Somo la 3: Chanzo cha Wahaka

Wagalatia 5, Mathayo 10 & 23, Luka 12
Swahili
Year: 
2021
Quarter: 
3
Lesson Number: 
3

(Wagalatia 5, Mathayo 10 & 23, Luka 12)

 

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

 

Utangulizi: Watu wengi wanayatafakari maisha yao ya nyuma na kustaajabu kwa nini mambo yao hayakwenda vizuri. Baadhi walio na umri mdogo wanashangaa kwa nini watu wengine wanaonekana kufurahia maisha mazuri. Hata watu waliofanikiwa sana wanajihisi kuwa na wahaka na kutoridhika. Vipi kuhusu wewe, je, umeridhika na maisha yako, au unajisikia kuwa na wahaka? Kwa ujumla kujihisi kutoridhika hutokana na mitazamo mibaya. Ulimwengu umeipa mitazamo sahihi jina la Kutawala Hisia (Emotional Intelligence). Biblia huiita Tunda la Roho. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tujifunze zaidi.

  1.    Tunda la Roho na Matendo ya Mwili
    1.    Soma Wagalatia 5:19-21. Kama maelezo haya yanayaashiria maisha yako, unadhani unajisikiaje?
    1.    Soma Wagalatia 5:22-23. Kwa upande mwingine haya yanaonekanaje?
      1.    Yumkini baadhi ya maeneo katika orodha hii ya matendo ya mwili na tunda la Roho yanaelezea baadhi ya tabia zetu. Changamoto iliyopo ni kuondoka kikamilifu kutoka kwenye orodha ya matendo ya mwili na kujongea kikamilifu kwenye tunda la Roho. Hebu tuangalie vipengele vya Biblia vinavyotusaidia kutuelekeza kwenye mwelekeo sahihi.
  1.   Amani na Utengano
    1.    Soma Mathayo 10:34-36. Hii inaendanaje na orodha zilizopo katika Wagalatia 5? (Inatofautiana na orodha. Utengano ni kazi ya mwili na amani ni tunda la roho. Yesu na Paulo wanaonekana kuwa kwenye pande zinazotofautiana.)
    1.    Soma Mathayo 10:37-38 na Kutoka 20:12. Je, unaweza kulinganisha vifungu hivi?
    1.    Wanasheria wa Marekani wana kanuni ya kulinganisha sheria ambazo kwa dhahiri zinakinzana, jambo ambalo ninadhani ni la msingi hapa. Kabla mahakama haijahitimisha lazima ichague sheria moja dhidi ya nyingine, lazima ijaribu kulinganisha sheria hizo mbili. Je, kauli ya Yesu kwamba analeta upanga, na si amani, inakinzana na dhana ya kwamba Roho Mtakatifu atakupatia mtizamo wa amani?
      1.    Je, tuhusianishe kauli za Yesu kuhusu kuleta upanga na kauli zake kuhusu kuleta mtafaruku katika familia? (Yesu anahusianisha kauli hizi mbili. Mathayo 10:35 inaanza kwa kusema “Kwa maana nalikuja kumfitini mtu na babaye....”)
      1.    Kama ningekuwa ninajaribu kuhusianisha kauli hizi mbili, ningehitimisha kwamba kumjua Mungu huleta amani, isipokuwa katika familia yako. Je, upatanisho huo unakidhi?
    1.    Soma Mathayo 10:20-22 na pitia kwa haraka haraka Mathayo sura ya 10. Je, tumechukulia kauli za Yesu juu ya kuleta upanga na si amani nje kabisa ya muktadha? (Muktadha ni mgumu. Yesu anawatuma wanafunzi wake kupeleka injili na kutenda miujiza. Anawaonya (anatuonya na sisi) kwamba kusambaza injili kutaleta mateso, na mateso mabaya kuliko yote yatatoka kwa watu wa familia yako. Na, kwa kuongezea, Yesu anagusia kwa nguvu (Mathayo 10:22) kwamba anazungumzia juu ya matukio ya siku za mwisho.)
      1.    Kwa kuwa sasa umeshazingatia muktadha, ni nani ambaye kimsingi analeta upanga wa mateso? (Wale wanaoikataa injili. Upinzani wa injili huleta mgongano, lakini kwa yenyewe injili huleta amani. Hakuna mgongano usiopatanishika.)
    1.    Mada yetu inahusu kwa nini baadhi ya watu wanafanya vizuri maishani. Ni kwa jinsi gani kile tulichokijadili hivi punde kina umuhimu kwenye mada yetu? (Kufuata uongozi wa Roho Mtakatifu huleta matokeo yote haya chanya ambayo huboresha maisha yetu. Lakini, kuna maadui wa injili wasiofuata kanuni za Mungu, wanazichukia kanuni, na wanavuruga matumizi ya kawaida ya kanuni.)
  1. Upendo na Wivu
    1.    Soma Luka 12:13-14. Yesu hatoi jibu la swali lake mwenyewe. Ungelijibuje?
      1.    Unapodhani kuwa kitendo kisicho cha haki kimetokea, je, huwa unasali ili kwamba Mungu atende lililo sahihi?
      1.    Je, Mungu wetu anaamini katika haki?
    1.    Soma Luka 12:15. Maoni haya yanaingiza kipengele gani kipya kwenye kisa chetu? (Yesu anaashiria kwamba mtu anayetoa wito wa haki kwenye suala la urithi ana tamaa tu. Hii inaashiria kuwa kitendo kisicho cha haki hakijafanyika.)
    1.    Hebu tusome Luka 12:16-18. Kama wewe ndiye ungekuwa mkulima huyu, je, ungefanya jambo hilo hilo?
      1.    Je, umenunua nyumba kubwa ili uwe na nafasi kubwa zaidi kwa ajili ya familia yako inayoongezeka pamoja na vitu vyako? Vipi kuhusu kununua gari kubwa? Kukodi chombo cha kuhifadhia vitu?
    1.    Soma Luka 12:19. Je, ungependa kustaafu mapema? Kama unaweza, je, utafanya hivyo? Je, unawaonea wivu wale walio matajiri vya kutosha kiasi cha kustaafu mapema? Kwa ujumla, je, unawaonea wivu matajiri?
    1.    Soma Luka 12:20-21 na usome tena Luka 12:15. Yesu anazungumzia kipengele gani kipya hapa kwenye kisa cha mkulima? (Mkulima hakuwa “tajiri kwa Mungu.”)
      1.    Je, hii inamaanisha kuwa mkulima hakutoa zaka? (Hakuna kilichosemwa kuhusu zaka. Hata hivyo, kutoa zaka ni sehemu ndogo tu ya mali zako iliyoahidiwa kukufanya kuwa na mali zaidi ili uwe katika nafasi ile ile kama mkulima huyu – unahitaji nafasi kubwa zaidi ya kuhifadhi mali zako. Angalia malaki 3:10.)
      1.    Ikiwa kisa hiki hakihusiani na fedha au mali, kinahusu nini basi? Ni kwa jinsi gani mkulima huyu “hakuwa tajiri kwa Mungu?” (Angalia tena Luka 12:19 na ujikite kwenye jinsi mkulima anavyotarajia kutumia muda wake katika siku zijazo. Sidhani kama tatizo ni suluhisho la kimantiki la utunzaji wa nafaka, tatizo ni kwamba mkulima anakusudia kutumia muda wake wote wa siku zijazo kwa ajili yake. Hazungumzii chochote kuhusu kuutangaza Ufalme wa Mungu. Kifo chake cha ghafla hakibadili chochote kwa ajili ya Ufalme wa Mungu.)
      1.    Angalia tena Luka 12:13. Unadhani ndugu hawa walikuwa na uhusiano gani? Kipaumbele kikuu cha mtu huyu kilikuwa ni kipi? (Fedha. Maisha yetu hayahusishi utajiri wetu na kupumzika pekee. Badala yake “upendo” na “uaminifu” kwa Mungu ni sehemu ya kile anachokitaka Mungu kutoka kwetu bila kujali kiasi cha mali tulichonacho.)
  1.   Uaminifu na Uchafu
    1.    Soma Mathayo 23:1-3. Kuna tatizo gani kwa hawa viongozi wa dini? (Wanasema mambo sahihi, lakini hawatendi mambo sahihi.)
    1.    Soma Mathayo 23:4. Je, Yesu anatuambia tubebe mizigo mizito kwa sababu viongozi wa dini wanasema tubebe mizigo mizito? (Soma Mathayo 23:13 na Mathayo 23:15. Yesu hawaambii makutano kufanya kila wanalolisema viongozi wa dini, kwani kwa kufanya hivyo kutawafanya kuwa “wana wa jehanum mara mbili zaidi” kama viongozi.)
    1.    Soma Mathayo 23:5-7. Unalielezeaje tatizo hapa? Je, unataka kuheshimiwa? Je, hilo ni dhambi?
      1.    Nimejiuliza siku za nyuma sehemu gani ya hamasa yangu ya kufundisha na kuhubiri ni kutaka kuonekana na watu wengine? Je, hilo ndilo tatizo hapa? (Hicho sicho anachokielezea Yesu. Tatizo ni kile wanachokivaa na mahali wanapokaa. Wanatafuta heshima kutokana na mambo ya nje, na si kutokana na kile wanachokifanya ili kuutangaza Ufalme wa Mungu.)
      1.    Je, umewaona washiriki wa kanisa wanaoombwa kuimba, kuomba (kusali), kusoma Maandiko, au kusifu, na ambao wanabadili fursa hiyo na kuanza kuhubiri? Je, hiki ndicho kinachoelezewa katika Mathayo 23:5-7?
    1.    Soma Mathayo 23:8-11. Wanafunzi wangu katika shule ya sheria huniita “Profesa” na watu kanisani kwangu waliniita kuwa “Mzee” na “mwalimu.” Yesu anabainisha dhambi gani? Je, vyeo hivi ni vya kidhambi? (Tatizo ni kushindwa kutambua kwamba tuna Baba mmoja mbinguni na Mkufunzi mmoja, Yesu. Kilichopo hapa ni vyeo vya kutisha, na si alama za kazi.)
      1.    Je, sehemu ya tatizo ni kwamba maprofesa, wazee, na walimu “wanajivuna na vyeo hivi?
      1.    Je, sehemu ya tatizo ni kwamba viongozi wa kanisa wanadhani kuwa mawazo yao ni ya muhimu zaidi kuliko mawazo ya Mungu? (Soma Mathayo 23:11-12. Lazima jibu kwa maswali haya liwe ni “ndiyo.” Viongozi wanahitaji mtazamo wa kitumishi. Tatizo ni kujikweza na kujivuna.)
      1.    Hebu turejee kwenye swali la awali la kuimba, kuomba, kusoma Maandiko, au kusifu na kubadili mambo hayo kuwa hubiri. Kama ambavyo unaweza kuwa umebashiri, sipendi kitendo hicho. Lakini, je, mtazamo wangu unaakisi jambo jingine zaidi ya mtazamo wa kitumishi?
    1.    Rafiki, je, una wahaka? Roho Mtakatifu ndiye chanzo cha Tunda la Roho. Kwa nini usimwombe Roho Mtakatifu, sasa hivi, akusaidie kuishi maisha yanayoongozwa na Roho?
  1.    Juma lijalo: Gharama ya Pumziko.