Unapokuwa Peke Yako
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Baada ya miaka 33 ya ndoa, kituo changu cha kazi kilibadilika kiasi kwamba nilikuwa ninakwenda nyumbani kwangu mwishoni mwa juma pekee. Katika siku za juma nilikuwa huru kula chakula cha usiku mahali popote nitakapo, na kwenda mahali popote nitakapo. Hapakuwepo na haja ya kufanya uamuzi wa pamoja na mke wangu. Mwanzoni ilikuwa ni burudani. Hata hivyo, baada ya muda fulani, nilijisikia upweke nilipokuwa ninakula chakula peke yangu. Ingawa kiuhalisia sikuwa peke yangu kwa kuwa nilikuwa naishi na binti wangu mkubwa, na nilikuwa ninafanya kazi kwa saa nyingi, nilipata uzoefu wa jinsi inavyofanana kuwa peke yangu. Hebu tuchimbue kile Biblia inachokisema kuhusu vipengele chanya na hasi vya mtu kuwa peke yake!
- Kamba
-
- Soma Mhubiri 4:9. Kwa nini watu wawili wanapata “ijara njema kwa kazi yao?” (Soma Mhubiri 4:8. Muktadha unaonesha kwamba kuwa na mtu wa kushiriki/kugawana naye utajiri wako hutengeneza “ijara” kwa kazi yako.)
-
- Soma Mhubiri 4:10. Je, kauli hii inahusu masuala ya dharura pekee? (Nimejifunza kwamba kwenye ndoa nyingi mume na mke wanashiriki majukumu yanayofanana. Kwa mfano, wanashirikiana kupika. Katika ndoa yetu, mimi na mke wangu tuna mgawanyo wa majukumu. Mke wangu nafanya baadhi ya kazi na mimi ninafanya kazi nyingine. Mfano uliopitiliza ni kwamba sijui kupika, lakini mimi ndiye niliyefunga jiko na kufanyia matengenezo vifaa vingine vya nyumbani kama vile pasi, jiko la umeme, n.k. Nadhani kutokumudu kwangu katika baadhi ya maeneo kunakidhi rejea ya “kupungukiwa.” Linapokuja suala la mapishi, mimi ni mshindwa.)
-
- Soma Mhubiri 4:11-12. Nilikuwa ninafuatilia vizuri hadi tulipofikia kwenye kamba ya nyuzi “tatu.” Sulemani alikuwa na mamia ya wake. Je, anaashiria kwamba ndoa za mitala ni bora? (Tumekuwa tukichukulia kwamba kifungu kinazungumzia ndoa. Kimsingi, hakizungumzii ndoa kwani kinazungumzia “rafiki” kumsaidia aliyeanguka.)
-
-
- Kwa kuwa vifungu hivi vina matumizi nje ya ndoa, vinawafundisha nini wale wanaoishi peke yao? (Watafute marafiki! Ikiwa una mafariki kadhaa wa karibu, hilo ni jambo zuri zaidi.)
-
- Ndoa Dhidi ya Kuwa Peke Yako
-
- Soma 1 Wakorintho 7:25. Je, kuna mambo yaliyojumuishwa kwenye Biblia yasiyotoka kwa Mungu? (Paulo anatuambia kwamba anachotaka kukiandika hakitoki kwa Mungu. Hata hivyo, anasema kuwa anadhani ana shauri zuri.)
-
- Soma 1 Wakorintho 7:26-28. Kitu gani kinahamasisha ushauri huu? (“Dhiki iliyopo.” Huu sio ushauri kwa ajili ya nyakati za kawaida.)
-
-
- “Dhiki iliyopo” ni kitu gani?
-
-
- Hebu tujikite kwenye 1 Wakorintho 7:28. Je, una matatizo mengi kwenye ndoa yako? (Ninafurahi kwamba sina. Lakini ninawafahamu watu wenye matatizo.)
-
-
- Ikiwa unafanana nami katika hali ya ndoa, ni asilimia ngapi ya ndoa utakazosema kwamba zinakabiliana na “matatizo mengi?”
-
-
-
- Wale ambao hawajaoa wala kuolewa ambao wangependa kuingia kwenye ndoa wanapaswa kujifunza nini kutokana na uzoefu huu?
-
-
-
-
- Je, hili ni fundisho lililojengwa juu ya “dhiki iliyopo?” (Sidhani kama hicho ndicho anachokimaanisha Paulo.)
-
-
-
-
- Je, busara inaweza kuboresha uwezekano wa kuwa na matatizo machache kwenye ndoa? (Kwa miaka mingi, wanawake kadhaa wamezungumza na kujadiliana nami kuhusu wanaume wenye uwezekano mkubwa wa kuwa waume wao. Mara nyingi nilikuwa na uhakika kwamba kuolewa na mwanaume fulani kungesababisha matatizo mengi. Ingekuwa bora zaidi kusalia kuwa peke yako. Lazima nikiri kwamba, hakuna aliyezungumza nami aliyesalia kuwa peke yake. Ama walipuuzia ushauri wangu au waliwapata wanaume bora zaidi.)
-
-
- Soma 1 Wakorintho 7:29-31. Je, Paulo yuko sahihi kuhusu “muda ubakiao si mwingi?” (Ikiwa anazungumzia ujio wa Yesu Mara ya Pili, na ninaamini ndicho anachokizungumzia, basi hayuko sahihi.)
-
-
- Paulo hazungumzii tu suala la ndoa. Anabainisha vilio, kuwa na furaha, kununua vitu na kufurahia mambo. Jambo lenye mfanano ni lipi kwa namna tunavyoyaangalia mambo yote hayo? (Paulo anasema kwamba kwa kuzingatia ujio wa Yesu utarajiwao mapema, puuzia huzuni na furaha ya kile kinachotokea katika mazingira yanayokuzunguka, na uzingatie nyakati za mwisho.)
-
-
-
- Ni kitu gani kinachosukuma fundisho la jumla la Paulo katika sehemu hii? (Hii inahusu hali ya dharura.)
-
-
-
-
- Baraka ya njia anayoitumia Paulo ni ipi? (Nina uhakika Paulo aliutumia ushauri huu kwake binafsi. Tunachokijua ni kwamba Paulo aliandika sehemu kubwa ya Aano Jipya. Kupunguza furaha yake duniani kwa kiasi kikubwa sana kulitangaza Ufalme wa Mungu.)
-
-
-
- Soma 1 Wakorintho 7:32-34. Paulo anaonekana kuhamia kwenye “kujali,” njia tofauti kidogo kwenye mada ile ile. Je, ndoa inaongeza wasiwasi wako? (Paulo anasema mtu mwenye ndoa anajihusisha na kujali masuala ya mwenzi wake, na sio tu kumpendeza Mungu.)
-
-
- Je, unaona kwamba jambo hili ni kweli maishani mwako? (Nakumbuka mifano kadhaa nilipodhani kwamba nilikuwa na mgongano kati ya kile ambacho Mungu alikuwa ananiongoza kukitenda na kile ambacho mke wangu alitaka kukifanya. Kwa upande mwingine, nadhani mke wangu amepunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya “majishughulisho/kujihangaisha” na maisha yangu. Anafanya mambo mengi ambayo vinginevyo yangenipa mzigo endapo ningekuwa peke yangu bila kuwa na mke.)
-
-
- Soma 1 Wakorintho 7:35 na 1 Wakorintho 7:39-40. Paulo anasema kuwa kusalia bila kuwa na ndoa ni kwa manufaa yetu wenyewe. Pia anasema kwamba unakuwa na furaha zaidi. Kama huna ndoa (uko peke yako), unadhani kauli hii ni ya kweli? Je, kuna faida kuwa peke yako (bila kuwa na ndoa)?
-
-
- Je, ushauri huu ni wa muda wowote? Au, bado Paulo anatoa ushauri wa dharura?
-
-
-
- Utagundua kwamba katika 1 Wakorintho 7:39-40 Paulo anamwandikia mtu aliyekuwa kwenye ndoa. Anaandika kwamba mtu ambaye hapo awali alikuwa kwenye ndoa angekuwa na furaha zaidi kama angekuwa peke yake. Kama uko kwenye hali hiyo, una maoni gani?
-
- Ndoa Iliyofunguliwa
-
- Soma 1 Wakorintho 7:12-13. Haya ndio maoni ya Paulo? (Hapana. Anasema kuwa maneno haya yanatoka kwa Mungu.)
-
-
- Wanandoa wangapi unaowafahamu hawakubaliani linapokuja suala la imani ya dini?
-
-
-
- Mangapi kati ya mambo wasiyokubaliana yaliibuka baada ya wao kuoana?
-
-
-
- Paulo anashauri nini pale mwenzi mmoja anapoongoka kwenye Ukristo na mwingine anakuwa hajaongoka? (Anasema abakie kwenye ndoa.)
-
-
- Soma 1 Wakorintho 7:14. Kwa nini Paulo anashauri kubakia kwenye ndoa? (Mwenzi asiyeamini “ametakaswa.”)
-
-
- Hiyo inamaanisha nini?
-
-
-
- Utakumbuka kwamba tulipokuwa tunajifunza kama tunapaswa kuwa na urafiki na wapagani, ushauri wa 1 Wakorintho 15:33 unasema kwamba wema utaharibiwa na ubaya. Kwa nini ushauri huo hauhusiki hapa? (Mazingira haya ni tofauti sana. Wote wawili walikuwa wapagani na mwenzi mmoja akaamua kubadilika na kuwa Mkristo. Tayari mwenzi aliyebadilika ameonyesha uhuru na nguvu.)
-
-
-
- Watoto wanaingiaje kwenye ushauri uliopo kwenye 1 Wakorintho 7:14? (Watoto wananufaika kwa ndoa kuendelea kuwa salama.)
-
-
-
- Katika familia yangu, bibi wangu na babu wangu kwa upande wa mama wangu wanawakilisha ndoa isiyo na usawa. Bibi alikwenda kanisani mara kwa mara, wakati kamwe babu wangu hakwenda kanisani. Unabashiri kwamba kitendo hiki kiliathirije watoto wao? (Hii ilikuwa na athari kubwa kwa mama wangu. Alikataa kuolewa na baba wangu hadi alipokuwa mshiriki wa kanisa. Hata hivyo, mjomba wangu (kaka wa mama wangu) alifuata nyayo za babu wangu.)
-
-
-
-
- Uamuzi wa kuoa au kuolewa na asiyeamini unafikia wapi? (Kwangu inaonekana kwamba vizazi viliathiriwa na uamuzi huo.)
-
-
-
- Soma 1 Wakorintho 7:15-16. Vipi kama mpagani akiamua kuondoka kwenye ndoa? Je, Wakristo wanapaswa kutoa ushirikiano? (Paulo anasema, “ndiyo.”)
-
-
- Paulo anatoa thamani ya juu kwenye jambo gani? (Amani. Lakini, angalia, hii ni amani inayotokana na kumwacha asiyeamini aende zake. Paulo hapendekezi amani wakati ambapo Mkristo ndiye anayetaka kuondoka.)
-
-
-
-
- Unadhani kwa nini Paulo anabainisha tofauti hii? (Kwa sababu kama mwenzi asiyeamini anataka kusalia kwenye ndoa, Mkristo mwenye upendo ana fursa ya kweli ya kumwongoa mwenzi asiyeamini.)
-
-
-
- Rafiki, mtazamo wa jumla wa Biblia ni kutoa upendeleo kwenye suala la ndoa. Hata hivyo, Paulo anaamini kwamba katika mazingira fulani mtu kuwa peke yake ni jambo jema zaidi na linaweza kusababisha furaha kubwa. Ikiwa uko peke yako furahia jambo hilo. Ikiwa uko peke yako, kutengeneza marafiki kutayabariki maisha yako. Kwa nini usijiweke kwenye nafasi ya kubarikiwa?
- Juma lijalo: Maneno ya Busara kwa Familia.