Somo la 6: Watu wa Mungu Waliotiwa Muhuri

(Ufunuo 7)
Swahili
Year: 
2019
Quarter: 
1
Lesson Number: 
6

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Tulipojifunza “Mihuri Saba” juma lililopita, je, uligundua kwamba tuliukosa mhuri mmoja? Hiyo ni kweli, Ufunuo 6 iliishia na mhuri wa sita! Mhuri wa saba unapatikana katika Ufunuo 8. Tutajifunza Ufunuo 8 juma lijalo. Ufunuo 6 ilimalizikia na ishara za maana sana zinazotokea mbinguni. Kinachotokea kwenye sayari na anga kinawafanya viongozi wa dunia watambue kwamba Yesu anakuja na “siku ya ghadhabu” inaanza. Ufunuo 8 inaanzisha mjadala wa kipindi cha kutisha hapa duniani. Sasa je, Ufunuo 7 inahusu nini? Kama tutakavyojifunza juma hili, inawahusu wale waliookolewa! Utagundua kwamba kuna mambo ya muhimu katika Ufunuo 7 ambayo ni magumu kuyaelewa. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tuone kile tunachoweza kujifunza!

 

  1.     Kutiwa Mhuri Dhidi ya Madhara

 

    1.     Soma Ufunuo 7:1-3. Jambo gani linataka kutokea duniani? (Madhara! Sura zinazofuata katika kitabu cha Ufunuo zinajadili juu ya nyakati za kutisha.)

 

      1.     Nani anayeshughulikia nyakati za mambo ya kutisha? (Mungu. Malaika wa Mungu wanaonekana “kusitisha” nyakati za kutisha.)

 

      1.     Kwa nini nyakati za kutisha zinazokuja zinacheleweshwa hadi “mhuri wa Mungu aliye hai” unapotiwa kwenye “vipaji vya nyuso vya watumwa wa Mungu wetu?” (Mhuri unatusaidia au kutulinda kwa namna fulani. Vinginevyo, ucheleweshwaji hautakuwa na maana yoyote.)

 

        1.     Je, unadhani kwamba walio na mhuri wanakingwa dhidi ya madhara yote?

 

      1.     Mhuri unatiwa wapi? (Kwenye paji la uso.)

 

        1.     Kwa nini? (Mhuri unaakisi uamuzi wa kuwa mtumishi wa Mungu.)

 

    1.     Soma Ufunuo 7:4-8. Hawa watu 144,000 ni akina nani? (Ni watumishi wa Mungu wanaoonekana kuhusianishwa kwa namna fulani na makabila ya Israeli.)

 

    1.     Soma Ufunuo 7:9. Je, hawa pia wametiwa mhuri? (Ufunuo 7:3 inabainisha kuwa mchakato wa kutia mhuri unataka kuanza. Ufunuo 7:4 inawaelezea waliotiwa mhuri “kwenye makabila yote ya Israeli.” Kisha Ufunuo 7:9 inawaelezea watu kutoka kwenye “kila taifa, kabila, jamaa, na lugha.” Jinsi jambo hili linavyoandikwa inaashiria kwamba wote wametiwa mhuri, lakini jambo hili ni lenye mjada.)

 

    1.     Kwa nini utiwaji mhuri kwa “makabila ya Israeli” unaelezewa tofauti na utiwaji mhuri kwa mataifa mengine yote? Kwa nini wale waliotiwa mhuri kutoka kwenye mataifa mengine yote ndio pekee wanaoelezewa kuwa “wamevaa mavazi meupe?” (Njozi ya Yohana inahusu sehemu mbili tofauti. Watu 144,000 wapo duniani na kundi kubwa lisilo na idadi lipo mbinguni. Lugha iliyotumika kwenye Ufunuo 7:3 inaashiria kwamba watu 144,000 wako hai kabla tu ya ufunguzi wa mhuri wa saba! Kundi la watu lisilo na idadi linaonekana kuwa ni wale waliookolewa katika historia ya dunia. Yumkini uhusiano na makabila kumi na mawili si wa muhimu, na watu 144,000 wako ndani ya hilo kundi lisilo na idadi.)

 

      1.     Je, idadi ya watu 144 inaonekana kama jambo lisilo la kawaida kwako? (Kwenye hiki kitabu cha ishara, inaonekana kuwa ni jambo la kiishara.)

 

  1.   Tangazo!

 

    1.     Soma Ufunuo 7:10-12. Ni kwa jinsi gani watu wote wanaokolewa? (Ni kwa uwezo wa Mungu. Si kwa matendo yetu wenyewe.)

 

      1.     Unadhani tangazo hili linahusiana kivyovyote vile na kutiwa kwao mhuri?

 

      1.     Soma Ufunuo 4:11 na Ufunuo 5:12. Sababu za hizo kauli za awali za kumtukuza Mungu ni zipi? (Mungu kama Muumbaji na kafara ya Yesu msalabani.)

 

        1.     Jambo gani linakumbushia matukio yote hayo mawili? (Sabato. Mungu aliifanya Sabato kuwa takatifu kwa kuihusianisha na Uumbaji wake (Mwanzo 2:2-3), na Yesu alitunza pumziko la Sabato baada ya kuteswa kwake. Mathayo 28:1-2.)

 

        1.     Je, kuitunza Sabato kuna uhusiano wowote ule na mhuri?

 

    1.     Soma Ezekiel 9:3-6. Ezekieli anaelezea aina fulani ya mchakato wa “kutia mhuri” kwenye paji la uso. Nani anayechukua mhuri unaowaepusha kuangamizwa? (Watu “wanaougua na kulia kwa sababu ya machukizo yanayofanyika.”)

 

      1.     Ikiwa maelezo ya Ezekieli yanasaidia katika kufanya kwetu uamuzi, inaonekana wale waliotiwa mhuri wanaiangalia kazi ya Mungu kwa namna ya pekee kabisa. Wanasheherekea Uumbaji wake, ushindi wake msalabani and wanachukia sana kitendo cha watu wanaofanya mambo ya machukizo kumkataa Mungu.)

 

        1.     Hii inanifanya nikumbuke kwamba juma hili Jimbo la New York limepiga kura kuruhusu utoaji mimba kwa watoto ambao bado hawajafikia umri wa kuzaliwa! Je, unahuzunika na kuomboleza juu ya jambo hilo? Unakumbuka mwanao alivyokuwa anaonekana baada ya kuzaliwa?

 

    1.     Soma Ufunuo 7:13-14. Unaliwekaje jibu la Yohana kwa lugha ya kisasa? (Kwa nini unaniuliza? Unajua jibu la swali lako.)

 

      1.     Tunachukulia kwamba wazee ni washauri wa Mungu. Kwa nini mmoja wao aulize swali kama hilo? (Alitaka Yohana alifikirie. Alitaka tulitafakari.)

 

      1.     Unafahamu nini kuhusu hili kundi la watu wasio na idadi? (“Wametoka katika dhiki iliyo kuu” na wanaokolewa kwa neema pekee.)

 

    1.     Soma Ufunuo 12:17. (Soma sura yote kama unataka kupata mtazamo mpana wa jambo hili.) Je, sisi ndio “wazao waliosalia?” (Ndiyo!)

 

      1.     Angalia tena Ufunuo 7:14. Unadhani hii “dhiki kuu” ni ipi? (Ni pambano kati ya Yesu na Shetani hapa duniani. Kwa umahsusi, ni “vita” ambavyo Shetani amekuwa akivifanya dhidi ya Wakristo tangu Yesu arejee mbinguni. Angalia Ufunuo 12:17. Huu ni ushuhuda kwamba kundi la watu lisilo na idadi ni Wakristo walioishi baada ya msalaba. Lakini, pendekezo bora zaidi ni kwamba watu 144,000 ni sehemu moja tu ya kundi kubwa la watu wasio na idadi. Tofauti ni kwamba wale 144,000 tu ndio walioishi kipindi cha kabla ya ufunguzi wa mhuri wa saba.)

 

  1. Matokeo

 

    1.     Soma Ufunuo 7:15. Kundi la watu wasio na idadi linaishi wapi? (“Mbele ya kiti cha enzi.”)

 

      1.     Soma Ufunuo 21:1-4. Yesu ataishi wapi siku zijazo? (Duniani.)

 

      1.     Tunaishi wapi? (Duniani na katika Yerusalemu Mpya!)

 

        1.     Kwa nini? (Kwa sababu sisi ni mashahidi tulio hai kwa Yesu kumshinda Shetani na dhambi!)

 

      1.     Inamaanisha nini kwenye Ufunuo 7:15 kwamba Mungu “atatanda hema yake” juu yetu? (Soma Ufunuo 7:16. Tunakingwa dhidi ya njaa, kiu, na joto.)

 

        1.     Unadhani kwa nini nguvu kubwa imeelekezwa kwenye joto? (Soma Ufunuo 16:8. Inawezekana ni kwa sababu katika eneo hili la dunia, joto lilikuwa tatizo mahsusi. Inawezekana ni kwa sababu mojawapo ya mapigo ya mwisho ni jua kuwaunguza watu.)

 

    1.     Soma Ufunuo 7:17 na usome tena Ufunuo 21:4. Kitu gani hakipo katika nchi mpya? (Huzuni na maombolezo!)

 

    1.     Rafiki, je, unataka kuwepo pale? Je, unataka kuishi bila wasiwasi na huzuni? Je, unataka kuishi katikati ya milki ya dunia? Kwa nini usioshe vazi lako kwenye damu ya Mwana-Kondoo? Kwa nini usifanye hivyo kwa kubatizwa na kumtumaini Yesu kwa ajili ya wokovu wako?

 

      Juma lijalo: Baragumu Saba.