Mapigo Saba ya Mwisho

Swahili
(Ufunuo 15-16)
Year: 
2019
Quarter: 
1
Lesson Number: 
11

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Je, unampenda Mungu? Je, una shukrani kwa kile alichokutendea wewe na wale unaowapenda? Somo letu juma hili linabainisha upande wa pili wa spektra. Tunaona kwa undani mkubwa kinachowatokea wale wanaomchukia Mungu na kuwadhuru watakatifu wake. Ni jambo la kutisha kuanguka mikononi mwa Mungu anayeshughulika na haki! Hebu tuzame kwenye kitabu cha Ufunuo na tujifunze zaidi!

 

 1.    Malaika Saba

 

  1.    Soma Ufunuo 15:1. Ni wapi tulipowaona malaika saba hapo awali? (Tumejifunza kwamba malaika saba “wanasimama mbele za Mungu” katika kiti chake cha enzi mbinguni. Ufunuo 8:2. Tumewaona malaika saba mara kwa mara kwenye masomo yetu: kwa makanisa saba (Ufunuo 1:20), baragumu saba (Ufunuo 8:6), na sasa mapigo saba ya mwisho.)

 

   1.    Kwa nini hayo ni “mapigo ya mwisho? (“Maaana katika hayo ghadhabu ya Mungu imetimia.”)

 

    1.    Je, unaona ajabu kwamba Mungu anashusha ghadhabu yake kwa watu? Kwani yeye si Mungu mwenye upendo?

 

  1.    Soma Ufunuo 15:2. Kundi hili ni la akina nani? Je, kundi hili ndilo walengwa wa mapigo ya hasira? (Utakumbuka kwamba tulipojifunza Ufunuo 7 tulijifunza kuwa Watu wa Mungu walikuwa wametiwa mhuri, na miongoni mwa kundi hilo ni lile la watu 144,000. Katika Ufunuo 14 tunaona rejea nyingine ya watu waliotiwa mhuri, lakini mara hii ni watu 144,000 pekee. Ufunuo 4:6 inatuambia kuwa kuna “bahari ya kioo” mbele ya kiti cha enzi cha Mungu mbinguni. Kutokana na hili tunajifunza kwamba taswira ya wale ambao wamekuwa waaminifu kwa Mungu ipo mbinguni. Hawatakuwa na haja ya kukabiliana na mapigo!)

 

  1.    Soma Ufunuo 15:3-4. Waliookolewa wanafanya nini mbinguni? Je, hapa ndipo wanapopata wazo la kwamba tuna vinubi mbinguni?

 

   1.    Unadhani ujumbe wao mkuu ni upi?

 

   1.    Shauku yangu kubwa ipo kwenye lugha iliyotumika ya “Ni za haki, na za kweli, njia zako.” Tunakaribia kujifunza juu ya adhabu ya kutisha inayotolewa. Unadhani watu wa Mungu wanafikiria nini juu ya haki ya jambo hili? (Wanakubaliana na Mungu.)

 

 1.   Chimbuko la Mapigo Saba

 

  1.    Soma Ufunuo 15:5-6. Mapigo haya yanawaangukia akina nani? (Kwa kuwa mapigo haya yanatimiza ghadhabu ya Mungu (Ufunuo 15:1) kimantiki yanawaangukia waovu. Ikiwa Yohana anatupatia mpangilio wa muda, basi wenye haki tayari wapo mbinguni. Bila kujali kama huu ni mpangilio wa muda au la ni jambo tulilolijadili juma lililopita. Wakati mwingine Yohana anatuonesha mbingu kwa uchache tu na haidhamirii kuwa mpangilio wa muda.

 

   1.    Kwa nini malaika saba wamevikwa mavazi ya kitani? Kwa nini Yohana anaelezea mwonekano wao? (Fikiria kwamba umekuwa ukikabiliana na dhambi wakati wote. Fikiria kwamba ulishuhudia mateso ya Yesu na wafuasi wake – mateso ambayo waovu wameyasababisha. Kumalizika kwa pambano hili inaweza kukufanya ujivike mavazi kwa ajili ya kujibu pigo la mwisho.)

 

  1.    Soma Ufunuo 15:7-8. Tofauti na moshi, unaweza kufikiria kwa nini hapakuwepo na mtu aliyeweza kuingia ndani ya hekalu mbinguni? (Pendekezo moja ni kwamba upatanisho wa Yesu, Kuhani wetu Mkuu aliyeelezewa katika kitabu cha Waebrania umefikia ukomo. Uamuzi wote umekwishafanywa.)

 

   1.    Soma Kutoka 19:18. Hii inaashiria maelezo gani mbadala? (Moshi unawakilisha utukufu na uwezo wa Mungu kwa namna ya hatari sana. Wakazi wa mbinguni wanafahamu vizuri zaidi ya kutembelea sasa hivi Mungu anapoanzisha mapigo saba ya mwisho.)

 

 1. Mapigo Saba

 

  1.    Soma Ufunuo 16:1-2. Je, hii inakukumbusha juu ya jambo lolote uliloliona hapo kabla kwenye Biblia? (Soma Kutoka 9:8-9. Pigo kama hilo lilipelekwa Misri. Utaona kwamba pigo hili limo ndani ya mipaka ya nchi na haliwaathiri wanyama.)

 

   1.    Nani anayeteseka kutokana na pigo hili? (Wale wenye alama ya mnyama.)

 

  1.    Soma Ufunuo 16:3. Je, kuna mfanano wowote na mapigo ya Misri? (Soma Kutoka 7:19 kwa ajili ya mlinganisho.)

 

   1.    Kitu gani kimelengwa hapa? (Bahari. Kumbuka kwamba pigo la kwanza liliilenga nchi.)

 

   1.    Aina gani mahsusi ya damu inahusika? (Damu ya mfu. Matokeo yake ni kwamba kila kitu chenye uhai kinakufa.)

 

   1.    Tafakari ukubwa wa maafa hayo. Hilo litaathirije maisha ya kila siku?

 

  1.    Soma Ufunuo 16:4-6. Kitu gani kimelengwa hapa? (Maji yote yaliyosalia: mito na chemchemi.)

 

   1.    Tatizo gani halisi lililetwa na pigo hili? (Hakuna maji ya kunywa. Hii inalenga maji baribi (maji yote tofauti na yale ya bahari.))

 

   1.    Tofauti na mapigo ya awali, haki ya mapigo haya inaelezewa kwa umahsusi. Soma Mambo ya Walawi 7:26-27, Mambo ya Walawi 17:11, na Matendo 21:25. Unaweza kuelezea sababu ya Mungu kutoa pigo hili? Kuna haki gani ya kutoa pigo? (Kula damu kumezuiliwa kimahsusi katika Agalo la Kale na Jipya kwa kuwa uhai uko kwenye damu, na damu inatuokoa kutoka dhambini. Watu hawa ni tofauti na Yesu. Yesu alimwagika damu yake ili tupate uzima. Watu hao wamekuwa wakiondoa uhai. Hivyo ni wanywa damu. Wako nje kabisa ya wokovu.)

 

  1.    Soma Ufunuo 16:7. Madhabahu imeingiaje kwenye taswira hii? Hakuna chochote kwenye sura hii kilichoizungumzia. (Damu ya kafara ilimwagika chini ya madhabahu hekaluni. Mambo ya Walawi 4:7. Hivyo, kiishara, madhabahu yana maslahi ya pekee kwenye damu. Inaidhinisha matumizi haya ya damu ambayo hayakuthibitishwa. Inathibitisha haki ya jambo hili.)

 

  1.    Soma Ufunuo 16:8-9. Je, patakuwepo na ongezeko la joto? (Ndiyo! Pamoja na ustahili wa mjadala unaoendelea sasa hivi, jua “litawaunguza” wanadamu.)

 

   1.    Kwa nini tunaambiwa kwamba Mungu ana “mamlaka juu ya mapigo hayo?” (Hii ni hukumu. Wale wanaokana kwamba Mungu wetu mwenye upendo pia ni Mungu wa hukumu wanapuuzia kifungu cha wazi cha Biblia.)

 

   1.    Waovu wanaonyesha hisia zao kwa nani kwenye hii hukumu?

 

  1.    Soma Ufunuo 16:10-11. Je, mnyama ana kiti cha enzi? (Tulipojadili habari za joka, mnyama mwenye Pembe Kumi, na mnyama akaaye juu ya nchi katika ufunuo 13, tulihitimisha kwamba kuna uthibitisho mzuri kwamba Pembe Kumi ni Rumi ya Kipagani na Kipapa. Hilo ndilo hitimisho la maoni mengi ya kale.)

 

   1.    Soma Ufunuo 2:13. Hii inatupatia ishara gani kwenye swali la mahali kilipo kiti cha enzi cha mnyama? (Hii inatuambia kwamba kiti cha enzi cha Shetani (joka, na si mnyama) kipo Pergamu. Pergamu ulikuwa mji wa kwanza kule Asia uliokuwa na hekalu kwa ajili ya ibada ya Mfalme wa Rumi. Hii inatoa uthibitisho kwamba kimsingi tunauangalia mji mahsusi hapa duniani.)

 

  1.    Angalia tena Ufunuo 16:10-11. Pigo la giza linamaanisha nini katika mji wa kisasa? (Hakuna umeme.)

 

   1.    Je, watu wangetafuna ndimi zao kwa maumivu endapo wangenyimwa vifaa vyao vya kielektroniki? (Usikivu wao haujabadilishwa kutokana na vifaa vyao vya kielektroniki. Mji una giza na wamejikita kwenye maumivu yao.)

 

   1.    Angalia kauli inayojirudiarudia kwamba bado wanakataa kutubu na kumpa Mungu utukufu. Watu hawa wamedhamiria kiasi gani kuendelea kuwa dhambini? (Tunaweza kuona kwa nini wao ni waasi wakubwa dhidi ya Mungu.)

 

  1.    Soma Ufunuo 16:12. Hii inakukumbusha jambo gani? (Inanikumbusha juu ya kuhamisha mamlaka yaliyobainishwa katika Danieli 5:30 kutoka Babeli kwenda Medo-Persia. Chimbuko ni kwamba Cyrus iliuhamisha mto Frati na kuingia Babeli chini ya mto na kuuteka mji. Hii imezungumziwa katika Isaya 44:27-28.)

 

   1.    “Wafalme kutoka mashariki” ni wapi hao? (Soma Mathayo 24:27 na Ezekieli 43:2. Nadhani hii inamaanisha Yesu akija kutoka mbinguni na malaika wake.)

 

  1.    Soma Ufunuo 16:13-15. Nguvu za wema na uovu zinajipangaje? (Yesu anakuja, na wale walio waovu wanajiandaa kwa ajili ya pambano dhidi ya Mungu.)

 

  1.    Soma Ufunuo 16:16-20. Jeshi hili kubwa linapokusanyika, kitu gani kinatokea ikiwa ni matokeo ya pigo lililoletwa na malaika wa saba? (Tetemeko la nchi kubwa duniani kote.)

 

   1.    Kwa nini Mungu analishinda jeshi kupitia kile kinachoonekana ni majanga ya asili? (Sidhani kama waovu wanachanganywa na jambo hili. Badala yake, inaonesha uwezo mkuu wa Mungu unaodhibiti nguvu za asili. Mungu hayuko ndani ya ukomo wa uwezo wa wanadamu.)

 

  1.    Soma Ufunuo 16:21. Kitu gani kinaachwa juu ya jeshi ovu baada ya tetemeko la nchi la kutisha? (Mvua ya mawe makubwa yanayolingana na watu!)

 

  1.    Rafiki, fanya uchaguzi kwa umakini! Upande gani unaonekana kuwa wenye uchaguzi bora? Kwa nini usiwe upande wa Yesu leo, na sasa hivi?

 

     Juma lijalo: Hukumu Dhidi ya Babeli.