Somo la 8: Toka Bahari Iliyochafuka Hadi Mawingu ya Mbinguni

(Danieli 7)
Swahili
Year: 
2020
Quarter: 
1
Lesson Number: 
8

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Maendeleo mapya juma hili! Danieli ndiye anayepokea njozi, na sio tu mtafsiri wa ndoto za mfalme. Ndoto hii binafsi inaendana na ndoto ya “historia ya ulimwengu” aliyopewa Nebukadreza katika sura ya 2 ya kitabu cha Danieli. Ndoto ile ilihusiana na nguvu ya kisiasa ya mfululizo wa falme kadhaa. Hiyo ilileta mantiki kwa kuwa Nebukadreza alikuwa mtu aliyejali uwezo wa kisiasa. Ndoto tunayojifunza juma hili katika Danieli 7 inahusiana na suala binafsi au la kiroho la falme hizi. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tuone kile tunachoweza kujifunza!

 

 1.     Kuota Ndoto

 

  1.     Soma Danieli 7:1. Je, Danieli ana tatizo la usingizi?

 

   1.     Je, ndoto zinakukosesha usingizi? (Kwa kawaida, ninapoota ndoto niwapo usingizini, huwa ninakuwa na wakati mgumu kuzikumbuka ninapoamka. Kwa ujumla huwa haziingilii usingizi wangu.)

 

   1.     Kuna jambo gani la muhimu kuhusu tarehe ya haya maono? (Majuma mawili yaliyopita tulijifunza mwisho wa utawala wa Belshaza. Inaonekana kwamba Danieli alikuwa amesahauliwa na ofisi ya kifalme, isipokuwa kwa mke wa Nebukadreza, Malkia.)

 

   1.     Belshaza alikuwa na mtazamo gani dhidi ya Mungu wa Danieli? (Alikuwa na uhasama. Yumkini hii ni sababu nyingine kwa ndoto hii kupewa Danieli na si Belshaza.)

 

  1.     Soma Danieli 7:2. Pepo za mbinguni zilivuma kwa nguvu juu ya “bahari kubwa.” “Bahari kubwa” inawakilisha nini? (Maoni ya watu mbalimbali yanatofautiana, lakini ninadhani uwezekano mkubwa ni kwamba hii ni Bahari ya Mediterania. Ni bahari ambayo Danieli alikuwa anaifahamu. Tutakapojifunza zaidi habari za wanyama, tutaona kwamba wote wanapakana na Mediterania.)

 

 1.   Wanyama

 

  1.     Soma Danieli 7:3. Anachokiona Danieli ni wanyama. Ndoto inayoendana na hiyo katika Danieli 2 inahusisha metali tofauti tofauti. Kwa nini kuwakilisha nguvu hizi za kisiasa kama wanyama? (Hapa ndipo tunapoona ubinafsi wa falme. Hii inaakisi kipengele cha kiroho/kimaadili cha falme hizi.)

 

  1.     Mke wangu anapokuwa anasoma kitabu, mara zote huwa anaangalia nyuma ya kitabu ili kujua jinsi kinavyimalizikia. Kamwe huwa sifanyi hivyo. Lakini, tutafanya hivyo hapa. Danieli 7 inatupatia ndoto na kisha tafsiri yake. Tutapenyeza macho kwenye tafsiri ili itusaidie katika uelewa wetu.

 

  1.     Hebu turukie mbele hapa. Soma Danieli 7:9. Utakumbuka katika Danieli 2:34, jiwe linaangamiza sanamu. Tulihitimisha kwamba jiwe hili liliwakilisha nini? (Ujio wa Yesu Mara ya Pili.)

 

   1.     Danieli 7:9 inaashiria nini kuhusu usahihi wa mtazamo wetu kuhusu jiwe? (Inaonesha kwamba tuko sahihi.)

 

   1.     Kwa nini falme hizi zinawakilishwa na wanyama na Ujio wa Mara ya Pili unawakilishwa na mtu? (Inaakisi tofauti kati ya nguvu za kipagani za kidunia na Mungu. Pia inaakisi tofauti kubwa kati ya uwezo wetu na asili yetu na uwezo na asili ya Mungu.)

 

  1.     Hebu tuangalie tena Danieli 7:3. Mwisho wa kifungu hiki unasema kuwa wanyama hawa “wakatoka baharini.” Bado una amani kusema kwamba bahari hii ni ya Mediterania? Kwa nini ni haki kusema kuwa “walitoka” baharini wakati wanapakana nayo tu? (Soma Ufunuo 17:15, Isaya 57:20, na Zaburi 65:7. Vifungu hivi vinatumia “bahari” kama ishara ya watu. Maoni ya Pulpit yanajenga hoja kwamba bahari zinamaanisha “idadi kubwa ya mataifa ya watu wa Mataifa.” Sidhani kama mataifa ya watu wa Mataifa ni sahihi, kwa sababu ya rejea ya “bahari kuu” – ambayo inaashiria Mediterania. Hata hivyo, uelewa wa “bahari” kumaanisha watu wa mahali fulani inaleta mantiki.)

 

  1.     Hebu tuangalie tafsiri ya haraka haraka kwa kusoma Danieli 7:17. Hii inasema nini kuhusu chanzo cha wanyama wanne? (Inasema kuwa walitokea duniani. Hii inaweka wazi kwamba rejea ya “bahari” inawazungumzia watu katika mataifa yanayopakana na bahari.)

 

  1.     Kwa kuiangalia Danieli 7:17 inatuambia kuwa wanyama ni “wafalme wanne.” Hiyo si mahsusi sana. Soma Danieli 7:4 na Yeremia 4:7. Simba huyu anawakilisha ufalme gani? (Sanaa ya Kibabeli ilitumia simba wenye mabawa kuwakilisha ufalme. Yeremia anamrejelea Nebukadreza kama “simba.” Danieli 4 inaweka kumbukumbu kwamba Nebukadreza alikuwa kama mnyama mwenye akili ya mnyama. Lakini, alipomkiri Mungu wa kweli alikuwa kama mtu tena mwenye uwezo wa kufikiri kama mwanadamu.)

 

  1.     Soma Danieli 7:5. Dubu huyu anawakilisha ufalme gani? (Umedi-Uajemi unaifuatia Babeli katika ndoto ya Danieli 2. Mgongo usio sawa unaakisi utawala wa Waajemi dhidi ya Wamedi. Mfananisho wa dubu unatuambia kuhusu uwezo wa ufalme huu.)

 

  1.     Soma Danieli 7:6. Chui huyu anawakilisha ufalme gani? (Uyunani. Nne ni ishara ya kitarakimu ya nguvu ya Kiyunani, kwa mujibu ya maoni ya mtu mmoja, na kasi ya ushindi wa Alexander Mkuu inafahamika vizuri. Mwendo kasi huu unawakilishwa kwenye mabawa manne.)

 

  1.     Soma Danieli 7:7. Mnyama huyu ana utofauti gani? (Haonekani kuwa mnyama ambaye Danieli anamtambua.)

 

  1.     Soma Danieli 7:19 na Danieli 7:23. Huyu mnyama wa nne ni nani? (Kwa kutumia Daniel 2 kama rejea, huu unaonekana kuwa Ufalme wa Rumi, kwa kuwa ni ufalme wa nne.)

 

 1. Vichwa na Pembe

 

  1.     Danieli 7:7 inatuambia kuwa hili jitu la kutisha la nne lina pembe kumi. Hebu tusome Danieli 7:8 na tuangalie Danieli 7:24. Hizi pembe kumi ni kitu gani? (Pembe hizi ni falme zinazotoka kwenye ufalme wa Rumi.)

 

  1.     Kati ya hawa wafalme kumi, kwa mujibu wa Danieli 7:7 inatokea pembe “ndogo” inayowang’oa wafalme watatu. Hii pembe ndogo sio mnyama, inaelezewa kama mtu, kama mfalme. Hebu tuangalie Danieli 7:20-21 na Danieli 7:24-26 ili tuone pembe ndogo inawakilisha nini. Ni kitu gani hico? (Ni mamlaka yenye kutesa. Inaanzisha vita dhidi ya “watakatifu” na kuwashinda. “Itawakandamiza na kuwatesa” watu wa Mungu. Inajaribu kubadili majira na sheria. Inapata mafanikio kwa “wakati, na nyakati mbili, na nusu wakati.”)

 

   1.     Utakumbuka kwamba tunazungumzia historia ya kale. “Mfalme” gani anaibuka kutoka katika Ufalme wa Rumi na kuwakandamiza watu wa Mungu?

 

   1.     Unadhani “pembe ndogo” ni kitu gani?

 

   1.     Fundisho maarufu ni kwamba “pembe ndogo” ni Mfalme mdogo wa Seleucide aliyeitwa Antiokasi Epifanesi aliyetawala kwa miaka kumi na moja kuanzia mwaka 175-164 K.K. Antiokasi aliingia madarakani baada ya kifo cha Alexander Mkuu mwishoni mwa ufalme wa Kiyunani. (Angalia, Goldstein, Graffiti in the Holy of Holies, p. 39-42). Je, Antiokasi Epifanesi anaendana na maelezo ya pembe ndogo? (Hapana. Muda uliobainishwa sio sahihi kabisa. Antiokasi aliingia madarakani kabla, na sio baada, ya Ufalme wa Rumi. Hazina ya Maarifa ya Maandiko yananukuu kwamba falme kumi ambazo Ufalme wa Rumi ya magharibi uligawanyika ilitokea kati ya mwaka 356 B.K na mwaka 526 B.K. Hivyo, Antiokasi ni zaidi ya miaka 500 ya karibu sana kuendana na unabii huu. Kwa kuongezea, miaka yake kumi na moja ya utawala haionekani kuendana na kipindi cha hukumu ya mwisho. Angalia Danieli 7:21-22.)

 

  1.     Angalia tena Danieli 7:25. Inasema kwamba pembe ndogo inajaribu kubadili “majira na sheria.” Unadhani hii inamaanisha nini? (Linganisha na Danieli 2:19-21. Kubadili nyakati na majira ni haki ya pekee ya Mungu. Hivyo, hii pembe ndogo na mateso yake kwa watakatifu, na madai yake ya haki ya pekee ya Mungu inaonekana kuwa kwa kiasi fulani ni nguvu ya kidini.)

 

   1.     Unapofikiria wakati ambao Mungu ameuweka kama sheria, kitu gani kinakujia akilini? (Kinachonijia akilini ni Kutoka 20:8-11, amri ya ibada ya Sabato.)

 

  1.     Kwa kuwa sasa tumelijadili hili zaidi, unadhani “pembe ndogo” inawakilisha nini? (Kuna kutokubaliana kati ya watoa maoni mbalimbali katika jambo hili, lakini ninaamini ushahidi unaashiria kwa dhahiri kabisa kwamba hii ni Rumi ya Kipapa. Uliibuka baada ya Rumi ya Kipagani (Ufalme wa Rumi) ilipokuwa inasambaratika. Ilikuwa tofauti na falme nyingine kwa maana ya kwamba madai yake ya mamlaka ya kidini yalikuwa makubwa zaidi kuliko madai yake ya mamlaka ya kidunia. Unajitambulisha na kujifananisha na mwanadamu. Rumi ya Kipapa inajifananisha na Papa. Rumi ya Kipapa ilikuwa na kipindi cha kusikitisha katika Zama za Kati ilipowatesa wale ambao hawakukubaliana nayo. Ninawataka wasomaji wangu wafahamu kwamba nina historia ndefu ya kuwatetea mahakamani uhuru wa dini wa Wakatoliki na taasisi za Kikatoliki. Ninapenda na kupendezwa na jinsi Kanisa Katoliki linavyosimama kidete dhidi ya uaviaji mimba na uovu mwingine. Lakini, nadhani unabii huu uko dhahiri.)

 

 1.   Hukumu

 

  1.     Angalia tena Danieli 7:25, lakini mara hii angalia sehemu ya mwisho. Nini kinatokea kwa mateso haya? (Yanakoma baada ya “wakati, na nyakati mbili na nusu wakati.” Baadhi ya watoa maoni wanatoa sababu za msingi kwamba hii ni miaka 3.5, au siku 1,260. Kwa kutumia kanuni ya unabii ya “mwaka-siku” hii inawakilisha miaka 1,260. Angalia pia Ufunuo 11:3 na Ufunuo 12:6.)

 

  1.     Soma Danieli 7:26-27. Hatimaye nini kitatokea? (Mungu analeta “ufalme wake wa milele!” sisi ndio huo ufalme!)

 

  1.     Rafiki, hapa habari njema ni zipi? (Mungu anashinda! Watakatifu wake wanashinda! Je, utakuwa na ujasiri na uhakika kwamba Mungu ndiye mwenye udhibiti, bila kujali chochote kinachotokea?)

 

 1.     Juma lijalo: Toka Unajisi Hadi Usafi.