Somo la 10: Toka Ungamo Hadi Faraja

(Danieli 9)
Swahili
Year: 
2020
Quarter: 
1
Lesson Number: 
10

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Tulipojifunza Danieli 7 na 8, je, ulijiuliza kwamba, “Utakaso wa patakatifu una umuhimu gani kwangu?” Natumaini ulibaini umuhimu kwenye masomo haya. Lakini, ikiwa ulikuwa na hisia hizi, unaweza kuwa na uhakika kwamba Danieli hakuwa nazo. Dhana ya kuwa na patakatifu tena ilikuwa mada ya mvuto mkubwa kwa Danieli. Ingemwambia lini watu wake wangeruhusiwa kurejea katika nchi yao na kulijenga upya hekalu. Hebu tuzame kwenye somo letu la Danieli na tujifunze zaidi!

 

 1.     Sala (Ombi)

 

  1.     Soma Danieli 9:1-3. Danieli alikuwa akiomba lini? (Katika mwaka wa kwanza wa mfalme Dario. “The Bible Knowledge Commentary” inaubainisha huu kama mwaka 539 K.K. – miaka 66 baada ya Danieli kufukuzwa mbali na kwao.)

 

   1.     Je, Dario alikuwa rafiki wa Mungu wa kweli? (Ndiyo! Alimpenda Danieli na baada ya Danieli kukingwa dhidi ya simba, Dario alitangaza ukweli kuhusu Mungu wa kweli wa mbinguni. Danieli 6:25-27.)

 

  1.     Angalia tena Danieli 9:2. Danieli anaomba kuhusu jambo gani? (Danieli anaomba kuhusu unabii wa Yeremia (Yeremia 29:10) kwamba kuangamizwa kwa Yerusalemu na Wayahudi kuwa mateka kutadumu kwa miaka 70 pekee. Kwa kuwa Danieli yupo ugenini kwa miaka 66, tunaweza kuelewa kwa nini anaomba kuhusu hii mada.)

 

  1.     Soma Danieli 9:4-19. Ni kwa msingi gani Danieli anamwomba Mungu kufikiria na kutenda jambo juu ya ahadi yake kuhusu Yerusalemu? (Danieli 9:16: Mungu ni mwenye haki. Danieli 9:19: jina la Mungu.)

 

   1.     Hebu tujikite kwenye Danieli 9:18. Matendo yetu mema yanahusianaje na rehema za Mungu? (Danieli anaashiria kwamba Mungu ni mwenye rehema kwetu hata pale tunapokuwa hatuna haki.)

 

   1.     Kuna fikra ya kiteolojia katika Biblia iliyopo kwenye Kumbukumbu la Torati 28 (na katika maeneo mengine) inayosema kwamba Mungu anatubariki tunapokuwa watiifu, na tunadhuriwa tusipokuwa watiifu. Unalinganishaje jambo hili na Danieli 9:18? (Kumbukumbu la Torati 28 inaakisi kanuni za msingi za maisha kwamba amri za Mungu zipo ili kuyaboresha maisha yetu. Zikiuke nawe utajihatarisha mwenyewe. Lakini, rehema za Mungu zipo kwa ajili yetu hata pale tunapofanya maamuzi mabaya.)

 

 1.   Gabrieli na Jibu

 

  1.     Soma Danieli 9:20-21. Nani anayejitokeza? (Gabrieli – malaika aliyekuja kumwona hapo kabla. Hapo awali tulijifunza kwamba Gabrieli anasimama mbele za Mungu na kumpatia Mariamu ujumbe wa Mungu kuhusu Yesu.)

 

   1.     Una maoni gani kuhusu muda ambao jibu la Mungu linatolewa? (Gabrieli aliondoka mbinguni wakati Danieli alipoanza sala yake na akawasili wakati bado akiendelea kuomba!)

 

    1.     Hiyo inazungumzia nini juu ya muda wa safari kati ya hapa duniani na mbinguni?

 

   1.     Gabrieli alijitokeza katika muda gani wa siku? (Wakati wa dhabihu ya jioni.)

 

    1.     Ni “dhabihu gani ya jioni” anayoizungumzia Danieli? (Danieli alikuwa amejikita sana kwenye huduma ya patakatifu kiasi kwamba “anaelezea muda” kutokana na muda ambao dhabihu ya jioni ingekuwa inatolewa. Kimsingi hakuna dhabihu inayotolewa duniani kwa sababu hekalu lilishaangamizwa kitambo sana.)

 

  1.     Soma Danieli 9:22-23. Kuyafahamu mambo gani? Ni mada gani ambayo Danieli anahitaji ufahamu mkubwa? (Kwa dhahiri ni mada ya hekalu kwenye ndoto ya Danieli 8. Danieli anafikiria na kuomba kuhusu patakatifu (Danieli 9:17).  Mara ya mwisho Gabrieli alipozungumza naye (Danieli 8:14) ilikuwa inahusu huduma ya patakatifu (Danieli 8:14). Lakini, Danieli hakuelewa (Danieli 8:27). Hivyo, Gabrieli anaendelea kutokea pale alipoachia na kuendeleza mjadala wake wa awali.)

 

  1.     Jambo la muhimu ni neno la Kiebrania lililotumika kwenye ndoto katika Danieli 8:26, 8:27 na 9:23 ni neno lile lile: “mareh.” Hivyo, utambuzi na uelewa wa Danieli kuhusu “ndoto” katika Danieli 9:23 ni sawa na ndoto iliyozungumziwa katika Danieli 8:26 & 27.

 

  1.     Soma Danieli 9:24. Je, hii ni habari njema? (Inaonekana kuwa hivyo kwa kuwa inabainisha “Patakatifu pa Patakatifu” ambapo ni sehemu ya hekalu.)

 

   1.     “Sabini ‘saba’” ni neno la ajabu. Unadhani “saba” inamaanisha nini? (Kimantiki “saba” inamaanisha juma moja. Juma moja lina siku saba. Hivyo, Gabrieli anazungumzia majuma 70.)

 

   1.     Majuma sabini ni marefu kiasi gani? (Majuma sabini ni takriban mwaka mmoja na theluthi moja.)

 

  1.     Soma Danieli 9:25. Unadhani “Aliyetiwa Mafuta” ni nani? (Angalia Matendo 10:37-38. Hii inamrejelea Masihi – Yesu.)

 

   1.     Kwa kuchukulia kwamba kipindi cha jumla ni kutoka kipindi cha kutangazwa kuijenga upya Yerusalemu, hadi kipindi cha Yesu, je, tunaweza kuwa tunazungumzia muda wa zaidi kidogo ya mwaka mmoja? (Hapana. Kama ilivyo kwa Danieli 8, haya majuma 70 ni ya kiishara (siku 1 = mwaka 1). Hivyo, 70 x 7 (siku 490) yumkini zinamaanisha miaka 490. Hii inaimarisha hitimisho letu la awali kwamba siku 2,300 za Danieli 8:14 zinaashiria miaka 2,300 na sio siku.)

 

  1.     Angalia tena Danieli 9:24-25. Nini kinatokea katika kipindi hiki cha miaka 490? (Muda unatolewa kwa Wayahudi na Yerusalemu ili “kukomesha makosa, kuishiliza dhambi, kufanya upatanisho kwa ajili ya uovu na kuleta haki ya milele.”)

 

   1.     Wahayudi wangewezaje kuishiliza dhambi na kuleta haki ya milele? (Wasingeweza. Hii inatoa ushahidi zaidi kwamba “Aliyetiwa Mafuta” ni Yesu. Yesu alitoa hakikisho la ukomo wa dhambi na uzima wa milele kwa wenye haki.)

 

  1.     Soma Danieli 9:26. Inamaanisha nini kwa Masihi “kukatiliwa mbali” au “kuuawa?” (Inaonekana kama vile Masihi ameuawa. Linganisha unabii wa Kimasihi wa Isaya 53:7-8.)

 

  1.     Hebu tuangalie kwa ukaribu zaidi tarakimu hizi tunazoziona katika Danieli 9:24-27. Unaona vipindi vya aina ngapi? (Vitatu. Jumla, miaka 490 (70 x 7) inapatikana katika kifungu cha 24. Mgawanyo wa kwanza wa miaka hii ni miaka 49 (“saba zikiwa saba”) na unapatikana katika kifungu cha 25. Mgawanyo wa pili wa miaka 434 (62 x 7) unapatikana katika vifungu vya 25-26. Mgawanyo wa mwisho ni miaka saba “’saba’ moja” na unapatikana katika kifungu cha 27. Kwa pamoja jumla yake ni miaka 490 au “saba” sabini.)

 

   1.     Nini kinatokea katika kipindi cha miaka 49? (Inaonekana hii inarejelea ujenzi upya wa Yerusalemu.)

 

   1.     Nini kinatokea mwishoni mwa miaka 483 (49 + 434)? (Masihi anakuja (Danieli 9:25). Ingawa kulikuwa na amri tatu za ujenzi upya wa Yerusalemu, maoni kadhaa yana utofauti mdogo katika tarehe za kuanza. Maoni ya “The SDA Bible Commentary” yanabainisha amri ya kuujenga upya kama mwaka 458/457 K.K. (Amri ya Artashasta. Angalia Ezra 7:1-26.) Kwa kuanzia mwaka 457 K.K., miaka 483 inatupeleka hadi mwaka 27 B.K. – mwaka wa ubatizo wa Yesu na mwanzo wa huduma yake kwa umma.)

 

   1.     Nini kinatokea katika kipindi cha miaka saba? (Danieli 9:26 inatuambia kuwa baada ya miaka 483 Masihi “atakatiliwa mbali” na Danieli 9:27 inatuambia kuwa Masihi atakomesha sadaka na dhabihu katikati ya “saba.” Tukiendelea na kipindi chetu kuanzia mwaka 457 K.K. hadi mwaka 27 A.D., miaka ya ziada 3-4 (katikati ya saba) hutufikisha mwaka 31 A.D. – mwaka wa kusulubiwa kwa Yesu. Maelezo ya Gabrieli yanaleta mantiki kwa sababu kusulubiwa kwa Yesu kulikomesha hitaji la kafara za wanyama katika hekalu jipya la Yerusalemu.)

 

    1.     Unaelewaje (Danieli 9:27) “uthabiti” wa agano kwa “saba” iliyosalia? (Katika Mathayo 21:43-45 Yesu anatabiri kwamba ufalme wa Mungu utachukuliwa kutoka kwa maafisa wa Kiyahudi waliomkataa Yeye na kupewa watu wengine – ambao, kama tunavyoona kwenye kitabu cha Matendo, uliwajumuisha Mataifa. Maoni ya “The SDA Bible Commentary” yanabainisha kwamba mwaka 34 K.K (miaka 7 baada ya mwaka 27 K.K.) yaliashiria kupigwa mawe kwa Stefano na mwanzo wa kupeleka injili kwa Mataifa. Angalia Matendo 7 & 8.)

 

    1.     Unaielewaje rejea ya Danieli 9:26 inayohusu kuuangamiza “mji na patakatifu?” (Rumi iliiangamiza Yerusalemu na hekalu lililojengwa upya mwaka 70 B.K. Hii inaendana na maelezo ya “mtawala atakayekuja.” Zaburi 79:1 inatabiri kwamba hekalu “limenajisiwa” na wale wanaoifanya Yerusalemu kusalia kuwa kifusi – hivyo kuendana na “chukizo linalosababisha uharibifu.)

 

  1.     Ungejisikiaje kama ungekuwa Danieli ukisikiliza ujumbe huu kutoka kwa Gabrieli? (Kama ambavyo ninasikia habari njema, kisha ninasikia habari za kutisha. Hekalu litajengwa upya na kisha kuangamizwa tena!)

 

  1.     Unajisikiaje, maelfu ya miaka baadaye, kusoma tafsiri ya ndoto ya Gabrieli? (Inanipatia uthibitisho wa ziada kwamba: a) Mungu anaishikilia historia; b) Yesu ndiye Masihi aliyetabiriwa; na, kwa kuwa Yesu alikuja mara ya kwanza kama ilivyotabiriwa, c) Kwamba Mungu atasimamia neno lake la ujio wa Yesu Mara ya Pili!)

 

  1.     Rafiki, Yesu anakuja tena! Je, uko tayari? Je, umetubu dhambi zako na kutegemea rehema za Mungu kwa ajili ya wokovu wako?

 

      Juma lijalo: Toka Vita Hadi Ushindi.