Somo la 7: Mungu Wetu Anayesamehe

(Nehemia 9)
Swahili
Year: 
2019
Quarter: 
4
Lesson Number: 
7

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Inamaanisha nini “kutubu?” Inamaanisha nini “kuungama dhambi?” Nilidhani ninafahamu. Lakini katika miaka michache iliyopita nimeanza kutafakari upya maneno hayo kutokana na ujifunzaji wangu wa Biblia. Hebu tuzame kwenye somo letu la Nehemia na tuone kile tunachoweza kujifunza. Huenda utauangalia upya uelewa wako wa maneno hayo!

 

 1.    Ungamo

 

  1.    Soma Nehemia 9:1-2. Je, unaona jambo lolote la ajabu kwenye hivi vifungu viwili? Jambo lisiloendana na uelewa wako juu ya ungamo la dhambi? (Waliungama dhambi “za baba zao.”)

 

   1.    Upi umekuwa uelewa wako wa “kuungama dhambi zako” pale mtumishi wa Mungu anapotoa wito wa kutubu na kuungama? (Kwa kawaida nimekuwa nikilielewa kama suala la kuungama jambo nililolitenda.)

 

  1.    Soma Mathayo 6:12. Unadhani hapa Yesu anazungumzia nini? (Nadhani anazungumzia juu ya uelewa wangu wa kawaida kuhusu ungamo la dhambi.)

 

  1.    Soma 1 Yohana 1:9. Unadhani hapa Biblia inazungumzia nini?

 

  1.    Soma tena Nehemia 9:2. Nitachukulia kwamba angalao baadhi ya “baba zao” ambao Nehemia alikuwa anawazungumzia walikuwa wamefariki. Kwa dhahiri watu wasingekuwa wanarejelea dhambi zao binafsi wakati walipoungama dhambi za baba zao. Unaelewaje kuhusu matumizi haya ya neno “wakaziungama dhambi zao?” (Kimantiki, hii ni aina fualni ya ungamo la “pamoja.” Ni kinyume na jinsi ungamo linavyorejelewa katika 1 Yohana 1:9 au Mathayo 6:12.)

 

  1.    Soma Mathayo 3:1-2. Umewahi kufikiria juu ya mantiki ya wito huu wa Yohana Mbatizaji? Kwa nini utubu kwa sababu ya jambo lililo karibu kwa kuzingatia muda au mahali? Kwa nini utubu kwa sababu ya jambo ambalo mtu mwingine analitenda?

 

  1.    Soma Mathayo 4:17. Yesu anasema jambo lile lile. Unadhani “ufalme wa mbinguni” ni kitu gani? (Nadhani Yesu anajirejelea yeye mwenyewe.)

 

   1.    Ikiwa niko sahihi, kwa nini watu watubu kuhusu jambo hilo? Kwa nini wasifurahie?

 

  1.    Soma Mathayo 11:20. Kwa nini utubu kwa sababu mambo makuu yalitendeka katika mji wako? Kwa nini badala yake usifurahie?

 

  1.    Unapotafakari njia zote ambazo “kuungama” na “kutubu” zinatumika, je, maana gani itayajumuisha maneno yote mawili? (Nadhani jambo la kufanana miongoni mwa yote haya ni mtazamo. Wito wa Nehemia ni kuungama mtazamo usio sahihi ambao vizazi vya watu wa Mungu walikuwa nao dhidi ya Mungu. Yohana Mbatizaji na Yesu walipotoa wito wa kuungama, wanawataka watu wabadili uelewa wao juu ya Masihi. Watu wanapewa wito kubadili mtazamo wao kuhusu asili ya dhambi na msamaha – kwa maana Ufalme wa Mbinguni umekaribia! Hata pale tunapozifikiria dhambi zetu binafsi, Yesu anatutaka tubadili mtazamo wetu kuhusu dhambi maishani mwetu. Kwa uwezo wa Roho Mtakatifu uwe mwaminifu kuhusu dhambi maishani mwako na udhamirie kubadili mwelekeo.)

 

 1.   Kumtukuza Mungu

 

  1.    Soma Nehemia 9:3. Unafikiria nini juu ya mpangilio wa matukio haya? Kwanza kusoma Biblia, kisha kuungama, halafu kuabudu. Je, hiyo inaonekana kuleta mantiki?

 

   1.    Hiyo inaonekana kuendana na mjadala wetu juu ya kile kinachomaanishwa na toba? (Sababu moja kwa nini mara zote maswali ya GoBible yanaanza kwa usomaji wa kifungu cha Biblia ni kwamba ni muhimu kulifahamu neno la Mungu. Mara baada ya kulitafakari neno lake [Mungu], ndipo tunapoona ni wapi maisha yetu yako nje ya msitari. Tunapokuwa dhati kuhusu kumfuata Mungu, mitazamo yetu inabadilishwa na Roho Mtakatifu, na tunapata uzoefu wa furaha inayogeuka na kumtukuza Mungu.)

 

  1.    Soma Nehemia 9:4-5. Je, kuna jambo lolote kama hili linatokea kanisani kwako? Je, watu “wanalia kwa sauti kuu” na “kusimama na kumhimidi” Mungu?

 

   1.    Ikiwa sivyo, kwa nini? (Ninakumbuka washiriki wa kanisa wakikosoa aina hii ya kuhimidi kwa sababu ilifanana sana na “Upentekoste,” au ilikuwa ya “kiuinjilisti” zaidi. Hizi ni hoja za uongo. Suala si kama baadhi ya washiriki wa kanisa (au kundi la watu) wanafanya hivyo, bali suala ni kwamba Biblia inasema nini kuhusu suala hilo.)

 

  1.    Soma Nehemia 9:6. Sababu ya kwanza ya kumtukuza Mungu ni ipi? (Yeye ni Muumbaji.)

 

   1.    Kukiri suala hili ni muhimu kiasi gani? (Nimejifunza suala hili hapo kabla. Madai ya msingi ya Mungu kwa utii wetu ni kwamba yeye ni Muumbaji wetu.)

 

    1.    Je, imani kwa Mungu wetu kama Muumbaji ina athari kwenye mtazamo wetu juu ya mitafaruku inayoendelea sasa hivi?

 

  1.    Soma Nehemia 9:7-12. Sababu inayofuata ya kumtukuza Mungu ni ipi? (Kutokana na kile alichokitenda maishani mwao na katika maisha ya baba zao.)

 

   1.    Mke wangu anatunza matukio ya nyakati ambazo Mungu alitutendea mambo makuu maishani mwetu katika familia yetu. Je, unafanya hivyo? Ikiwa sivyo, unakosa chanzo kikubwa cha utiwaji moyo.)

 

  1.    Soma Nehemia 9:13-14. Je, Amri Kumi na Sabato ni sababu ya kumtukuza Mungu?

 

   1.    Ikiwa umejibu, ndiyo, elezea sababu? (Sabato na sheria zimemaanishwa kuwa baraka kwetu. Watu wengi sana wana mtazamo usio sahihi kuhusu asili ya sheria ya Mungu.)

 

   1.    Dakika chache zilizopita nimeona makala kuhusu uongofu katika “kitanda cha mauti.” Dhana iliyopo ni kwamba nitatenda kile ninachotaka kukitenda, na katika dakika za mwisho kabisa za uhai wangu nitaungama ili niweze kwenda mbinguni. Ikiwa kuungama ni suala la kimtazamo, hiyo inazungumzia nini kuhusu mtazamo wako? (Hii ni sawa na ahadi ya kukufanya uwe tajiri – na ukafanya uamuzi kwamba utaikataa hii ofa hadi muda mfupi tu kabla hujafa. Kwa dhahiri, una mtazamo usio sahihi juu ya kile kinachoahidiwa!)

 

  1.    Soma Nehemia 9:15. Ni jambo gani jingine ambalo Mungu amewatendea watu wake? (Aliwalisha, aliwapa maji, na akawapa makao.)

 

 1. Uasi na Mwitiko

 

  1.    Soma Nehemia 9:16-19. Unapoomba (unaposali), je, kwa kawaida huwa unaorodhesha makosa ya baba zako?

 

   1.    Kwa nini kinafanyika hapa? (Utaona kwamba sala sio tu suala la uasi, bali inahusu mwitiko wa rehema wa Mungu kwa uasi huo.)

 

   1.    Je, una maelezo yoyote kwa nini watu waorodheshe uasi uliotokea kwenye safari ya kutoka utumwani Misri, kinyume na uasi wa hivi karibuni kabisa uliotokana na kutekwa kwao Babeli? Ni muda mfupi tu walikuwa wametoka utumwani Babeli!

 

  1.    Soma Nehemia 9:20. Hii inatufundisha nini kuhusu Roho Mtakatifu? (Wakati mwingine tunadhani kwamba Roho Mtakatifu yuko hai (kiutendaji) katika Agano Jipya pekee. Hii inatuonesha kwamba alikuwa wa muhimu sana katika Agano la Kale kiasi kwamba watu walikuwa wanatambua kazi yake kwa umahsusi kabisa.)

 

   1.    Angalia kawaida ya kile kinachojadiliwa: maji, chakula, na Roho Mtakatifu. Maji na chakula ni vya muhimu kiasi gani? Hii inazungumzia nini kuhusu Roho Mtakatifu?

 

  1.    Hebu turuke vifungu kadhaa hadi chini na tusome Nehemia 9:25-28. Je, hii inajibu swali letu la awali juu ya sababu ya wao kuungama dhambi za safari yao kutoka utumwani Misri na si dhambi zao za baadaye? (Ndiyo. Bado walikuwa hawajafikia hatua hiyo katika historia yao.)

 

  1.    Hebu turuke vifungu kadhaa chini na tusome Nehemia 9:36-38. Watu wanafikia hitimisho gani katika ombi lao? (Watafanya “agano la hakika” na Mungu!)

 

  1.    Tutajifunza agano hili juma lijalo. Kwa sasa, hebu tuchambue ombi hili. Tumekuwa tukiliita ombi, ingawa linaonekana kuwa ni sifa iliyobadilika na kuwa kauli ndefu ya historia ya watu. Je, unapaswa kuwa unapitia mara kwa mara historia yako yote na Mungu?

 

   1.    Vidokezo vya mapitio haya ni vipi? (Mungu amekuwa mwaminifu ingawa kwa kiasi kubwa watu wamekuwa si waaminifu.)

 

   1.    Je, hiki ndicho unachokisikia kutoka kwa watu leo? Watu wanapoteseka, je, kwa ujumla wanakiri sehemu yao katika mateso?

 

   1.    Bibi yangu (mama wa baba yangu) aliolewa tena alipokuwa na umri wa miaka 62. Mwanaume aliyemwoa alikuwa mtu aliyepona kutoka kwenye uraibu wa pombe aliyekuwa na moto mkali katika kumfuata Mungu. Nakumbuka akiniambia jinsi alivyohuzunika kwamba alipoteza muda mwingi sana maishani mwake katika uraibu. Aina hii ya uaminifu iliacha alama kubwa sana kwangu!

 

  1.    Rafiki, sehemu ya msingi ya toba na ungamo, sio suala linalohusu dhambi moja, bali linahusu mtazamo wako. Hakuna kinachosaidia mtazamo wetu kuwa sahihi zaidi kuliko kujifunza neno la Mungu na kisha kutafakari historia yetu na Mungu. Je, utadhamiria kutoa muda wako kupitia upya kwa uaminifu historia yako na Mungu? Je, utapitia upya wema wa Mungu kwako? Je, utajitoa kwa dhati kujifunza Biblia?

 

 1.      Juma lijalo: Mungu na Agano.