“Wote Wawe na Umoja”

(Yohana 17, Marko 9)
Swahili
Year: 
2018
Quarter: 
4
Lesson Number: 
3

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Je, unapenda sifa? Je, wewe ni kati ya watu wanaojulikana kama “fidhuli wa sifa?” Unapokuwa unaangalia timu ya mchezo fulani, na mchezaji mmoja anatafuta kupata sifa zote, je, unadhani timu hiyo ina umoja? Njia ya ulimwengu ni kutafuta sifa binafsi. Lakini, unaweza kushangazwa kufahamu kwamba kuwa Mkristo wa kweli pia hukupatia sifa. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi!

 

 1.    Ombi la Yesu kwa Ajili Yake

 

  1.    Soma Yohana 17:1-2 na Mathayo 6:5. Je, umewahi kuwa na wasi wasi kwamba inawezekana kuwa unafanya kazi nzuri ambayo kwa kiasi kikubwa ni kwa ajili ya kujipatia sifa? Kwa mfano, kama unafundisha darasa la Biblia, je, unafundisha kwa sababu unapenda kuonekana mbele ya darasa, au kwa sababu unataka watu wengine wamjue Mungu zaidi? Au, je, ni mchanganyiko wa yote mawili?

 

   1.    Yesu anabainisha utukufu wa nani kwanza? (Utukufu wake.)

 

    1.    Muktadha wake ni upi? (Yesu anaposema “saa imekwisha kufika” anamaanisha muda wa kusulubiwa kwake. Hivyo, utukufu kwake inamaanisha wokovu kwa ajili yetu sote.)

 

  1.    Soma Yohana 17:3. Kumjua Mungu kunahusianaje na uzima wa milele? (Uzima wa milele ni kumjua Mungu.)

 

   1.    Hii inahusianaje na ombi la Yesu kuhusu utukufu na uzima wa milele? (Yesu anakaribia kutupatia sote fursa ya uzima wa milele. Kitendo hiki cha kuutoa uhai wake kwa ajili yetu kinatuambia mambo mengi sana kuhusu Mungu – kinatupatia uelewa wa upendo wa Mungu.)

 

  1.    Soma Yohana 17:4-5. Utaona kwamba ombi la Yesu linaanza na mjadala wa mahitaji yake. Je, huo ndio mwelekeo wetu? (Ni sahihi zaidi kusema kwamba ombi la Yesu linaanza kwa mjadala kuhusu utukufu, kwa Mwana na Baba. Ombi la Yesu la mfano (Mathayo 6:9-13) pia linaanza kwa kumtukuza Mungu.)

 

 1.   Ombi la Yesu kwa Wanafunzi Wake

 

  1.    Soma Yohana 17:6-7. Mhusika ni nani kwenye sehemu hii ya ombi la Yesu? (Wanafunzi wake.)

 

   1.    Lengo la Yesu ni lipi katika makabiliano yake na wanafunzi wake? (Kumfunua Mungu kwao.)

 

   1.    Je, hili pia ni lengo maishani mwetu? (Ndiyo! Watu wangapi wanamkataa Mungu wasiyemjua? Wana taswira ya kutisha ya Mungu, na kisha wanaikataa hii taswira.)

 

  1.    Soma Yohana 17:8-9. Kwa nini Yesu hauombei ulimwengu? (Tutajadili jambo hili baadaye.)

 

  1.    Soma Yohana 17:10. Je, umewahi kuimba wimbo wa “Yote Namtolea Yesu?” Je, kweli ulimaanisha yale uliyoyaimba?

 

   1.    Angalia kwa makini kile anachokisema Yesu. Je, kuyatoa mambo yote kulimpa nini Yesu? (Vyote vilivyo vya Mungu Baba.)

 

   1.    Tafakari jambo hili: Unampa Bill Gates kila kitu unachokimiliki, naye anakupatia kila kitu anachokimiliki. Je, hayo ni makubaliano utakayoyakubali?

 

  1.    Soma Yohana 17:11. Hii kauli ya “kwa jina lako” ni kauli ya zamani nje ya Ukristo, na ninapata ugumu kuielewa. Yesu anaposema, “uwalinde hawa kwa jina lako - jina ulilonipa” anamaanisha nini?

 

   1.    Hebu tuliangalie hili. Unaposikia jina la mtu, nini hukujia mawazoni mwako? (Jinsi anavyofananishwa. Jinsi anavyoenenda. Endapo unampenda. Kimsingi, tunaposikia jina la mtu, tunaifikiria asili ya mtu huyo.)

 

    1.    Yesu anapotoa wito wa ulinzi kwa njia ya uwezo wa jina la Mungu, na anasema kuwa analo jina hilo hilo, hiyo inahusianaje na wazo letu kwamba jina linaakisi asili ya mtu? (Asili ya Mungu ni upendo na uwezo wake. Yesu alituonesha upendo wa Mungu kwa njia ya kujitoa kwake, na akatuonesha uwezo wa Mungu kwa ufufuo wake.)

 

     1.   Jina hili litawalindaje wanafunzi?

 

  1.    Angalia tena Yohana 17:11, na uzingatie sehemu ya mwisho. Ni kwa jinsi gani uwezo wa jina la Yesu unawasukuma wanafunzi wa Yesu kuwa na umoja? (Upendo ndio nguvu ya mwisho inayounganisha. Kwa kuwa Yesu anaomba kuhusu kuwalinda dhidi ya ulimwengu, kutokea ndani ya ukanda wa ulinzi, ukanda wa upendo, huleta umoja.)

 

  1.    Soma Yohana 17:12. Yesu aliwafanyaje wanafunzi kuwa salama kwa “kuwalinda kwa jina lako [Mungu] ulilonipa mimi [Yesu]?” (Unakumbuka kwamba hapo awali Yesu alisema katika ombi lake kuwa alimfunua Mungu kwa wanafunzi wake? Kuufunua upendo wa Mungu, kuonesha upendo wa Mungu, na kuonesha uwezo wa Mungu (kwa mfano, kwa njia ya miujiza) kuliwafanya kuwa salama. Hiyo pia ilikuwa ramani ya mustakabali wao.)

 

  1.    Soma Yohana 17:13. Uelewa kamili wa asili ya Mungu hutupatia nini? (Furaha!)

 

  1.    Soma Yohana 17:14-15. Tumejadiliana kwamba Yesu aliwapa wanafunzi wake “maneno” yaliyoufunua upendo na uwezo wa Mungu. Kwa nini ulimwengu uwachukie kwa wao kuwa na ujumbe huo? (Tunaona rejea ya “yule mwovu.” Hiki ndicho chanzo cha chuki kwa jambo lililo zuri na la kupendeza.)

 

  1.    Soma Yohana 17:16-19. Jambo gani linatutofautisha na ulimwengu? Nilipokuwa mdogo, mara kwa mara niliweza kuwabainisha washiriki wa kanisa langu kutokana na jinsi walivyovaa – walionekana wa kawaida, na si wenye mavazi ya gharama yenye urembo mwingi. Baadhi ya wanafamilia wangu walikuwa maafisa katika Jeshi la Wokovu. Mara zote waliendesha magari ya kawaida, na kamwe si magari ya kifahari. Je, hicho ndicho anachokifikiria Mungu? (Kifungu cha 17 kinatuambia kuwa tunatakaswa kwa kweli ya neno la Mungu. Nadhani hii inazungumzia jambo linalotokea ndani kuliko lile linalotokea kwa nje. Kimsingi kile kinachotokea ndani kinapaswa kuathiri cha nje.)

 

   1.    Kifungu cha 18 kinatuambia kuwa wanafunzi walitumwa ulimwenguni. Kwa nini ulimwengu unawachukia? (Lengo ni kuuongoa ulimwengu, kuwaokoa wale walio ulimwenguni dhidi ya ushawishi wa yule mwovu.)

 

 1. Ombi la Yesu kwa Ulimwengu

 

  1.    Soma Yohana 17:20. Je, hapa Yesu anauombea ulimwengu? (Nimegundua kwamba baadaye tutajadili ombi la Yesu kwa ajili ya ulimwengu. Ombi lake ni kwa wale wanaotoka ulimwenguni kwa kuuamini ujumbe wa Mungu.)

 

  1.    Soma Yohana 17:21-23. Lengo la huu umoja ni lipi? (Kwamba ulimwengu umwamini Yesu.)

 

   1.    Majuma machache yaliyopita tulijadili shambulizi la Mungu kwa umoja wa wanadamu katika Mnara wa Babeli. Msingi wa umoja wa Kikristo ni upi? (Utukufu wa Mungu na upendo. Utaona kwamba Yesu alianza kuomba kuhusu utukufu. Kifungu cha 22 kinazungumzia utukufu wetu. Sote tuna utukufu!)

 

   1.    Utukufu huu ni upi? Je, ni wa ghali sana au wa kawaida?

 

   1.    Inamaanisha nini kumpa Mungu utukufu? (Inamaanisha kumfanya afae na kutamanika. Maisha yako yanapaswa kumwakisi Mungu wako katika hali chanya. Watu wanapaswa kutaka kumjua Mungu wako kwa sababu maisha yako yanaonesha manufaa ya kuwa na uhusiano na Mungu.)

 

    1.    Inamaanisha nini kwa sisi kuwa na utukufu? (Kama mtu anataka kuwa wewe, au kuwa kama wewe, basi anakupa utukufu. Unaona jinsi jambo hili linavyofanya kazi? Neno la Mungu, kweli yake, upendo wake, vitaboresha mtazamo wako na maisha yako. Watu watataka hilo. Wanapotambua kwamba utukufu wako unatokana na uhusiano wako na Mungu, basi unampa Mungu utukufu.)

 

    1.    Ni kwa jinsi gani umoja ni sehemu ya huu utukufu? (Watu wa kawaida hawapendelei ugomvi. Mgawanyiko una kawaida ya kukanusha ukweli na upendo wa pamoja.)

 

  1.    Soma Yohana 17:24-26. Lengo la maisha yetu ni lipi? (Kumfanya Mungu ajulikane kwa watu wengine.)

 

   1.    Njia ya mwisho ya kumjua Mungu ni ipi? (Yesu anaomba kwamba tuwepo “mahali nilipo.” Tunaona hatma ya utukufu wa Yesu mbinguni!)

 

 1.   Umoja Upitao Ukomo wa Madhehebu

 

  1.    Soma Marko 9:38-40. Yesu anazungumzia nini kuhusu kuingilia kazi ya “makundi” mengine yanayomtangaza Yesu? (Anasema “Msiwakataze.”)

 

   1.    Yesu anatumia kipimo gani? (“Yeyote asiye kinyume chetu, yu upande wetu.”)

 

   1.    Unapata fundisho gani kutokana na jambo hili linapokuja suala la kufanya kazi na makanisa mengine au madhehebu mengine?

 

  1.    Angalia tena Marko 9:39. Utendaji miujiza unamaanisha nini? (Hutasema mara moja jambo baya kumhusu Yesu.)

 

   1.    Soma Mathayo 7:22-23. Hawa watenda miujiza wanawezaje kupotea? (Mungu anatumia mbinu za aina zote kuutangaza Ufalme wake. Lakini, muujiza kama muujiza hauoneshi kuwa mtu anamjua Mungu.)

 

  1.    Rafiki, utakumbuka kwamba tulipoanza kujifunza somo hili Yesu alitaarifu kuwa alimfanya Mungu ajulikane kwa wanafunzi wake. Huo ndio utume wetu – kumjua Mungu na kuwafundisha watu wengine kuujua upendo wake. Hiyo humpa Mungu utukufu pamoja na kutupatia sifa pia. Hiyo huleta umoja miongoni mwa waumini.

 

 1.    Juma lijalo: Msingi wa Umoja.