Somo la 13: Toka Mavumbini Hadi Kwenye Nyota

(Danieli 12)
Swahili
Year: 
2020
Quarter: 
1
Lesson Number: 
13

Somo la 13: Toka Mavumbini Hadi Kwenye Nyota

 

(Danieli 12)

 

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2017, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Juma hili tunahitimisha njozi ya mwisho ya Danieli na kitabu cha Danieli kwa ujumla. Je, uko tayari kwa ajili ya marejeo ya Yesu na kukomesha dhambi na kifo? Hii sura ya mwisho sio tu kwamba inazungumzia kuhusu kukoma kwa dhambi, bali pia inatupatia taarifa ya ziada kwenye kile tulichoambiwa hapo awali kuhusu njozi. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tuone kama tunaweza kujifunza zaidi!

 

 1.     Wakati wa Mwisho

 

  1.     Soma Danieli 12:1. Je, unaona kama vile kuna mvutano katika kifungu cha kwanza? Tunaye Mikaeli, “asimamaye upande wa watu wako” na “wakati wa taabu” ambao haujawahi kutokea. Unazielewaje hizo kauli mbili? (Badala ya mvutano, inaonekana kwamba Mikaeli anakuja wakati mwafaka kabisa kutusaidia.)

 

   1.     Mikaeli analeta msaada wa namna gani? (Watu wa Mungu wanaokolewa. Watu wa Mungu wanaelezewa kama “kila mmoja atakayeonekana ameandikwa katika kitabu kile.”)

 

    1.     Ni kitabu gani hiki? (Soma Ufunuo 7:13-14 na Ufunuo 3:5. Hiki ni kitabu cha uzima. Walioandikwa humo ni wale wanaookolewa kwa imani katika Yesu.)

 

    1.     Utaona kwamba Danieli 7:13-14 inasema kuwa hawa wametoka katika “dhiki kuu.” Je, hiyo ni mada inayofahamika? (Inafanana kabisa na kile tunachokisoma katika Danieli 12:1.)

 

  1.     Angalia tena sehemu ya kwanza ya Danieli 12:1. Inasema, “Wakati huo.” Ni wakati gani huu? (Soma Danieli 11:40. Hii ni rejea ya “wakati wa mwisho” tuliyoiangalia katika sehemu iliyopita. Sina uhakika wakati wa mwisho unakwenda hadi lini, lakini wafalme wa Kaskazini na Kusini wapo kwenye pambano kubwa. Hii inathibitisha mawazoni mwangu kwamba sasa hatuwazungumzii majenerali waliomfuatia Alexander Mkuu.)

 

  1.     Soma Danieli 12:2. Hii inatuambia nini kuhusu hali ya wafu? (Inasema kuwa kifo ni sawa na “usingizi.” Itakuwa jambo la ajabu kuwa na roho iliyo na ufahamu mbinguni na wakati huo huo iwazungumzie wafu kama watu waliolala na kisha waje wakiwa “macho.” Huu ni uthibitisho madhubuti juu ya fundisho la “kusinzia kwa roho” – imani ya kwamba wafu hawana fahamu badala ya kwamba wana ufahamu mbinguni.)

 

   1.     Tunakabiliana na matokeo ya aina gani mawili maishani? (Uzima wa milele au aibu na kudharauliwa milele.)

 

    1.     Unataka matokeo gani?

          

    1.     Ni nani pekee, anayepewa uzima wa milele? (Wenye haki pekee ndio wanaopewa “uzima wa milele.” Wapotevu wanapewa aibu na kudharauliwa milele. Utaona kwamba wapotevu pia hawapewi uzima wa milele.)

 

  1.     Soma Danieli 12:3. Lengo lako ni lipi? (Kuwa na “hekima” inamaanisha kwamba umempokea Yesu kama Mwokozo wako na unautamani mwongozo wake kwa ajili ya maisha yako. Kuwaleta wengine kwenye wokovi inamaanisha kwamba umetumia hekima yake ya kimungu maishani mwako. Umewashirikisha wengine hiyo hekima. Sio tu maarifa ya kinadharia.)

 

 1.   Kutia Muhuri Kitabu

 

  1.     Soma Danieli 12:4. Je, tunapaswa kuwa na uwezo wa kuyaelewa maono haya ambayo tumekuwa tukijifunza kwa majuma mawili yaliyopita? (Nadhani uelewa wetu we sehemu za awali za maono uko bayana kabisa. Hata hivyo, kwa kadri tunavyoendelea kuyaangalia maono ndivyo ninavyozidi kutoyaelewa vizuri. Hii inaashiria kuwa baadhi ya maono yanasalia kutiwa muhuri na hayako wazi kwa ajili ya kueleweka hadi “wakati wa mwisho.”)

 

   1.     Wakati wa mwisho ni lini? (Angalia tena Danieli 11:40. Hapo awali tulijadili uhusiano wake na Danieli 12:1. Danieli 11:40 haionekani kuwa ya kinadharia au ya kiroho. Inaelezea kwa kina sana kuhusu asili ya silaha zinazotumika. Juma lililopita nilipendekeza kwamba kujihusisha kwa Marekani katika Mashariki ya Kati ni uwezekano mmojawapo ya tafsiri. Ikiwa hali ndio hiyo, basi angalao “wakati wa mwisho” ni sasa.)

 

   1.     Ikiwa “wakati wa mwisho ni sasa,” kwa nini tuna migongano mingi juu ya kile kinachomaanishwa na Danieli 11 na 12? (Jibu mojawapo ni kwamba “kuondoa muhuri” ni jambo linaloendelea. Tunapoona matukio haya yakitokea tunasema, “Sasa ninaelewa.”)

 

  1.     Soma Danieli 12:5-6. Tuna “watu” wangapi hapa, tofauti na Danieli? (Danieli anawaona “wengine” wawili wakiwa wamesimama katika pande mbili za mto. Na kwa kuongezea, kuna “mtu aliyevikwa nguo ya kitani” aliyesimama juu ya maji ya mto kati yao.)

 

   1.     Watu hawa ni akina nani? (Wanaonekana kuwa ni malaika. Maelezo ya “mtu” juu ya maji ya mto yanaonekana kama mtu aliyeelezewa katika Danieli 10:5. Pia yupo mahali pale pale (Danieli 10:4). Mjadala unaofuatia katika Danieli 10:13 unanielekeza kuamini kwamba kwa mara nyingine huyu ni Gabrieli.)

 

   1.     Angalia swali linaloulizwa kumhusu mtu aliye juu ya maji ya mto: “Itachukua muda gani kabla mambo haya hayajatimia?” Mambo gani? (Lazima hii inarejelea matukio yanayojielekeza kwenye ufufuo. Nimeangalia tafsiri nyingine na swali linaonekana kuwa ni “Ufufuo utatokea lini?”)

 

  1.     Soma Danieli 12:7. Utaona kwamba hiki ni kipindi kile kile kilichobainishwa katika Danieli 7:25. Utakumbuka kwamba hapo kabla tulibainisha kuwa hii ni miaka 3.5 (au miezi 12 au siku 1,260). Kama hizi ni siku za kinabii, basi hii inamaanisha miaka 1,260. Je, hicho ndicho kipindi cha mwisho wa dunia? (Hapana. Gabrieli anasema kuwa hapa ndipo ambapo “hatimaye uwezo wa watakatifu umevunjwa.” Hiyo haionekani kama ni mwisho wa dunia. Badala yake, unapoilinganisha Danieli 7:25 inatuambia kuwa “watakatifu” “watatiwa mikononi” mwa pembe ndogo kwa kipindi hicho. Tukio hilo linafanana zaidi na kitendo cha watakatifu kushindwa.)

 

   1.     Kwa nini Gabrieli anaapa kwamba jambo hili ni kweli? Tunapaswa kuelewa nini kutokana na jambo hili? (Anatuambia kuwa jambo hili ni sahihi kabisa.)

 

  1.     Soma Danieli 12:8-9. Je, hadi kufikia hapa unajisikia kama Danieli? Kama Gabrieli anaapa kwamba hili ni jambo la kweli, kwa nini hajali zaidi kwamba Danieli halielewi? (Gabrieli anasema kuwa uelewa utakuwepo katika siku zijazo.)

 

   1.     Unadhani kwamba miaka 1,260 ndio jibu kamili kwenye kipindi cha mwisho? (Siamini kwamba Gabrieli ametoa jibu kamili kuhusu mwisho wa dunia. Amejadili tu sehemu ya kipindi chote.)

 

  1.     Soma Danieli 12:10. Je, kutokuelewa kwetu kunatokana na ukweli kwamba sisi ni “waovu?”

 

  1.     Soma Danieli 12:11. Hii inatuambia nini kuhusu siku 1,260 zinazofikia hadi mwisho wa dunia? (Ikiwa tuna tarehe moja ya kuanzia, hii inaweka bayana kwamba Gabrieli anatupatia majibu nusu nusu.)

 

   1.     Una maelezo gani kwa ajili ya hii miaka 1,290? (Hapo awali tulimkataa Antiokasi Epifanesi kama “pembe ndogo” ya Danieli 7. Badala yake, inaendena vizuri zaidi na Rumi ya Upapa. Ukitumia mwaka 508 B.K. kama sehemu ya kuanzia kwa sababu Clovis, Mfalme wa Ufaransa, alibadili dini na kuingia kwenye imani ya Kikatoliki, basi siku 1,290 zinafikia mwaka 1798, Papa alipochukuliwa mateka na Generali wa Kifaransa Berthier. Papa alifariki akiwa uhamishoni.)

 

    1.     Unadhani kwamba matukio mawili yaliyobainishwa katika Danieli 12:11 yanaziweka pamoja siku 1,290 au ndio sehemu ya kuanzia ya siku 1,290? (Binafsi naona hizo siku ni sehemu ya kuanzia.)

 

    1.     Je, maelezo ya Mfalme Clovis yanaleta mantiki kwako? (Kidhahania, kuna uwezekano zaidi kwamba kukomeshwa kwa kafara ya kila siku kulirejelea ama kifo cha Yesu msalabani au kuangamizwa kwa hekalu mwaka 70 B.K., badala ya kuongoka kwa mfalme wa Kifaransa. Hata hivyo, kuna uwezekano mkubwa kwa maelezo ya Mfalme Clovis kuwa ya kweli endapo utaangalia Danieli 8:8-11 ambayo ina maelezo ya “Pembe Ndogo” kuondoa kafara ya kila siku. Tukikubali kwamba “Pembe Ndogo” ya Danieli 7 ni sawa na ile ya Danieli 8, hiyo inaimarisha maelezo ya Mfalme Clovis.

 

  1.     Soma Danieli 12:12. Je, siku (miaka) 1,335 inaonekana kuwa tarehe ya Gabrieli kwa ajili ya kipindi cha ufufuo?

 

  1.     Soma Danieli 12:13. Je, ushauri wa Gabrieli kwa Danieli pia unahusika kwetu? (Gabrieli anamwambia Danieli kwamba atakufa na Mungu atatimiza kile alichokiahidi. Nadhani hiyo ni ahadi nzuri kwa ajili yetu.)

 

  1.     Rafiki, huenda wale walio na “hekima” zaidi kuliko mimi wanaelewa vizuri zaidi kitabu cha Danieli 11 na 12. Binafsi, si kila kitu “kimeondolewa muhuri” kwangu. Ninasubiria, ninatumaini, na niko macho. Jambo ambalo kitabu cha Danieli linatufundisha kwa dhahiri kabisa ni kwamba Mungu ndiye mdhibiti wa mambo yote. Je, utampokea na kumtumaini leo?

 

 1.   Juma lijalo: Tutaanza mfululizo mpya jinsi ya kutafsiri Biblia.