Somo la 7: Toka Kwenye Tundu la Simba Hadi Tundu la Malaika

(Danieli 6)
Swahili
Year: 
2020
Quarter: 
1
Lesson Number: 
7

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Juma lililopita utawala wa Babeli ulishindwa wakati Danieli aliporejeshwa kwenye nafasi ya juu kabisa – mtu wa tatu katika ufalme kiutawala. Utawala wa Kimedi-Kiajemi ulichukua nafasi na Danieli alikabiliana na machafuko haswaa maishani mwake. Anaweza kuwa na wasiwasi kwamba uhai wake utaondolewa na watawala wapya. Tunafahamu kwamba maisha ya Danieli yapo mikononi mwa Mungu. Hebu tuzigeukie Biblia zetu tuone anachokifanya Danieli na tumfuatilie katika tukio jingine!

 

 1.     Juu

 

  1.     Soma Danieli 6:1-3. Mfalme mpya – Mfalme Dario anao mpango wa kiutawala. Danieli anaangukia wapi kwenye huu mpango mpya? (Danieli anafanya vizuri sana kwenye haya mabadiliko ya ufalme. Kwanza, yeye ni mmojawapo wa viongozi watatu wa juu. Dario anapanga kumweka Danieli kuwa kiongozi juu ya ufalme wote.)

 

   1.     Je, ufalme huu ni utawala wa zamani wa Babeli au ufalme wa sasa wa Umedi-Uajemi? (Hauko wazi. Hata hivyo “ufalme” umetafsiriwa, Danieli ana kazi ya muhimu kupita maelezo.)

 

   1.     Unadhani kwa nini Danieli anaendelea kushikilia nyadhifa zilizo za muhimu sana?

 

  1.     Soma Danieli 6:4. Kitu gani kinawahamasisha hawa maliwali na watawala? Kwa nini hawamtaki Danieli kama bosi wao? (Biblia haisemi chochote.)

 

   1.     Je, ungependa kuwa na bosi mwaminifu, mkweli, na mwenye juhudi? (Inaonekana tatizo ni kwamba atakuwa bosi, na sio kwamba atakuwa bosi mbaya.)

 

   1.     Soma Mhubiri 4:4. Je, wivu ni mzuri? Unadhani wivu ndio hamasa iliyo nyuma ya tamaa yao ya kutafuta mashtaka dhidi ya Danieli?

 

   1.     Ikiwa watawala hawa watatu wanakaa pamoja ili kufanya maamuzi, unadhani Danieli amekuwa akikabiliana na matatizo ya namna gani? Unadhani matatizo ya namna hii ndio yaliyomhamasisha Dario kuamua kumuweka Danieli kuwa mtoa maamuzi?

 

  1.     Soma Danieli 6:5. Viongozi hawa wanafahamuje habari za Mungu wa Danieli? Hii inazungumzia nini kumhusu Danieli? (Jambo zuri kiasi gani kusemwa juu yako! Wewe ni mwaminifu, mchapa kazi, na hodari. Njia pekee ya kuleta mashtaka dhidi yako itakuwa ni kuhusu uaminifu wako kwa Mungu wako.)

 

 1.   Njama

 

  1.     Soma Danieli 6:6-7. Unadhani wote walikubali? (Kwa dhahiri Danieli hakukubaliana na jambo hili.)

 

   1.     Utaona kwamba amri hii itatumika kwa kila mtu. Kwa nini? (Inaficha lengo halisi la hatua hii – kumwua Danieli.)

 

   1.     Kufa kutokana na shambulizi la simba ni jambo la kutisha. Viongozi hawa wanamchukia Daniel kwa kiasi gani? (Kwa dhahiri chuki yao ni ya kishetani.)

 

   1.     Je, unaona kiwango hicho cha chuki dhidi ya Wakristo katika zama za leo?

 

    1.     Kwa nini amri inatangazwa kwa muda wa siku 30 pekee? (Ubashiri wangu ni kwamba washauri hawa wana miungu yao wenyewe wanayotaka kuiabudu. Huu utakuwa muda wa kutosha kuweza kumkamata Danieli.)

 

     1.   Unadhani kwamba Danieli ataahirisha ibada yake kwa Mungu kwa siku 30?

 

  1.     Soma Danieli 6:8-9. Unadhani kwa nini watawala walitaka Dario aliweke jambo hili kwenye maandishi? (Tutajadili jambo hili baadaye.)

 

   1.     Unadhani kwa nini Dario alikubali?

 

   1.     Ikiwa watawala walijua kuhusu imani za kidini za Danieli, je, ungetarajia Dario angefahamu juu ya imani hizo?

 

  1.     Soma Danieli 6:10. Je, madirisha yana haja ya kufunguliwa? Je, itakuwa tatizo kuyafunga katika siku 30 zijazo?

 

   1.     Una hoja gani zinazounga mkono uamuzi wa Danieli? Una hoja gani zinazokinzana na uamuzi wake? (Kuna sababu za msingi katika pande zote mbili. Hebu tuangalie baadhi ya ushauri kwenye sehemu inayofuata katika Agano Jipya.)

 

   1.     Soma Mathayo 6:6. Hii inatuambia kwamba tunayo thawabu kutoka kwa Mungu hata pale tunaposali sirini. Je, ingekuwa dhambi kwa Danieli kufunga madirisha yake?

 

   1.     Soma Mathayo 17:27. Yesu anatoa ushauri unaoepusha kuwakwaza wale tunaotofautiana nao imani za kidini. Je, Yesu asingekubaliana na uamuzi wa Danieli kuhusiana na madirisha yake?

 

   1.     Soma Warumi 14:22. Sura hii inashughulika na “mambo yenye kuzua mjadala” (Warumi 14:1). Suala la kimaadili ni ombi (sala) na sio nafasi ya madirisha, sawa? Tumekuwa tukibishana endapo madirisha yalitakiwa kufungwa. Je, hiyo inamaanisha kwamba Danieli alipaswa kufunga madirisha yake? (Ikiwa madirisha ni jambo lenye kuzua mjadala, basi Danieli angeweza kufanya uchaguzi kwa mujibu wa kifungu hiki. Nina uhakika ningeegemea kwenye uchaguzi “usio wa simba.”)

 

  1.     Angalia tena Danieli 6:10. Angalia maneno yasemayo “kama alivyokuwa akifanya tokea hapo [awali].” Kwa nini Danieli anaongezea jambo hili? (Habadili chochote kwa sababu ya hii amri.)

 

   1.     Hii inaakisi mtizamo gani? (Imani kamili kwa Mungu. Mungu wake ndiye aliyeyashikilia maisha yake, na hakuna chochote ambacho wenye chuki walio chini yake wanachokipanga kinabadili mtizamo wake.)

 

  1.     Soma Danieli 6:11. Kwa nini walienda kama kikundi? (Walikuwa wanaogopa. Walihitaji uthibitisho kwa ajili ya mashtaka yao.)

 

   1.     Ombi la Danieli kwa Mungu ni lipi? (Alikuwa anaomba msada, hakuna shaka kuhusu hali hii.)

                                

   1.     Je, umewahi kusikia msemo usemao, “Mungu anawasaidia wale wanaojisaidia wenyewe?” Je, hiyo ni kweli? Danieli hajisaidii mwenyewe kwa maana ya kuficha ukiukaji wake wa amri.

 

   1.     Ungesalije katika mazingira kama haya? Je, ungemwomba Mungu akupe maelekezo kuhusu uelekeo wa madirisha yako?

 

  1.     Soma Danieli 6:12-13. Hii inaakisije kwenye kundi kuleta mashtaka dhidi ya Danieli?

 

   1.     Angalia jinsi wanavyomwelezea Danieli – mmojawapo wa watumwa! (Tumeona kwenye masomo yetu yaliyopita kwamba haya ni matusi endelevu kwa Danieli.)

 

   1.     Kwa nini walishindwa kubainisa kwamba alikuwa kiongozi (mtawala) mkuu?

 

  1.     Soma Danieli 6:14. Unadhani Dario aliliangaliaje kundi lililotoa taarifa juu ya Danieli? (Anatambua kwamba walimfanyia hila.)

 

  1.     Soma Danieli 6:15. Hii inatufundisha nini kuhusu kuwategemea wanadamu tofauti na kumtegemea Mungu? (Si hata mtu mwenye mamlaka na uwezo mkubwa kabisa kuliko wote katika ufalme huu ambaye angeweza kumwokoa Danieli.)

 

 1. Uokozi

 

  1.     Soma Danieli 6:16. Linganisha mtizamo wa Dario na Nebukadreza? (Nebukadreza alisema kwamba Mungu wa kweli asingeweza kuwaokoa marafiki wa Danieli kutoka kwake. Dario anasema kuwa Mungu wa kweli anaweza kumwokoa Danieli.)

                                

  1.     Soma Danieli 6:17. Unadhani kutia mhuri mlango wa tundu la simba lilikuwa wazo la Dario?

 

  1.     Soma Danieli 6:18-22. Hebu tupitie swali tulilotumia muda mrefu kulijadili hapo awali. Je, ingekuwa heri kufunga madirisha nyumbani kwa Danieli? (Lengo la kufunga madirisha ilikuwa ni kwa ajili ya usalama wa Danieli. Danieli yuko salama, lakini angalia jinsi Dario alivyopata fundisho linalompa Mungu utukufu! Kuyaacha madirisha wazi ni njia bora ya kumpa Mungu utukufu! Utaona kwamba Dario anasema kuwa Danieli anamtumikia Mungu “daima.” Hakuna kuahirisha ibada kwa siku 30 kwa Danieli.)

 

  1.     Soma Danieli 6:23-24. Kifungu kinasema kuwa watu wale “walimshitaki Danieli kwa uongo.” Je, hiyo ni kweli? (Kilichokuwa uongo, ilikuwa ni juhudi za kumwua Danieli. Kilichokuwa uongo ni pendekezo kwamba Danieli alijihusisha kwenye matendo mabaya kwa mfalme.)

 

   1.     Je, matokeo haya ni ya haki? Unadhani Danieli alipendekeza adhabu hiyo? Je, Yesu angependekeza adhabu hiyo?

 

   1.     Angalia matokeo ya Danieli na washtaki wake. Walikuwa na lengo gani katika kumshtaki Danieli? Mambo yalibadilikaje?

 

   1.     Linganisha matokeo ya wivu na uovu na matokeo ya kumtumaini Mungu?

 

  1.     Soma Danieli 6:25-27. Linganisha na Danieli 4:1-3. Ni nani aliye wakala wa Mungu katika kuandaa amri hizi za kifalme duniani kote? (Danieli! Tafakari ushawishi wake kwa ajili ya matendo mema!)

 

   1.     Kama wewe ni mwaminifu, ikiwa lengo lako kuu ni kumpa Mungu utukufu, je, jambo kama hili linaweza kutokea kupitia kwako?

 

  1.     Soma Danieli 6:28. Lengo la kumpa Mungu utukufu linafanikiwaje kwa Danieli?

 

  1.     Rafiki, uaminifu, kinyume na hila, ndio njia ya kuwa baraka kwa wengine na wewe kubarikiwa. Je, utajitoa leo, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, kuwa mwaminifu?

 

 1.   Juma lijalo: Toka Bahari Iliyochafuka Hadi Mawingu ya Mbinguni.