Somo la 11: Biblia na Unabii

(1 Wakorintho, Danieli 2)
Swahili
Year: 
2020
Quarter: 
2
Lesson Number: 
11

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Je, kuna mtu katika siku za hivi karibuni amekwambia kwamba “si nilikwambia?” Unamchukuliaje mtu huyo? Kuna nyakati huwa siipendi kauli hiyo (hususan pale ninapokuwa nimekosea), lakini tayari ninakuwa nimeshaisikia. Kama mtu anaendelea kuwa sahihi katika mambo yake, ninakuwa makini zaidi kwa mtu huyo kuliko kwa watu wanaoendelea kufanya makosa. Hivi karibuni tumejadili madai ya Mungu kututaka tumwabudu kwa sababu yeye ni Muumbaji wetu. Mungu ana hoja zaidi ya moja kwa nini tumwamini. Mojawapo ya hizo hoja kuu ni kwamba anaufahamu mustakabali. Kwa uhakika na kujiamini kabisa anaweza kusema, “si nilikwambia.” Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tujifunze zaidi!

 

 1.     Kaa Macho

 

  1.     Soma 1 Wakorintho 10:1-2. Vifungu hivi vinarejelea tukio gani? (Safari ya wana wa Israeli. Angalia Kutoka 13 & 14.)

 

   1.     Lugha iliyotumika katika 1 Wakorintho 10:2 haionekani kuwa ya kushangaza kwako? Watu “walibatizwaje” kwa Musa “katika wingu na katika bahari?”

 

    1.     Mfanano kati ya ubatizo na bahari uko dhahiri kabisa. Vipi kuhusu kubatizwa katika wingu?

 

    1.     Wingu lilikuwa na lengo gani wakati wa safari ya wana wa Israeli? (Soma Kutoka 13:21-22. Liliwaongoza watu. Liliwapa kivuli na kuwafariji. Liliwakumbusha uwepo wa Mungu wakati wote.)

 

    1.     Katika zama za leo tuna mfanano gani? (Roho Mtakatifu! Biblia inatukumbusha kwamba ubatizo wa maji na Roho Mtakatifu viliashiriwa katika kitabu cha Kutoka.)

 

     1.   Unadhani Mungu alipanga jambo hilo?

 

  1.     Soma 1 Wakorintho 10:3-4 na Kutoka 17:6. Je, mwamba ulikuwa na maji? (Lazima huo utakuwa mwamba usio wa kawaida!)

 

   1.     Kwa nini huu “Mwamba wa kiroho” ni Yesu? (Hii inatukumbusha kwamba Yesu aliumba ulimwengu bila kutumia kitu chochote.)

 

   1.     Unapokabiliana na matatizo, je, unaanza kujisikia vizuri unapoanza kuona jinsi mambo yatakavyotendeka?

 

    1.     Fikiria jinsi maisha yako yatakavyokuwa ya amani endapo utaamini kwamba Mungu anaweza kutatua matatizo yako pasipo kutumia “kitu chochote?” Mwamba, chanzo cha maji kisichotarajiwa kabisa, mikononi mwa Mungu unatoa maji.

 

  1.     Soma 1 Wakorintho 10:5. Licha ya haya manufaa yote, mambo yaliwaendeaje watu wa Mungu wakati wa safari ya wana wa Israeli? (Takriban wote waliotoka Misri walifia jangwani.)

 

   1.     Kwa nini? Walikuwa na manufaa yote haya?

 

  1.     Angalia mambo mawili yanayoendelea katika 1 Wakorintho 10 hadi kufikia hapa. Kwanza, tuna aina ya unabii kuhusu siku zijazo: ubatizo wa maji, kazi ya Roho Mtakatifu, na kwamba Yesu ni “Mwamba” wa wokovu wetu. Ana nguvu na uwezo juu ya vyote. Pili, tunafahamu kile kilichowatokea watu wa Mungu kama fundisho la historia maishani mwetu. Mungu anatutaka tufanye nini na unabii huu na historia hii? (Kujifunza jambo fulani! Hebu tuliangalie hilo katika sehemu inayofuata.)

 

 1.   Mifano

 

  1.     Soma 1 Wakorintho 10:6. Ni vigumu kiasi gani kudhibiti matamanio yako? (Kudhibiti matendo yako ni jambo moja, kudhibiti matamanio yako ni jambo jingine kabisa.)

 

   1.     Mifano hii inatusaidiaje kudhibiti matamanio yetu? (Unatamani jambo fulani ambalo linafurahisha. Mifano hii inaonyesha kwamba matokeo si ya kufurahisha hata kidogo. Kupigwa na kufia jangwani si jambo tutakalolifurahia.)

 

  1.     Soma 1 Wakorintho 10:7. Tunapenda kula, kunywa, na kucheza! Je, huo ni uabudu sanamu? (Soma Kutoka 32:1 na Kutoka 32:4-6. Tatizo si kula, kunywa, na kucheza. Ni kutenda mambo haya ili kusherehekea kumkataa Mungu wa kweli na kumbadilisha na sanamu ya ndama wa dhahabu.)

 

  1.     Soma 1 Wakorintho 10:8. Je, uasherati utatuangamiza kwa kutuua?

 

   1.     Hebu tusome Hesabu 25:1-3 ili tuone anachokinukuu Paulo kama uthibitisho wa ushawishi wake. Je, hili ni tatizo mchanganyiko? (Kwa mara nyingine, uabudu sanamu ni maarufu.)

 

    1.     Je, kuna tofauti kati ya kuinama na kuabudu sanamu? (Kauli iliyotumika hapa inaonekana kuashiria jambo ambalo si ibada, bali jambo tofauti na Baali.)

 

    1.     Unadhani hitimisho gani sahihi linapaswa kufikiwa kutokana na kile tulichokisoma hapa? (Uasherati hukuelekeza kwenye kulegeza msimamo kwenye mambo mengine maishani mwako.)

 

  1.     Soma 1 Wakorintho 10:9-10 na Hesabu 21:5-6. Watu “wanamjaribuje Kristo?” (Wanalalamika na hawana shukrani. Hawamtumaini Mungu.)

 

   1.     Je, unaona mwelekeo hapa? (Ndiyo. Uabudu sanamu unaonyesha uhaba wa kumtumaini Mungu. Uasherati na malalamiko vinaonyesha kutotumaini mpango wa Mungu na upaji wake.)

 

  1.     Soma 1 Wakorintho 10:11. Je. Mafundisho haya yanakomea kwa watu wanaoonekana kama washenzi (wasiostaarabika) katika safari ya wana wa Israeli? (Paulo anatuhabarisha kwamba mafundisho haya ni kwa ajili ya wale wanaoishi katika nyakati za mwisho. Mafundisho hayo ni kwa ajili yetu!)

 

  1.     Soma 1 Wakorintho 10:12. Kwa nini onyo hili? (Mtazamo ule ule kwamba watu hawa hawakuwa wastaarabu na sisi ni wastaarabu, ndio sababu ya kutuonya sisi. Hatupaswi kuwa na majigambo na wenye kujisifu.)

 

   1.     Unaelezeaje ukweli kwamba uabudu sanamu ulikuwa tatizo kubwa sana kipindi hicho, lakini umepotea katika zama za leo? Je, hiyo inaonyesha ustaarabu na usasa wetu? (Tuna miungu ya kisasa zaidi. Sanamu/miungu ni kitu unachokitumaini badala ya kumtumaini Mungu.)

 

    1.     Sanamu/miungu ambayo wanadamu wa kisasa wanaitumaini ni ipi?

 

 1. Mustakabali

 

  1.     Hivi karibuni tulijifunza kitabu cha Danieli. Kwa mapitio ya haraka-haraka, Mfalme Nebukadreza aliota ndoto ambayo watu wake wenye hekima na uerevu mkubwa hawakuweza kuielezea upya wala kuitafsiri. Soma Danieli 2:27-28 na Danieli 2:31-36. Tulijifunza kwamba ndoto hii iliwakilisha jambo gani? (Ni unabii wa historia ya ulimwengu hadi mwisho wa wakati – ujio wa Yesu Mara ya Pili.)

 

   1.     Kwa nini Mungu aliweka kisa hiki kwenye Biblia? (Kinatuthibitishia kwamba Mungu wetu ndiye anayeishikilia historia. Anaufahamu mustakabali!)

 

  1.     Unabii wa Danieli 2 ni wa muhimu sana, lakini ni mmojawapo wa unabii mwingi katika Biblia. Tunapaswa kuwa na mwitiko gani kwenye huu unabii mwingi? (Tunapaswa kumtumaini Mungu tunapoona unabii unatimia.)

 

  1.     Hebu tuunganishe somo letu la 1 Wakorintho 10 na Danieli 2. Ujumbe wao wa jumla ni upi? (Katika 1 Wakorintho Mungu anatuambia kwamba dhambi za nyuma ni dhambi za watu wanaoishi katika siku za mwisho. Kitabu hicho kinabashiri majaribu yetu yajayo! Danieli 2 inabashiri matukio ya ulimwengu yajayo. Kwa pamoja vitabu hivi vinatuambia kuwa Mungu anajua mustakabali wetu na ametuambia nini cha kufanya.)

 

  1.     Je, umeona ujumbe huu kuwa wa kweli katika zama za leo? Je, Mungu anaweza kusema, “si nilikwambia?” (Ninapoandika ujumbe huu, ulimwengu unapitia mabadiliko ambayo hayajawahi kutokea (angalao nchini kwangu) katika utawala wa sheria. Serikali za Mitaa, kutokana na hatari ya virusi vya COVID-19, zinakwenda mbali zaidi ya kitu chochote kinachoruhusiwa na Katiba ya Marekani, hata kufunga makanisa kwa ajili ya ibada wa watu. Kuunganisha tatizo hili ni kwamba askari polisi, ambaye anapaswa kusimamia sheria, alizikiuka kwa kumuua mshukiwa aliyetiwa pingu. Hii ilisababisha uharibifu mkubwa wa mali uliofanywa na watu wasioheshimu utawala wa sheria. “Sheria” hizi zilizokataliwa zinaakisi kanuni ya msingi kabisa ya Mungu kwamba tumpende Mungu na tumpende jirani yetu kama tunavyojipenda wenyewe.)

 

   1.     1 Wakorintho 10 na Danieli 2 zinaelekeza kwamba Mkristo anapaswa kufanya nini katika nyakati kama hizi? (Kumtumaini Mungu! Uwe na amani kwamba Mungu ataadhibu vitendo visivyo vya haki na kukomesha dhambi na mateso.)

 

  1.     Rafiki, Mungu anaweza kusema “si nilikwambia.” Anatumia mambo ya nyuma kutuonya juu ya majaribu yetu ya sasa na yajayo. Anaelezea mustakabali wa ulimwengu. Je, utadhamiria kumtumaini bila kujali tatizo unalokabiliana nalo? Kwa nini usimwombe Roho Mtakatifu, sasa hivi, ili akusaidie kumtumaini Mungu?

 

 1.   Juma lijalo: Kushughulika na Aya Ngumu.