Mhuri wa Mungu au Alama ya Mnyama?

Swahili
Mhuri wa Mungu au Alama ya Mnyama?
Year: 
2018
Quarter: 
2
Lesson Number: 
11

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Je, unapenda alama au ishara zinazoonesha kuwa upo chini ya kundi fulani? Nilikuwa na kawaida ya kuweka “sticker” ya Chuo Kikuu cha Andrews kwenye dirisha la gari langu, chuo ambacho vizazi vitatu vya familia yangu vilisoma. Nina kofia, shati na jaketi la Corvette (manowari). Pia nina nguo zenye nembo ya Regent, kwa sababu ndio shule ninapofundisha. Vipi kuhusu wewe, je, una alama na ishara zinazoonesha kuwa una uhusiano na kundi, bidhaa au shule fulani? Biblia inahitaji baadhi ya alama na inaonya dhidi ya alama nyingine. Baadhi ya alama zinaonekana kuwa ni za muhimu ndani ya kipindi fulani na kwa kundi fulani. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tuone kile tunachoweza kujifunza!

 

 1.    Tohara

 

  1.    Soma Mwanzo 17:9-11. Tohara ni nini? (“Ishara ya agano kati ya [Mungu] na [Ibrahimu na uzao wake].”

 

   1.    “Agano” (au mkataba) ni nini? (Soma Mwanzo 17:7-8. Vifungu hivi vinaelezea ahadi ya Mungu kwamba atakuwa Mungu wao na kuwapa nchi.)

 

   1.    Soma Wagalatia 5:3. Watu wa Mungu wanatoa ahadi gani? (Utii. Mwanzo 17 haiko wazi juu ya kile watu wanachokiahidi.)

 

   1.    Soma Warumi 4:11. Hii inaielezeaje tohara? (Inaiita “muhuri wa haki” kwa imani ambayo Ibrahimu alikuwa nayo kabla hajatahiriwa.)

 

  1.    Soma Wakolosai 2:11-12. Mara kwa mara kampuni zinabadili “alama” zinazozitumia kufanya biashara. Je, alama (ishara) ya tohara imebadilika? (Kifungu hiki kinasema kuwa ubatizo ndio tohara mpya. Katika Matendo 15 tunaona kwamba kanisa la awali lilifanya uamuzi, kwa mwongozo wa Roho Mtakatifu na kauli zilizopo kwenye Agano la Kale, kwamba tohara haikuhitajika kwa Mataifa ili wawe na uhusiano sahihi na Mungu. Ama kwa hakika, 1 Wakorintho 7:18-19 inasema kuwa “kutahiriwa si kitu.” Badiliko zuri ajabu!)

 

  1.    Soma Mwanzo 17:12-13. Unaweza kusamehewa kwa kudhani kuwa kamwe tohara haitakoma kama ishara? (Nadhani Mungu anasema kuwa mkataba wake ni wa milele kwa wale wanaochagua kuwa watu wake. Hata hivyo, hiyo ishara mahsusi inaweza isiwe ya milele.)

 

  1.    Hii inatufundisha nini kuhusu ishara? (Zinaweza kubadilika. Zinaweza kutumika kwa kipindi fulani, kwa kundi fulani, au kwa mazingira fulani. Mwisho wa ishara unaweza kuwa mgumu kuubaini.)

 

 1.   Sabato

 

  1.    Soma Kutoka 31:12-13. Je, Sabato ni ishara? (Ndiyo.)

 

   1.    Ni ishara juu ya nini? (Kwamba Mungu anatutakasa.)

 

  1.    Soma Kutoka 31:17. Je, kuna maana moja tu ya Sabato? (Hapana. Hapa tunaambiwa kuwa ni ishara kwamba Mungu ni Muumbaji wetu. Aliziumba mbingu na nchi katika siku sita na kupumzika siku ya saba.)

 

   1.    Je, hii ni ishara na “wana wa Israeli” pekee? Utaona kwamba kwa mahsusi vifungu vyote viwili vinawazungumzia “wana wa Israeli.” Je, vinafanana na tohara, jambo lililoelekezwa kwa uzao wa Ibrahimu? (Soma Ufunuo 14:6-7. Wito wa kumwabudu Mungu Muumbaji wetu bado unahusika hadi mwisho kabisa wa wakati. Inawezekana Mungu alisema kuwa Sabato ilikuwa ni ishara kwa wana wa Israeli, lakini hiyo haimaanishi kuwa Sabato ilikuwa ni kwa ajili yao pekee. Ukweli kwamba Wakristo wanaamini kuwa Amri zote Kumi ni kwa ajili ya waamini wote inaonesha kutumika kwa Sabato ulimwenguni kote.)

 

 1. Muhuri wa Mungu

 

  1.    Soma Waefeso 1:13-14. Muhuri wa Mungu ni upi kwa Wakristo wa nyakati za mwisho? (Roho Mtakatifu.)

 

   1.    Kwa nini Roho Mtakatifu ni muhuri wetu? (Anaitwa “arabuni auhakikishaye urithi wetu.” Hiyo inamaanisha kuwa Roho Mtakatifu ni ishara kwamba Yesu ametupatia uzima wa milele na anarudi kutuchukua na kutupeleka nyumbani pamoja naye mbinguni.)

 

 

  1.    Soma Ufunuo 7:1-4 na Ufunuo 7:9-10. Muhuri huu ni kitu gani? Je, ni ishara kwa “makabila ya Israeli” pekee? (Watu 144,000 wanaelezewa kuwa wanatoka kwa makabila, lakini pia pana “mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa na lugha.” Hii inaonesha kuwa waliookolewa sio tu watu 144,000.)

 

   1.    Kundi kubwa la watu limevaa nini? (“Mavazi meupe.”)

 

   1.    Unadhani kuwa mavazi meupe ni ishara? (Kwa upande mmoja, sivai vazi langu kwenye paji la uso wangu. Angalia Ufunuo 7:3. Kwa upande mwingine, neema ni uamuzi wa akili.)

 

   1.    Unapotafakari Ufunuo 7:2-9, je, makundi yote mawili yanatiwa muhuri kwenye vipaji vya nyuso, au ni wale 144,000 pekee?

 

    1.    Ikiwa si wote wanatiwa muhuri, je, tuhitimishe kwamba si kila mtu anayeokolewa pia ametiwa muhuri kwenye paji la uso? Baadhi wanaingia mbinguni tu kwa kuvaa vazi jeupe?

 

  1.    Soma Warumi 8:5-8. Hii inatufundisha nini kuhusu Roho Mtakatifu na kuwa na uhusiano sahihi na Mungu? (Kuwa na Roho Mtakatifu (muhuri) akilini mwetu (paji la uso?), ni muhimu katika kuwa na uhusiano sahihi na Mungu na kujitoa kwa sheria yake.)

 

  1.    Soma Ufunuo 7:13-14. Tunajifunza nini kuhusu mkutano mkubwa wa watu wanaovaa mavazi meupe? (Wameokolewa kwa neema! Wanaitegemea damu ya Mwana-Kondoo kwa ajili ya uhusiano wao sahihi na Mungu.)

 

  1.    Tunaona kwamba wale waliopo kwenye kundi kubwa sana wanaokolewa kwa neema pekee. Wanatiwa muhuri na Roho Mtakatifu ambaye anaziongoza akili zao na matendo yao ili waishi kwa kuifuata sheria ya Mungu. Je, wewe ni sehemu ya kundi hilo?

 

 1.   Alama ya Mnyama

 

  1.    Soma Ufunuo 14:9-11. Tunataka kuepuka alama gani? (Alama ya mnyama.)

 

  1.    Soma tena Ufunuo 14:6-7. Tunaona jambo gani kinyume na kumwabudu mnyama? (Wale wanaomwabudu Mungu wetu Muumbaji. Ibada ndio kiini cha pambano!)

 

  1.    Unapotafakari chaguzi hizi mbili mbadala za ibada, unadhani kwa nini uumbaji unatajwa kwa mahsusi? (Uchaguzi wa ibada unahusiana na uumbaji.)

 

  1.    Tafakari jambo hili: mtafaruku gani wa kiteolojia unaoendelea sasa hivi kwa kiasi kikubwa unaangalia kama maelezo ya uumbaji katika kitabu cha Mwanzo ni halisi na sahihi?

 

   1.    Soma Mwanzo 3:1-5. Suala lililopo hapa ni lipi? (Kumtumaini Mungu. Kuamini kwamba wadhambi wanakufa.)

 

   1.    Soma Mwanzo 2:18 na Mwanzo 2:21-24. Suala lililopo hapa ni lipi? (Ndoa kati ya mwanaume na mwanamke ndio mpango pekee “unaostahili.”)

 

   1.    Soma Mwanzo 1:31. Suala lililopo hapa ni lipi? (Kwamba Mungu aliumba kila kitu. Havikuibuka, si matokeo ya bahati na mambo ya asili.)

 

   1.    Soma Mwanzo 2:2-3. Suala lililopo hapa ni lipi? (Kumbukumbu ya Sabato ya siku ya saba kwa kazi ya Mungu wetu Muumbaji.)

 

   1.    Je, mambo yote haya yanatukia sasa hivi? (Dunia ina mkanganyiko, na Mungu yu dhati. Kwa ujumla wanadamu wanaangukia upande mmoja au mwingine kwenye mitazamo yao juu ya haya mambo manne ambayo kwa kiasi kikubwa yanaegemea kwenye kile wanachokiamini kuhusu asili ya mwanadamu.)

 

  1.    Angalia tena Ufunuo 14:9-10. Ni balaa kubwa kupokea alama ya mnyama ama kwenye paji la uso au mkononi. Unadhani “paji la uso” au “mkono” inamaanisha nini? (Paji la uso inaashiria uchaguzi uliofanywa kwa uhuru kuwa kwenye upande usio sahihi wa masuala ya uumbaji. Mkono unaashiria kufuata kwa kusitasita upande usio sahihi wa masuala ya uumbaji. Kufuata kile unachoambiwa, ingawa hukubaliani nacho.)

 

   1.    Juma niandikapo somo hili, Mahakama Kuu ya Marekani imetoa hukumu kwa faida ya mwoka mikate, Jack Phillips, ambaye alikataa kutumia talanta yake ya kisanii kutangaza ndoa ya jinsia moja. Kukataa kwake kulijengwa juu ya imani zake [Jack] za kidini. Kwa kuwa Jack alikataa kutia matatani imani zake za kidini, aliingia kwenye matatizo mengi na serikali ya jimbo la Colorado. Je, Jack ni Mkristo aliyekataa kukubali alama ya suala la kiuumbaji kwenye mkono wake? (Nadhani.)

 

  1.    Rafiki, hizi ni nyakati nzito ambazo tunaziishi. Kuna maamuzi yenye matokeo thabiti unayotakiwa kuyafanya. Je, utaupokea muhuri wa Mungu, Roho Mtakatifu? Je, utaikubali haki kwa njia ya imani pekee? Je, utauzingatia uongozi wa Roho Mtakatifu ili kuwa kwenye upande sahihi wa masuala ya Mungu Muumbaji kiakili na kimwili? Kwa nini usifanye uamuzi sasa hivi?

 

 1.    Juma lijalo: Babeli na Har-Magedoni.