Uongofu wa Paulo

Swahili
(Matendo 9 & 26)
Year: 
2018
Quarter: 
3
Lesson Number: 
5

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Je, unawafahamu watu wenye uhasama mkubwa na injili kiasi cha kudhani kuwa kamwe hawawezi kubadilika? Huenda hauko sahihi. Juma hili tunajifunza habari za mtu aliyeichukia sana injili kiasi cha kuazimia kuwafunga au kuwaua Wakristo. Licha ya hayo, Mungu alimbadilisha kabisa. Kamwe hatupaswi kuutilia shaka uwezo wa Mungu! Hebu tuchimbue somo letu la Biblia na tujifunze zaidi!

 

 1.    Mharibifu

 

  1.    Soma Matendo 26:1-5. Hapa Paulo yupo njiani. Anayaelezeaje maisha yake ya awali? (Alikuwa kwenye madhehebu ya Kiyahudi kikamilifu, aliishi kama Mfarisayo.)

 

  1.    Soma Matendo 26:6-8. Je, si dhahiri kwamba kisa cha kuwafufua wafu kinatiliwa mashaka kiuhalisia?

 

   1.    Kwa nini Paulo anasema kuwa halipaswi kuwa jambo la “kushangaza?” (Huenda Paulo anasema kuwa endapo angeweza kubadilishwa kutoka kwenye madhehebu yake ya Kiyahudi hadi kushtakiwa kwa kumwamini Yesu, basi kuwafufua wafu si jambo la kushangaza kwa kiasi hicho. Huenda anamaanisha kuwa wapagani wanaweza kuamini kuwa miungu inaweza kuwafufua wanadamu.)

 

  1.    Soma Matendo 26:9-11. Je, mambo aliyoyafanya Paulo dhidi ya Wakristo yalikuwa halali? (Anasema aliyatenda chini ya mamlaka. Rejea yake juu ya “kura” inaonekana kama aina fulani hivi ya uamuzi wa kikundi wa kidemokrasia.)

 

  1.    Soma Matendo 7:54-58. Kumbuka jinsi tulivyojifunza kupigwa mawe kwa Stefano, je, tulidhani kuwa kitendo hiki kilifanywa kihalali? (Maelezo yanaonekana kama matendo ya genge la watu lisiloweza kudhibitika. Baadaye “Sauli” aliitwa “Paulo.”

 

  1.    Soma Matendo 9:1-2. Je, hapa Sauli anaenenda chini ya mamlaka?

 

   1.    Kwa nini viongozi wa dini wa Yerusalemu wawe na mamlaka ya kisheria kwenye miji ya kigeni kama vile Dameski? (Maoni kadhaa niliyoyasoma yanasema kuwa Warumi walimpa Kuhani Mkuu na Baraza mamlaka juu ya Wayahudi katika miji ya kigeni. Hivyo, kitendo hiki kilikuwa halali kisheria.)

 

 1.   Uongofu

 

  1.    Soma Matendo 9:3-5. Kwa nini Sauli anaiita sauti “Bwana?” (Kuna mjadala unaoendelea ikiwa jambo hili linatakiwa litafsiriwe kwa uzuri zaidi kama “U nani wewe ndugu?” Paulo alidhani kuwa hii ni nguvu yenye hadhi.)

 

   1.    Unadhani jambo gani lilikuwa linaendelea mawazoni mwa Paulo anapoambiwa kuwa huyu mzungumzaji mtukuka ni Yesu?

 

  1.    Soma Matendo 22:10 ili kupata taarifa za ziada zilizoachwa kwenye sura ya 9. Taarifa hii ya ziada inatuambia nini kuhusu mawazo ya Sauli wakati huo?

 

  1.    Soma Matendo 9:6-9. Kwa nini Sauli hakula wala kunywa kwa muda wa siku tatu? (Hii inaakisi mshtuko wa mfumo wake. Sio tu kwamba sasa hivi ni kipofu, bali anagundua kuwa amekuwa akimpinga Mungu, kwa kutotenda mapenzi ya Mungu.)

 

   1.    Mama kwa mara huwa nasikia wito kwa waumini kurejea kwenye “nguzo za imani,” “mizizi,” na “misingi.” Paulo angezungumzia nini kuhusu wito kama huo? (Tunatakiwa kuwa na uhakika kwamba “misingi” na “nguzo” zinajengwa kikamilifu. Ukweli kwamba hapo awali tulikuwa tunaamini jambo fulani hailifanyi jambo hilo kuwa la kweli. Tunatakiwa kuhakikisha kuwa imani zetu zote zimejengwa madhubuti kwenye Biblia.)

 

 1. Anania

 

  1.    Soma Matendo 9:10-12. Anania anapewa jukumu gani? Je, jukumu hilo liko dhahiri?

 

   1.    Je, ungependa kufahamu anachokiomba Sauli?

 

  1.    Soma Matendo 9:13-14. Je, Anania ana wasiwasi kwamba Mungu amekuwa hafuatilii habari zinazoendelea? Je, ana wasiwasi kwamba uelewa wake juu ya hali ya mambo yanayotokea katika eneo lao ni mkubwa zaidi ya Mungu aelewavyo habari hizo?

 

  1.    Soma Matendo 9:15. Unapenda nini kizuri zaidi kwenye jibu la Mungu? (Mungu mkuu wa mbinguni hasemi, “Kwa hakika ninafahamu!” Badala yake, anamfunulia Anania mipango yake kwa Sauli. Mungu wa rehema kiasi gani!)

 

   1.    Kifungu hiki ni cha pekee kwa sababu kadhaa. Je, unadhani kuwa Mungu ana mpango mahsusi kwa kila mtu?

 

   1.    Ikiwa jibu ni hapana, kwa nini alikuwa na mpango mahsusi kwa Sauli?

 

   1.    Ikiwa Mungu ana mpango mahsusi kwa kila mtu, kwa nini watu wengi sana wanaonekana kutokuwa na habari na mpango wa Mungu kwa ajili ya maisha yao?

 

   1.    Kwa nini Mungu aliingilia kati moja kwa moja maisha ya Sauli, lakini haingilii kati moja kwa moja maisha ya watu wengine? (Nadhani jibu la maswali haya linaenda moja kwa moja kwenye uamuzi wa awali wa Sauli wa kujitoa kikamilifu kwenye kazi ya Mungu. Hakuielewa kazi ya Mungu, kimsingi hakuelewa kuwa alikuwa anaipinga kazi ya Mungu, lakini alikuwa amejitoa kikamilifu. Kama umejitoa kikamilifu kuitangaza kazi ya Mungu, basi Mungu atakueleza kile anachokuwazia.)

 

  1.    Soma Matendo 9:16. Kwa nini hii ni sehemu ya ujumbe kwa Anania? (Anania anazingatia sana mateso yote ambayo Sauli ameyasababisha. Ana wasiwasi kwamba Sauli atamtesa. Mungu anamhakikishia Anania kuwa kinyume cha mambo yanayotokea ndicho kinataka kuanza kutokea.)

 

   1.    Mungu alipomwambia Sauli kuwa atateseka kwa ajili ya injili, unadhani Sauli alijibu nini? (Nadhani Sauli alijisikia hatia kubwa sana katika hatua hii, na hiyo ilirahisisha zaidi kwa yeye kuukubali mustakabali wake kwa sababu aliweza kuona “haki” ndani yake. Watu wengine wangeweza kuwa na mtazamo potofu kwenye kazi yake, kama alivyokuwa na mtazamo potofu wa injili katika siku za nyuma.)

 

  1.    Soma Matendo 9:17. Anania anamtumaini Mungu! Unadhani kwa nini Anania alizungumzia ujazwaji wa Roho Mtakatifu? Ukiangalia nyuma katika Matendo 9:12, Yesu alitoa tu maono ya kumrejeshea Sauli uoni? (Ili kuwa na uoni “wa kweli,” unamhitaji Roho Mtakatifu. Nadhani upofu wa Sauli kubadilishwa na kupata kuona kunaashiria safari ya Sauli ya kujazwa Roho Mtakatifu.)

 

  1.    Soma Matendo 9:18-19. Kwa nini Sauli anakula tena? (Anauelewa utume wake. Ametatua mgogoro maishani mwake.)

 

 1.   Utume

 

  1.    Soma Matendo 9:20. Je, Sauli anapoteza muda wowote kwenye kazi yake mpya?

 

  1.    Soma Matendo 9:21-22. Unadhani kwa nini Sauli “alizidi kuwa hodari?”

 

  1.    Soma Matendo 9:23-25. Wayahudi wanawazia tiba gani kwa Sauli? (Kwa mara nyingine, tunaona kwamba hawajaridhishwa na mjadala, wanataka kuua upinzani. Mara zote hii ina kiashiria muhimu wa nani mwenye hoja bora. Hoja zilizoshindwa zinageuka na kuwa vurugu.)

 

  1.    Soma Matendo 9:26, Wagalatia 1:11-12, na Wagalatia 1:15-19. Kipindi cha Sauli katika Matendo 9 hakijumuishi rejea ya miaka yake mitatu Arabuni kabla hajaenda Yerusalemu. Kutokana na kauli za Sauli kuhusu ufunuo wa moja kwa moja kutoka kwa Yesu, unadhani anarejea jambo gani? (Inaonekana ni vigumu kubainisha kitendo cha Mungu kuingilia kati moja kwa moja njiani kuelekea Dameski kama “ufunuo kutoka kwa Yesu,” kwa kuwa tunamwona “Anania” akishauriana na Sauli kabla ya hapo, na kipindi hicho kilikuwa kifupi. Sauli anaweza kuwa anamaanisha kwamba Yesu alijifunua kule Arabuni.)

 

   1.    Kwa nini jambo hili lihusike zaidi? Kuna ubaya gani kufundishwa na mmojawapo wa mitume? (Utofauti huu ni wa muhimu kwangu kwa sababu huenda ningekuwa na mtazamo tofauti juu ya kuhesabiwa haki kwa imani ikiwa tungeondoa maandiko ya Paulo kutoka kwenye Agano Jipya. Roho Mtakatifu ana urahisi wa kunifundisha kuhusu neema ninapomsoma Paulo!)

 

  1.    Soma Matendo 9:28-30. Kwa mara nyingine maisha ya Sauli yako hatarini. Je, unauona mkono wa Mungu katika jambo hili? (Kama vile Mungu alivyotumia mateso ya Sauli kueneza injili nje ya Yerusalemu, vivyo hivyo alitumia mateso ya Sauli kupeleka ujumbe wake kwa mataifa.)

 

   1.    Je, kuna jambo ulilolichukulia kuwa ni baya ambalo limegeuka na kuwa jambo jema maishani mwako?

 

  1.    Soma Matendo 9:31. Machafuko yote haya yanatendaje kazi? (Kipindi cha amani kinalijia Kanisa.)

 

  1.    Rafiki, ikiwa unaombea uongofu wa adui wa Mungu, usikate tamaa! Uongofu wa Sauli unatuonesha kuwa lipo tumaini kwa mpinzani mwenye shauku kuliko wote. Uongofu wa Sauli unatuonesha kuwa Mungu anayachukua mambo mabaya na kuyafanya kuwa mazuri. Kwa nini usidhamirie kumtumaini Mungu bila kujali matokeo?

 

     Juma lijalo: Huduma ya Petro.