Somo la 8: Msimu wa Malezi

Swahili
(Luka 15, 1 Wafalme 17)
Year: 
2019
Quarter: 
2
Lesson Number: 
8

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Jana (Jumatano tarehe 16/05/2019) ilikuwa siku nzuri sana maishani. Ilikuwa ni Siku ya Mama! Mke wangu, binti wangu, na mjukuu wangu wa kike walikuwa nyumbani. Binti wangu hakuwa na furaha kutokana na mwingiliano wake na mjukuu wangu. Kitendo hicho kilinikumbusha miongo kadhaa iliyopita ambapo binti wangu hakuwa na furaha na mama wake (au mimi) kwa sababu hizo hizo. Nilicheka kichinichini. Jambo hilo (la kinyume cha mambo yanavyotokea) lilifurahisha. Malezi ni fursa nzuri kwa wazazi kuweza kuuelewa vizuri zaidi uhusiano wao na Mungu na kupandikiza kwa watoto wao upendo na uelewa wa Mungu. Ni fursa ya muda mfupi (yenye ukomo), na hatari ni nyingi. Hebu tuzame kwenye Biblia na tuone kile tunachoweza kujifunza kuhusu malezi!

 

 1.    Changamoto za Malezi

 

  1.    Soma Luka 15:11-12. Kuna chochote kinachoonekana kuwa kibaya kwenye ombi hili? (Mambo mengi si sahihi. Kwanza, baba hajafariki. Pili, huyu ni kijana mdogo, hivyo anapaswa kuwa wa mwisho kuomba mali. Tatu, nani aliye juu ya vyote? Kwa dhahiri si kijana mdogo. Mwisho, mtoto huyu hana subira hata kidogo kiasi kwamba anatamani muda ufike baba wake afariki.)

 

   1.    Unazungumzia nini juu ya jibu la baba? (Anamwacha mwanaye ajitawale mwenyewe.)

 

   1.    Ungejibuje? Je, ungekasirika kwamba mwanao hataki kukaa nawe na kukutendea kana kwamba umefariki?

 

   1.    Je, ungemwambia mwanao kuwa kama anataka uhuru, anapaswa kufanya kazi ili awe huru – na si kutegemea kile ulichonacho?

 

    1.    Je, hii inatufundisha chochote kuhusu malezi? (Jambo la msingi hapa ni kwamba mwana huyu ni mtu mzima.)

 

    1.    Je, tunapaswa kuwapa watoto wetu vitu ambavyo tunajua kuwa si vizuri kwao?

 

    1.    Je, kijana huyu angejifunza chochote kwa kukaa nyumbani bila kuwa na subira?

 

   1.    Utaona kwamba baba “akagawanya mali yake.” Inaonekana kwamba pia alimpa mwanaye mkubwa sehemu yake, ambayo ilikuwa mara mbili zaidi ya mali aliyomgawia mwanaye mdogo. (Angalia Kumbukumbu la Torati 21:17.) Hii inatufundisha nini? (Hatupaswi kumpuuzia mtoto aliye mtiifu.)

 

  1.    Soma Luka 15:13-14. Unadhani baba alilitarajia hili? Ikiwa ndivyo, kwa nini alitupa fedha zake?

 

   1.    Je, kijana ana kisingizio kwa matatizo yake? (Angeweza kushutumu anguko lake juu ya “njaa kuu.”)

 

  1.    Soma Luka 15:15-16. Je, Myahudi aliyetamani kujilisha chakula cha nguruwe amefikia kiwango cha chini kabisa cha hadhi yake?

 

  1.    Soma Luka 15:17. “Alipozingatia moyoni mwake.” Kitu gani kimempa fundisho mwana huyu ambacho baba hakuweza kukifundisha?

 

   1.    Soma Mithali 22:6. Je, kipindi cha “kuzingatia moyoni mwake” kinaakisi mithali hii?

 

    1.    Je, kila mtoto atafikia hatua ya kuzingatia moyoni mwake wakati fulani maishani mwake? (Kwenye kisa cha kusikitisha cha Samsoni hakuzingatia moyoni mwake hadi siku alipofariki. Waamuzi 16.)

 

  1.    Angalia tena Luka 15:17. Kama baba singekuwa na mafanikio, je, huyu kijana angejifunza alichojifunza? (Baba wake alikuwa anafundisha kile inachomaanisha kuwa na akili ya utambuzi na bidii katika kazi yako.)

 

  1.    Soma Luka 15:18-19. Mitazamo gani imebadilika kwa mwana huyu? (Kwanza, anatambua kwamba ametenda dhambi. Badala ya kufikiria kuwa ayapendayo yawe ya kwanza, na anapaswa kumwambia baba wake nini cha kufanya, sasa moyo wake umebadilika kuhusu thamani yake. Hajisikii tena kuwa na haki.)

 

  1.    Soma Luka 15:20-22. Mwana anatubu kama alivyopanga. Je, alitubu mambo yote kama alivyopanga? (Hapana. Ukilinganisha na Luka 15:19, utaona kwamba mwana hakufikia hatua ya kusema “nifanye kama mmoja wa watumishi wako.” Baba aliingilia mpango wake!)

 

   1.    Unauelezeaje mtazamo wa baba?

 

   1.    Tunapata fundisho gani la malezi hapa? (Msamaha wa papo hapo na upendo.)

 

   1.    Vipi kama ungesema, “nimeendelea kumsamehe na kumpenda mtoto wangu, lakini kamwe hajifunzi?” Kisa hiki kinakufundisha nini? (Anguko la mwana ndilo lililomfanya aweze kuzingatia moyoni mwake. Ukiendelea kuvumilia chaguzi mbaya, mtoto wako atakuwa na uwezekano mdogo wa kutubu.)

 

  1.    Soma Luka 15:23-24. Kwa nini kumzawadia mdhambi? Hii inatufundisha nini juu ya malezi? (Baba anazawadia marejeo. Anazawadia toba. Wazazi wanapaswa kuweka kando makosa ya watoto wao na si kuendelea kuyaibua. Badala yake, wanapaswa kutia moyo na kuzawadia tabia njema.)

 

   1.    Kama ungekuwa mwana, ungeonesha hisia gani kwa baba wako sasa hivi? (Moyo wangu ungejaa furaha na upendo. Mjibizo (reaction) wa baba ni chanya sana zaidi ya alivyotarajia.)

 

  1.    Soma Luka 15:25-28. Je, unamwonea huruma kaka mkubwa mwaminifu?

 

   1.    Mjibizo wa baba unatufundisha nini kuhusu malezi? (Anawajali watoto wako wote. Anatenga muda kwa ajili ya kijana mkubwa.)

 

  1.    Soma Luka 15:29. Ungekuwa na mjibizo gani kama ungekuwa baba? (Hili ni kofi la uso. Kufanya kazi na baba wake ni sawa na utumwa!)

 

   1.    Ungejaribika kuwa na mjibizo gani kwa kijana mkubwa? (Kijana mkubwa anaonesha upungufu halisi wa upendo kwa ndugu wake. Anaonesha mtazamo usio sahihi kabisa kwa baba wake. Watoto wote hawa wawili ni “watoto wenye matatizo.”)

 

  1.    Soma Luka 15:30. Je, kijana mkubwa anatamani angefanya yale aliyoyafanya kijana mdogo? Je, mtazamo huu ni ule ule, kwamba alipungukiwa tu ujasiri wa kufanya hivyo? (Kupoteza fedha na tabia isiyo na maadili vinakuathiri. Kijana mkubwa anaweza kuwa analiangalia jambo hili kama aina fulani hivi ya manufaa.)

 

  1.    Soma Luka 15:31-32. Baba anajibuje mashtaka dhidi yake? (Wewe si mtumwa wangu, unamiliki kila kitu.)

 

   1.    Je, watoto wote wawili wameleta machungu kwa baba yao? Je, wote wamemtuhumu kimakosa? (Ndiyo!)

 

    1.    Tunaweza kupata mafunzo gani ya malezi kwenye mashtaka haya ya uongo? (Si rahisi mara zote kuwa mzazi.)

 

  1.    Huu ni mfano. Baba anamwakilisha nani? (Mungu Baba.)

 

   1.    Hiyo inatufundisha nini juu ya malezi? Sisi ni wanadamu wadhambi. Sisi sio Mungu. Lakini, kisa hiki kinatupatia malengo ya malezi.)

 

   1.    Je, huu ni mfano wa mzazi mmoja? (Hebu tuangalie suala hilo katika sehemu inayofuata.)

 

 1.   Mzazi Mmoja

 

  1.    Soma 1 Wafalme 17:7 kwa utangulizi. Nini kinaendelea hapa? (Kuna njaa.)

 

  1.    Soma 1 Wafalme 17:8-9. Je, mara zote maelekezo ya Mungu yana mantiki? Kwa nini amwendee mjane kwa ajili ya kulishwa chakula?

 

  1.    Soma 1 Wafalme 17:10-12. Sasa unasemaje kuhusu maelekezo ya Mungu?

 

  1.    Soma 1 Wafalme 17:13. Je, Eliya anakuwa mbinafsi? Je, anasema, nilishe kwanza, na kisha “ujifanyie nafsi yako,” kwamba yeye na mwanaye wale na kisha wafe?

 

   1.    Je, utamtii nabii?

 

  1.    Soma 1 Wafalme 17:14-16. Tunapata mafunzo gani ya malezi hapa? (Tunatakiwa kumtii Mungu hata pale jambo linapokuwa halileti mantiki kwetu. Tunatakiwa kuamini kwamba Mungu ni mwanzilishi wa yasiyowezekana.)

 

  1.    Soma 1 Wafalme 17:17-18. Mzazi huyu mmoja anaenendaje sasa? (Kwa dhahiri ana dhambi kubwa sana ya zamani. Mashtaka yake dhidi ya Eliya hayana mantiki.)

 

  1.    Soma 1 Wafalme 17:19-22. Sasa, hata nabii anaonekana kuleta mashtaka ya uongo dhidi ya Mungu! Tunapata fundisho gani la malezi kutoka kwenye kisa hiki? (Ilimradi bado tunamwangalia Mungu, hatatuacha hata kama tutakuwa tunafanya mambo yasiyo na mantiki. Tunapaswa kuwa na mtazamo huo huo watoto wetu wanapokuwa wanafanya mambo yasiyo na mantiki.)

                                          

  1.    Rafiki, kama wewe ni mzazi, je, utamwomba Roho Mtakatifu, sasa hivi, akujaze mitazamo sahihi ambayo tumejifunza juma hili?

 

 1.        Juma lijalo: Nyakati za Kupoteza.