Somo la 12: Kushughulika na Aya Ngumu

(1 Timotheo 4, Yakobo 4, Matendo 17)
Swahili
Year: 
2020
Quarter: 
2
Lesson Number: 
12

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Tunafanyaje ili Biblia ieleweke kwa urahisi? Mahala pazuri pa kuanzia ni kutumia tafsiri ya Biblia unayoweza kuielewa! Kwa muda mrefu nimekuwa na mawazo ya kwamba watakatifu wanaojenga hoja kwa kutumia Biblia ngumu kabisa kueleweka, na kujaribu kuwalazimisha watu wengine kuisoma Biblia hiyo, wanafanya kazi ya Mwovu. Hataki tulielewe Neno la Mungu. Tunaweza kufanya jambo gani jingine ili kuelewa vizuri zaidi aya ngumu za Biblia? Hebu tuzame kwenye somo letu la juma hili na tujifunze zaidi!

 

  1.     Juhudi za Dhati

 

    1.     Soma Mithali 2:6-7 na 1 Timotheo 4:16. Tabia yetu binafsi inahusianaje na kuielewa Biblia? (Inadhihirisha tamaa ya kutenda mapenzi ya Mungu. Kwa nini Mungu atake kutupatia utambuzi wa kina ikiwa hatutumii faida ya kile ambacho tunakielewa kwa sasa?

 

      1.     Zingatia sehemu ya kwanza ya 1 Timotheo 4:16 inayotoa wito wa “kudumu katika mambo hayo.” Hiyo inamaanisha nini? (Kuwa makini kwa mambo yanayofundishwa na watu wengine. Mawazo yangu yamebadilika juu ya mada za Biblia kutokana na mafundisho ya watu wengine. Hata hivyo, nadhani ujumbe wa msingi hapa ni kuwa macho kwa mafundisho ya uongo.)

 

      1.     Zingatia sehemu ya mwisho ya 1 Timotheo 4:16. Nani mwingine aliye hatarini ikiwa hatuchukui juhudi za dhati kumtii Mungu na kufundisha jambo sahihi? (Wale wanaosikiliza mafundisho yetu. Kwa wengi wetu, hao ni watoto wetu.)

 

    1.     Soma Yakobo 4:6-7. Unaposoma kifungu cha Biblia usichokipenda, unapaswa kufanya nini? (Tunahitaji mtazamo sahihi kuhusu Biblia. Tunatakiwa kuwa wanyenyekevu, ikimaanisha kwamba tuwe wazi kupokea kile kinachofundishwa na Biblia.)

 

    1.     Soma Yakobo 4:11, na uzingatie sehemu ya mwisho. Tunaonywa dhidi ya jambo gani? (Mungu hakudhamiria tuihukumu sheria, bali kuifuata sheria.)

 

      1.     Hili linafanyaje kazi kivitendo? Je, hatupewi wito wa kutoa hukumu katika aya ngumu?

 

      1.     Soma Yakobo 4:9 kama mfano. Niliposoma kifungu hicho leo mara moja nilikikataa kwa sababu mawazo yangu yalienda hadi kwenye Wagalatia 5:22. Tunda la Roho Mtakatifu ni “furaha.” Hakuna sehemu hata moja katika Biblia tunapoambiwa kwamba matokeo ya Roho Mtakatifu kukaa ndani yetu ni kuhuzunika na kuomboleza. Ninawezaje kuepuka kuwa hakimu juu ya kile alichokiandika Yakobo? (Kuna hukumu sahihi na hukumu isiyo sahihi. Ikiwa tunasema tu kwamba hatutaifuata Biblia kwa sababu tuna ufahamu zaidi, hiyo ni hukumu isiyo sahihi. Kama tukilinganisha aya za Biblia na kuchunguza muktadha ili kubainisha fundisho la jumla la Biblia, hiyo ndio njia bora zaidi.)

 

  1.   Uelewa wa Shauku

 

    1.     Soma Matendo 17:10-11. Paulo na Sila walipeleka ujumbe gani? (Yesu ni Masihi.)

 

      1.     Nini kiliwafanya wale walioishi Beroya kuwa “waungwana zaidi” kuliko wale wa Thesalonike? (Waliposikia jambo jipya, walilichunguza kwa uangalifu ili kuona kama linaendana na Maandiko.)

 

      1.     Tunapaswa kuzishughulikiaje aya ngumu za Biblia? (Tunapaswa kuwa wazi kupokea uelewa mpya.)

 

    1.     Nimebainisha jambo hili hapo kabla. Katika siku za awali kanisani kwangu viongozi walikuwa wanatupilia mbali uelewa wa kale na kukubali na kupokea uelewa mpya wa Biblia. Leo ninasikia “simamia katika nguzo,” na uwe na “msingi imara.” Je, njia sahihi ya kuifikia kweli inabadilika kutokana na muda katika hitoria? Je, “ukweli mpya” wa awali mara zote ni sahihi? Au, je, mara zote njia sahihi ni kujifunza Biblia kwa makini na kuwa wazi kupokea ukweli mpya?

 

      1.     Soma tena Yakobo 4:6. Tahadhari ni ipi tunapotafakari ukweli mpya? (Tunatakiwa kuliendea jukumu hili kwa unyenyekevu, na si kwa majivuno.)

 

      1.     Moja ya hoja nyepesi ninayoisikia ni kwamba ninapaswa kuukataa mtazamo bayana wa Biblia kwa sababu ni wa “Kikatoliki” au wa “Kipentekoste.” Fundisho la Kikatoliki linaweza kuwa la zamani sana na fundisho la Kipentekoste linaweza kuvuviwa na Roho Mtakatifu. Kukataa fundisho lolote kati ya hayo kunaonyesha kupungukiwa unyenyekevu. Badala yake, kama ilivyo kwa Waberoya, tunatakiwa kuyachunguza Maandiko kwa shauku ili kuona kilicho cha kweli.)

 

    1.     Soma Matendo 8:26-28. Tunajifunza nini juu ya huyu afisa wa mahakama kwenye hivi vifungu vichache? (Mkushi ni mtu muhimu, mwenye mamlaka, na kwa dhahiri ni mwongofu wa Kiyahudi. Pia anasoma Biblia yake.)

 

      1.     Je, unapenda kusoma wakati unaendesha gari? Unaweza kufikiria kitendo cha kusoma wakati unaendesha kibandawazi cha kukokotwa na farasi (chariot)?

 

        1.     Hiyo inatuambia nini kumhusu Mkushi? (Ana shauku ya kujifunza zaidi habari za Mungu.)

 

    1.     Soma Matendo 8:29-31. Je, utamkaribisha mtu mgeni kabisa garini mwako? Je, utakuwa radhi kwa Roho Mtakatifu kukwambia kukimbilia na kusogea karibu na gari na kuanzisha mazungumzo? (Katika hali zote mbili tunawaona watu ambao wako tayari kuyatenda mapenzi ya Mungu.)

 

    1.     Soma Matendo 8:32-34. Je, hii ni aya ngumu? (Ni ngumu kwa Mkushi.)

 

    1.     Soma Matendo 8:35. Msingi wa kuelewa aya ngumu katika Biblia ni upi? (Tunaye mtu ambaye ana hamu ya kujifunza zaidi habari za Mungu. Yuko radhi kujaribu bahati kwa mgeni kumfundisha. Roho Mtakatifu amepangilia tukio hili – kwa kifungu kusomwa na Filipo kuwepo mahali pale.)

 

      1.     Hii inatufundisha nini kuhusu kujifunza kutoka kwa watu wengine? (Ingawa kifungu kilikuwa kigumu kwa Mkushi, kilikuwa kirahisi kwa Filipo. Kujifunza Biblia kivikundi huleta pamoja uelewa wa watu wengine, ambao wanaweza kuwa wataalam kwenye mada inayojadiliwa.)

 

    1.     Soma Matendo 8:36-38. Je, Mkushi ana msukumo? (Nina mashaka kama mtu aliyekuwa mwangalizi wa hazina ya Mkushi alikuwa na msukumo?

 

      1.     Kwa nini asisubiri hadi arejee nyumbani ili abatizwe? Alikuwa na mali na mamlaka, na angeweza kubatiziwa nyumbani mahali pazuri na marafiki zake wakasherehekea pamoja naye. (Nadhani hii inatupatia utambuzi wa maisha ya Mkushi. Kama jambo linatakiwa kufanyika, anataka kulifanya mara moja.)

 

      1.     Zingatia jinsi Mkushi anavyouliza habari za kubatizwa. Yeye ni mtu mwenye uwezo na mamlaka, je, analazimisha kubatizwa? Kwa nini sivyo? (Yeye ni mtu mwenye mamlaka, lakini anakubali kushindwa na mwalimu wake mpya kwenye hili suala la kiroho.)

 

    1.     Soma Mathayo 19:23-24. Mkushi wetu ni tajiri na ana uwezo na mamlaka. Kitu gani kinamfanya awe tofauti?

                                                       

  1. Jambo la Msingi

 

    1.     Soma 2 Timotheo 2:14. “Mashindano ya maneno” ni kitu gani?

 

      1.     Kwa nini yanawaharibu wanaoyasikia?

 

    1.     Soma 1 Timotheo 6:3-4. Vifungu hivi vinatoa mwanga gani kwenye “mashindano ya maneno?” (Onyo ni kwa wale wanaotaka kuleta mjadala usio na maana kwenye mambo madogo madogo.)

 

      1.     Kifungu hiki kinatusaidiaje kuelewa jinsi wasikilizaji wanavyodhuriwa na aina hizi za mijadala? (Unapochukua upande kwenye mabishano madogo, hiyo husababisha mtazamo wa kudhamiria “husuda, ugomvi, matukano, [na] wasiwasi wa kiovu.”)

 

      1.     Mafarakano ya maneno yanatofautianaje na mjadala wa kifikra? (Ni tofauti kati ya kilicho muhimu na kisicho muhimu. Tunataka jambo la msingi liendelee kuwa jambo la msingi.)

 

    1.     Soma 1 Timotheo 6:5. Tunawezaje kutofautisha kati ya mjadala wa vifungu vigumu na tamaa ya “misuguano ya mara kwa mara?” (Mtu wa mafarakano si mwanafunzi wa Biblia. “Ameharibikiwa akili na kuikosa kweli.”)

 

    1.     Rafiki, je, una shauku ya kumjua Mungu? Je, una kiu ya kutaka kuyaelewa mapenzi yake vizuri zaidi? Kuyaelewa mapenzi ya Mungu vizuri zaidi sio tu suala la maneno matupu, Mungu anataka tuenende na kutenda kutokana na maarifa yetu. Kwa nini usimwombe Roho Mtakatifu akusaidie kuishi kwa kufuata mapenzi ya Mungu na kuyaelewa kikamilifu mapenzi yake?

 

  1.   Juma lijalo: Kuishi Kulingana na Neno la Mungu.