Somo la 6: Huduma ya Petro

Swahili
(Matendo 9:32-11:3; Matendo 12)
Year: 
2018
Quarter: 
3
Lesson Number: 
6

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.                           

 

Utangulizi: Ikiwa unafuatilia masomo ya Gobible.org mara kwa mara, utagundua kwamba huwa ninakukumbusha kila mara kuwa wokovu unapatikana kwa njia ya neema pekee, matendo yetu hayatuokoi. Hata hivyo, hiyo haipaswi kutia wingu ukweli kwamba kwa ujumla matendo yetu yanaleta tofauti kwenye ubora wa maisha yetu. Mungu anawapendelea wale wanaomtii. Wakati huo huo, mara nyingi maisha hayatendi haki. Wajibu wetu ni kumpa Mungu utukufu, na si kuwa na wasiwasi kama tunatendewa haki na matukio yanayotokea maishani. Somo letu juma hili linagusia suala hili la kwa nini Wakristo wengine wanafanya vizuri zaidi ya wengine. Hebu tuchimbue somo letu la Biblia na tujifunze zaidi!

 

 1.    Ainea

 

  1.    Soma Matendo 9:32-35. Kwa nini Petro alitenda huu muujiza?

 

   1.    Unadhani walikuwepo wagonjwa wengine au watu waliopooza katika eneo hilo?

 

   1.    Matokeo ya huu muujiza ni yapi, tofauti na kumponya Ainea? (Ilikuwa chanzo cha kuwaongoa “watu wote” walioishi kwenye ile miji miwili.)

 

  1.    Soma Yohana 9:1-3. Yesu anasema kuwa kwa nini mtu huyu alizaliwa kipofu? (“Ili kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake.” Nadhani kuponywa kwa Ainea hakukuwa katika kumsaidia yeye zaidi kwani ilikuwa ni kwa ajili ya kuwaongoa watu wengine. Hii ni ngumu kuielewa kwa watu ambao bado hawajatambua kwamba maisha yanahusiana na kumpa Mungu utukufu, badala ya kutuhusu sisi binafsi.)

 

 1.   Tabitha

 

  1.    Soma Matendo 9:36-38. Ukiachilia mbali kufa kwake, badala ya kupooza, tofauti kati ya Tabitha na Ainea ni ipi? (Tabitha si mtu anayehitaji msaada, ni mtu ambaye maisha yake yamekuwa yakihusiana na kutenda mambo mema.)

 

   1.    Kwa nini tumaambiwa juu ya habari za “kuoshwa” kwa mwili wake? (Hii inatuambia kuwa kweli alikuwa amekufa. Utamaduni wa Kiyahudi ni kuzika mwili haraka iwezekanavyo, na kuosha mwili ni maandalizi ya maziko.)

 

  1.    Soma Matendo 9:39-42. Unadhani kwa nini Petro alitenda huu muujiza? (Kwa mara nyingine, tunasoma kuwa watu wengi wanaongolewa. Lakini, msisitizo mkubwa kwenye matendo mema ya Tabitha inayafanya matendo yake yaonekane kuwa nayo ni sehemu ya sababu ya kuponywa kwake.)

 

 1. Kornelio

 

  1.    Soma Matendo 10:1-6. Kwa nini Kornelio alipokea maono haya na si watu wengine wa Mataifa? (Kwa umahsusi kabisa malaika anataja “sala na sadaka zake kwa masikini.”)

 

   1.    “Sadaka ya ukumbusho” ni ipi? (Zipo tofauti katika Agano la Kale kwenye sadaka ya ukumbusho, lakini nadhani hii inamaanisha kuwa Mungu anamkumbuka Kornelio kutokana na haya matendo ya moyo wa kumwabudu Mungu na rehema.)

 

  1.    Unapotafakari visa hivi, unadhani kwa nini Biblia inabainisha matendo mema ya mtu anayesaidiwa kwenye visa viwili kati ya vitatu? (Maisha yanahusiana na kumtukuza Mungu. Lakini, Mungu pia anawabariki na kuwatukuza wale walio waaminifu kwake. Hii si kuhesabiwa haki kwa njia ya matendo, huu ni ubainishaji wa upendeleo wa Mungu kwa wale wanaotafuta kuyatenda mapenzi yake.)

 

  1.    Soma Matendo 10:9-14. Hii ilitokea mara tatu. Unapaswa kufanya nini maono yanapokinzana na Biblia? Angalia Mambo ya Walawi 11, kuhusu suala la chakula najisi.

 

  1.    Soma Matendo 10:17. Petro anafanya nini kuhusu maono yake kukinzana na Biblia? (Anapata ugumu jinsi ya kupatanisha maono na uelewa wake wa Biblia.)

 

  1.    Soma Matendo 10:28-29. Mgongano unatatuliwaje? (Petro anatambua kuwa hakuna mgongano kati ya Biblia na maono yake, kwa sababu maono yaliwahusu watu “najisi,” na si chakula. Kwa kawaida Petro asingeingia malangoni mwa Mataifa kama vile Kornelio, lakini maono yalisahihisha dosari hii.)

 

  1.    Soma Matendo 10:34-35, na Matendo 10:44-48. Jambo gani jipya limetokea katika kanisa la awali? (Waongofu wa Kiyahudi sasa wanatambua kuwa Mataifa wanakaribishwa katika kanisa la Kikristo. Utakumbuka kwamba Yesu na wanafunzi wake walikuwa Wayahudi. Utakumbuka kwamba Wayahudi waliamini katika ujio wa Masihi. Hivyo, waliamini (kwa usahihi) kwamba Yesu alikuwa kilele cha imani ya Kiyahudi. Hiyo iliwafanya “washangazwe” kwamba Mataifa wasiotahiriwa waliweza kuwa sehemu ya imani yao. Walidhani kuwa Yesu alikuwa tu enzi ya mwisho katika Uyahudi.)

 

  1.    Soma Waefeso 2:11-12. Wayahudi waliwatazamaje Mataifa? (Hawakuwa na tumaini.)

 

  1.    Soma Matendo 11:1-3. Wakristo wa Kiyahudi walikuwa na mwitiko gani waliposikia kisa cha Kornelio?

 

  1.    Soma Waefeso 2:13-15 na Matendo 11:18. Yesu amewatendea nini Mataifa? (Ameangamiza ukuta wa uhasama uletao utenganishi. Kornelio, mtu aliyemtii Mungu, alikuwa mwanzo wa kulifanya jambo hili kuwa wazi katika kanisa la awali.)

 

 1.   Yakobo na Petro

 

  1.    Soma Matendo 12:1-3. Unakumbuka kisa cha mamaye Yakobo kumwendea Yesu akiomba kwamba wanaye (Yakobo na Yohana) wakae mkono wa kuume wa Yesu katika ufalme wake? Kisa kinapatikana kwenye Mathayo 20:20-23.

 

   1.    Soma Mathayo 20:22-23. Je, Yakobo amekinywea kikombe cha Yesu? Je, hiki ndicho alichokiwazia mamaye Yakobo? (Haya ni maelezo sahihi ya ukinzani wa injili. Yesu anataka tubarikiwe. Amri zake zinalenga kutusaidia tuishi maisha bora. Lakini, kuwa mfuasi wa Yesu mara nyingine humaanisha kuwa tunapata mateso. Waebrania 11 inaelezea matendo haya tofauti kabisa, lakini inatuahidi kuwa hatimaye watu wote watapata kile ambacho Mungu amekiahidi.)

 

  1.    Soma Matendo 12:4-5. Je, hii imepita kiasi? Askari kumi na sita kumlinda mhubiri mmoja aliyefungwa mnyororo gerezani?

 

  1.    Soma Matendo 12:6-10. Je, Petro anapendelewa na Mungu? (Naam!)

 

   1.    Kwa nini Yakobo alikufa? Kwa nini hakuokolewa? (Tunatakiwa tu kuyaacha mambo haya mikononi mwa Mungu tukijua kwamba Yakobo atapokea thawabu yake.)

 

  1.    Hebu turuke vifungu kadhaa na tusome Matendo 12:18-19. Je, hii ni haki? Kuna chochote ambacho walinzi wangeweza kukifanya vinginevyo? (Hapana, si haki kwa sababu hakuna ambacho walinzi wangeweza kukifanya. Huu ni mfano wa jambo ambalo wakati mwingine linatokea maishani.)

 

  1.    Soma Matendo 12:12-15. Je, hili limewahi kukutokea? Ulikuwa ukiomba jambo fulani na baadaye hukuweza kuamini Mungu alipojibu maombi yako?

 

 1.    Herode

 

  1.    Soma Matendo 12:20-23. Chanzo cha kifo cha Herode ni kipi? (Ni hukumu ya Mungu kutokana na Herode kupokea sifa iliyomstahili Mungu pekee. Lakini, pia ni aina fulani ya ugonjwa unaohusisha minyoo kumla.)

 

   1.    Herode alikuwa anapingana na injili kwa muda mrefu. Utakumbuka kuwa alisababisha Yakobo auawe, na Petro kukamatwa. Bila shaka alidhamiria kumwua Petro. Kwa nini Herode anaangushwa sasa hivi? Vipi kuhusu walinzi wasio na hatia waliouawa?

 

   1.    Soma Mwanzo 15:12-16. Inamaanisha nini kusema kwamba uovu (dhambi) wa Waamori bado “haujatimia?” (Hii inatupatia utambuzi wa fikra ya Mungu. Mungu anachelewesha adhabu hadi dhambi zetu, kikombe chetu cha uovu, kinapofikia “kipimo kamili.” Hatimaye Herode alifikia “kipimo kamili” na alikufa kifo kichungu.)

 

  1.    Soma Matendo 12:24. Je, uovu unaweza kusitisha kazi ya Mungu? (Hapana! Yakobo alikufa. Kufungwa kwa Petro kulisababisha wasiwasi mkubwa na maombi. Lakini, Kazi ya Mungu inasonga mbele!)

 

  1.    Rafiki, hauujui mustakabali wako. Unaweza kuongezea uwezekano wa kuwa na mustakabali chanya hapa duniani kwa kuwa mtiifu. Lakini, mambo mabaya yanatokea kutokana na sababu mbalimbali. Mungu anatuita tuwe waaminifu bila kujali mambo yanayotokea. Je, utadhamiria leo, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, kuwa mwaminifu?

 

 1.   Juma lijalo: Safari ya Kwanza ya Paulo ya Kimisionari.