Somo la 6: Mwabudu Muumba

(Zaburi 115, Kumbukumbu la Torati 10, Amosi 5, Isaya 58)
Swahili
Year: 
2019
Quarter: 
3
Lesson Number: 
6

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Mfikirie rafiki ambaye kamwe hakuwahi kukusikilizi! Ushauri wako haukuwa wa muhimu kwake. Mahitaji yako kwake hayakuwa ya msingi. Yumkini ingekuwa heri kwako kukaa kimya kuliko kumwambia rafikiyo kile unachokipenda na usichokipenda. Sasa hebu mfikirie mwajiriwa kama huyo. Mwajiriwa asiyezingatia maelekezo. Utamchukuliaje rafiki kama huyo? Tukitafakari jambo hili hutupatia hisia ya jinsi inavyofanana kuwa Mungu Muumbaji na kuwa na wafuasi ambao hawadhani kweli kwamba utii ni muhimu. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tujifunze zaidi!

 

 

 1. Sanamu

 

  1. Soma Zaburi 115:1-4. Mungu wetu anatofautianaje na miungu wengine? (Hana hadhi ya chini kama aina fulani hivi ya sanamu.)

 

  1. Soma Zaburi 115:5-8. Kuna tatizo gani la kimantiki la sanamu? (Hakuna kinachofanya kazi! Haziwezi kusema, kuona, kusikia, kunusa, kuhisi, kuzungumza au kutembea. Huu ni upungufu mkubwa sana!)

 

   1. Matokeo ya kuitumainia sanamu ni yapi? (Unakuwa na kasoro kama ilivyo sanamu. Huwa uwezo.)

 

  1. Soma Zaburi 115:14-16. Ni kwa namna gani nyingine Mungu yu tofauti? (Aliumba mbingu na nchi. Anaziongoza mbingu na alitupatia nchi.)

 

  1. Soma Kumbukumbu la Torati 10:17. Mungu wetu anayatumiaje mamlaka yake kwetu? (Anatenda haki na hapokei rushwa. Tofauti na sanamu (mungu) isiyoweza kuona wala kusikia, Mungu wetu anatoa hukumu.)

 

  1. Soma Kumbukumbu la Torati 10:18. Utendaji haki wa Mungu kama hakimu unajidhihirishaje wenyewe? (“Anawatetea” wale wasio na nguvu [uwezo]. Wale wasio na baba (yatima), wasio na waume (wajane) au wasio na marafiki.)

 

   1. Unadhani inamaanisha nini kuwa na hakimu “anayemtetea” mtu? (Ikiwa hapa bado Mungu anaenenda kama hakimu, upendeleo wa Mungu ni kutenda haki kwa wasio na uwezo, hata kama hawana uwezo. Hata hivyo, wajibu wa Mungu unawezakuwa umebadilika hapa.)

 

  1. Soma Kumbukumbu la Torati 10:19. Hii inaonekana kuwa na uhitaji zaidi kuliko kutenda haki, sawa? Kifungu kinasema kuwa tunapaswa “kumpenda” mgeni. Ulimwengu wa magharibi una tatizo kubwa sana la wageni. Ulaya na Marekani zimepitia uzoefu wa watu kufurika kwenye nchi zao. Mungu anatutarajia tufanye nini tunapoambiwa kuwa “tumpende” mgeni? (Soma Mambo ya Walawi 19:34. Mungu anaendelea kurejelea ukweli kwamba watu wake walikuwa “wageni” katika nchi ya Misri. Watu wake wanapaswa kuwatendea wageni kama ambavyo wangependa kutendewa kule Misri.)

 

   1. Kwa kutumia muktadha na kipimo hicho, Mungu anatutarajia tufanye nini leo kwa kuwazingatia wahamiaji wanaomiminika kwa wingi? (Wamisri waliwafanya watu wa Mungu kuwa watumwa. Hii haiweki kipimo cha juu sana. Wamisri wangeweza kuwaonesha upendo kwa kuwaacha wafanye mambo yao kwa nguvu zao wenyewe na si kuwafanya kuwa watumwa.)

 

    1. Unadhani hicho ndicho anachokimaanisha Mungu hapa?

 

  1. Soma Kumbukumbu la Torati 10:20-22. Hii inatoa ushauri gani makinifu kwa mgeni? (Rafiki wa muhimu zaidi kwa mgeni ni Mungu! Hii inaturejesha kwenye mjadala wetu kuhusu sanamu. Sehemu ya ujumbe wa Mungu kwa watu wake kuhusu kukumbuka asili yao kama wageni ni kwamba Mungu aliwabariki sana.)

 

 1. Uaminifu

 

  1. Soma Amosi 5:18. Je, unapenda Yesu aje kukuchukua kwenda mbinguni?

 

   1. Je, hiki ndicho ambacho watu hawa walikitaka? (Ndiyo, walitamani “siku ya Bwana” ifike.)

 

   1. Je, siku hiyo itakuwa ya kupendeza sana kama walivyotarajia? (Kwa dhahiri, hapana. Itakuwa ni “giza” na “si nuru.”)

 

  1. Soma Amosi 5:19-20. Je, mtu huyu ana siku mbaya ya kutisha? (Ndiyo! Tatizo lolote analoliepuka, anakutana na matatizo mengine.)

 

  1. Soma Amosi 5:21. Tatizo ni lipi? Kwa nini wale wanaomfuata Mungu, wanaotaka arejee, wamepotoka sana kuhusu jinsi ambavyo jambo hili litatokea? (Kuna kasoro fulani kwenye uhusiano wao na Mungu.)

 

  1. Soma Amosi 5:22-23. Je, hiki si kile ambacho Mungu aliwataka watu wake wakifanye? (Naam! Katika upande wa ibada, watu wanafanya kile ambacho Mungu anakitaka, lakini kuna kitu ambacho hakipo sawa kabisa.)

 

  1. Soma Amosi 5:24. Hii inatupatia ishara gani juu ya kile kisicho sahihi kwenye uhusiano kati ya Mungu na watu wake? (Mungu anatoa wito wa “kutenda haki” na “usawa” kama jambo la kujirudiarudia. Haya yanapaswa kuwa mazao endelevu maishani mwako.)

 

   1. Hebu tujadili jambo hili. Hapo awali tulihitimisha kwamba “kutenda haki” ni nini? (Ni kuwapatia watu kile wanachostahili.)

 

   1. “Haki/usawa” ni nini? (Katika huu muktadha ni kuishi maisha sahihi. Utii kwa Mungu.)

 

  1. Yote haya ni kwa ujumla. Hebu turejee nyuma kwenye sura hii na tuchunguze sababu mahsusi na ukataliwaji wa Mungu. Soma Amosi 5:7-8. Anguko ni lipi hapa? (Kumkiri Mungu Muumbaji wetu.)

 

   1. Je, kumkiri Mungu ndio kile kilichokuwa kinawatokea watu walipokuwa wanamwabudu Mungu na kuleta kafara? (Ninadhani hivyo. Bado hatujabaini tatizo mahsusi.)

 

  1. Soma Amosi 5:10. Sasa tunazidi kuwa mahsusi. Hapa tatizo ni lipi? (Baadhi ya watu wanachukia mfumo wa utendaji haki ambapo utawala wa sheria unafuatwa (haki) na pale ukweli unaposemwa.)

 

   1. Angalia maneno “humzira anenaye maneno ya adili.” Hivi karibuni nilisoma habari ya raia wa Canada kupewa adhabu ya $55,000 kwa sababu alimrejelea mtu aliyejibadili jinsia (transgender) kama “mwanaume kibaiolojia.” Je, huo ni mfano wa kuuchukia ukweli?

 

   1. Angalia tena muktadha. Je, tunazungumzia kuhusu kusema ukweli kanisani? (Hapana. Muktadha ni mfumo wa utendaji haki. Mfumo wa serikali. Hii inahusiana na waovu kutokuwa waaminifu juu ya kile kinachotokea kiuhalisia.)

 

  1. Soma Amosi 5:11. Nani yuko nyuma ya huu uovu? (Hii ni serikali inayotoza kodi kwa maskini afanyaye kazi.)

 

   1. Ni kwa jinsi gani leo serikali inasababisha matatizo kwa maskini wafanyao kazi?

 

   1. Unapowafikiria masikini wa hapa duniani, watu wangapi ni maskini kwa sababu ya serikali yao? (Serikali ni tatizo kubwa. Vita, rushwa, na uhafifu wa uhuru wa kiuchumi huwafanya watu kuwa maskini. Kuna uhusiano wa muhimu kati ya uhuru wa dini na uhuru wa kiuchumi. Nchi nyingi zilizo na uhuru wa dini pia zina uhuru wa kiuchumi. Matokeo ya kufufuka kwa demokrasia na masoko huru kwa kiasi kikubwa yamepunguza idadi ya maskini duniani kote.)

 

   1. Mungu anaingiliaje kati pale viongozi wa serikali wanapowadhuru maskini? (Mungu anaonya kwamba viongozi hawatafurahia utajiri wao.)

 

  1. Soma Amosi 5:12-13. Amosi anarudia asili ya tatizo, upotovu wa utawala wa sheria. Watu wanaitikiaje suala hili? (“Mwenye busara atanyamaza kimya wakati kama huo.”)

 

   1. Je, hiki ndicho anachokitaka Mungu? Je, tunapaswa kukaa kimya juu ya uovu wa serikali? (Mungu anakiri kwamba ni busara kukaa kimya. Lakini, haiko wazi kwamba hicho ndicho anachokitaka Mungu.)

 

    1. Ni kwa namna gani nyingine mambo yatabadilika? (Hebu turukie mbele na tusome Amosi 5:17. Mungu anasema kuwa atabadilisha mambo. “Atapita katikati yenu.”)

 

  1. Soma Amosi 5:14-15. Je, tuna nafasi kwenye serikali aminifu na utawala wa sheria? Au, je, ni bora zaidi kuwa na busara? (Mungu anatutaka tulete utofauti na tusikae kimya. Kama jinsi tulivyo mawakala wa Mungu kwa ajili ya kuwasaidia maskini, vivyo hivyo tu mawakala wa Mungu wa kuifanya serikali kuwa aminifu zaidi na yenye kutenda haki.)

 

  1. Utakumbuka kwamba Mungu anawaambia watu kuwa anachukia ibada yao. Badala yake anataka haki. Tumegeukia kwenye sehemu ya kwanza ya Amosi kuona kile ambacho Mungu alikuwa anakizungumzia. Mungu alikuwa anazungumzia nini? (Mungu anachukia ibada yetu pale tunaporuhusu mahakama zetu na serikali zetu kuwa na uozo.)

 

 1. Badiliko

 

  1. Soma Isaya 58:6. Ni aina gani ya matendo ya kidini ambayo Mungu anayatolea wito hapa? (Kuwaweka watu huru.)

 

   1. Je, hii inaihusisha serikali? (Serikali inapokuwa tatizo, itamaanisha kuwapatia watu serikali ya haki.)

 

  1. Soma Isaya 58:7. Je, haya ni maagizo kwa serikali? (Hapana. Hii inahusu mtu binafsi kuwasaidia walio wahitaji.)

 

  1. Soma Isaya 58:8-10. Nini kitatokea kwenye ibada yetu ya kidini ikiwa tutafanya hivi? (Mungu atasikiliza na kujibu. Atatubariki na kutulinda.)

 

  1. Rafiki, kwa mara nyingine tunafikia kwenye hitimisho lisilo geni. Mungu anatutaka tuwatendee haki maskini na kuwahurumia. Je, utamwomba Roho Mtakatifu ili akusaidie kuelewa kile unachopaswa kukifanya?

 

 1. Juma lijalo: Yesu na Walio Wahitaji.