Babeli na Har-Magedoni

Swahili
(Ufunuo 11, 14, 16, 18, Mwanzo 11, Waamuzi 5)
Year: 
2018
Quarter: 
2
Lesson Number: 
12

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.                           

 

Utangulizi: Majina yanayojulikana sana kwenye kitabu cha Ufunuo ni “Babeli Kuu” na “Har-Magedoni.” Je, Babeli ni taifa kubwa, mahali, suala la kufikirika, au ni kitu gani? Kuna jambo gani zuri kuhusu Babeli? Ikiwa Har-Magedoni ni pambano la mwisho, je, linafanyikia wapi? Wapambanaji ni akina nani? Mshindi ni nani? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tuone kile tunachoweza kujifunza!

 

 1.    Babeli Kuu

 

  1.    Soma Ufunuo 14:8. Je, hii ni rejea kwa Babeli ya Danieli na Mfalme Nebukadreza? (Muktadha ni mwisho wa dunia. Lazima hii Babeli “mji ulio mkubwa” iwe Babeli ya sasa kabisa.)

 

   1.    Rejea ya “kunywa mvinyo wa ghadhabu ya uasherati wake” inaashiria nini kuhusu hii Babeli Kuu? (Hii inaakisi ujumbe wa Biblia. Watu wa Mungu wanapoigeukia miungu mingine, Mungu anakilinganisha kitendo hicho na uasherati. Hivyo, hii ni nguvu inayowageuza wanadamu kumwacha Mungu wa kweli.)

 

   1.    Biblia inapouita mvinyo “wa ghadhabu,” je, inamaanisha kuwa Mungu anaghadhabika? (Hapana. Watu wanaomkataa Mungu hawafikiri vizuri. Ni wajinga, wakiwa wametiwa sumu kwa udanganyifu wa Babeli akuu.)

 

  1.    Soma Ufunuo 16:17. Jambo hili lilitokea katika kipindi gani? (Malaika wa saba anakuja katika kipindi ambacho hukumu imekwishatolewa.)

 

  1.    Soma Ufunuo 16:18-21. Tutakiangalia kifungu hiki kwa kina zaidi baadaye. Hii inatuambia nini kuhusu Babeli Kuu? (Inaashiria kuwa ipo mahali fulani. Kifungu hakipo wazi kabisa, lakini Babeli hiyo inaweza kuwa kwenye “mji mkuu.”)

 

  1.    Soma Ufunuo 11:7-8. “Mji mkubwa” ni upi? (Lazima utakuwa ni Yerusalemu, kwa sababu kifungu kinasema “Bwana wao alisulibiwa” pale.)

 

   1.    Kwa nini Yerusalemu pia inaitwa “Sodoma na Misri?” (Huu ni uthibitisho zaidi kuwa jambo baya la kutisha limeitokea Yerusalemu.)

 

  1.    Soma Ufunuo 11:8-15. Kuna uhusiano gani kati ya matukio yaliyoelezewa hapa na yale yaliyoelezewa kwenye Ufunuo 16:18-21? (Tunaona tetemeko kuu la ardhi linalouathiri vibaya “mji mkuu.” Pia tunamwona malaika wa saba. Hii inatoa uthibitisho fulani kwamba katika hatua fulani hivi Babeli Kuu itakuwa na nguvu katika Yerusalemu.)

 

  1.    Soma Ufunuo 18:1-3. Tunaona tangazo jingine kuwa Babeli Kuu imeanguka. Tunaona taarifa gani ya muhimu hapa inayotusaidia kuitambua Babeli Kuu? (Ni mahali pa mashetani na roho wachafu.)

 

   1.    Je, hiyo inafanana na Yerusalemu? (Itafakari. Leo Yerusalemu ni mji uliogawanyika. Kitu gani kinauepusha usigawanyike katika siku za usoni? Je, inawezekana kuwa mmojawapo wa migawanyiko ya sasa ni makao ya wale wanaompinga Yesu? Utakumbuka kuwa katika Ufunuo 11:8 Yerusalemu inaitwa “Sodoma na Misri.” Hii inaakisi nguvu inayopingana na Mungu.)

 

   1.    Wafalme (Ufunuo 18:3) wanawezaje kuzini na Babeli? (Hii nguvu inawafanya viongozi wa kisiasa kutokuwa waaminifu kwa Mungu.)

 

   1.    “Wafanyabiashara” na “starehe kupita kiasi” vinahusianaje na huku kutokua na uaminifu? (Kwa namna fulani Babeli inahusianishwa na umiliki wa vitu kupita kiasi.)

 

   1.    Soma Mithali 18:10-11. Utajiri na umiliki wa vitu unawezaje kuwa mbadala wa kumtegemea Mungu? (Kuzitumaini fedha badala ya kumtumaini Mungu ni kutokuwa na uaminifu. Hii ni sehemu ya ujumbe wa Babeli Kuu: weka tumaini lako kwenye kitu kingine tofauti na Mungu.)

 

 1.   Babeli 1.0

 

  1.    Soma Mwanzo 10:32-11:2. Faida ya kuunganika kwa watu ni ipi? (Wanazungumza lugha moja tu.)

 

  1.    Soma Mwanzo 11:3-4. Hamasa ya kujenga mnara na mji inatokana na nini? (Walitaka kujijengea jina. Hawakutaka kutawanyika.)

 

   1.    Kwa nini walikuwa na wasiwasi kuhusu kutawanyika? (Utakumbuka jambo hili lilitokea “mara” baada ya gharika. Gharika lilibadilisha historia ya mwanadamu na likasababisha kupangwa upya makao ya ulimwengu. “Mnara wenye kilele kifikacho mbinguni” ni ishara kwamba walitaka kujenga makao “yanayozuia gharika.” Mara zote wangeweza kukaa hapa, bila kujali kama gharika jingine lingetokea.)

 

   1.    Waliwezaje kujenga mnara mrefu sana kiasi hicho? (Walikuwa na teknolojia ya hali ya juu. Walijifunza jinsi ya kutengeneza matofali imara. Walikuwa na lugha moja na malengo mamoja.)

 

  1.    Je, watu hawa wanamuunga Mungu mkono? Je, lengo lao ni kumpa Mungu utukufu? (Tunaona mwanzo wa Babeli Kuu. Wao ni wapinzani wa Mungu. Watampinga kwa kutumia mnara wao. Wataishi mahali wanapotaka. Watajipatia utukufu, na si kumpa Mungu utukufu.)

 

  1.    Soma Mwanzo 11:5-7. Je, Mungu anapingana na mafanikio ya wanadamu? (Soma Yeremia 29:11. Hapana, Mungu anataka kutustawisha. Hata hivyo, Mungu hataki kustawisha uasi wetu dhidi yake.)

 

  1.    Hebu tuone kama tunaweza kuangalia ishara zote hizi za kinabii na kuona jambo la kujifunza kivitendo. Unawezaje kuitambua Babeli Kuu? (Inapingana na Mungu. Inajaribu kuhamasisha kuvitumaini vitu tofauti na Mungu. Inahamaisha kutokuwa na uaminifu kwa Mungu. Ina sura ya kidini, lakini moyo wa kishetani. Wakati fulani ina uwepo wa kimwili katika mji wa kale wa Yerusalemu. Historia yote ya “Babeli” inahusu uhamasishaji wa kuwatumaini wanadamu, na si kumtumaini Bwana wetu.)

 

 1. Har-Magedoni

 

  1.    Soma Ufunuo 16:12. Mji wa kale wa Babeli ulipitiwa na mto Frati. Unadhani ishara hii inamanisha nini? (Tumejifunza kuwa Babeli Kuu ni nguvu inayowageuza watu na kuwaweka mbali na Mungu. Sehemu ya ushawishi wake ni starehe zilizopita kiasi. Kifungu hiki kinaashiria kuwa malaika anaangamiza rasilimali za Babeli Kuu. Anakausha maji ya mto, chanzo cha uhai wake.)

 

   1.    Kukatishwa kwa utegemezaji wa Babeli kunatokana na sababu gani? (Kuandaa njia kwa ajili ya wafalme kutoka Mashariki.)

 

  1.    Angalia tena sehemu ya mwisho ya Ufunuo 16:12. Je, hawa “wafalme kutoka Mashariki” ni nguvu kwa ajili ya wema au uovu? (Kwa kuwa kupunguza nguvu ya Babeli ni jambo zuri kwao, wanaonekana kuwa na nguvu kwa ajili ya wema.)

 

   1.    Je, kuna nguvu zozote kubwa kwa ajili ya wema mashariki mwa Yerusalemu?

 

   1.    Soma Ufunuo 7:1-2. Malaika wanatokea upande gani? (Mashariki.)

 

   1.    Soma Isaya 41:1-2. Huyu mshindi wa wafalme anatokea wapi? (Mashariki.)

 

   1.    Soma Isaya 46:9-11. Mungu anamwita “ndege’ mkali kutoka upande gani, “mtu wa kutekeleza ahadi [ya Mungu]?” (Mashariki.)

 

   1.    Vifungu hivi tulivyovisoma vinaashiria nini kuhusu maana ya “wafalme kutoka Mashariki?” (“Mashariki” inaweza isiwe rejea ya mahali au uelekeo, bali mahali ambapo vitu vizuri vinatokeao. Wafalme hawa ni nguvu ya Mungu.)

 

  1.    Soma Ufunuo 16:13-14. Kwa nini vyura hawa wanatoka vinywani? (Utakumbuka kwamba katika kitabu cha Mwanzo 1, Mungu alitamka na akatoa ukamilifu. Nguvu hizi tatu za uovu zinapozungumza, zinatoa vyura. Zinatoa pepo wachafu. Hizi ni aina fulani ya mashetani wenye nguvu wanaoweza kutoa “ishara za maajabu.” Wanashindana na wafalme wa ulimwengu dhidi ya Mungu na wafalme wake kutoka Mashariki.)

 

  1.    Soma Ufunuo 16:15. Hilo linawezekanaje? Tunayo hii mipango ya vita, lakini bado watu wengi wanashangaa kwamba Yesu anakaribia kuja? (Fikiria jambo hili. Nguvu za uovu lazima ziamini kuwa zitashinda, vinginevyo hazitashangazwa. Lazima watu wa Mungu watakuwa wametingwa sana na matatizo ya sasa kiasi kwamba wanapoteza mwelekeo wa taswira pana.)

 

  1.    Soma Ufunuo 16:16. Kwa nini wamekusanyika Har-Magedoni? (Ufunuo 16:14 inasema wamekusanyika “kwa ajili ya vita.”)

 

  1.    Soma Ufunuo 16:17-21. Je, pambano linaendelea? (Badala ya taarifa ya pambano, tunasoma kuhusu tetemeko la ardhi la kutisha na mvua ya mawe. Mungu anamimina ghadhabu yake kwa Babeli Kuu. Inaonekana Mungu anatumia mambo ya asili kuushinda uovu kimiujiza.

 

  1.    Soma Waamuzi 5:19. Je, umewahi kuisikia “Megido” hapo kabla? (Neno la Kiebrania lililotafsiriwa kama “Har-Magedoni” linamaanisha mahali fulani katika Megido.)

 

  1.    Soma Waamuzi 5:20-21. Vita hii inayoendelea Megido inapataje ushindi? (Kwa mambo ya asili! Mafuriko yanasababisha mto Kishoni kuwachukua watu wabaya. Tunacho kigezo, mahali hapa hapa, kwa Mungu kutumia nguvu za asili kuushinda uovu!)

 

  1.    Rafiki, dunia inachukua pande. Nchini Marekani, mgawanyiko unaonekana kuwa mkubwa na wenye dhamira kubwa. Ingawa kimahsusi mgawanyiko si kati ya Wakristo na wasio Wakristo, kwa kiasi kikubwa mgawanyiko upo kwa walio kwenye uasi dhidi ya Neno la Mungu na wale wanaotamani kumfuata Mungu. Je, utachagua upande sahihi? Kwa nini usifanye uamuzi huo sasa hivi?

 

 1.   Juma lijalo: Kurudi kwa Bwana Wetu Yesu Kristo.