Somo la 8: Mungu na Agano

(Nehemia 10, Yeremia 31, Waebrania 8
Swahili
Year: 
2019
Quarter: 
4
Lesson Number: 
8

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Mojawapo ya mambo chanya kuhusu kuwa mwanasheria wa Kimarekani na mwanafunzi wa Biblia ni kwamba dhana nyingi za kisheria zinaakisi mawazo ya Kibiblia. Agano, ambayo ndio mada yetu katika somo hili, ni sawa na mkataba. Mkataba ni wa hiari, unalenga kuzinufaisha pande zote  mbili, na unatekelezeka. Mikataba haipaswi kutegemea jinsi unavyojisikia katika siku moja mahsusi, na haipaswi kuvunjwa kwa kuwa tu huoni tena manufaa. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tuchimbue mada ya agano la Mungu kwa watu wake!

 

 

  1. Mkataba

 

    1. Hebu tufanye mapitio kwa kusoma Nehemia 9:1-2 na Nehemia 9:38. Nini kilichofanya kuwepo kwa hili “agano la hakika?” (Kwanza, watu walisikiliza usomwaji wa sheria ya Mungu. Walifurahia uelewa wao mpya na walihuzunishwa kwa jinsi ambavyo hawakuwa na maelewano na mapenzi ya Mungu kwa ajili yao. Walipitia upya historia yao pamoja na Mungu na wakafanya uamuzi kwamba wataingia kwenye makubaliano ya kimaandishi ili kumtii Mungu.)

 

    1. Pitia kwa haraka haraka Nehemia 10:1-27. Inaorodhesha viongozi “waliotia muhuri” makubaliano. Hiyo inamaanisha nini? (Mojawapo ya maoni yalibainisha kuwa ilimaanisha kutumia kifaa kutia alama kwenye jina lako. Huenda pia inamaanisha kuitia saini. Inaonekana kwamba hawa walikuwa watu waliokuwa na kawaida ya kuandaa nyaraka rasmi.)

 

    1. Soma Nehemia 10:28-29.  Watu waliosalia walifanya nini? (Kimsingi walikubaliana na mkataba bila hata kuusaini. Ninahisi hawa walikuwa watu ambao hawakuzoea kuwa sehemu ya nyaraka rasmi.)

 

      1. Je, huu mkataba ulitekelezwa dhidi ya wale ambao kimsingi hawakuusaini? (Wale ambao hawakusaini, walikula kiapo na kukubaliana na laana endapo watashindwa kuufuata mkataba. Hili lilikuwa jambo zito.)

 

  1. Vigezo

 

    1. Soma Nehemia 10:30. Je, utakifanya hiki kuwa kipengele cha kwanza kwenye mkataba? (Kwa mujibu wa Mwanzo 2:24, mnakuwa “mwili mmoja” katika ndoa. Unawezaje kubakia kuwa mwaminifu kwa Mungu ikiwa nusu ya sehemu yako ina matamanio na malengo tofauti?)

 

      1. Nilikuwa ninasoma gazeti la washiriki wa zamani wa kanisa wanaopenda kulishambulia kanisa. Mshambuliaji mmojawapo, wakati akielezea msururu wa matatizo yaliyomsababisha aliache kanisa, alibainisha kuwa alimwoa mtu wa imani tofauti na yake. Papo hapo, nikajua sababu halisi ya yeye kuliacha kanisa.

 

    1. Soma Nehemia 10:31. Kwa nini kipengele kinachohusu mwendendo katika siku Sabato kijumuishwe, achilia mbali kuorodheshwa katika sehemu inayofuata (ibara ya pili)?

 

      1. Je, kinafanana na kipengele cha kwanza? (Nadhani hivi vipengele viwili vina lengo linalofanana – kuwafanya watu wa Mungu wasiondoshwe kwenye uhusiano wao na Mungu. Kama Sabato inakuwa siku ya kawaida ya kazi na kufanya biashara, unapoteza muda huo wa pekee wa kuwa na Mungu.)

 

    1. Nehemia 10:32-39 inahusu habari za kulitegemeza hekalu. Vipengele hivi vinakamilisha makubaliano. Unayaelezeaje makubaliano haya? Hayazungumzii chochote kuhusu kukubali kumpenda Mungu. Je, utafanya uamuzi kwenye hivi vipengele vilivyobainishwa kwa ajili ya makubaliano na Mungu?

 

      1. Kwa nini Mungu aanzishe mkataba kwa njia hii? (Ukirudi nyuma na kutafakari jambo hili, mkataba huu unawahusu watu wa Mungu kuchangamana naye. Yesu anaposema “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote,” (Mathayo 22:36-38), nadhani hilo linaakisi huu mkataba. Mkataba ulikuwa ni kuwasaidia watu wakuze uhusiano na Mungu.)

 

  1. Agano la Milele

 

    1. Soma Mwanzo 17:1-2. Vigezo vya mkataba huu ni vipi?

 

      1. Abramu aliahidi nini? (Abramu alitakiwa “kutembea” katika njia ya uaminifu isiyo na mawaa. Nadhani “kutembea” inamaanisha mwelekeo wa jumla wa maisha yake.)

 

      1. Mungu aliahidi nini? (Kwamba Abramu atakuwa na uzao mkubwa.)

 

    1. Soma Mwanzo 17:7. Lengo la msingi la agano hili ni lipi? (Kuwa na uhusiano wa pekee kati ya Mungu, Ibrahim na uzao wa Ibrahim.)

 

    1. Wasomo wengi wa Biblia wanaorodhesha maagano mengi kati ya Mungu na watu wake. Wanazungumzia “Agano la Kale” na “Agano Jipya.” Unadhani lengo la Mungu kwa ajili ya wanadamu limebadilika?

 

      1. Ikiwa sivyo, Mungu ana sababu gani kwa haya maagano tofauti?

 

      1. Unadhani makubaliano kati ya Mungu na wafuasi wake yalibadilika baada ya kufufuka kwa Yesu?

 

    1. Hebu tuchimbue maswali haya kwa kuzingatia agano ambalo Mungu analizungumzia katika Agano la Kale. Soma Yeremia 31:31-32. Mungu anasema nini katika Agano la Kale kuhusu haya maagano mawili? (Anasema kuwa agano jipya halitafanana na agano la kale.)

 

      1. Kwa nini yanatofautiana? (Watu wa Mungu hawakulishika Agano la Kale.)

 

      1. Mungu analibainishaje Agano la Kale? (Analihusianisha na safari alipowatoa katika nchi ya Misri.)

 

    1. Soma Yeremia 31:33. Je, hili Agano Jipya linaondokana na sheria? (Hapana.)

 

      1. Unadhani inamaanisha nini kuiweka sheria “ndani yao” na kuiandika “katika mioyo yao?” (Amri Kumi ziliandikwa kwenye mawe. Hii inaashiria kuwa Agano Jipya linahusisha kutaka kuyatenda mapenzi ya Mungu.)

 

    1. Soma Ezekieli 36:26-27. Kifungu hiki cha Agano la Kale kiaashiria kuwa jambo hili litatendekaje? Kwa nini tutake kumtii Mungu? (Roho Mtakatifu atakuwa ndani yetu. Tutakuwa na “moyo mpya.”)

 

    1. Soma Ezekieli 36:28-29. Wajibu wa Mungu ni upi katika huu mpangilio mpya? (Yeye sio tu Mungu wetu, jambo ambalo ni makubaliano ya kihistoria, bali pia anatuokoa kutoka dhambini.)

 

    1. Soma Yeremia 31:34. Kwa nini hatutahitaji walimu wa Biblia? (Sina hakika kama hii inamaanisha kuwa hatutahitaji walimu wa Biblia kabisa, lakini inaimarisha dhana ya kwamba sheria ya Mungu imeandikwa ndani yetu na mioyoni mwetu.)

 

    1. Soma Waebrania 8:10-12. Unalikumbuka jambo hili? (Ndiyo, hii inanukuu kile tulichokisoma hivi punde katika Yeremia 31!)

 

      1. Rejea nyuma kidogo na utafakari jambo hili. Je, Mungu amebadili agano na wanadamu? (Ndiyo. Soma Waebrania 8:13.)

 

      1. Je, mara zote Mungu amepanga kufanya mabadiliko haya? (Kwa dhahiri inaonekana hivyo. Hapo zamani manabii wa Agano la Kale Yeremia na Ezekieli walizungumzia juu ya ujio wa huu mpangilio mpya.)

 

    1. Hebu tuchunguze hili badiliko. Soma Waebrania 8:1-2. Hii inalihusishaje Agano la Kale na Agano Jipya? (Inatuambia kuwa bado tuna mfumo wa kafara.)

 

    1. Soma Waebrania 8:3-6. Angalia maneno “lililoamriwa juu ya ahadi zilizo bora.” Hiyo inamaanisha nini kwetu? (Tuna vigezo bora zaidi! Mkataba wetu umeboreshwa!)

 

    1. Soma Waebrania 7:23-25. Kwa nini neno hili ni bora zaidi?

 

    1. Soma Waebrania 7:26-27 na Waebrania 10:14. Ni kwa jinsi gani hili ni neno bora zaidi? (Yesu alijitoa kafara mara moja. Hiyo ilishinda tatizo la dhambi milele kwa wale wanaodai kafara yake. Kafara yake moja ilichukua nafasi ya kafara ya kujirudiarudia.)

 

    1. Soma Waebrania 10:4 na Waebrania 10:14. Jambo gani linafanana kati ya Agano la Kale na Agano Jipya? (Dhambi huleta mauti. Huo ndio ujumbe wa vifo vyote vinavyohusishwa na mfumo wa kafara. Habari njema katika kipindi hicho na sasa hivi ni kwamba dhambi zetu hazituletei mauti ya kudumu. Kamwe watu wa Mungu hawakutolewa kafara kwa ajili ya dhambi zao. Mungu alitafuta mbadala wa kifo. Kifo kinachotuweka huru milele kutoka dhambini mwetu ni kifo cha Yesu!

 

    1. Rafiki, unapomjua Yesu unataka kuingia kwenye mkataba wake. Huyu ni Mungu mkuu, mkarimu na mwenye upendo kiasi gani! Je, utafanya uamuzi, sasa hivi, kuikubali ofa ya Mungu?

 

  1. Juma lijalo: Majaribu, Dhiki (Mateso), na Uwanja wa Mapambano.