Somo la 10: Elimu Katika Sanaa na Sayansi

(Mithali 1, Warumi 1, 1 Timotheo 6, Zaburi 96)
Swahili
Year: 
2020
Quarter: 
4
Lesson Number: 
10

Somo la 10: Elimu Katika Sanaa na Sayansi

 

(Mithali 1, Warumi 1, 1 Timotheo 6, Zaburi 96)

 

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Baada ya kufikisha umri wa miaka 50, niliyachunguza maisha yangu, hususani kazi ninayoipenda. Cha kufurahisha, kazi niliyoipendelea ni kufundisha kikundi changu cha kujifunza Biblia kanisani. Basi nikafanya uamuzi wa kuyarekebisha maisha yangu ili kujikita kwenye ufundishaji. Baada ya kufanya makosa machache kwa upande wangu, Mungu aliingilia kati na kuniongoza kwenye kazi ya kufundisha ambayo ilikuwa bora zaidi kuliko nilivyotarajia au kuota. Mpango wangu ulikuwa ni kufundisha madarasa yatakayofungamanisha imani na vipengele vya sheria. Katika mkutano wangu wa kwanza na Mkuu wa Shule ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Regent, nilielezea yaliyokuwa mawazoni mwangu. Jibu lake lilikuwa la papo kwa papo, “Hicho ndicho hasa tunachokifanya!” Somo letu juma hili linahusu ufungamanishaji wa imani na “sanaa na sayansi.” Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tuone kile tunachoweza kujifunza!

 

 1.     Elimu ya Kweli

 

  1.     Soma Mithali 1:2-4. Angalia orodha hii ya mafundisho. Je, imani imefungamanishwa? (Ndiyo! Kufundishwa “katika haki.”)

 

  1.     Soma Mithali 1:7. Msingi wa kujifunza ni upi? Kitu gani kinatakiwa kujifunzwa ili kupata elimu ya kweli? (“Kumcha Bwana.” Kifungu hiki kinasema kuwa kumtii Mungu ni hatua ya kwanza ya muhimu kuifikia elimu ya kweli.)

 

   1.     Elimu ya kisasa ikoje? Hebu tuliangalie hilo katika sehemu inayofuata.

 

 1.   Kuwafichua Wakandamizaji

 

  1.     Soma Warumi 1:18. Inamaanisha nini kusema “kweli?” (Huu ni ukweli kuhusu haki – jambo lile lile ambalo Sulemani anasema ndilo msingi wa maarifa yote.)

 

  1.     Ni nini unaopaswa kuwa uhusiano kati ya elimu na kweli? (Elimu ni kupata uelewa mkubwa. Uelewa ni kujifunza ukweli.)

 

   1.     Siku hizi sifurahishwi kabisa na taarifa zinazohusu kile kinachofundishwa katika shule za elimu ya juu. Je, hili ni tatizo jipya? (Warumi inatuambia kuwa ni tatizo la kale sana – walimu wasio na haki wanaukandamiza ukweli.)

          

  1.     Soma Warumi 1:19. Ninaposikia baadhi ya mambo yasiyo na mantiki yanayofundishwa, ninashangaa kama kweli walimu wanaamini jambo hili. Kifungu hiki kinaashiria kuwa jibu ni lipi? (Kifungu kinasema kuwa ukweli ni “dhahiri ndani yao.” Hivyo, walimu hawa wa uongo kwa kujua kabisa wanafundisha mawazo yasiyo ya Kibiblia.)

 

   1.     Bila shaka usomaji mwingine utajibu, “haiko dhahiri sana. Baadhi ya wale wanaouendeleza uovu wana dhamira ya dhati lakini wamechanganyikiwa.” Ni kwa jinsi gani hayo kati ya maoni haya yanaelezea “dhahiri kwao?”

 

   1.     Lengo la asili la elimu ya juu ni kulinda uwezo wa mwalimu kufundisha ukweli. Unasikia nini leo kuhusu walimu wanaotangaza ukweli wa Mungu? (Wanapigiwa kelele za kunyamazishwa, wananyimwa vyeo na nafasi za kiutendaji, hata kuachishwa kazi.)

 

   1.     Sijayafanyia utafiti mengi ya madai haya, lakini nimeyasikia vya kutosha kiasi cha kuamini kuwa kwa ujumla ni ya kweli. Warumi 1:18 inapozungumzia ukandamizaji wa ukweli kupitia “vitendo visivyo vya haki,” unadhani hilo litaonekanaje? (Inaonekana kama matumizi ya nguvu na kutokuwepo kwa haki – uonevu wa namna mbalimbali.)

 

   1.     Tafakari jambo hili kidogo. Dhana iliyo nyuma ya uhuru wa kutoa maoni ni kwamba kila mtu anapata fursa ya kutoa maoni yake, bila kujali maoni hayo hayatakuwa sahihi kwa kiasi gani, na kisha wasikilizaji wanaamua kilicho cha kweli. Ikiwa wakandamizaji hawataki wasikilizaji wafanye uamuzi baada ya kusikiliza maoni mbalimbali, hiyo inazungumzia nini kuhusu mtazamo wa wakandamizaji? (Wanajua kuwa hawako sahihi. Kama wangedhani kuwa wako sahihi, wangekuwa na ujasiri kwamba mtazamo wao sahihi ungeshinda.)

 

  1.     Soma Warumi 1:20. Fundisho gani kumhusu Mungu liko dhahiri duniani, bila kujali mahali watu wanakoishi au lugha wanayozungumza? (“Uweza wa Mungu wa milele na Uungu wake” “unaonekana dhahiri” kwenye “mambo yaliyoumbwa.”)

 

   1.     Je, hapa kuna fundisho kwetu kuhusu namna tunavyoiendea injili? (Ukatishaji tamaa mkubwa kwangu katika huduma binafsi ya kupeleka injili ulitokana na watu ambao kiukweli hawakutaka kuielewa injili. Tunatakiwa kuelekeza juhudi zetu kwa watu wanaoutafuta ukweli.)

 

  1.     Soma Warumi 1:21. Je, kukataa ushahidi unaomhusu Mungu unafanana na mazoea mabaya yaliyo mengi, ukataaji unazidi kuwa mbaya zaidi? (Hii inatuambia kuwa mioyo yenye “upumbavu” hutiwa giza. Wanakuwa wabaya kupindukia.)

 

  1.     Soma Warumi 1:22-23. Upumbavu huu unajielekeza kwenye giza gani? (Badala ya kuangalia na kuhitimisha kuwa lazima yupo Mungu Muumbaji wa mambo yote tunayoyaona, badala yake watu hawa wapumbavu wanatengeneza sanamu na kuziabudu.)

 

   1.     Je, unaweza kufikiria jambo lolote lisilo na mantiki kupita hilo?

 

  1.     Soma Warumi 1:24-27. Fikra hii isiyo na mantiki na iliyotiwa giza inaelekea wapi? (Kwenye tabia ya usenge.)

 

   1.     Ubunifu wa miili ya mwanaume na mwanamke unadhihirisha kuwa wanadamu hawakuumbwa kwa ajili ya kufanya ngono ya kisenge/kibasha. Kwa kuwa tumejifunza kuwa giza hili ni endelevu, unaona kitu gani kinachofuatia kwenye ukataaji wa jinsi tulivyoumbwa? (Jambo jipya ni kufundisha kuwa sisi sio tu jinsia za aina mbili, bali kuna mambo mengi tunayoweza kufanana nayo yasiyojihusisha kivyovyote vile na jinsi tulivyozaliwa.)

 

   1.     Mshiriki wa darasa langu la kujifunza Biblia anamiliki kampuni ya ujenzi. Aliniuliza kama ninadhani kuwa fikra hii iliyotiwa giza hatimaye itafika kwenye masuala ya ujenzi. Alibainisha kuwa kuna vitu vya “kiume” na vya “kike.” Lugha hii ipo ulimwenguni kote kwenye masuala ya ujenzi. Unadhani jibu sahihi kwa swali hili ni lipi?

 

  1.     Soma Warumi 1:28. Tulianza na mfano wa kufungamanisha neno la Mungu na sanaa na sayansi. Tukiliacha neno la Mungu, matokeo yake ni nini? (Mungu “aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa.”)

 

   1.     Hebu tupitie mjadala tulioufanya hapo awali. Mtu anapofikia hatua ya kuwa na “akili isiyofaa,” je, bado ukweli wa Mungu ni dhahiri kwake?

 

  1.     Soma Warumi 1:29-31. Je, unaona mojawapo ya dhambi zako au mbili zikielezewa hapa?

 

   1.     Kama jibu lako ni “ndiyo,” je, hii inamaanisha kuwa unafanya kazi na “akili yako ya udhalimu?”

 

  1.     Ukitafakari kile tulichokisoma hivi punde, hususani Warumi 1:25-31, tunaonekana kuwa na orodha ya dhambi: kuabudu sanamu, ubasha/usenge, na kisha kila aina ya dhambi inayotendwa na Wakristo wote. Ni nani ambaye hajadharau, hajasengenya, hajajivuna, au kuwa mpumbavu? Je, uabudu sanamu na usenge ni “dhambi kuu” zinazosababisha usengenyaji na majivuno? (Jambo hili limenikanganya kwa muda mrefu. Maoni ya Albert Barnes yanatoa nuru katika hili. Anasema kuwa akili ya udhalimu imejawa dhambi hizi. “Mambo aliyoyabainisha yalikuwa ya kawaida au yalisheheni miongoni mwao.”)

 

  1.     Soma Warumi 1:32. Hii inatufundisha nini kuhusu kujinasibisha na dhambi moja au mbili (au dhambi chache) zilizoorodheshwa katika Warumi 1:29-31? (Hii inaendana na maoni ya Barnes kwamba dhambi hizi zinambainisha na kumwelezea mtu. Sio dhambi moja au mbili, bali dhambi hizi kwa ujumla “zinatendwa” nao.)

 

   1.     Angalia maneno ya mwisho ya kifungu cha 32. Hiyo inatuambia nini kuhusu “akili ya udhalimu” isiyo ya kweli kwa Mkristo anayepambana na dhambi? (Inathibitisha vitendo vya dhambi.)

 

   1.     Angalia mfungamano huu – mwalimu anakuza dhambi katika ufundishaji wa mambo ya kidunia! Je, hilo linatokea hadi kanisani?

 

 1. Kufichua Nia Mbaya

 

  1.     Hebu tuangalie eneo jingine ambalo elimu inahitajika kufungamanishwa na ushauri wa Mungu. Soma 1 Timotheo 6:9-10. Ni nani asingependa kuwa tajiri?

 

   1.     Kwa nini shauku ya kuwa tajiri inasababisha mitego na vishawishi?

 

   1.     Utaona kwamba kifungu cha 10 kinasema kuwa kupenda fedha “ni chanzo cha uovu wa aina zote.” Je, hapa tunawaelezea watu masikini au matajiri? (Utaona kwamba kifungu hakisemi kwamba kuwa na fedha ni tatizo. Ingawa matajiri wanaweza kutamani sana kuwa matajiri zaidi, nadhani huu ni ushauri ambaao unaelekezwa zaidi kwa watu wasio na fedha.)

 

  1.     Soma 1 Timotheo 6:11. Badala ya kutamani sana fedha, tunapaswa kutamani nini? (Maisha ya uadilifu. Malengo yako maishani yanaweza kuwa ni kwamba uwe tajiri, au kutembea na Mungu. Fanya uchaguzi kwa busara!)

 

  1.     Soma Zaburi 96:9. Tofautisha hili na wale wanaojenga hoja kutetea dhambi, wale wanaotangaza na kukuza dhambi. Hii ina utofauti gani kiuhalisia? (Njia ya Mungu ya maisha inachukuliwa kuwa nzuri sana – “uzuri wa utakatifu.” Badala ya kupambana na mapenzi ya Mungu, tunatetemeka katika furaha kwa ajili ya mtindo wake wa maisha.)

 

  1.     Rafiki, je, utatangaza na kuendeleza ufungamanishaji wa imani na ujifunzaji? Tafakari jinsi unavyoweza kutimiza hili katika eneo lako la ushawishi kuanzia sasa hivi.

 

 1.   Juma lijalo: Mkristo na Kazi.