Somo la 3: Wito wa Mungu

(Danieli 9, Nehemia 1, Warumi 9)
Swahili
Year: 
2019
Quarter: 
4
Lesson Number: 
3

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Je, Mungu amekuita? Je, amekuita kwa ajili ya jukumu mahsusi? Nadhani amekuita. Tunawezaje kujua kama tumeitwa? Tunawezaje kujua kama tumekosa wito wetu? Je, kuna wito mwingine ikiwa tumekosa miito wa awali? Ninaamini kwamba Mungu anamuita kila mmoja wetu kumtumikia kwa namna ya pekee. Somo letu juma hili linahusu wito wa Mungu. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tujifunze zaidi!

 

 1.    Wakati Mwafaka

 

  1.    Soma Danieli 9:24-26. 70x7 ni kitu gani? Hukutarajia swali la hisabati, sawa? (490!)

 

   1.    Kitu gani kinaanzisha kipindi hiki na kitu gani kinakihitimisha? (“Neno” na kurejesha na kuijenga upya Yerusalemu linaashiria kuanza kwa kipindi hiki. Inaonekana kama mwisho wa wakati unahusisha ujio wa Yesu (Aliyetiwa Mafuta) na uangamivu wa pili wa Yerusalemu.)

 

  1.    Soma Nehemia 1:3-6. Tunaweza (na tumesha) kujadili unabii wa muda kwenye masomo mengine. Hebu tuangalie kipengele tofauti cha jambo hili. Kichwa cha somo letu ni “Wito wa Mungu.” Juma lililopita tulijadili ombi la Nehemia na jinsi Mungu alivyomtumia kumshawishi Artashasta kuamuru ujenzi upya wa Yerusalemu. Unadhani wito na unabii vinafanyaje kazi? Je, Nehemia alikuwa anaomba wakati ule ule kwa sababu Danieli alipewa maono ya majuma sabini?

 

   1.    Je, Nehemia alizaliwa ili kutenda masuala ya kutimiza unabii?

 

   1.    Je, Nehemia alikuwa anasali kwa kuwa aliufahamu unabii?

 

   1.    Je, Mungu aliyajua mambo yote haya mapema na kumpa Danieli tarakimu zinazoendana na kile ambacho Mungu anajua kitatokea?

 

   1.    Majibu yako kwa maswali haya yanaendanaje na dhana ya wito wa Mungu? Yanaendanaje na dhana ya uhuru wa kuchagua wa mwanadamu?

 

  1.    Umewahi kuwa kwenye thieta yenye “Mwonekano wa Duara?” Unasimama katikati ya thieta na sinema inaoneshwa kuwazunguka nyote mliomo ukumbini? Ninamwangalia Mungu akiwa amesimama katikati ya mzunguko wa muda. Anaweza kuangalia ndani mahali popote na kile kinachotokea. Kutokana na hilo, nadhani Mungu alijua kabla Nehemia hajazaliwa kwamba Nehemia atakuwa akiomba katika muda huu. Hivyo, Mungu alimpa Danieli maono yatakayohusisha muda mwafaka wa ombi la Nehemia. Hii inaendana na dhana ya uhuru wa kuchagua.

 

 1.   Uratibu Mzuri

 

  1.    Soma Warumi 8:28. Hii inaashiria nini kuhusu wito na matendo ya Mungu anapokuwa amesimama katikati ya duara la muda? (Mungu “anarekebisha” matukio ili kuwabariki watu wake.)

                    

  1.    Soma Warumi 8:29-30. Ni kwa jinsi gani tunajaaliwa kufanana na Yesu? (Mungu haingilii uhuru wetu wa kuchagua. Anawaona wale wanaomchagua na kumpeleka Yesu kuishi maisha makamilifu kwa niaba (ajili) ya wale wanaomchagua yeye (Mungu). Hii inatufanya kufikia lengo la kuhesabiwa haki na kutukuzwa.)

 

 1. Mifano Halisi

 

  1.    Soma Kutoka 3:1. Je, kuwa mchungaji ni wito? (Ndiyo. Lakini, ni wito ambao watu wengi wameutimiza.)

 

  1.    Soma Kutoka 3:2-4. Kama unafahamu kisa hiki, je, huu ndio mwanzo wa wito wa Musa? (Baadhi ya watu wanaweza kusema kwamba hapo kabla Musa alikuwa na wito kule Misri.)

 

   1.    Je, wito wako unaweza kuwa wa kuvutia kama huu?

 

  1.    Soma Kutoka 3:5-6. Kuna fundisho gani hapa kuhusu kuitwa? (Kuna mafundisho kadhaa, lakini ujumbe mkuu ni kuwa na uhakika kwamba Mungu ndiye anayekuita.)

 

  1.    Hebu turuke mafungu kadhaa na tusome Kutoka 3:9-10. Wayahudi walikuwa Misri mamia ya miaka. Ukilinganisha Matendo 7:23 na Matendo 7:30, Musa alikuwa na umri wa miaka 80 alipokuwa amesimama kwenye kijiti kinachowaka moto. Kwa nini Mungu anasema utumwa wa watu wake “umenifikilia” baada ya mamia ya miaka?

 

   1.    Kwa nini Musa anapokea wito wake akiwa na umri wa miaka 80?

 

   1.    Kama ungekuwa mtu ya nje ukiangalia mambo yote haya, ungehitimisha nini kumhusu Mungu? Mungu anatenda mambo pole pole? Ana ratiba yake ya muda? Ana shughuli nyingi za mambo mengine?

 

    1.    Je, mahitimisho haya yanahusika kwenye wito wako na ni suluhisho kwa matatizo maishani mwako?

 

 1.   Jibu la Mungu

 

  1.    Soma Warumi 9:14-16. Angalia swali la aina ile ile – “kuna udhalimu kwa Mungu?” Jibu ni lipi? (Hapana. Biblia inatuambia kwamba Mungu atamrehemu yeyote apendaye kumrehemu.)

 

   1.    Je, hivyo ndivyo tunavyoielezea “haki?” Mfalme anaamua nani wa kumrehemu na yupi asiye wa kumrehemu? (Hicho ni kinyume cha utawala wa sheria. Hiyo si haki.)

 

  1.    Soma Warumi 9:17-19. Ikiwa tupo mikononi mwa Mungu ili atutende kama apendavyo, Biblia inauliza “kwa nini [Mungu] anaona dosari kwetu (mbona angali akilaumu)?”

 

   1.    Kwa kawaida hatuoni mashambulizi kwenye utendaji haki wa Mungu katika Biblia. Kwa nini maswali haya yapo kwenye kitabu cha Warumi? (Yanaakisi kile ambacho wapinzani wa Mungu wanakisema kumhusu. Biblia inataka kutupatia majibu kwa aina hii ya maswali magumu.)

 

  1.    Soma Warumi 9:20-21. Je, jibu hili linakutosheleza? Je, linawatosheleza wakosoaji wa Mungu? (Hili ni jibu lile lile ambalo Mungu anamjibu Ayubu katika Ayubu 38. Kimsingi jibu linasema “Unajua nini ukijilinganisha na mimi [Mungu]?” Kaa chini na unyamaze kimya!)

 

  1.    Soma Warumi 9:22-24. Ndani ya vifungu hivi ni jibu kuhusu utendaji haki wa Mungu. Ni jibu gani hilo? (Sote tunastahili kifo. Sote tunastahili uangamivu. Sote tulichagua dhambi na mauti. Kama Mungu atatuacha na uchaguzi wetu, tunaweza kuwa na malalamiko gani? (Haki yetu ni mauti ya milele. Lakini, Mungu hatuachi kwenye thawabu ya haki tunayostahili, Mungu ametuonesha rehema.)

 

   1.    Hii inafanyaje kazi kwa mtu kama Farao? Soma tena Warumi 9:17-18. Je, Farao hatendewi haki? (Farao alimkataa Mungu. Farao alistahili mauti ya milele. Ukweli kwamba Mungu “anaufanya mgumu” moyo wa Farao ni uthibitisho tu wa chaguzi ambazo tayari Farao alizifanya.)

 

   1.    Hii inafanyaje kazi tunapojikuta kwenye mazingira yasiyo ya haki (kwa mfano, utumwa) au pale tunapokuwa na umri wa miaka 80 kabla hatujauona wito wa Mungu? Je, tuna vigezo vya kulaumu kuhusu wakati mwafaka wa Mungu au kuchelewa kwake? (Jibu la moja kwa moja ni kwamba tunastahili kifo. Mungu ametupatia kila kitu. Sisi ni nani hadi kutilia shaka au kuuliza jinsi anavyotenda au wakati mwafaka wa mipango yake?)

 

  1.    Soma Warumi 9:30-31. Je, Mungu hatendi haki kwa jinsi anavyowatendea Waisraeli? Walitia bidii ili kuhesabiwa haki?

 

  1.    Soma Warumi 9:32-33. Ni kosa gani baya lililotendwa na Israeli? (Kuitafuta haki kwa kutegemea matendo na si kutegemea imani kwa kile ambacho Yesu amekitenda kwa ajili yetu.)

 

   1.    Hii inahusikaje na wito wetu na haki ya Mungu? Je, sura hii inaishia kwa kuibua suala jipya? (Sura yote inajishughulisha na jambo lile lile – uwezo wa Mungu. Tunayo dhana yetu ya jinsi mambo yanavyopaswa kutendeka. Tunasema kwamba bidii ya kazi huleta mafanikio. Tunasema kwamba mambo yanapaswa kuwa ya haki na kuamuliwa kwa utawala wa sheria. Mungu anajibu kwamba kama tukisisitiza juu ya utawala wa sheria sote tungeshakufa – milele. Mungu anatenda haki isivyo kawaida. Hatuelewi miito yote ya Mungu, lakini anatuwazia mambo bora.)

 

  1.    Soma Hesabu 20:7-8 na Hesabu 20:10-12. Musa amefanya nini isivyotakiwa? Ni nini adhabu kwa kosa lake?

 

  1.    Soma Kumbukumbu la Torati 3:25-28 na Kumbukumbu la Torati 34:4-7. Musa anajitetea kwa Mungu ili amruhusu, baada ya miaka yote hii ya uongozi, kuingia katika nchi ya ahadi. Kwa nini Mungu hamruhusu?

 

   1.    Unazungumzia nini kuhusu utendaji haki wa Mungu?

 

  1.    Soma Yuda 1:9 na Luka 9:28-31. Sasa unazungumzia nini kuhusu haki ya Mungu na kuzingatia kwake usawa? (Mungu anatenda zaidi ya haki. Alimpatia Musa zaidi ya kile alichokitumainia. Angalia Waefeso 3:20.)

 

  1.    Rafiki, wito wa Mungu maishani mwetu wakati mwingine uko wazi sana na mara nyingine hauko wazi. Kuna wakati inaweza kuonekana kwamba hakuna haki inayotendeka. Lakini Bwana wetu anatuonesha kwamba anatupatia zaidi ya haki. Mungu anatenda zaidi ya haki na usawa. Je, utaomba uwezo wa Roho Mtakatifu uwe ndani yako ili Mungu aweze kukuonesha wito wako na kutenda mambo makuu kupitia kwako?

 

 1.    Juma lijalo: Kukabiliana na Upinzani.