2
Lesson Number: 
5

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Katika kipindi cha ujana wangu, nilifundishwa Biblia yote, sio Agano Jipya pekee. Agano la Kale lilizungumzia kuishika sheria, Agano Jipya lilimzungumzia Yesu. Kilichonivutia ni kwamba haya maagano mawili yalikuwa tofauti sana. Msisitizo wa Agano la Kale ulihusu wokovu kwa njia ya matendo na Agano Jipya lilisisitiza wokovu kwa njia ya Yesu. Ni katika kipindi cha baadaye maishani ndipo nilipoanza kutafakari kwa kina njia za Agano la Kale za kuondoa dhambi. Haikuwa mfululizo wa matendo. Hukuhitajika kupata mateso kwa namna fulani ili kufanya upatanisho wa dhambi. Badala yake, mnyama alichinjwa ili kuchukua (kuondoa) dhambi zako. Agano la Kale, kama ilivyo kwa Agano Jipya, lilifundisha juu ya msamaha wa dhambi kwa njia ya kifo mbadala. Juma hili somo letu linahusu kile ambacho Yesu, kwa kufuata ishara ya Agano la kale, anakifanya sasa hivi kwa niaba yetu ili kuondoa dhambi zetu. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia!

 

  1.    Mfano wa Melkizedeki

 

    1.    Soma Waebrania 7:1-3. Melkizedeki alishika nyadhifa gani? (Alikuwa mfalme na kuhani wa Mungu wa kweli.)

 

      1.    Kutokana na uelewa wako wa Biblia, jambo hili ni la kawaida kwa kiasi gani? (Kamwe halikutokea miongoni mwa watu wa Mungu. Waliongozwa na mitume hadi walipodai kuwa na mfalme. Kisha baada ya hapo, kamwe mfalme hakuwa kuhani. Kwa njia hii, Mungu alitenganisha “kanisa na dola” miongoni mwa watu wake.)

 

      1.    Tunafahamu nini kumhusu huyu kuhani-mfalme aliyeitwa Melkizedeki? (Nadhani hatujui chochote nje ya mwingiliano na uhusiano wake na Ibrahimu.)

 

      1.    Unadhani kiuhalisia Melkizedeki, kama ilivyo kwa Yesu, anasalia kuwa kuhani milele? Ikiwa ndivyo, tunao makuhani wawili wa milele, Yesu na Melkizedeki! (Watoa maoni mbalimbali wanaamini, na ninakubaliana nao, kwamba mwandishi wa kitabu cha Waebrania anamaanisha kuwa, tofauti na ukuhani halisi wa Lawi, kiukweli hatujui chochote kuhusu habari za Melkizedeki. Hatujui ukoo wake, hatujui alizaliwa lini au alikufa lini. Ikiwa jambo hili halijaandikwa kiishara basi tunaye mungu wa namna fulani ambaye Ibrahimu alikuwa mtiifu kwake! – kamwe hakuumbwa na hana mwisho. Hilo haliendani na Biblia yote.)

 

    1.    Soma Waebrania 7:11-16. Unadhani kwa nini mwandishi wa kitabu cha Waebrania anamtaja Melkizedeki? (Kinachomaanishwa ni kutomfanya Melkizedeki kuwa Mungu, badala yake ni kubainisha kigezo cha Kibiblia kwa ajili ya “mfalme-kuhani” ambaye hakuzaliwa kutoka nje ya kabila la Lawi. Ingawa ulinganifu mkubwa kati ya Melkizedeki na Yesu ni wa kiishara, anachokimaanisha mwandishi ni kwamba Yesu ni Mfalme wetu na Kuhani wetu Mkuu hata kama hakutokana na kabila la Lawi.)

 

  1.   Yesu Kuhani Wetu Mkuu

 

    1.    Soma Waebrania 7:26-28. Kuna manufaa gani kwa Makuhani Wakuu wa Lawi wa Yesu kuwa Kuhani wetu Mkuu? (Yesu si mwanadamu mdhambi. Yesu alitakiwa kutoa dhabihu (kafara) moja tu kwa ajili yetu, kafara ya kujitoa kwake yeye mwenyewe.)

 

    1.    Soma Waebrania 8:1-2. Yesu anafanya nini sasa hivi? (Anatumika kama Kuhani wetu Mkuu.)

 

      1.    Anafanyia wapi kazi hii? (Mbinguni!)

 

    1.    Soma Waebrania 8:3-5. Tunajifunza nini kuhusu ubunifu wa patakatifu pa mbinguni? (Panafanana na pale ambapo Mungu alimwagiza Musa apajenge.)

 

      1.    Mambo haya mawili yanafananaje? (Tulichokuwa nacho hapa duniani ni “kivuli,” lakini hata hivyo nakala, ya patakatifu pa mbinguni.)

 

        1.    Patakatifu pamekuwepo mbinguni kwa muda gani? (Hii inaashiria kwamba palikuwepo mbinguni wakati Musa alipokuwa hai.)

 

          1.   Kwa nini? Tatizo la kimantiki ni muda: hii ni kabla Yesu hajafa kwa ajili yetu. (Lazima jibu lenye mantiki liwe ni kwamba patakatifu pa mbinguni panatumika zaidi kuliko lengo moja la kazi aifanyayo Yesu sasa hivi kushughulikia tatizo letu la dhambi. Kutoka 25:8-9 inatupatia mwanga kuhusu jambo hilo. Inatuambia kuwa Mungu alielekeza ujenzi wa patakatifu pa duniani ili Mungu aweze kukaa nasi. Hekalu halisi la mbinguni linaweza pia kuwa mahali anapokaa Mungu.)

 

    1.    Soma Waebrania 9:11-14. Kazi ya Yesu kwa ajili yetu imeboresheka zaidi kwa kiasi gani? (Yesu anajitoa kwa ajili yetu, kitendo ambacho “husafisha dhamiri zetu na matendo mafu, ili tupate kumwabudu na kumtumikia Mungu aliye hai.”)

 

      1.    Jambo gani lililo jema kwako kwenye hiyo sehemu niliyoinukuu? (Nimependa kwamba sasa dhamiri yangu i safi – imesafishwa. Sasa njia yangu si tena ile inayyoelekea kifoni. Hii inaniruhusu kumtumikia Mungu.)

 

  1. Kazi ya Agano

 

    1.    Soma Waebrania 9:15. Hii inazungumzia kitendo cha Yesu kufa kwa ajili ya dhambi zetu chini ya “agano la kwanza,” lakini kifungu kinasema kuwa Yesu ni Mpatanishi (mjumbe) “wa agano jipya.” Agano ni mkataba, je, tunao mkataba mpya? Ikiwa ndiyo, je, vigezo gani vimebadilika?

 

    1.    Hebu tuchunguze hili agano jipya zaidi. Soma Waebrania 8:10-12. Hiki ni kipindi gani? (Kifungu cha 10 kinasema tu kwamba “baada ya siku zile.” Kinarejea kipindi cha agano la kwanza. Kwa kuwa Waebrania inatuambia kuwa kwa sasa Yesu ni mjumbe wa agano jipya, lazima hiyo ijumuishe kipindi cha sasa.)

 

      1.    Tunaambiwa kuwa Mungu atatupatia sheria zake katika nia zetu na kuziandika katika mioyo yetu. Pia tunaambiwa kuwa hatuwahitaji watu kama mimi – walimu! Hii inamaanisha nini? (Kimsingi, ujio wa Roho Mtakatifu kwa uwezo mkuu hutimiza wajibu huu. Angalia, Yohana 16:7-13. Ikiwa kipindi hiki hakina mwisho, basi huenda pia kinaizungumzia mbingu, mahali ambapo Mungu anatufanya upya ili kwamba tusiwe tena na asili ya anguko la dhambi.)

 

    1.    Soma Waebrania 10:1-4. Unakumbuka tumesoma (kwenye Waebrania 8:5) kwamba patakatifu pa duniani palikuwa tu ni “kivuli” cha patakatifu pa mbinguni? Je, hapa tunaona kivuli gani kingine? (Sheria ni “kivuli” cha mambo mema yajayo.)

 

      1.    Hilo “jambo jema” ni lipi? (Agano letu la sasa – Yesu katika patakatifu pa mbinguni akijitoa kwa ajili ya dhambi zetu.)

 

      1.    Jifunze (pitia) kwa umakini kile kisemwacho na vifungu hivi kisichoweza kufanywa na sheria, lakini kinachoashiriwa kwamba agano letu jipya linaweza kukifanya. Je, makubaliano mapya kati yetu na Mungu yanatufanya “tusafishwe mara moja kwa ajili ya [nyakati] zote?”

 

    1.    Soma waebrania 10:11-14. Taswira iliyopo akilini mwangu kuhusu kazi ya Yesu ni kwamba yeye yupo patakatifu kila siku akituombea (akitufanyia upatanisho). Vifungu hivi vinaweka bayana jambo gani? (Kazi ya Yesu si kama ya makuhani wa kibinadamu. Yesu alitoa “dhabihu moja kwa ajili ya dhambi” na kisha “akaketi katika mkono wa kuume wa Mungu.” Sasa “anangojea adui zake wawekwe chini ya miguu yake.” Yeye aliyeufanya ulimwengu kwa kutamka amehitimisha kazi yake kwa ajili yetu.)

 

      1.    Mara kadhaa kwenye somo hili nimemzungumzia Yesu akiwa mbinguni akitufanyia upatanisho (akituombea). Je, hii si sahihi, kwa kuwa vifungu hivi vinatuambia kuwa Yesu alitoa “dhabihu moja” na sasa amekaa huku akingojea? Je, tuseme kwamba sasa hivi Yesu “anangojea,” na hafanyi upatanisho kwa ajili yetu mbinguni? (Mambo kadhaa yako bayana. Dhabihu moja ya Yesu inatosha. Ninafahamu kwamba ninaendelea kutenda dhambi na siko peke yangu. Kazi ya Yesu ya upatanisho inaendelea kwa namna iyo hiyo.)

 

    1.    Soma tena Waebrania 10:14. Je, Maneno “amewakamilisha hata milele” yanamaanisha nini? Je, inamaanisha kuwa dhambi zetu za sasa na zijazo zimesamehewa na kweli Yesu anangojea badala ya kutuombea? Je, mantiki hiyo haiakisiwi kwenye Waebrania 10:2? (Kuna mambo mawili: Kwanza, kitovu katika vifungu hivi kinazungumzia tabia ya Kuhani Mkuu na asili ya dhabihu. Hakipo kwenye asili ya wanadamu wanaotafuta upatanisho kwa ajili ya dhambi zao. Hata hivyo, maana ya pili ni kwamba kwa uwazi kabisa kifungu kinasema kuwa wadhambi “wanakamilishwa hata milele.” Katika kusawazisha mambo, nadhani “kukamilishwa hata milele” kunazungumzia uwezo na ukamilifu wa nyakati zote wa kile ambacho Yesu amekifanya. Vinginevyo, maneno yaliyopo kwenye Sala ya Bwana “utusamehe dhambi zetu” (Luka 11:4) yasingekuwa na maana kwenye maombi ya mara kwa mara. Yangetakiwa tu kusemwa mara moja.)

 

      1.    Kwa nini Waebrania 10:14 inatuzungumzia sisi “kutakaswa?” (Yesu alituokoa kwa maisha, kifo na ufufuo wake na kazi yake ya Ukuhani Mkuu mbinguni. Ni haki kwa njia ya imani pekee. Haki kwa njia ya imani hutufanya kuwa wakamilifu kwa ajili ya wokovu kwa sababu Mungu anaizingatia haki ya Yesu, si haki yetu. Hata hivyo, Roho Mtakatifu anatenda kazi pamoja nasi kila siku ili tusonge mbele kwenye njia inayoelekea kwenye utakatifu. Maisha yetu yanachukuliwa kuwa ni makamilifu, lakini yanahitaji kuboreshwa.)

 

  1.   Ujasiri

 

    1.    Soma Waebrania 10:19-22. Unaona vidokezo vingapi kwenye Siku ya Upatanisho ya kidunia? (Kidokezo kimojawapo cha muhimu sana ni kwamba tunao ujasiri wa kuingia Patakatifu pa Patakatifu. Mambo ya Walawi 16:2 inatuambia kuwa endapo Kuhani Mkuu angeingia Patakatifu pa Patakatifu (ndani ya pazia) kila alipotaka kufanya hivyo, angekufa. Hatuna haja ya kukiogopa kifo.)

 

    1.    Soma Waebrania 10:23-25. Ujasiri huu katika wokovu wako unapaswa kuathirije maisha yako? Je, unapaswa kufanya uamuzi kwamba haijalishi jinsi unavyoishi? (Unapaswa kutuhimiza “katika upendo na kazi nzuri.”)

 

      1.    Je, hiyo inaleta mantiki kwako? Kama “unafanywa kuwa mkamilifu” je, matokeo yake ya kawaida si ni kutoyajali sana matendo yako? (Soma Waebrania 10:26-29. Tunapoitafakari kafara (dhabihu) ya kutisha ambayo Yesu aliitoa kwa ajili yetu, tutahamasika kuikataa dhambi.)

 

    1.    Rafiki, Yesu alilipa adhabu ya kutisha kwa ajili ya dhambi zako. Kafara yake na kazi yake katika patakatifu pa mbinguni hukupatia uzima wa milele. Onesha heshima na shukrani kwa kile ambacho Yesu amekifanya. Fanya uamuzi sasa hivi, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, kuishi maisha yako kwa mujibu wa mapenzi ya Mungu.

 

  1.    Juma lijalo: “Badiliko” la Sheria.