Somo la 1: Injili Kutoka Patmo

(Ufunuo 1:1-8)
Swahili
Year: 
2019
Quarter: 
1
Lesson Number: 
1

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Tuna siku za kufurahisha sana mbele yetu! Tunajifunza Kitabu cha Ufunuo. Kusema kweli, ninapendelea masomo juu ya kitabu, badala ya juu ya mada. Kati ya vitabu vya Biblia, kitabu cha Ufunuo ni mojawapo ya vitabu vinavyofurahisha sana, kinasisimua, na kutatanisha. Tuna changamoto mbele yetu! Hebu tuzame kwenye somo letu na tuone kile tunachoweza kujifunza kutoka kwenye Kitabu cha Ufunuo!

 

 1.     Neno

 

  1.     Soma Ufunuo 1:1. Nani aliye chanzo cha ujumbe wa kitabu hiki? (Inasemwa kwamba “Mungu” alitoa ufunuo kwa “Yesu Kristo,” ambaye alimpatia malaika, ambaye alimpatia Yohana.)

 

   1.     Wasikilizaji wa ujumbe huu kutoka kwa Mungu ni akina nani? (Watumishi wa Mungu. Hiyo inamaanisha kuwa kitabu hiki kiliandikwa mahsusi kwa ajili yako na mimi!)

 

   1.     Sababu ya ujumbe huu kutolewa ni ipi? (Kutuonesha “yatakayokuwako upesi.”)

 

    1.     Mungu anawezaje kusema inazungumzia masuala yatakayokuwako upesi, kwani sasa ni takribani miaka 2,000 tangu kilipoandikwa na bado Yesu hajarejea? (Kitabu cha Ufunuo hakizungumzii tu kuhusu ujio wa Yesu Mara ya Pili. Kinazungumzia mambo yaliyokuwa yanatokea na matukio yatakayoendelea kutokea. Kimsingi, tutajifunza kwamba kitabu cha Ufunuo kina historia ya kanisa la Kikristo!)

 

    1.     Kwa nini tutake kujua mambo yajayo? (Yanatupatia ujasiri.)

 

     1.   Ujasiri katika jambo gani? (Kwamba mustakabali wetu uko mikononi mwa Mungu. Miongoni mwa wale wanaomwamini Mungu baadhi yao ni wale wanaodhani kwamba anaangalia tu jinsi mambo yanavyotokea. Hajihusishi nayo kwa undani zaidi. Hii inatuambia kwamba Mungu anafahamu mambo yajayo, na anataka kushiriki nasi mambo hayo. Hii inatupatia imani na ujasiri kwa Mungu.)

 

  1.     Soma Ufunuo 1:2. Yohana anatuambia mambo mengi kwa kiasi gani? (Habakizi jambo lolote aliloliona.)

 

   1.     Inaonekana kuna ujumbe wa aina mbili kwenye kitabu cha Ufunuo: “neno la Mungu na ushuhuda wa Yesu.” Unadhani hii inamaanisha nini? (Ushuhuda unahusianisha uzoefu uliokusudiwa kutuhamasisha. Hivyo, kwa namna fulani kitabu cha Ufunuo sio tu kauli ya Mungu Baba, bali kinathibitishwa na Yesu, Mwana.)

 

  1.     Soma Ufunuo 1:3. Baraka nyingi kiasi gani zipo kwa ajili yetu kwenye mfululizo wa masomo haya? (Ninaona angalao baraka za aina mbili. Tunabarikiwa kwa kusoma tu kile kitakachotokea. Tunabarikiwa mara mbili kwa kuwa makini zaidi na kuenenda kile tunachokisoma.)

 

   1.     Unataka baraka za aina ngapi? (Ninataka baraka zote ninazoweza kuzipata! Hivyo, hebu tusome kitabu cha Ufunuo kwenye mfululizo wa masomo haya, na tuone kama, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, tunaweza kukielewa. Kisha, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, hebu tuweke kivitendo maishani mwetu kile tunachojifunza.)

 

 1.   Makanisa Saba

 

  1.     Soma Ufunuo 1:4-5. Ni nani anayeandika sasa? (Mtume Yohana.)

 

   1.     Anamwandikia nani? (Makanisa saba yaliyopo Asia. Hii inathibitisha, miongoni mwa mambo mengine, kwamba Yohana anawaandikia watu wa kipindi chake. Hiyo inaonesha kuwa kitabu cha Ufunuo kina ujumbe, angalao kwa kiasi fulani, juu ya mambo yatakayotokea hivi karibuni. Baadaye tutajifunza maana kamili ya haya makanisa.)

 

   1.     Nani ambaye ni “yeye aliyeko, na aliyekuwako, na atakayekuja?” (Lazima hii iwe inamzungumzia Mungu Baba kwa sababu Yesu anatajwa baadaye kidogo. Mungu anaishi nyakati zote.)

 

   1.     Mungu anataka tuwe na nini? (“Rehema na amani.” Je, ungependa kuwa na imani zaidi maishani mwako?)

 

   1.     Nani mwingine anatusalimia? (“Roho saba” mbele ya kiti cha enzi [cha Mungu].”)

 

    1.     Hawa roho saba ni akina nani? (Hawa “roho saba” pia wanaweza kutafsiriwa kama “Roho wa mara saba.” Katika Ufunuo 5:6 tunasoma juu ya Yesu (“Mwana-Kondoo” “aliyechinjwa”) mwenye “macho” “ambao ni Roho saba za Mungu zilizotumwa katika dunia yote.” Hii pia inaweza kutafsiriwa kama “Roho wa mara saba.” Kwangu hii inaonekana kuwa huyu ni Roho Mtakatifu. Hadi kufikia hapa, bado hatujapokea salaam kutoka kwa Roho Mtakatifu, hivyo ninaelekea kudhani kwamba huyu ni Roho Mtakatifu ambaye pia anatupatia salaam.)

 

   1.     Hatimaye tunayo salaam kutoka kwa Yesu, ambaye anaitwa “shahidi aliye mwaminifu.” Kwa nini Yesu anaitwa “shahidi?” (Utakumbuka kwamba hapo awali tuliona kwamba kitabu hiki ni “ushuhuda” kutoka kwa Yesu, kitendo kinachoonekana kama shahidi. Yohana aliishi na Yesu. Maisha ya Yesu hapa duniani yalithibitisha asili ya Mungu wetu Baba.)

 

    1.     Vipengele gani vingine vya Yesu vinabainishwa? (Kwamba alikishinda kifo, anatawala dunia, anatupenda, na ametuweka huru dhidi ya dhambi kwa kafara yake.)

 

  1.     Soma Ufunuo 1:6. Hadhi yetu mpya mbele ya Mungu ni ipi? (Sisi ni “ufalme” na pia ni “makuhani.”)

 

   1.     Unadhani Biblia inamaanisha nini inapotuita “ufalme?” (Yesu ni Mfalme wetu mshindi. Yeye ni “mtawala wa falme za duniani.” Sasa tumeunganishwa naye katika ufalme wake.)

 

   1.     Ni kwa namna gani sisi ni makuhani? (Hili ni badiliko la muhimu sana. Badala ya ukuhani wa Walawi, kila mmoja wetu sasa ni kuhani.)

 

    1.     Hii ina matumizi gani maishani mwetu kivitendo? (Makuhani walimwendea Mungu hekaluni. Sasa sote tunaweza kumwendea Mungu kwa sababu ya kile ambacho Yesu ametutendea msalabani.)

 

   1.     Lengo la kutufanya sote kuwa makuhani ni lipi? (Tunatakiwa kumtumikia Mungu.)

 

    1.     Makuhani walimtumikiaje Mungu katika mfumo wa hekalu?

 

    1.     Ikiwa sisi sote ni makuhani, je, jukumu hili linabadilika kwa namna yoyote ile? (Makuhani walikuwa daraja kati ya Mungu na watu. Walifundisha habari za Mungu, waliendesha mfumo wa hekalu, na walikuwa sehemu ya kuwasaidia watu kutakaswa dhambi zao. Kazi yote hii, katika mfumo ulioboreshwa, ipo kwa kila mmoja wetu leo.)

 

    1.     Unadhani kipengele kipi ni cha muhimu zaidi kwa sisi kuwa makuhani leo? (Kumwendea Yesu moja kwa moja. Sehemu nyingine ya muhimu ni kusawazishwa kwa mfumo. Sasa sote tunastahili kuwa makuhani. Tafakari athari chanya ya jambo hilo!)

 

  1.     Soma Ufunuo 1:7. Kwa nini jambo hili liko kwenye utangulizi, sura ya kwanza ya kitabu cha Ufunuo? (Kitabu kinazungumzia tukio hili! Bwana wetu anakuja!)

 

   1.     Litakuwa tukio la aina gani? (Sio tukio binafsi. “Kila jicho” litamwona. Isipokuwa kama utamwona Yesu akirejea, basi huyo hatakuwa yeye. Usikubali kauli zozote kutoka kwa mtu wa tatu (mtu mwingine) kuhusu kuwasili kwa Yesu.)

 

   1.     Inamaanishwa nini kusema kwamba wale waliomtesa Yesu watamwona? (Zungumzia juu ya kutambua kwamba umefanya kosa kubwa! Wale walio kiini cha mateso na kifo chake watamwona akija katika utukufu!)

 

   1.     Kwa nini tutaomboleza? Unaweza kutafakari tukio lenye utukufu zaidi ya hilo? (Hii inafuata hoja ya wale waliomtesa Yesu wale wanaomkataa Yesu wataiona siku hii kuwa siku ya huzuni kuliko siku zote tangu wazaliwe.)

 

  1.     Soma Ufunuo 1:8. Yesu amesema kwamba anarejea kwa utukufu. Kwa nini katika sehemu inayofuata Yohana anaandika kuwa Mungu ni mwanzo na mwisho (“Alfa na Omega”) na kwamba mara zote yupo na mara zote atakuwepo?

 

   1.     Utaona kwamba kauli ile ile ya “yeye aliyeko, na aliyekuwako, na atakayekuja” ilitolewa kwenye Ufunuo 1:4. Kwa nini inarudiwa? Mungu anamwambia nini Yohana na sisi? (Kitabu cha Ufunuo kinahusu ushindi wa mwisho wa Mungu dhidi ya dhambi. Tunayo haya madai ya ushindi (ujio wa Mara ya Pili) na ya uwezo mkubwa wa kutupatia ujasiri kwamba Mungu ana uwezo wa kutenda kile anachotabiri kwamba atakifanya. Anatutaka tutumaini kile tunachotaka kukisoma kwenye kitabu hiki.)

 

   1.     Angalia uhusiano kati ya kauli mbili “Alfa na Omega” na “yeye aliyeko, na aliyekuwako, na atakayekuja.” Hii inaendanaje na dhana ya kwamba Mungu ana uwezo wa kutenda kile anachokitabiri? (Mungu ndiye wa kwanza na wa mwisho kusimama. Kama kuna mtu yeyote mwenye uwezo wa kupangilia siku zijazo, Mungu anao uwezo huo.)

 

  1.     Rafiki, wewe ni kuhani wa Mungu! Yesu anatuambia mambo yajayo, anatuambia kwamba ameshinda pambano dhidi ya uovu. Anatuambia kuwa ana mamlaka yote. Mungu anatutaka tuhamasike! Anatutaka tuwe na ujasiri naye na tuwe na ujasiri wa mambo yajayo. Je, umehamasika?

 

 1. Juma lijalo: Miongoni mwa Viango.