Madanganyo ya Siku za Mwisho

(Ufunuo 12 & 20, Mhubiri 9, Mwanzo 1 & 3)
Swahili
Year: 
2018
Quarter: 
2
Lesson Number: 
9

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Je, wakati mwingine huwa unapata wakati mgumu kupima ajali? Intaneti ilipogunduliwa na kuanza kutumika kwa mara ya kwanza, nilihakikisha kuwa mawasiliano yote ya watu niliyokuwa nayo yalikuwepo kwa sababu nilidhani kuwa mtandao wa intaneti ulikuwa na mustakabali katika kushiriki habari mbalimbali na watu. Sasa, ninatambua kuwa ninapaswa kuwa mwangalifu kuhusu kuwa na taarifa nyingi kupita kiasi kwenye mtandao wa intaneti kwa sababu wahalifu wanaweza kutumia taarifa hizo dhidi yangu. Tafakari mtandao wa Facebook. Ni kifaa kizuri sana cha kuongeza ukaribu na marafiki wako wa zamani. Wanaweza “kuyashiriki” maisha yako hata kama wapo umbali wa maelfu ya maili. Facebook haitupatii hii zawadi nzuri bure. Badala yake, inauza taarifa zinazotuhusu kwa watu wasio marafiki wetu. Je, umewahi kuona jambo kama hili hapo kabla? Kitu kinachoonekana kuwa rafiki na chema kina siri iliyofichika? Some letu juma hili linahusu jambo hilo. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi!

 

 1.    Shetani

 

  1.    Soma Ufunuo 12:7-9. Je, Shetani ni kitu halisi?

 

   1.    Kazi yake ni ipi kwa mujibu wa vifungu hivi? (Kuuelekeza “ulimwengu wote upotevuni.”)

 

  1.    Soma Ufunuo 20:1-3. Jambo gani limemtokea Shetani hapa? (Malaika wa Mungu anamzuia Shetani asifanye kazi yake ya udanganyifu.)

 

   1.    Vifungu hivi vya Ufunuo 12 na 20 vinatuambia nini kuhusu Shetani na kazi yake? (Shetani yu halisi, kazi yake ni kutudanganya, na kazi hiyo inaendelea.)

 

  1.    Soma Mwanzo 3:1-3. Je, kweli huyu anayeongea na Eva ni nyoka? (Umegundua kuwa Ufunuo 12:9 na Ufunuo 20:2 zinamzungumzia Shetani kama “yule nyoka wa zamani.” Shetani anachukua mwonekano wa nyoka mzuri ili kujaribu kumwingiza Eva dhambini.)

 

   1.    Kwa nini Shetani anatumia njia hii? Kwa nini asimwendee Eva na kusema, “Mimi ni chama cha upinzani. Mungu hajakuamini na kukupatia ukweli au kukufanya ufanane naye kwa kuujua wema na uovu. Kwa nini usiungane na upande wangu, upande wa maarifa, ukweli na haki?” (Kushindwa kwa Shetani kutumia njia hii kunatuonesha kuwa sehemu ya udanganyifu wa Shetani ni kuficha utambulisho (sura) wake na asili ya kazi yake.)

 

  1.    Soma 2 Wakorintho 11:13-15. Tunaambiwa nini hapa kuhusu kazi za Shetani zilizojificha? (Anataka tuamini kuwa yeye ni “malaika wa nuru.”)

 

   1.    Hii inaashiria nini kuhusu madanganyo ya “siku za mwisho?” (Hapa shetani alianzisha kazi yake ya udanganyifu kwa kuficha sura (utambulisho) yake. Tunapaswa kutarajia kwamba ataendeleza tabia hii.)

 

   1.    Unawafahamu watu wasioamini kwamba Shetani yupo?

 

 1.   Mwongozo wa Roho

 

  1.    Siku chache zilizopita, nilimsikiliza daktari maarufu wa binadamu ambaye ni Mkristo. Alikuwa na mgonjwa ambaye alifariki. Baada ya mgonjwa kuwa amefariki kwa muda wa dakika 40, Roho Mtakatifu alimvuvia daktari ili kujaribu kumfufua. Aliomba na kumshtua marehemu, ambaye alifufuka na siku mbili baadaye aliweza kuzinduka. Mgonjwa huyu alitaarifu kwamba alikuwa amekwenda kuzimu, na uzoefu huo ukamfanya aongoke na kuwa Mkristo. Tunapaswa kufikiria nini kuhusu kisa hiki? Sitilii shaka uaminifu wa daktari huyu.

 

  1.    Soma Mhubiri 9:5-6. Je, habari hii inaleta suluhu mawazoni mwako? Kwamba “wafu hawajui neno lolote?”

 

  1.    Hebu tuchambue ujumbe wote wa Sulemani. Soma Mhubiri 9:1-2. Je, hii inaendana na maneno ya Biblia – kwamba wenye haki na waovu “mambo yote yatawatukia sawasawa?”

 

  1.    Soma Mhubiri 9:3-4. Je, katika maeneo mengine Biblia inafundisha kuwa wafu hawana tumaini? Kwamba “mbwa aliye hai” ni bora zaidi ya mtu mwenye haki aliyekufa?

 

  1.    Soma Mhubiri 9:7-9. Je, katika maeneo mengine Biblia inatufundisha kuwa maisha yetu hayana maana – na kwamba huko kutokuwa na maana ndilo kusudio la Mungu kwetu? (Kama wewe ni msomaji wa muda mrefu wa masomo haya, utafahamu kwamba ninadhani kuwa hakuna mwanafunzi makini wa Biblia atakayenukuu sura hii kwa ajili ya kuthibitisha hali ya wafu. Sulemani ana msongo wa mawazo, na Biblia inaandika huu msongo wake ili kuwapa tumaini watu ambao pia wanateseka na ugonjwa huu. Ikiwa tunaamini Sulemani alidhamiria jambo hili liwe ukweli kuhusu maisha na kifo, tunaweza kuhitimisha kuwa maisha yetu ya hapa duniani hayana maana, tunapaswa tu kuwa na wakati mzuri sasa hivi kwa sababu bila kujali kama sisi tu wema au wabaya thawabu yetu ni moja. Hakuna chochote kati ya haya kinachofundishwa vinginevyo kwenye Biblia.)

 

  1.    Soma Mwanzo 3:2-5. Shetani anamwambia Eva uongo gani wa asili? (Anakana kwamba adhabu ya dhambi ni mauti. Mungu, kwa upande mwingine, anamwambia Eva kuwa kifo ni matokeo ya dhambi. Tofauti na kauli zenye msongo za Sulemani, huu ndio ujumbe wa Biblia: kifo hufuata dhambi. Ikiwa wadhambi wanaishi milele kama roho au wanaungua milele kuzimu, basi Shetani alikuwa sahihi na Mungu hakuwa sahihi.)

 

  1.    Soma Ezekieli 18:19-23. Vifungu hivi vinasema kuwa nini kinaitokea “roho” itendayo dhambi? Hii inasema kuwa matokeo ya kuishi maisha sahihi ni yapi? (Hii inakinzana na Sulemani kuhusu habari ya endapo maamuzi yetu yanaleta tofauti linapokuja suala la hatima yetu ya milele. Pia inasema kuwa roho zitendazo dhambi hufa, haziishi milele.)

 

  1.    Soma 1 Timotheo 6:12-16. Ni nani pekee asiyekufa? (Mungu! Shetani, malaika walioanguka na roho za wadhambi hatima yao ni mauti, sio kutokufa. Tunapewa “uzima wa milele” tunapokiri kwamba Yesu ni Bwana.)

 

  1.    Soma 1 Yohana 5:10-12. Wenye haki wanapewa nini ambacho wale wanaokataa kumkiri Yesu wananyimwa? (Uzima. Huu ni “ushuhuda ambao Mungu ameutoa kuhusu Mwanaye.” Hii si kauli inayoibuka kutokana na msongo wa mawazo. Wale wanaomkiri Yesu wana uzima. Wale wasiomkiri wananyimwa uzima. Kama wewe ni mwanafunzi wa Biblia wa dhati unapaswa kuacha kunukuu Mhubiri 9 na badala yake unukuu kifungu hiki.)

 

  1.    Hebu turejee kwa daktari wetu Mkristo. Tunaielezeaje taarifa yake? Je, inawezekana kwamba alimfufua mtu huyu? (Ndiyo, Biblia inatoa mifano kadhaa ya tukio hili kwenye Agano la Kale na Agano Jipya. Angalia, 1 Wafalme 17:19-22; 2 Wafalme 4:32-35; Matendo 9:40-41; na Matendo 20:9-12.)

 

   1.    Inawezekana kweli kwamba marehemu yule alikwenda kuzimu? (Vifungu tulivyovisoma vinaashiria kuwa kifo ndio mwisho wa waovu. Hawana mwendelezo wa maisha kama roho au vinginevyo. Tafakari jambo hili kwa mtazamo wa mwanasheria. Wanasheria wanaangalia kuaminika kwa ushahidi kutokana na uwezo wa shahidi kutambua kile kilichotokea. Daktari anahusianisha tu kile alichoambiwa na mtu aliyekuwa amepoteza fahamu kwa muda wa siku mbili na ambaye akili yake haikuwa na hewa ya oksijeni. Huo si ushahidi wa kuaminika. Ama kwa hakika haupaswi kutufanya tusiamini mafundisho ya dhahiri ya Biblia.)

 

 1. Uibukaji

 

  1.    Kwenye masomo ya hivi karibuni tumejifunza udanganyifu ambao nadharia ya uibukaji inahoji maelezo ya Mungu ya uumbaji. Tunaelezeaje ushahidi wa kisayansi kwamba mbingu na nchi ni vitu vya kale sana?

 

  1.    Soma Mwanzo 1:1. Je, mbingu na nchi zina mwanzo? (Ndiyo.)

 

  1.    Soma Mwanzo 1:2-3. Je, maelezo haya yanasema kuwa nchi iliumbwa katika juma la uumbaji? (Ni kinyume chake. Inaashiria kwamba nchi ilikuwepo kabla ya juma la uumbaji. Tayari ilikuwa “ukiwa na yenye utupu,” ilikuwa na “vilindi vya maji” na ilihusisha giza na maji.)

 

  1.    Soma 2 Petro 3:5. Hii inaashiria nini kuhusu muda? (Petro anasema kuwa Mungu alisema na mbingu zikawepo. Hata hivyo, kwa namna kifungu hiki kinavyoandikwa inaonekana kuashiria kuwa nchi ilifanywa baada ya mbingu.)

 

  1.    Soma Mwanzo 1:4-5 na Mwanzo 1:14-19. Ni lini Mungu aliumba “alama za kutenganisha majira na siku na miaka?” (Alifanya hivyo katika siku ya nne ya uumbaji.)

 

   1.    Hiyo inatuambia nini kuhusu muda na siku tatu za kwanza za uumbaji? (Inaruhusu uwezekano kwamba “siku” tatu za kwanza hazikupimwa kwa namna ile ile zilivyopimwa baada ya siku ya nne ya uumbaji.)

 

  1.    Soma 2 Petro 3:8. Hii inazungumzia nini kuhusu upimaji muda wa Mungu? (“Siku” kwa Mungu ni ndefu zaidi kuliko siku yetu ya kawaida.)

 

  1.    Soma Mwanzo 2:4 katika tafsiri ya Biblia ya Mfalme Yakobo (King James Version). Tafsiri hiyo inatumiaje neno “siku?” (Inaakisi kwamba neno la Kiyahudi (yom) kwa ajili ya siku linatumika hapa. Tafsiri ya Biblia ya NIV inatafsiri neno “yom” kama “wakati gani (lini).” Inachokionesha hii ni kwamba hata maelezo ya uumbaji yanatumia neno “yom” (siku) kumaanisha jambo jingine zaidi ya muda wa saa 24.)

 

  1.    Ikiwa ilikuwa kweli kwamba angalao baadhi ya “siku” za uumbaji hazikuwa na urefu wa saa 24, je, hiyo inahafifisha umuhimu wa Sabato? (Hapana! Hata Sabato inatumika kwa muktadha tofauti na ule wa siku zenye saa 24. Angalia Mambo ya Walawi 25:2-4. Ujumbe wa Mungu ni kukumbuka uumbaji wake katika siku yetu ya saba. Hii haihusiani na idadi ya saa zilizokuwepo katika kila siku ya uumbaji. Ingawa bado ninajifunza jambo hili, ninachokizingatia ni kusababisha ukinzani usio na msingi kati ya Biblia na sayansi. Hatutakiwi kuihafifisha Biblia na madai ya Mungu kwamba yeye ni Muumbaji wetu kutokana na mambo tusiyoyaelewa.)

 

  1.    Rafiki, je, utakuwa macho dhidi ya madanganyo? Je, utapima kila jambo unalolielewa kwa Neno la Mungu? Kwa nini usifanye jambo hilo kuwa sehemu ya muhimu maishani mwako sasa hivi?

 

 1.   Juma lijalo: Marekani na Babeli.