Somo la 4: Nguvu ya Maombi: Kuwaombea Wengine

(2 Wakorintho 10, Waefeso 6, Yohana 11)
Swahili
Year: 
2020
Quarter: 
3
Lesson Number: 
4

Somo la 4: Nguvu ya Maombi: Kuwaombea Wengine

 

(2 Wakorintho 10, Waefeso 6, Yohana 11)

 

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Umewahi kusikia malalamiko kuhusu maombi ya watu wengine? Mtumishi mmoja Mkristo maarufu anafanya maombi ili Mungu amsaidie kupata mahala pa kuegesha gari lake, na anakosolewa na mwingine anayefanya maombi ili Mungu amponye mama yake anayeugua saratani ya titi. Vipi kama mama anafariki na mtumishi anakutana na kikwazo kikubwa? Je, Mungu anavurugwa na mambo madogo madogo? Aina hii ya ukosoaji inatokana na dhana potofu kwamba uwezo wa Mungu wetu una kikomo. Tukimvuruga kwa mambo madogo madogo, hawezi kushughulikia vizuri masuala ya uhai na kifo. Huu ni upuuzi. Uwezo wa Mungu hauna kikomo. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tupanue uelewa wetu juu ya uwezo wa Mungu na maombi yetu!

 

 1.     Jambo Lisilo la Kawaida (Supernatural

 

  1.     Soma 2 Wakorintho 10:3-4. Maana ya shujaa ni nini? (Kwa muda mrefu tasnia ya burudani imekuwa ikiwainua na kuwakuza watu wenye uwezo usio wa kawaida wa wanadamu. Mfikirie Superman - Kama wewe ni mtu mzima!)

 

   1.     Je, kifungu hiki kinatuambia kuwa sisi ni mashujaa? (Ndiyo! Kinatuambia kuwa tuna “silaha” ambazo ni zaidi ya silaha “za mwili.” Hiyo inamaanisha kuwa tunaweza kuufikia uwezo usio wa kawaida.)

 

   1.     Inamaanisha nini “kuangusha ngome?” Kwani hatujapewa wito wa kujenga na si kubomoa? (“Ngome” ni mji ulioimarishwa kwa uzio imara. Uwezo wetu usio wa kawaida unaweza kuushinda upinzani ulio imara sana.)

 

  1.     Soma 2 Wakorintho 10:5. Uwezo wetu usio wa kawaida unafanya kazi katika ngazi gani? (Mawazoni!)

 

   1.     Sinema maarufu inayohusisha “the force” ina mfululizo wa matukio ambapo mtu anayemshika “the force” anasema jambo kama lifuatalo kwa askari adui, “Hamkutuona, tuko huru kupita.” Je, hilo ndilo jambo ambalo kifungu hiki kinalizungumzia pale kinaporejelea “kuteka nyara kila fikra?”

 

  1.     Soma 1 Yohana 5:14-15. Kigezo gani kinatoa mwongozo katika matumizi ya uwezo wetu usio wa kawaida? (Mapenzi ya Mungu. Tunaomba mambo yanayoendana na mapenzi ya Mungu. Tukifanya hivyo, anatusikia, na “tunazo zile haja tulizomwomba.”)

 

  1.     Soma Waefeso 6:10-12. Mashujaa, tunakabiliana na wapinzani wa namna gani? (Mwovu – Shetani.)

 

   1.     Soma kifungu cha 11 kwa makini. Je, kiuhalisia tunakabiliana na Shetani? (Kifungu kinasema kuwa tunakabiliana na “hila” zake. Shetani si kama Mungu, hapatikani kila sehemu (omnipresent). Lakini, alibuni mwongozo kwa ajili ya malaika walioanguka (angalia Ufunuo 12:9). Majuma mawili yaliyopita tuliangalia kisa cha mtu aliyepagawa pepo na nguruwe (Mathayo 8:28). Pepo hawakuonekana kuwa werevu sana katika kisa kile. Watu wale wanahitaji mwongozo.)

 

  1.     Zingatia tena Waefeso 6:12. Adui wetu halisi ni yupi? Je, hii ndio sababu tunahitaji uwezo usio wa kawaida?

 

   1.     Tukipambana na adui asiye sahihi, je, huo ni upumbavu?

 

   1.     Fikiria vita ambapo una sare nzuri na silaha za kisasa kabisa. Unapangwa mahali ambapo hakuna mapigano. Una maana gani sasa kwa huo upande wako?

 

   1.     Kibaya zaidi, vipi kama utageuza mgongo wako katika mapigano hayo na kuanza kupigana na askari wenzako?

 

 1.   Kibanda Chetu cha Simu

 

  1.     Mashujaa wa leo katika tasnia ya burudani wanaonekana kuwa na uwezo wa kuamrisha uwezo wao mkubwa moja kwa moja. Nilipokuwa mdogo, Superman alikuwa akiingia kwenye kibanda cha simu ili kubadili nguo zake zilizokuwa za muhimu katika uwezo wake wa ajabu. Kama wewe ni kijana mdogo unaweza kuuliza, “kibanda cha simu” ni kitu gani? Soma Waefeso 6:13. Je, lazima tuvae nguo za kupendeza, “silaha zote za Mungu?”

 

   1.     Ikiwa ndivyo, hicho ni kitu gani? (Waefeso 6:14-17 inazungumzia sehemu fulani ya silaha na kuelezea kile zinachowasilisha. Juma hili tutajikita kwenye maombi.)

 

  1.     Soma Waefeso 6:18. Chanzo cha jumla cha uwezo wako wa ajabu ni kipi? (“Roho.” Hii ni rejea ya Roho Mtakatifu.”)

 

   1.     Inamaanisha nini kuomba “katika Roho?” Je, hili ni ombi maalum? Au, je, ni ombi la kawaida?

 

  1.     Ili kusaidia kuumba jibu sahihi kwenye swali la awali, hebu tusome vifungu kadhaa. Soma Waefeso 5:18 na Warumi 8:26-27. Baada ya kusoma vifungu hivi, unaweza kufikiria kufanya ombi lolote bila Roho Mtakatifu? (Hapana! Kwa dhahiri Roho Mtakatifu ni wa muhimu kabisa.)

 

   1.     Warumi 8:26 inasema kuwa Roho Mtakatifu anatusaidia kuelewa nini cha kuomba. Warumi 8:27 inasema kuwa Roho Mtakatifu “hutuombea” katika maombi yetu. Je, mambo haya yapo kwenye maisha yako ya maombi?

 

  1.     Hebu turejee kwenye Waefeso 6:18. Unadhani inamaanisha nini “mkisali kila wakati katika Roho?” Je, hiyo inamaanisha kuwa tunatakiwa kuomba kila wakati? Au, je, hiyo inamaanisha kuwa tunapoomba tunatakiwa kuomba katika Roho? (Jibu langu ni la kivitendo. Kwa kuwa maombi katika Roho ndio “kibanda chetu cha simu,” ikimaanisha kuwa yanafungua uwezo wetu usio wa kawaida, kwa nini tusiwe tayari na uwezo wetu mkubwa kabisa wakati wote? Kwa nini tusiwe na uwezo zaidi, badala ya kuwa na uwezo mdogo?)

 

 1. Kuwaombea Wengine

 

  1.     Soma tena 6:18, lakini mara hii zingatia sehemu ya mwisho “mkidumu katika kuwaombea watakatifu wote.” Yatafakari maombi yako. Je, kwanza huwa unajiombea na kuombea mahitaji yako?

 

  1.     Soma Waefeso 6:19-20. Tofauti kati ya maombi yaliyobainishwa kwenye utangulizi, zaidi ya umuhimu wa kadiri, ni kwamba ombi moja linamnufaisha mtu na ombi jingine linamnufaisha mama. Ombi hili ni kwa ajili ya Paulo. Kama ungekuwa kwenye nafasi ya Paulo (gerezani), je, hili ndilo ombi ambalo ungeliomba? (Ombi langu lingekuwa “ombeni ili niweze kufunguliwa (kuachiwa huru)!”)

 

   1.     Paulo anaomba aombewe nini? (Kwamba aweza kutangaza injili kwa ujasiri.)

 

   1.     Je, ombi la Paulo ni kwa ajili yake mwenyewe? (Sio kivile. Ni ombi kwa ajili ya kutangaza injili.)

 

  1.     Soma Danieli 2:17-18. Ombi hili ni kwa manufaa ya nani? (Danieli na marafiki wake. Hawataki kuangamizwa.)

 

  1.     Unapotafakari vifungu hivi, unahitimisha nini kuhusu kuwaombea wengine dhidi ya kujiombea mwenyewe? (Utakumbuka kwamba Warumi 8:26 inatuambia kuwa Roho Mtakatifu atatuongoza kwenye mambo ya kuombea katika maombi yetu. Danieli anaonyesha kwamba kwa hakika tunaweza kujiombea wenyewe. Msisitizo uliopo katika Waefeso 6 ni kuwaombea wengine. Hata pale Paulo alipotarajiwa kuomba kwa ajili ya kufunguliwa na kuachwa huru, badala yake aliomba kwamba avikwe vizuri zaidi kusambaza injili katika mazingira ya sasa yanayomkabili.)

 

 1.   Ucheleweshwaji

 

  1.     Soma Danieli 10:12-13. Hii inatuambia kuwa “maneno ya Danieli yalisikiwa” mbinguni. Gabrieli, malaika, anapeleka jibu lililochelewa. Kwa nini jibu limechelewa? (Limecheleweshwa na mambo mengine, huenda kutokana na nguvu ya uovu kwa sababu neno “kuhimili” limetumika, na kufanya ionekane kwamba Gabrieli alikuwa anazuiwa na mwovu.)

 

  1.     Soma Yohana 11:3-4. Ni nini lengo la Yesu katika mazingira haya? (Kumpa Mungu utukufu.)

 

  1.     Soma Yohana 11:6 na Yohana 11:21. Unakifahamu kisa hiki kuhusu ufufuo wa Lazaro. Kwa nini Yesu alichelewa? Kwa nini aliruhusu mioyo ya dada hawa kuvunjika? (Kwa sababu ya manufaa makubwa, muujiza mkubwa, utukufu mkubwa wa Mungu.)

 

  1.     Unapotafakari vifungu vya Danieli na Yohana tulivyovisoma katika sehemu hii, je, tunahakikishiwa kuwa Mungu atachukua hatua mara moja kwenye maombi yetu?

 

   1.     Ikiwa sivyo, una mtazamo gani kwenye vyanzo vya ucheleweshwaji vinavyofahamika?

 

  1.     Rafiki, unao uwezo wa kuwa shujaa! Je, utayachukulia manufaa ya kila siku ya uwezo wako usio wa kawaida? Je, utamwomba Roho Mtakatifu aunoe uwezo wako usio wa kawaida? Je, utawasaidia wengine kwa kutumia uwezo wako usio wa kawaida? Kwa nini usiamue sasa hivi kuwa shujaa hai?

 

 1.     Juma lijalo: Ushuhudiaji Unaowezeshwa na Roho.