Kuhesabiwa Haki kwa Imani Pekee

(Wagalatia 2:15-21)
Swahili
Year: 
2011
Quarter: 
4
Lesson Number: 
4

Utangulizi: Hebu tupitie kile tulichokwishajifunza hadi hivi sasa kwenye somo letu la barua ya Paulo kwa Wagalatia. Paulo ana ujumbe maalum wa injili alioupokea moja kwa moja kutoka kwa Yesu. Viongozi wa kanisa la awali waliamini jambo hili, lakini palikuwepo na mpambano mkali katika kanisa la Galatia, na miongoni mwa waumini wa mwanzo, juu ya huo ujumbe na matakwa ya injili. Juma hili Paulo anaelezea ujumbe wake wa injili. Tunapojifunza ujumbe huo, tunahitaji kujiuliza kama bado linakubalika miongoni mwa Wakristo? Je, bado linakubalika mawazoni mwetu wenyewe? Hebu tuzame kwenye somo letu na kuchunguza tena kiini cha ujumbe wa injili!

  1. Ujumbe wa Injili wa Paulo
    1. Soma Wagalatia 2:15-16. Je, kuitii sheria kuna wajibu gani katika wokovu wetu? (Hakuna wajibu wowote. “Kwa kuitii sheria hakuna mtu hata mmoja atakayehesabiwa haki.”)
      1. Je, huu ndio ujumbe ambao viongozi wa juu wa kanisa waliukubali? (Ndiyo. Inawezekana ilikuwa vigumu kukubaliana nao (angalia safari ya Petro pale ambapo Wayahudi kutoka kwenye ofisi yake ya nyumbani walipowasili Galatia), lakini hiyo ndio teolojia ambayo viongozi waliikubali.)
      2. Je, Paulo anaandika kuhusu “sheria’ipi? Amri Kumi? Sheria ya mapokeo? Maandiko yote ya Musa? (Haijalishi ni kwa namna gani sheria inavyotafsiriwa kama kuishika sheria hiyo hakutupatii wokovu. Kama wokovu ni suala la imani pekee, basi matakwa yoyote utakayojaribu kuyaongezea ni kinyume na ujumbe wa injili.)
  2. Tatizo la Wazi la Ujumbe wa Injili ya Paulo
    1. Soma Wagalatia 2:17. Hili ni swali la msingi ambalo ni la muhimu sasa kama ilivyokuwa katika kipindi kile – “Je, haki kwa imani pekee inahamasisha dhambi?” “Je, unawezaje kuwaambia watu kwamba sheria haijalishi tena – watakasirika!” Je, Paulo anatoa jibu gani? (Hapana, watu hawapaswi kukasirika. Injili ya haki kwa imani pekee haihamasishi dhambi.)
      1. Je, vipi kama swali katika fungu la 17 lingeulizwa kwako, je, ungelijibuje? Je, ni dhahiri kwako kwamba wakati ambapo ukitafuta kuhesabiwa haki kwa imani kuwa wewe ni mdhambi? (Kwangu mimi hiyo ni dhahiri.)
    2. Je, umejiingiza kwa Wakristo wanaosema kwamba wako huru dhidi ya dhambi?
      1. Kama hivyo ndivyo, je, walikuwa mawakili mahiri wa haki kwa imani? (Nawakumbuka watu wawili walioniambia kwamba walidhani kwamba walikuwa wanafanya vyema kwenye suala la kuitii sheria. Mmoja alidai kutokuwa na dhambi kwa muda wa miaka miwili. Hukumu yangu ilikuwa kwamba waliamini kuwa utii ulikuwa ni muhimu kwa ajili ya wokovu.)
      2. Angalizo langu kwamba wale wanaodhani kuwa wao ni wema sana pia wanaamini katika kuitunza sheria ili waweze kuokolewa sio suala la kisayansi. Lakini, kama umeona jambo hilo hilo, kwa nini unadhani kwamba watu wanaoamini kuwa wao ni watiifu wanaamini utii wao ni muhimu kwa wokovu?
        1. Na kama hili ni kweli, basi inaonekana kwamba wokovu kwa matendo unahamasisha utii, sawa?
    3. Soma Wagalatia 2:18-19. Kwa nini Paulo anahoji kwamba haki kwa imani pekee haihamasishi uvunjaji wa sheria (haihamasishi dhambi)? (Yesu alipokufa badala yetu kwa ajili ya dhambi zetu, nasi pia tulikufa katika sheria. Kwa hiyo, sheria haituhukumu tena. Lakini, kama tukiijenga upya sheria – katika hilo Paulo anamaanisha kuwa kama tunaamini kwamba utii wa sheria ni muhimu kwa ajili ya wokovu, basi dhambi zetu zipo dhidi yetu na tunaikiuka sheria.)
      1. Hebu tuliangalie hili tena. Paulo anasema kuwa shtaka dhidi ya teolojia yangu ni kwamba linahamasisha ukiukwaji wa sheria. Lakini, Paulo anadai kuwa kinyume chake ndio ukweli halisi. Wale wanaosema kwamba kuishika sheria ni muhimu kwa ajili ya wokovu wanawafanya wavunja sheria kuwa nje kabisa ya kila mtu – hata kwa Wakristo wenye kumcha Mungu kwa dhati kabisa!
        1. Je, huu ni “ujanja/werevu” mkubwa? Je, hoja ya Paulo ni kama ujanja wa mikono (kimiujiza)? Kama tukibatilisha sheria ya kudhibiti mwendokasi, basi hakuna hata mmoja kati yetu atakuwa mwenye kuendesha kwa mwendo wa kasi. Kama tukitekeleza sheria ya kutokwenda mwendo wa kasi, basi sisi sote ni waendeshaji wa mwendo wa kasi. Kubatilisha sheria ya kuendesha kwa mwendo wa kasi kunatufanya sisi sote tuwe wananchi tunaofuata/tunaozingatia sheria!
    4. Soma Wagalatia 2:20-21. Kama swali langu la mwisho linakuletea shida akilini mwako, elezea ni kwa vipi kuifuta sheria ikiwa kama chanzo cha wokovu hutoa watu wakamilifu zaidi? (Paulo anatuambia kuwa kama vile tulivyokufa pamoja na Yesu katika mauti yake, ndivyo vivyo hivyo tunapaswa kuishi pamoja na Yesu kwenye maisha yake ya ufufuo. “Tunaishi kwa ajili ya Mungu” na “Kristo anaishi ndani yangu.”)
      1. Hili linaonekana kama suala dhahania (la kuwazika tu). Hebu tuseme kwamba kesho mimi “nikiwa mfu” nitazishika sheria zote na alama za barabarani. Marehemu hajui kitu chochote. Kwa hiyo, sijui kitu chochote kuhusiana na sheria za barabarani. Je, hiyo itanifanyaje mimi kuwa dereva makini na mzuri zaidi? (Kwa hakika, haitafanya hivyo.)
      2. Vipi kama nikiongezea ukweli kuwa mtu aliyesanifu sheria zote za barabarani “anaishi ndani yangu.” Je, nitakuwa dereva wa aina gani? (Kama nilijazwa ujasiri na roho ya mtu aliyekuwa msanifu mahiri wa barabara, sheria za barabarani na alama za barabarani, ningekuwa na uelewa mzuri wa namna ya kuendesha. Nadhani hicho ndicho anachotufundisha Paulo.)
    5. Hebu turejee kwenye Wagalatia 2:19 na tuchunguze zaidi kauli inayosema “kuifilia sheria” kwa undani zaidi. Je, inamaanisha nini “kuifilia sheria?” Je, inamaanisha kuwa hatuijali? Yaani tunaishi kana kwamba haipo?
      1. Wagalatia 2:20 inasema “Nimesulubiwa pamoja na Kristo.” Kwa nini Yesu alikufa? (Alikufa ili alipe adhabu ya kuikiuka sheria. Hii inamaanisha kuwa sisi pia tulikufa pamoja na Yesu (“tulisulubiwa pamoja na Kristo”) kwa kuikiuka sheria.)
        1. Je, ni kwa namna gani niliifilia sheria? (Niliifilia hukumu ya sheria. Niliifilia adhabu kwa kuikiuka sheria.)
      2. Je, hiyo inamaanisha kuwa hatuijali tena sheria? (Hapana. Mungu ndiye aliyeiandika sheria. Sheria ni nzuri. Hata hivyo, haitishii tena kwa maana kwamba kama nisipoitii nitakufa. Tayari nimekwishaifilia sheria kupitia kwa Yesu.)
    6. Hebu turejee kwenye swali langu la msingi linalohusiana na masuala ya barabarani. Utakumbuka kwamba niliuliza kuwa kama sheria zote za barabarani zitabatilishwa, je, hiyo inamaanisha kuwa hakuna hata mmoja wetu ambaye atakiuka sheria za mwendokasi? Nadhani Paulo anasema kitu fulani tofauti kidogo: Yesu alilipa adhabu kwa ajili ya adhabu zote za ukiukaji wa sheria za barabarani. Kwa hiyo, sheria hizo hazitufanyi kuwa watunza sheria. Kinachotufanya tuwe watunza sheria ni kuwa na mbunifu wa barabara na mtoa sheria za usalama barabarani waishi akilini mwetu!
    7. Soma Warumi 6:5-7. Kwa mara nyingine tena Paulo anarejea kwa sisi kufa pamoja na Yesu pale alipokufa kwa ajili ya dhambi zetu. Hata hivyo, anaongezea kitu fulani zaidi ya “adhabu kulipiwa” kwa ajili ya ukiukwaji wa sheria. Je, anaongezea kitu gani? (Anasema kwamba “hali yetu ya kale” ilikufa “ili kwamba mwili wa dhambi uweze kupotea.”)
      1. Je, unadhani inamaanisha nini kwa miili yetu ya dhambi kufa? (Hii inamaanisha kuwa matamanio yetu ya kale ya kutenda dhambi yanakufa.)
        1. Anachokiandika Paulo hapa kinaonekana kuwa cha dhahiri kabisa, inachokifanya kisiwe cha dhahiri ni kwamba ninajua matamanio yangu ya kale yako hai. Je, nini kimetokea? Au, je, mimi ni Mkristo masikini tu? (Pitia kwa haraka haraka Warumi 7:14-24. Paulo ana uzoefu ule ule nilio nao mimi.)
        2. Ni kwa jinsi gani “hali yako ya kale inaweza kufa” na bado ukaendelea kuwa na mpambano ambao Paulo anauelezea? (Hebu tuliangalie hilo fungu.)
  3. . Kuishi kwa Uwezo wa Roho wa Mungu
    1. Soma Warumi 7:4. Kama tumeifilia sheria, je, lengo maishani mwetu ni lipi? (Tupate “kuwa mali” ya Yesu kusudi “tumzalie Mungu matunda.”)
    2. Soma Warumi 7:5-6. Sheria pamoja na mambo ya asili ya zamani vinahamasisha tamaa za dhambi. Je, ni kwa jinsi gani Roho Mtakatifu anabadili hilo?
    3. Soma Warumi 6:11-14. Je, hili linasema nini kuhusiana na dhana kwamba Roho Mtakatifu anaweza kutusaidia kuishi? (Kujitoa kwetu kwa Mungu lazima imaanishe kuwa tunamwambia Mungu “mimi hapa, naomba unisaidie kuishi maisha yanayokupendeza wewe!”)
    4. Soma Warumi 8:5-9. Je, hii inapendekeza kuwa tuishije? (Kwa mara nyingine tena, Paulo anatuambia kuwa lazima tufanye uchaguzi wa kuyafanya yale ambayo Roho Mtakatifu anayatamania.)
    5. Mjadala wetu unaonekana kuwa wa kuwazika sana. Hebu tuangalie maoni ya Yesu yanayoweza kutusaidia. Soma Mathayo 5:27-28. Je, ni kwa namna gani mtu anayeamini katika kuhesabiwa haki kwa matendo ataenenda ili aweze kuitunza amri hii? (Kutokufanya ngono nje ya ndoa.)
      1. Kwa mtazamo mwingine, Yesu anaifanya amri kuwa mbaya zaidi kwa watunza sheria – anasema kuwa pia unatakiwa kudhibiti mawazo yako ili uweze kuepuka kuikiuka hii amri, sawa?
      2. Je, Paulo anatuambia kuwa Yesu anafundisha kitu gani? (Kama unataka kutembea na Mungu, usijimakinishe kwenye amri iliyo kinyume na uzinzi, badala yake, makinika kwenye mtazamo wa akili yako. Mwombe Roho Mtakatifu akusaidie uielekeze akili yako kwenye kile ambacho Roho Mtakatifu anakitamania kwa ajili yako.)
      3. Je, huku kutembea katika Roho Mtakatifu ni muhimu kwa ajili ya wokovu? (Soma Warumi 5:19. Hapana. Ni maisha makamilifu ya Yesu pekee ndio yanayotufanya kuwa wenye haki. Hata hivyo, kuishi katika Roho ni matamanio ya wale wanaookolewa.)
    6. Sasa unajua kwa nini Petro alisema (juma lililopita) kwamba ni vigumu kumwelewa Paulo kwa nyakati fulani! Rafiki, je, utatubu dhambi zako na kudhamiria hivi leo kumwomba Roho Mtakatifu kila asubuhi ili akusaidie uielekeze akili yako kuishi kwa mujibu wa maelekezo ya Roho wa Mungu, na sio kuielekeza akili yako kwenye asili yako ya dhambi?
  4. Juma lijalo: Imani Katika Agano la Kale.