Umoja Katika Ibada

(Ufunuo 4 & 14, 2 Samweli 6, 1 Mambo ya Nyakati 15)
Swahili
Year: 
2018
Quarter: 
4
Lesson Number: 
11

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Kichwa cha habari cha somo letu kimenifanya nitabasamu. Kama kuna mahali ambapo tuna kila namna za mfarakano, basi ni kwenye ibada. Baadhi ya makanisa yana huduma za aina mbili zilizo na mtindo tofauti wa ibada, ili tu kwamba kila mtu awe na furaha. Je, ibada si jambo la kina zaidi kuliko tu mtindo? Je, wakati mwingine mtindo si kioo kionyeshacho moshi unaofuka kwa ajili ya mambo ya muhimu zaidi? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tuone kile tunachoweza kujifunza kuhusu ibada!

 

 1.     Ibada ya Kimbingu

 

  1.     Soma Ufunuo 4:8-9. Tunaona nini? (Mbingu.)

 

   1.     Ni nini ulio msingi wa kumwabudu Mungu? (Yeye “alikuwako na aliyeko na atakayekuja.”)

 

   1.     Hii inatufundisha nini kuhusu nyimbo za kusifu zinazotumia mashairi mepesi na yanayojirudiarudia?

 

  1.     Soma Ufunuo 4:10-11. Msingi wa wazee kumsifu Mungu ni upi? (Hiki ni mojawapo tu ya vifungu vingi vya Biblia vinavyosema kuwa Mungu anastahili sifa zetu kwa sababu yeye ni Muumbaji wetu.)

 

   1.     Hii inatufundisha nini kuhusu nadharia ya uibukaji? (Ni shambulio kubwa kwenye sababu ya Mungu kustahili sifa zetu.)

 

    1.     Vipi kuhusu “Uibukaji uliojengwa kwenye imani kwamba Mungu yupo na ni muumba na mtawala wa dunia,” dhana ya kwamba Mungu aliuweka uibukaji kazini na kuutumia kuumba kila kitu? (Uibukaji unategemea mambo ya asili, usemao kwamba wenye nguvu wanashinda na wanyonge wanakufa. Kama hiyo ndio kanuni ya msingi ya “uumbaji,” kwa nini haiko sawa sana na Biblia yote?)

 

  1.     Angalia tena Ufunuo 4:11. Unaposoma maneno “kwa sababu ya mapenzi yako vilikuwako, navyo vikaumbwa,” je, hiyo inaonekana kama uhusika usio na hisia? (Inatoa taswira ya Mungu kuendelea kujihusisha na maisha yetu. Mungu anaendelea kuutia nguvu ulimwengu.)

 

 1.   Ibada ya Siku za Mwisho

 

  1.     Soma Ufunuo 14:6-7. Ni mambo gani matatu tunayoambiwa tuyafanye? (Tumche Mungu, tumtukuze na kumsujudia.)

 

   1.     Kwa nini? (Tunapewa sababu mbili. Kwanza, kwa maana saa ya hukumu yake imekuja. Pili, kwa sababu yeye ni Mungu Muumbaji wetu.)

 

  1.     Soma Mwanzo 2:1-3. Uhusiano wa uumbaji unaashiria nini kuhusu kipindi cha kusujudu? (Ibada inayoakisi kazi ya Mungu Muumbaji wetu ipo kwenye “siku ya saba.”)

 

  1.     Soma Mwanzo 6:1-3 na Mwanzo 6:5-7. Mungu ametangaza nini kwenye mpango wake wa kukabiliana na dhambi? (Atawaangamiza wanadamu wadhambi kwa maji.)

 

  1.     Soma Ufunuo 14:9-11. Mungu ametangaza nini kwenye mpango wake wa kukabiliana na dhambi? (Ataiangamiza dhambi kwa moto.)

 

  1.     Unapoangalia tena Mwanzo 6:3 na Ufunuo 14:7, unaona mfanano gani kati ya gharika na moto ulivyotumika? (Mungu anahesabu muda wake. Kwenye gharika, alimwambia Nuhu muda wa watu kutubu na kumgeukia ni miaka 120. Katika mwisho wa dunia Mungu anatangaza muda ule ule wa rehema, anauita “saa ya hukumu yake.” Tofauti na ilivyokuwa kwa gharika, Mungu hatoi muda mahsusi.)

 

   1.     Unapotafakari uhusiano kati ya gharika na mwisho wa dunia yetu, tunapaswa kuzingatia nini? (Vifungu vya Ufunuo 14 vimejikita kwenye suala la ibada. Ni ama tunamcha na kumsujudia Mungu Muumbaji, au tunamwabudu “mnyama na sanamu yake.”

 

 1. Ibada ya Leo

 

  1.     Je, unadhani kwamba sasa tunaishi kwenye “saa ya hukumu yake,” sawa na miaka 120 kabla ya gharika?

 

   1.     Ikiwa jibu lako ni “ndiyo,” hiyo inazungumzia nini kuhusu aina ya ibada yako leo? (Kwanza, nitafanya ibada kwenye siku sahihi, siku iliyobainishwa wakati wa Uumbaji. Pili, tunaambiwa “tumche” Mungu “na kumtukuza.” Hebu tuyachimbue mawazo haya kwa kuangalia kile historia ya Kibiblia inachotufundisha.)

 

  1.     Soma 1 Samweli 6:1-2. Kisa kilichopo ni kwamba Wafilisti waliteka Sandulu la Agano katika pambano baina yao na Israeli. Haya yalikuwa maafa kwa Israeli, lakini pia maafa yasiyotarajiwa kwa Wafilisti. Unaweza kusoma kuhusu matatizo yote waliyoyapitia Wafilisti katika 1 Samweli 5. Matokeo yake ni kwamba Wafilisti waliamua kulirejesha. Wafilisti waliwasiliana na nani ili kufahamu namna Sanduku linavyopaswa kubebwa? (Makuhani wao wa kipagani na waaguzi wao.)

 

  1.     Soma 1 Samweli 6:7-9. Makuhani wa Wafilisti walifikia uamuzi kwamba namna bora ya kulisafirisha Sanduku ni ipi? (Kutumia gari jipya likokotwalo na ng’ombe. Lilirejea Israeli kwa njia hiyo.)

 

  1.     Soma 2 Samweli 6:1-3. Mfalme Daudi aliamua kulisafirishaje Sanduku alipoamua kulirejesha? (Alifanya vile vile walivyofanya Wafilisti.)

 

  1.     Soma Hesabu 4:4-6 na Hesabu 4:15. Je, Mungu alitoa maelekezo maalumu ya jinsi ya kulisafirisha Sanduku? (Ndiyo. Lilitakiwa kufunikwa na kubebwa na wana wa Kohathi, sehemu mahsusi ya kabila la Lawi.)

 

  1.     Soma 2 Samweli 6:4-8. Je, Daudi alikuwa anamwabudu Mungu? (Naam.)

 

   1.     Kwa nini Uza alikufa? (Kwa sababu Daudi hakutenga muda wa kujifunza maelekezo ya Mungu kuhusu jinsi ya kulisafirisha Sanduku. Matokeo yake ni kwamba baada ya Sanduku kuwekwa juu ya gari, badala ya kubebwa, ilionekana kuwa linaweza kuinamia upande mmoja.)

 

   1.     Je, Uza alikuwa na dhamira njema? (Ndiyo. Lakini, kwa umahsusi Hesabu 4:15 ilitoa onyo la kifo ikiwa mtu ataligusa Sanduku.)

 

   1.     Tunapaswa kujifunza nini kutokana na jambo hili? (Soma 1 Mambo ya Nyakati 15:13. Ibada sahihi ni ile iliyojengwa juu ya taarifa sahihi. Tunatakiwa kujifunza mapenzi ya Mungu. Hatutakiwi tu kufuata mitindo ya kipagani. Uza alikufa kwa sababu Mfalme Daudi alishindwa kujifunza maelekezo ya Mungu juu ya namna ya kulisafirisha Sanduku.)

 

  1.     Soma 2 Samweli 6:13, 1 Mambo ya Nyakati 15:1-2, 1 Mambo ya Nyakati 15:15. Daudi amejifunza nini? (Kwamba lazima Sanduku libebwe na Walawi, lisikokotwe na ng’ombe.)

 

  1.     Soma 2 Samweli 6:14-16 na 1 Mambo ya Nyakati 15:16. Unaielezeaje ibada ya Daudi? (Kwa taarifa zaidi juu ya mipango na utekelezaji, soma 1 Mambo ya Nyakati 15:17-29. Ibada hii imepangiliwa, kwa kelele na kucheza! Daudi anarukaruka. Wanapiga kelele, wanapiga tarumbeta. Ni sherehe!)

 

   1.     Umewahi kuwa kwenye ibada kama hiyo?

 

   1.     Je, hii inaonekana kuwa kinyume na ibada sahihi?

 

    1.     Ikiwa umesema, “ndiyo,” je, kuna mtu kwenye kisa chetu anayekubaliana nawe? (Mke wa Daudi, Mikali.)

 

  1.     Soma 2 Samweli 6:20. Mikali anatoa malalamiko gani juu ya mtindo wa ibada wa Daudi? (Ni ibada isiotakaswa. Ni ibada isio na adabu. Haitunzi heshima ya ofisi ya Daudi.)

 

   1.     Vipi kuhusu heshima ya Mungu? (Daudi hajavaa vizuri!)

 

  1.     Soma 2 Samweli 6:21-22. Je, Daudi anamwambia mkewe kuwa anaomba radhi kwa ibada yake isio na heshima? (Hapana. Anasema kuwa hata anapanga kutokuwa na heshima zaidi!)

 

  1.     Soma 2 Samweli 6:23. Ni nini matokeo ya ukosoaji wa Mikali juu ya mtindo wa ibada wa Daudi? (Mikali ni mgumba.)

 

   1.     Je, hili ni onyo kwa wale wanaodai mtindo wa ibada wenye utulivu na heshima?

 

   1.     Je, umewahi kuwa kwenye huduma ya ibada ambapo mazingira ni mazuri sana kwa mtu kuweza kulala? Kila kitu kinachosha, na hakuna anayeonekana kufurahia chochote?

 

   1.     Je, umewahi kuwa kwenye huduma ya ibada ambapo unatakiwa kufikia viwango fulani vya mavazi?

 

  1.     Soma 1 Mambo ya Nyakati 16:1-2 & 4. Nimesikia watu wakijenga hoja kwamba kisa hiki hakizungumzii suala la ibada. Ikiwa hakizungumzii ibada, je, ni nini hiki?

 

   1.     Unadhani kwa nini adhabu ya Mikali ni sehemu ya maelezo haya?

 

   1.     Je, umewahi kuwa kwenye huduma za ibada zilizo “tasa?” Huduma zilizokufa na zisizo na uchangamfu?

 

  1.     Rafiki, Mungu anatuita katika hizi siku za mwisho ili tumwabudu. Anatuita tumwabudu kama alivyotuamuru, katika siku inayomsheherekea kama Muumbaji! Anatuonesha kwamba kuwa naye katika uwepo wetu ndio msingi wa furaha, muziki na kucheza kusiko na vizuizi. Anatutaka tumpende kusiko na kifani na kuwa na shukrani kwa uwepo wake na kila kitu alichotutendea!

 

 1.   Juma lijalo: Mfumo wa Kanisa na Umoja