Somo la 8: Shetani, Adui Aliyeshindwa

(Ufunuo 12)
Swahili
Year: 
2019
Quarter: 
1
Lesson Number: 
8

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Nachukia kushindwa! Wanasheria hawatakiwi kuchukulia kesi zao kama jambo binafsi. Badala yake, wanasheria wanatakiwa kutenda kazi yao kwa ustadi mkubwa wa kuwasilisha ushahidi, na hakimu afanye uamuzi nani yuko sahihi. Kwa kuwa takribani kesi zangu zote zinahusisha utetezi wa uhuru wa dini au uhuru wa mawazo ya wateja wangu, ninachukulia suala la ushindi au kushindwa kama jambo binafsi. Kwa nini? Kwa kuwa matokeo ya kesi sio tu kwamba yanamwathiri mteja wangu, bali pia yanaathiri uhuru wa watu wengine wengi. Hiyo ni sababu moja ya kwa nini ninafurahi ninapokuwa mshindi inapokuja hatima ya pambano la uhuru wa dini! Shetani atashindwa! Hebu tuzame kwenye Biblia yetu na tujifunze kushindwa huko!

 

 1.    Mwanamke Aliyevikwa Jua

 

  1.    Soma Ufunuo 12:1. Mwanamke huyu ni nani? Katika historia, tunawaona wapagani walioliabudu jua. Je, mwanamke huyo ni mwabudu jua? (Soma Ufunuo 19:7, Ufunuo 21:9, na Wimbo Ulio Bora 6:10. Mwanamke huyu analiwakilisha kanisa, anawawakilisha watu wa Mungu. Kanisa ni bibi harusi wa Mungu. Agano la Kale lina rejea nyingi za watu wa Mungu kufananishwa na mke wake [Mungu].)

 

  1.    Soma Ufunuo 12:2 na Ufunuo 12:5-6. Mwanamke huyu anamzaa nani? (Yesu!)

 

   1.    Mwanzoni jambo hili linaweza kuonekana kama lina vipengele vingi: sisi ni bibi harusi wa Yesu na pia mama wa Yesu. Lakini, hebu angalia jambo hili kwa ukaribu zaidi. Ikiwa Kanisa la hapa duniani ni bibi harusi wa Mungu, na Yesu alizaliwa na mwanamke aliyeitwa Mariamu, basi Mungu Baba na Yesu Mwana wanaendana na maelezo haya kikamilifu kabisa.)

 

 1.   Joka Mwekundu Mwenye Pembe na Vilemba

 

  1.    Soma Ufunuo 12:3 na Ufunuo 12:7-9. Joka huyu ni nani? (Ufunuo inamwita kuwa Shetani.)

 

  1.    Joka huyu ni mkubwa na ana vichwa saba. Kwa nini vichwa saba? Tuna makanisa saba, mihuri saba, vinubi saba, na Sabato ya siku ya saba. Kwa nini Shetani ana vichwa saba? (Katika mambo mengi Shetani anamuiga Mungu. Ana ubandia wa kanuni nyingi na mali za Mungu.)

 

  1.    Soma Ufunuo 12:4. Katika masomo yaliyopita mara nyingi ninazungumzia juu ya ishara za Mungu katika anga na sayari zake. Je, hizi ni nyota halisi? (Hapana. Kimantiki hii inaeleweka kuwazungumzia malaika waliotumika mbinguni na si nyota halisi. Weka hili akilini mwako tunapojadili mambo yanayojitokeza kwenye anga na sayari zake.)

 

   1.    Tafakari jambo hili kidogo. Wewe na mimi tulizaliwa dhambini. Asili yetu ni ya dhambi. Malaika wa mbinguni waliumbwa wakiwa wakamilifu. Asili yao ilipaswa kuwa ya haki. Shetani ni mwerevu, mjanja na mdanganyifu kiasi gani? (Huenda hiyo ndio sababu ana vichwa “saba” – kuakisi werevu wake.)

 

    1.    Unamfahamu mtu aliyekuwa mwerevu sana, lakini kutokana na maisha ya dhambi alionekana kupoteza werevu huo? Unawafahamu watu ambao hisia zao ovu zinawafanya watende mambo ya kipumbavu? (Ubashiri wangu ni kwamba Shetani amepoteza baadhi ya werevu wake. Hisia zake ovu zinaweza kuwa zinatawala mara nyingi.)

 

 1. Joka Mshtaki

 

  1.    Soma Ufunuo 12:10. Shetani anakufanyia nini? (Anakushtaki.)

 

   1.    Je, mashtaka yake ni ya kweli? (Kuna uwezekano mkubwa kwamba ni ya kweli.)

 

   1.    Kifungu hiki kinasema kuwa Shetani anakushtaki mbele ya Mungu, je, Shetani pia anakushinda kwa dhambi zako ulizozitubu?

 

  1.    Soma Ufunuo 12:11. Yesu anakufanyia nini? (Anaondoa dhambi zetu kwa kafara yake pale msalabani. Toa madai haya pale Shetani anapojaribu kukushinda!)

 

   1.    Sehemu ya mwisho ya Ufunuo 12:10 inasema kuwa Shetani “ametupwa chini.” Tulishindaje? (Mungu alishinda. Lakini, sisi pia. Kipengele kimoja cha ushindi huu ni kwamba “tumemshinda” kwa neema na kipengele kingine ni “neno la ushuhuda wao.”)

 

    1.    Neno la ushuhuda wao inamaanisha nini? (Ushuhuda ni kutoa uthibitisho wa jambo fulani. Tunachokisema na kukitenda huthibitisha upande wa Mungu wa pambano.)

 

   1.    Angalia mtazamo wa wale walioshinda: hawayapendi maisha yao sana hata kufa. Kiuhalisia hii inamaanisha nini? (Wanamshuhudia Yesu hata kama kwa kufanya hivyo wanayahatarisha maisha yao.)

 

    1.    Linganisha na mtazamo wako. Je, unaepuka kusimama kwa ajili ya Yesu kwa sababu kwa kufanya hivyo kunaweza kuathiri hadhi yako, kazi yako, au hali yako ya starehe?

 

  1.    Soma Ufunuo 12:12. Je, pambano limekwisha? Je, sasa tunaishi mahali pasipo sahihi? (Mbingu zinafurahia kwa Shetani kuondolewa, lakini alihamia kwenye dunia yetu na anapambana vilivyo.)

 

  1.    Soma Ufunuo 12:13. Ni jambo gani la kwanza analolifanya Shetani baada ya kutupwa duniani? (Kumwandama mwanamke aliyemzaa mtoto.)

 

   1.    Hiyo inamaanisha nini? (Soma tena Ufunuo 12:5. Hiki ndicho tulichojifunza hapo awali. Mwanamke ni kanisa la Mungu, watu wake. Mtoto ni Yesu.)

 

  1.    Soma Ufunuo 12:14-16. Hiki ni kipindi kile kile ambacho tulikijadili hapo awali. Je, joka anamwangamiza mwanamke? (Hapana.)

 

   1.    Kwa nini haangamizwi? (Alipewa “mabawa” na alisaidiwa na “nchi.”)

 

   1.    Unadhani hiyo inamaanisha nini? (“Mabawa” inaonekana kama ni msaada usio wa kawaida. “Nchi” inaonekana kama vile alipata msaada kwa njia ya kijiografia. Kama ambavyo mabawa yalivyomchukua na kumpeleka nyikani, vivyo hivyo lazima hii pia itakuwa eneo salama kijiografia.)

 

  1.    Soma Ufunuo 12:17. Utorokaji huu unamfanya joka ajisikieje? (Amekasirika.)

 

   1.    Matokeo ya hasira hii ni yapi? (Anajiingiza kwenye vita dhidi ya watu wa Mungu.)

 

   1.    Je, unakabiliana na magumu? Vita ya Shetani dhidi ya watu wa Mungu inakuathirije?

 

  1.    Hebu tuangalie tena sehemu ya mwisho ya Ufunuo 12:17. Je, umejiuliza kama wewe ni sehemu ya watu wa Mungu?

 

   1.    Kifungu hiki kinawaelezeaje watu wa Mungu? (Wanazishika amri za Mungu na kuwa na ushuhuda wa Yesu.)

 

    1.    Je, rejea ya kuzishika amri za Mungu inamaanisha kuwa watu hawa ni wakamilifu? (Kwa kuwa sisi sote si wakamilifu, lazima imaanishe kwamba wanauchukulia utii kwa Mungu kwa dhati.)

 

    1.    Inamaanisha nini “kuwa na ushuhuda wa Yesu?”

 

  1.    Soma Ufunuo 19:10. Kifungu hiki kinasema kuwa “ushuhuda wa Yesu ndio roho ya unabii.” Mara kwa mara nimeona vifungu hivi viwili vikihusianishwa na kisha hitimisho kutolewa kwamba ikiwa kanisa lako lina nabii, basi unastahili. Je, hitimisho hilo lina mantiki? Vipi kama nabii wako alifariki miaka 100 iliyopita na bado Yesu hajarudi? Je, hili linapaswa kueleweka kumaanisha kwamba unang’ang’ania roho ya huyo nabii mmoja?

 

  1.    Soma Yoeli 2:30-31. Unabii huu wa Yoeli unahusisha kipindi gani? (Wakati wa mwisho.)

 

  1.    Soma Yoeli 2:28-29. Hivi ni vifungu viwili vinavyotangulia vifungu tulivyovisoma hapo juu. Yoeli anatuambia nini juu ya Roho kwa kuzingatia unabii wa nyakati za mwisho? (Mungu atamimina Roho wake “kwa watu wote.” Nabii mmoja anaweza kuwa sehemu ya utimilifu, lakini ikiwa unadhani nabii mmoja anatosha, unawapuuza Yoeli na Paulo. Angalia, kwa mfano, 1 Wakorintho 14:1 ambapo Paulo anafundisha kwamba watu wengi wanapaswa kuwa na karama ua unabii.)

 

  1.    Hebu turejee nyuma na tuangalie kwa mara nyingine tena Ufunuo 12:17. “Jambo kuu” lilikuwa ni lipi katika kipindi cha maisha ya wanafunzi kumi na wawili baada ya kifo cha Yesu? (Swali lilikuwa ni kama kweli Yesu alikuwa Masihi? Je, ni Mungu? Je, aliishi maisha makamilifu, akafa kwa ajili yetu, na kufufuka katika uzima wa milele ili kuhudumu kwa niaba (ajili) yetu?)

 

   1.    Ikiwa hilo ndilo jambo kuu, je, hiyo inaashiria kwamba maana ya kuwa na “ushuhuda wa Yesu” ni ipi? (Hiyo inajielekeza kwenye neema – kuyaosha mavazi yetu kwenye damu ya Mwana-Kondoo. Watu ambao Shetani anawageuzia ghadhabu yake ni wale wanaozichukulia amri za Mungu kwa dhati na kumtegemea Yesu kwa ajili ya wokovu wao.)

 

   1.    Je, unapaswa kuomba ili Roho Mtakatifu ashuke kwa uwezo mkuu na kuwajaa washiriki wote wa kanisa lako?

 

  1.    Rafiki, je, ungependa kuhesabiwa na kuwa miongoni mwa watu wa Mungu? Kwa nini usifanye uamuzi leo, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, kujitahidi kuishi kwa kufuata amri za Mungu na kuliita jina la Yesu kwa ajili ya wokovu wako? Mwombe Roho Mtakatifu akujazie uwezo wake!

 

 1.   Juma lijalo: Shetani na Washirika Wake.