Mwabudu Muumbaji

Swahili
(Ufunuo 14, Luka 23, Zaburi 19)
Year: 
2018
Quarter: 
2
Lesson Number: 
8

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Sehemu ya muhimu ya ujumbe wa injili wa wakati wa mwisho ni kwamba Mungu ni Muumbaji wetu. Je, hili ni jambo tunalotakiwa kulichukulia kwa imani? Je, huu ni ujumbe unaokinzana na sayansi? Hebu tuzame kwenye Biblia ili tuone kile inachokisema kuhusu Mungu na wajibu wake kama Muumbaji!

 

 1.    Mjumbe

 

  1.    Soma Ufunuo 14:6. Hebu tumwangalie malaika wa kwanza kidogo. Kifungu kinasema “Kisha nikaona malaika mwingine.” Unadhani inamaanisha nini kusema malaika “mwingine?” Je, huyu si malaika wa kwanza kati ya malaika watatu? Inawezaje kuwa “mwingine?” (Ukipitia kitabu cha Ufunuo, utaona kwamba kuna malaika wengi ambao ama wanatoa au kupokea ujumbe wa mbinguni.)

 

   1.    Malaika huyu aliruka “katikati ya mbingu.” Kuna umuhimu gani wa kuruka katikati ya mbingu? Je, malaika huyu ni mrukaji mwenye mwangalifu ambaye hana uwezekano wa kuanguka na kupasuka muda wowote? (Ukitaka kuonekana na kusikika basi utaruka juu kwa umbali ambao kila mtu anaweza kukuona – lakini sio juu sana. Umuhimu uliopo ni kwamba huyu malaika ana ujumbe unaotakiwa kusikika.)

 

   1.    Ujumbe wa malaika huyu ni upi? (“Injili ya milele.”)

 

    1.    Ujumbe huu unapelekwa kwa watu gani? (Kwa kila mtu wa kila kabila.)

 

    1.    Ni vigumu kiasi gani kufikia lengo hilo? Wafikirie watu wote wapya wanaozaliwa. Wafirikie watu wote wanaoishi kwenye maeneo ambayo yana uhasama na Ukristo. Je, Mungu anamtuma malaika kwa kuwa wanadamu hawapeleki injili kwa kila mtu? (Fikiria maana kadhaa zinazoweza kuwa zinamaanishwa hapa. Kwanza, hakuna mtu atakayepotea kwa kuwa tumeshindwa katika wajibu wetu wa kupeleka injili. Mungu atahakikisha kuwa kila mtu anafanya uamuzi baada ya kuwa na taarifa sahihi. Pili, mbingu (anga) ni njia fanisi sana ya kuwafikia makundi makubwa ya watu. Ifikirie redio, televisheni, na mtandao wa intaneti.)

 

    1.    Je, huyu ni malaika halisi? Au, hii ni ishara ya ujumbe tunaotakiwa kuupeleka? (Kitabu cha Ufunuo kimejaa ishara, lakini inaonekana kuleta mantiki kwamba kwa kiasi fulani malaika wa mbinguni amekasimishwa jukumu hili. Tunasaidia katika kutimiza lengo hili.)

 

  1.    Soma Ufunuo 14:7. Fikiria kwamba unataka kuongezewa mshahara au unataka kubadili saa zako za kazi. Je, utaingia tu ofisini kwa bosi wako bila kuwa umetafakari kabla kuhusu kile utakachokisema?

 

   1.    Tunaye malaika mwenye ujumbe kwa ulimwengu kuhusu injili na hukumu ya mwisho. Unadhani maneno ya malaika yalipangiliwa kwa makini? Au, Mungu alimwambia tu malaika, “Sema maneno machache kuhusu ujio wangu ulimwenguni” na malaika akaongezea mistari michache? Bila kujali kama ilikuwa ishara ama la, malaika huyu alipangilia njia sahihi ya kuruka ili aweze kuonekana na kusikika, hivyo kwa hakika njia hiyo ilizingatia jinsi atakavyowasilisha injili ya milele. Hiyo inamaanisha maelezo ni ya muhimu. Hebu tuangalie jambo hilo katika sehemu inayofuata.)

 

 1.   Ujumbe

 

  1.    Soma tena Ufunuo 14:7. Sehemu gani ya ujumbe wa malaika inagusa usikivu wako sana?

 

   1.    Je, umegundua jambo lenye mfanano kwenye mpangilio wa taarifa za habari, wachangishaji wa fedha, na matangazo ya biashara? Vyote hivi vinafuatilia mpangilio gani? (Vinaanza na jambo ambalo inadhaniwa litavuta usikivu wako. Duka letu litafunga biashara! Shirika letu lina uhitaji mkubwa wa fedha! Tunazo habari zilizotufikia hivi punde!)

 

   1.    Je, dhana ya kwamba unapelekwa mbele ya mahakama kwa ajili ya kuhukumiwa itavuta usikivu wako? (Bila shaka. Hii inaonesha kuwa wasilisho limezingatiwa kikamilifu.)

 

    1.    Je, kuna cha kujifunza katika jambo hili kwa jinsi tunavyowasilisha injili? (Miaka mia moja iliyopita Wakristo walipeleka injili kwa kuwaonya wadhambi kuhusu jehanamu. Watu wengi leo wanaicheka njia hiyo. Tunatakiwa kutafakari kwa makini jinsi tunavyoweza kuushawishi ulimwengu kwamba hukumu inakuja. Tunatakiwa kuelekeza nguvu kwenye huu ujumbe!

 

    1.    Unadhani watu wanataka hukumu? (Bila shaka wanataka hukumu ije. Lakini, ni sawa na watu wanaoendesha kwa mwendokasi mtaani kwako. Ungependa polisi wawaadhibu kwa kuwaandikia vijikaratasi ili wakalipe faini. Hutaki polisi afanye vivyo hivyo kwako.)

 

  1.    Soma Luka 23:35-42. Ilikuwa vigumu kiasi gani kuibua mada ya hukumu kwa “mhalifu mwingine?” (Tayari alikuwa anatumikia adhabu. Kwa kadiri hali ya dunia yetu inavyokuwa ngumu zaidi, tunatakiwa kuwa macho kwenye uwezekano wa kushiriki injili na watu wanaoamini kuwa mambo hayako sawa.)

 

  1.    Hebu tupitie Ufunuo 14:7 kwa kuizingatia Luka 23:35-42. “Mhalifu mwingine” alikuwa kwenye matatizo makubwa. Hukumu ya mwisho ni tatizo kubwa. Matokeo ya “mhalifu mwingine” yalikuwa ni yapi? (Yesu alimwokoa. Hiki ndio kitovu cha ujumbe wetu wa injili. Maneno yaliyopo katika Ufunuo 14:7 kama vile “mcheni,” “kumtukuza” na “msujudieni” yote yanazungumzia shukrani yetu kwa Yesu kwa kile alichokifanya ili kutuokoa kutoka kwenye hukumu. Neno la Kiyunani la kusujudu ni “Proskeneo.” “Pros” linamaanisha “dhidi,” na “kuneo” linamaanisha “kubusu.” Kumbusu Mungu! Sasa kuna njia kubwa ya kupeleka injili inayohusu hukumu. Tumeokolewa kutoka kwenye baa (maafa) linalokaribia!)

 

  1.    Hivi karibuni tulijadili kwenye mfululizo wa masomo haya umuhimu wa kukiri na kukubali kwamba Mungu ni Muumbaji wetu. Hiyo inamaanisha kuukataa uibukaji na “ibada” yake, muda na mambo ya asili. Malaika anasema kuwa Mungu aliumba kitu gani cha kwanza? (Mbingu.)

 

   1.    Nakumbuka nilipokuwa kijana mdogo nilibishana na rafiki wangu aliyesema kuwa baba wake alikuwa na nguvu kuliko sokwe. Alikuwa na uhakika kuwa baba yake alikuwa na nguvu zaidi ya sokwe, nami nilikuwa na uhakika kuwa sokwe alikuwa na nguvu zaidi ya baba wake. Unadhani kweli rafiki wangu alidhani kuwa baba wake alikuwa na nguvu zaidi ya sokwe? (Alidhani suala lililokuwa linajadiliwa ilikuwa ni endapo baba wake alikuwa bora zaidi – jambo ambalo kimsingi alikuwa bora zaidi. Lakini hilo si jambo lililokuwa linajadiliwa.)

 

   1.    Wakristo wanapojiingiza kwenye mjadala na wanasayansi, ni muhimu kiasi gani kwetu sisi kuyaelewa masuala kikamilifu na kuyapangilia? (Jambo baya kabisa ni kujenga hoja kuipinga sayansi ili kuthibitisha kutoelewana kwetu. Hatutakiwi kuibua mgogoro wakati mgogoro haupo.)

 

  1.    Soma Zaburi 19:1-4. Mbingu zinatuambia nini? (Zinaelezea utukufu, kazi, na maarifa ya Mungu kwa namna iipitayo vizingiti vya lugha.)

 

   1.    Nilikuwa nikisoma kitabu Hugh Ross kuhusu Uumbaji wa siku sita. Ross ni mwana-astrofizikia (sayansi ya hali ya nyota kikemikali na kimaumbile) anayeamini katika tafsiri halisi ya Biblia. Sikubaliani na Ross katika mambo yake yote, kwa mfano, hoja yake nzito kuhusu kuumbwa na kufa kwa wanyama. Hata hivyo, maelezo yake ya kisayansi juu ya kile kilichotokea kwenye “mlipuko” (the “Big Bang”) na uthibitisho wake kuhusu umri wa mbingu ni ya kufurahisha.

 

   1.    Unakumbuka maswali yako ya hesabu ulipokuwa katika shule ya sekondari? Chukulia kwamba umo ndani ya gari linalosafiri kwa mwendokasi wa maili 60 kwa saa. Nikikwambia muda uliotumika, je unaweza kuniambia safari imechukua umbali gani? Nikikwambia umbali uliotumika, je, unaweza kuniambia muda gani umetumika? (Ndiyo! Unakumbuka jinsi ya kukokotoa mambo haya.)

 

   1.    Ross anadai (na ninaamini) kwamba sayansi ya sasa inaweza kupima mwendo wa utanukaji na umbali wa mbingu. Hiyo inakuambia nini? (Unaweza kukokotoa muda ambao mbingu ziliumbwa! Unaweza kubainisha tarehe ya mlipuko (the “Big Bang”).)

 

   1.    Kuna jambo gani la kujifunza kwa wakanamungu? (Ufunuo 14:7 ipo sahihi kisayansi inaposema kuwa Mungu ni Muumbaji wetu. Mbingu zina tarehe ya kuzaliwa. Tukio la Uumbaji ambalo wanasayansi wanaliita mlipuko (the Big Bang) lilikuwa sahihi kabisa na lililopangiliwa kiasi kwamba hitimisho pekee lenye mantiki ni kwamba lilifanyika kwa umahiri upitao uelewa wetu.)

 

   1.    Zaburi 19 inaposema kuwa mbingu “zauhubiri” na “kutangaza kazi ya mikono [ya Mungu],” je, mtunga Zaburi anatuambia kuwa Mungu sio tu suala la imani? (Hili ndilo hitimisho unalopaswa kulifikia. Uwepo wa Mungu unathibitika. Hatupaswi kukiri kwamba ibada yetu na ujumbe wetu vimejengwa kwenye mawazo yetu.  Biblia inasema kuwa mbingu zinamshuhudia Mungu na sayansi ya kisasa kabisa inaunga mkono jambo hilo!)

 

  1.    Rafiki, ikiwa unatilia shaka kwamba Mungu ni Muumbaji wetu, tafadhali kubali ukweli huo wa msingi sasa hivi. Kushuhudia kwamba Mungu wetu Muumbaji anastahili kuabudiwa ni muhimu kwenye Ujumbe wa Malaika Watatu wa siku za mwisho.

 

 1. Juma lijalo: Udanganyifu wa Siku za Mwisho.