Somo la 9: Toka Unajisi Hadi Usafi

(Danieli 8)
Swahili
Year: 
2020
Quarter: 
1
Lesson Number: 
9

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Miaka miwili baada ya ndoto yake ya kwanza, Danieli anaota akitembea kando ya mto ambapo ghafla anajikuta yuko uso kwa uso na kondoo mume mwenye nguvu aliye na pembe mbili kubwa – na hakuna mtu aliye karibu wa kumwokoa. Matokeo yake ni kwamba ndoto yake haihusu sana suala la hatari, au tukio lisilo la kawaida, kama ilivyo kuhusu mustakabali ujao. Hebu tuzame kwenye ndoto ya Danieli na tuone kile tunachoweza kujifunza juu ya mustakabali!

 

 1.     Kondoo Mume

 

  1.     Soma Danieli 8:1-3. Ungekuwa na mwitiko gani kama ungeota ndoto hii? Danieli aliona wanyama wa kutisha sana kwenye ndoto yake ya awali, unadhani sasa ameogopeshwa?

 

  1.     Soma Danieli 8:4. Kutokana na muktadha wa ndoto zilizopita, una maoni gani juu ya kondoo huyu? (Kwa dhahiri anaonekana kuwa na uwezo mkubwa hapa duniani. Ufalme unaotawala mataifa mengine.)

 

 1.   Beberu

 

  1.     Soma Danieli 8:5-8. Una maoni gani kuhusu beberu huyu mwenye pembe iliyovunjika? (Haya yanaonekana kuwa mamlaka mengine ya dunia yanayoushinda ufalme wa “kondoo.”)

 

 1. Gabrieli Katika Kondoo na Beberu

 

  1.     Hebu turuke chini kidogo katika sura hii. Soma Danieli 8:15-16. Kwa nini Danieli anaandika kwamba “sauti kama ya ya mwanadamu?” Kwa nini asiseme tu kwamba, “mwanadamu akasimama mbele yangu?” (Danieli anatuambia kwamba huyu hakuwa mwanadamu. Anafanana tu na mwanadamu.)

 

   1.     Nani amesimama mbele ya Danieli? (Gabrieli.)

 

    1.     Gabrieli ni nani? (Soma Luka 1:19. Anasimama mbele za Mungu.)

 

    1.     Tofauti na kuzungumza na Danieli, Gabrieli ameshughulikia utume gani mwingine wa muhimu? (Soma Luka 1:26-28. Gabrieli alipeleka ujumbe wa ujio wa Yesu kwa Mariamu!)

 

   1.     Danieli 8:16 inataarifu kwamba “sauti ya mwanadamu” inampatia Gabrieli maelekezo. Nani anayempatia Gabrieli maelekezo? (Mungu!)

 

    1.     Hii inaashiria nini kwako kuhusu ujumbe wa Gabrieli kwa Danieli? (Mungu anapokuwa na ujumbe wa muhimu, anamtuma Gabrieli.)

 

  1.     Soma Danieli 8:17. Danieli anakuwa na mwitiko gani kwa Gabrieli? Kwa nini?

 

   1.     Gabrieli anasema kuwa ndoto hii inamaanisha nini? (Wakati wa mwisho.)

 

  1.     Soma Danieli 8:18. Nini kinatokea hapa? Je, bado Danieli anaota? (Ama hii ni ndoto ndani ya ndoto, au Danieli anatoka kwenye hali yake ya ndoto ili kusikiliza maelezo ya Gabrieli.)

 

  1.     Soma Danieli 8:19. Gabrieli anasema kwa mara ya pili kwamba hii inahusu wakati wa mwisho. Unatoka na hitimisho gani baada ya Gabrieli kuuita wakati wa mwisho “ulioamriwa?” (Mungu ana muda maalumu mawazoni mwake na angalao Danieli anashirikishwa baadhi ya taarifa.)

 

  1.     Soma Danieli 8:20-22. Wanyama hawa wawili ni kitu gani? (Umedi, Uajemi na Uyunani.)

 

   1.     Je, tumeliona hili hapo kabla? (Bashiri! Tuliona ishara ya hizi falme mbili kwenye ndoto ya Nebukadreza katika Danieli 2 na tuliziona tena kwenye ndoto ya Danieli katika Danieli 7.)

 

   1.     Kwa nini Mungu anaendelea kurudia unabii ule ule? (Je, umewahi kusikia kwamba unatakiwa kurudia jambo mara tatu ili msikilizaji wako aweze kuelewa? Kwa dhahiri Mungu anataka tuuelewe ujumbe huu. Kwa kuongezea, kwa kila ndoto mpya inaonekana tunapata taarifa zaidi. Mungu anaweza kuwa anarudia taarifa ya zamani ili kutusaidia kuelewa vizuri zaidi taarifa mpya.)

 

 1.   Pembe

 

  1.     Hebu turejee nyuma na tuendelee na kisa cha ndoto kilichosalia. Soma Danieli 8:8-12. Sasa tusikie anachokisema Gabrieli kuhusu jambo hili. Soma Danieli 8:22-23. Je, tumeona nguvu ya “pembe” hapo kabla? (Somo letu la Danieli 7 liliifunua “pembe ndogo” (Danieli 7:8). Gabrieli anasema kwamba pembe hii ni “mfalme mwenye uso mkali, afahamuye mafumbo.”)

 

  1.     Unadhani pembe “ndogo” ya Danieli 8 ni sawa na pembe ndogo ya Danieli 7? (Hii inatuweka katikati ya mjadala mkubwa wa kihistoria. Wanamaoni wengi wanaamini kwamba pembe hizi za Danieli 7 na 8 ni kitu kimoja, na kwamba zinawakilisha Antiokasi Epifanesi, mfalme wa Seleucid ambaye hapo kabla tulijifunza kuwa alitawala kwa miaka 11 (mwaka 175-164 K.K.). Tulipojifunza Danieli 7 (Somo la 8) tuliona kwamba muda uliokisiwa haukuwa sahihi kwa pembe ndogo kuwa Antiokasi. Sio tu kwamba Antiokasi alitangulia miaka 500 zaidi (akitawala baada ya Uyunani, na si utawala wa Rumi), lakini utawala wake haukuendelea hadi mwisho wa wakati.)

 

   1.     Je, muda unaokisiwa sio sahihi kwa Antiokasi kuwa pembe ya Danieli 8:9? (Kipindi cha Antiokasi kinaendana vizuri zaidi na Danieli 8. Alitoka Ufalme wa Kiyunani uliovunjikavunjika (ambayo ndio ilikuwa sababu asingeweza kuwa “pembe ndogo” ya Danieli 7 – iliyotokana na Ufalme wa Rumi uliovunjikavunjika). Binafsi naona wanamaoni wengi wanaoielewa pembe ya Danieli 8 kuwa ni Antiokasi, wanasoma tafsiri yao kwenye Danieli 7 – ambapo Antiokasi haendani nayo – na wanamwelewa kuwa ni “pembe ndogo” ya Danieli 7.)

 

   1.     Vipi kama tukibadili hili, tunaweza kusoma uelewa wetu wa “pembe ndogo” wa Danieli 7 (kwamba pembe ni awamu ya Kipapa ya Ufalme wa Rumi) kwenye Danieli 8? Je, muda unaokisiwa unaendana na Upapa wa Rumi?

 

    1.     Soma tena Danieli 8:8-9. Je, pembe inajitokeza kutoka kwenye mojawapo ya pepo nne au mojawapo ya pembe nne? (Haiko wazi. Mtazamo mmoja ni kwamba moja kati ya hizi pembe nne ni Ufalme wa Rumi unaoufuatia Umedi na Uajemi na Uyunani, na awamu ya Kipapa ya Rumi inaibuka kutoka kwenye hiyo pembe. Hiyo inaifanya hii ifanane zaidi na Danieli 7.)

 

  1.     Hebu tupitie tena Danieli 8:9-12. Tafakari maelezo yaliyosalia ya pembe hii. Je, yanaendana vizuri zaidi na Rumi ya Kipagani na ya Kipapa au Antiokasi? (Maelezo ya mamlaka ya pembe hii yanaendana au yanazidi maelezo ya mamlaka ya kondoo na beberu. (Kwa mfano, kondoo anaitwa “mashuhuri” (kifungu cha 8) na beberu anaitwa “mashuhuri sana” (kifungu cha 8). Tafsiri nyingi za Biblia (lakini si tafsiri ya NIV) zinatafsiri maelezo ya pembe (kifungu cha 9) kama “exceedingly great” KJV, NKJV, ASV, RSV). Kwa kuwa pembe inaelezewa kuwa kuu kuliko Umedi na Uajemi na Uyunani, haionekani kuwa sahihi kuhitimisha kwamba utawala wa miaka 11 wa Antiokasi, mfalme mdogo wa Seleucid, ni mkuu kuliko falme za Uajemi na Uyunani! Kwa upande mwingine, ufalme wa Rumi (katika awamu zake zote mbili za Kipagani na Kipapa, kwa dhahiri zinalinganishwa na falme za Uajemi na Uyunani.)

 

   1.     Usiku uliopita nilikuwa ninasoma maoni ya rafiki yangu, marehemu William H. Shea, kuhusu pembe ndogo ya Danieli 8. William Shea ni mtaalam wa dunia wa Danieli 8. Anahitimisha kwamba hii pembe ndogo si Antiokasi, bali ni Rumi ya Kipagani na ya Kipapa. William aliandika kwamba kabla ya “Vuguvugu la Miller” (vuguvugu kubwa la kiteolojia la mwanzoni mwa karne ya 19 lililojikita kwenye Danieli) kwa ujumla wasomi wa Kikristo walikubaliana kwamba pembe ndogo ya Danieli 7 ilikuwa ni Rumi, lakini waligawanyika kwenye suala la endapo pembe ndogo ya Danieli 8 ilikuwa sawa na ile ya Danieli 7 au iliwakilisha “Utume na Uasisi wa Uislamu” (Mohammedanism).)

 

   1.     Je, Rumi (Danieli 8:11) ilipaangusha patakatifu na kukomesha sadaka za kila siku? (Warumi waliangamiza hekalu la Mungu mwaka 70 B.K.)

 

  1.     Hebu tusome tena anachokisema Gabrieli katika Danieli 8:23-25. Mkuu wa wakuu anayerejelewa katika kifungu cha 25 ni nani? (Lazima atakuwa Yesu.)

 

   1.     Je, Rumi ilichukua msimamo dhidi ya Yesu?

 

   1.     Je, Rumi (Danieli 8:10) ilifika mbinguni, ikaangusha sehemu ya raia wa mbinguni hadi chini na kuwakanyaga? (Rumi ilimsulubisha Yesu. Nadhani kwa haraka haraka hii inaendana na maelezo ya kuwakanyaga raia wa mbinguni na kusimama dhidi ya Mkuu wa wakuu.)

 

 1.     Hekalu (Patakatifu)

 

  1.     Soma Danieli 8:13. Tukio gani linaelezewa? (Sehemu ya mwisho ya ndoto ya Danieli inayoelezea uangamivu wa hekalu. Mara mbili tunaambiwa kuwa ndoto hii inahusu mwisho wa wakati.)

 

  1.     Soma Danieli 8:14 na Danieli 8:25-26. Nyakati za jioni na asubuhi “2,300” ni muda kiasi gani? (Ikiwa inamaanisha siku halisi, itakuwa zaidi kidogo ya miaka sita. Ikiwa ni unabii, ambapo siku moja ni sawa na mwaka mmoja (angalia Ezekieli 4:6), hiyo itaendana vizuri zaidi na jambo linaloelezea uangamivu wa hekalu na kisha kuliweka wakfu upya.)

 

   1.     Nini kinatokea mwisho wa kipindi hiki – kuliweka wakfu upya hekalu maana yake ni nini? (Vuguvugu la Miller nililolibainisha hapo awali lilidhani kwamba ilimaanisha Ujio wa Yesu Mara ya Pili. Walifanya hesabu (angalia somo letu juma lijalo) na wakafikia mwaka 1843-44. Ningekuwa ninaishi katika kipindi hicho, ningekubaliana kwa sababu ndoto za Danieli 2 na 7 zinaishia na ujio wa Mara ya Pili. Kwa dhahiri, nisingekuwa sahihi.)

 

   1.     Kamwe hekalu la Yerusalemu halikujengwa upya baada ya mwaka 70 B.K., hivyo kamwe halikuwekwa wakfu upya. Hata hivyo, Waebrania 8 inatuambia kwa mahsusi kwamba kuna patakatifu mbinguni. Je, hicho ndicho anachokimaanisha Gabrieli?

 

  1.     Rafiki, Mungu ana ujumbe wa muhimu wa unabii kwa ajili yetu. Je, utaendelea kujifunza pamoja nasi ili kuelewa vizuri ujumbe wa Mungu kuhusu mwisho wa dunia?

 

 1.   Juma lijalo: Toka Ungamo Hadi Faraja.