Kurudi kwa Bwana Wetu Yesu

Swahili
(Isaya 13, Ufunuo 19, 1 Wakorintho 15, Danieli 2)
Year: 
2018
Quarter: 
2
Lesson Number: 
13

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Je, unakumbuka kusimamishwa na polisi kwa sababu ulikuwa unakiuka sheria za usalama barabarani? Ulijisikiaje? Kuna gari lilikuwa linanifuata kwa karibu sana nilipokuwa ninaendesha kwenda kanisani, ingawa nilikuwa ninaendesha bila kuzidi kiwango cha mwendo unaotakiwa. Tulikuwa tunapita katika eneo la makazi na barabara ilikuwa pana na yenye vilima. Nilipofika kileleni, niliona paa la gari la polisi kwa mbele. Bila kupunguza mwendo, nilisogea upande wa kulia mwa barabara kiasi cha kutosha ili gari lililo nyuma yangu liweze kupita, ingawa kitendo hicho kilikuwa ni uvunjaji wa sheria. Gari hili lilinisogelea, likapanda kileleni mwa kilima, kisha nikaona gari la polisi ambalo mara moja lililisimamisha gari hilo kwa kosa la kuendeshwa kwa kasi kupita ukomo. Ungejisikiaje endapo ungekuwa mimi? Hizi ni sura mbili za hukumu. Hatutaki kuhukumiwa, lakini tunataka wavunjaji wa sheria, hususani wale walio wasumbufu kwetu, wakabiliane na hukumu. Ujio wa Yesu Mara ya Pili ni kipindi chenye hisia mchanganyiko. Hebu tuchimbue kile ambacho Biblia inakisema kuhusu kipindi hicho!

 

 1.    Kukabiliana na Ujio wa Mara ya Pili

 

  1.    Soma Isaya 13:6-9. Hisia gani zitawachukua wadhambi Yesu atakaporejea? (Watatiwa hofu.)

 

   1.    Kwa nini? (Vifungu hivi vinasema kuwa wanakabiliana na kifo.)

 

   1.    Ni mara moja tu maishani mwangu nilidhani kuwa ningeweza kufa dakika chache zijazo. Mikono yangu haikuwa milegevu na sikugaagaa sakafuni. Badala yake, nilifanya kazi ili kuyaokoa maisha ya watoto wangu. Nawe ungefanya vivyo hivyo, sijidai kwamba mimi ni mwerevu zaidi. Ikiwa wewe na mimi tunadhani kuwa tutakabiliana na kifo kwa utulivu, unaelezeaje hisia na mwitiko wa waovu? (Wakristo wanakabiliana na kifo kwa ahadi ya uzima wa milele Yesu atakapokuja tena. Hata hivyo, nadhani kuna jambo la ziada kwenye aina hii ya kuogofya. Sidhani kama aina hii ya mwitiko inatokana na hisia za hatia au mshangao kwamba Mungu anaingilia kati.)

 

   1.    Utaona kwamba Biblia inazungumzia ujio wa Yesu Mara ya Pili kama “siku kali.” Kwa nini Mungu anaiita hii siku kubwa “kali?) (Sidhani kama Mungu anafurahia hukumu. Huenda hukuwa na raha kwa kiasi fulani kutokana na kisa nilichokielezea kwenye utangulizi.)

 

  1.    Soma Mathayo 24:30-31. Mataifa yana mwitiko gani kwa ujio wa Yesu Mara ya Pili? (Yanaomboleza.)

 

  1.    Soma Isaya 13:10, Isaya 34:4 na Mathayo 24:29. Katika kitabu cha Mathayo Yesu anatongoa (anakariri) alichokitabiri Isaya kuhusu ujio wake wa Mara ya Pili. Je, hii inatupatia sababu nyingine ya kutiwa hofu miongoni mwa wasiookolewa? (Ulimwengu unaparanganyika. Tuchukulie kwamba sayansi inaendelea kukua na kufanya uvumbuzi kwenye elimu ya falaki, wanadamu watakuwa na onyo la mapema kabisa kwamba jambo la kutisha litatokea katika miaka michache ijayo ulimwenguni.)

 

  1.    Soma 2 Wathesalonike 1:5-10. Jambo gani linamhamasisha Mungu kuwaogofya na kuwaadhibu waovu? (Mungu anawapatia watu wake ahueni. Anatoa “malipo” kwa wale wanaosababisha mateso.)

 

   1.    Angalia asili ya hukumu. Unaona jambo gani la kufurahisha kuihusu? (Waovu wanaelezewa kama “watu wasiomjua Mungu.” Hata hivyo, kuwekwa nje ya uwepo wa Mungu na uwezo wake ni adhabu inayojulikana. Naliona jambo hili kuwa la kufurahisha kwa sababu waovu tayari wanajiadhibu kwa kujitenga na Mungu. Angamizo la milele pia linabainishwa.)

 

 1.   Kuokolea kwa Ujio wa Mara ya Pili

 

  1.    Soma Ufunuo 19:11-13. Ni nani huyu afanyaye vita iliyojengwa juu ya haki? (Soma Yohana 1:1-3 na Yohana 1:14. Huyu ni Yesu! Yeye ni Neno la Mungu.)

 

  1.    Soma Ufunuo 19:14-16. Kwa nini majeshi ya mbinguni, yale yatokayo angani, yanaendesha farasi? Je, hao ni farasi warukao? (Wakati huficha uelewa wetu. Farasi walikuwa zana ya hali ya juu katika teknolojia ya kijeshi. Askari aliye kwenye kigari kinachokokotwa na farasi alikuwa ni mpinzani wa kutisha. Ili kuelewa taswira hii kikamilifu, fikiria kwamba majeshi ya mbinguni yana teknolojia ya usafiri ya hali ya juu. Fikiria “Star Wars!”)

 

   1.    Kwa nini upanga mkali unatoka kinywani mwa Yesu? (Hii ni ishara nyingine ya uwezo mkuu. Mwanzo 1 inatuambia kuwa Yesu alitamka na ulimwengu ukapata kuwepo.)

 

  1.    Soma 1 Yohana 2:28. Mtazamo wetu unaweza kuwaje Yesu anapokuja tena? (Kuwa na ujasiri na kutoaibika.)

 

  1.    Soma Ufunuo 5:13-14. Mwitiko wa pili wa wale waliookolewa ukoje? (Wanamsifu Mungu.)

 

  1.    Soma Ufunuo 7:14-17. Ni nini matokeo ya watu waliookolewa? (Hawana tena njaa, kiu, joto au huzuni. Kwa dhahiri hawajaogofwa.)

 

  1.    Soma 1 Wathesalonike 4:16-18. Tunapotafakari ujio wa Yesu Mara ya Pili, waliookolewa wana mtizamo gani wa asili? (Wanatiwa moyo kwa ahadi hii, hawana wasiwasi.)

 

  1.    Soma 2 Wathesalonike 1:10. Watu waliookolewa watafanya jambo gani jingine Yesu atakapokuja? (Watamstaajabia Bwana wetu. Tutampa utukufu.)

 

  1.    Tunaweza kuona kwamba ujio wa Yesu Mara ya Pili unaleta miitiko miwili tofauti kabisa, kutegemeana na endapo umeokolewa au la. Unataka kuwa na mwitiko gani?

 

 1. Mambo Yote Mapya

 

  1.    Soma 1 Wakorintho 15:42-44. Miili yetu itabadilikaje Yesu atakapokuja? (“Hatutaharibika,” wenye fahari, utukufu na wa kiroho.)

 

  1.    Soma Wafilipi 3:20-21. Miili yetu mipya inalinganishwa na nini? (Miili yetu itafanana na mwili wa Yesu. Tutakuwa na mwili wa kimbingu.)

 

  1.    Soma 1 Wakorintho 15:50-54. Kifungu hiki kinarudia baadhi ya mabadiliko ya miili yetu. Kitu gani kingine kinabadilika? (Kifo kinashindwa. Hakina ushindi wala uchungu. Badala yake, “kimemezwa” na kutokufa na ushindi kwa wale waliookolewa.)

 

  1.    Soma Danieli 2:31-35. Unadhani jiwe lililoipiga sanamu miguuni ni kitu gani? (Soma Danieli 2:44-45. Jiwe ni Ufalme wa Mungu.)

 

   1.    Kitu gani kimesalia kwa falme za zamani? (Zinafanana na makapi, “zinaangamizwa bila kuacha chembechembe ya enzi yake.”)

 

  1.    Soma Ufunuo 21:1. Kitu gani kimeitokea nchi ya kwanza? (“Imekwisha kupita.”)

 

   1.    Randy Alcorn ana kitabu kinachoitwa “Mbingu,” ambapo anakisia kuwa nchi mpya inafanana na nchi ya zamani kutokana na ukweli kwamba ina sehemu zile zile. Haiko sawa kwa asilimia mia moja, ni kubwa kwa sababu haina bahari. Ninapenda pendekezo lake kuhusu jinsi tunavyoweza kuishi kwenye toleo lililo na utukufu katika mahala tulipokulia. Lakini, vifungu vya Biblia tulivyovisoma punde vinatufanya tuyatilie shaka maono ya Alcorn. Una maoni gani?

 

  1.    Soma Ufunuo 21:2-4. Yerusalemu Mpya inatoka wapi? (“Mbinguni kwa Mungu.”)

 

   1.    Unashuka hadi wapi? (Kwenye nchi mpya.)

 

   1.    Tunakaa wapi? (Tunaishi kwenye nchi mpya.)

 

   1.    Makao makuu ya Mungu yapo wapi? (Makao mapya ya Mungu yapo kwenye nchi mpya. Anakaa pamoja nasi!)

 

    1.    Unadhani kwa nini Mungu anakuja kukaa kwenye nchi mpya? (Hili ni eneo la pambano kuu na ushindi dhidi ya uasi. Lazima ushindi wa Mungu uwe kiini cha umilele wote uliosalia.)

 

  1.    Soma Ufunuo 21:5. Je, Mungu aliiweka ahadi hii kwenye maandishi? (Ndiyo!)

 

  1.    Rafiki, unaweza kuitegemea ahadi ya Mungu. Anakuja tena! Ujio wake wa Mara ya Pili utakuwa wa kuogofya kwa waovu, bali ukaribisho wa wokovu kwa wale walio waaminifu. Si tu kwamba tutaokolewa, bali tutajazwa furaha na kusifu kwamba uovu umeangamizwa. Mambo yote yatafanywa upya. Mungu mwenyewe atakaa pamoja nasi. Ushindi wa Yesu dhidi ya dhambi, na sehemu yetu kwenye hiyo historia itashangiliwa milele! Je, utachagua kuwa miongoni mwa wenye haki? Kwa nini usiutoe moyo wako kwa Yesu sasa hivi?

 

 1.   Juma lijalo: Tutaanza mfululizo mpya wa masomo katika Kitabu cha Matendo.