Mungu wa Neema na Hukumu
(Yohana 3, Hesabu 21, Ufunuo 14)
Swahili
Year:
2012
Quarter:
1
Lesson Number:
4
Utangulizi: Juma hili tunajifunza vipengele viwili vya Mungu: neema na hukumu. Ukisoma mafungu machache yanayohusu hukumu – hususan ukirejea hukumu inayolenga matendo – unaweza kushangaa jinsi ambavyo neema na hukumu vinavyoendana sawia kwenye injili hiyo hiyo. Kimsingi, kwa muda mrefu sana nimekuwa nikiichukulia kwa dhati sana dhana ya kwamba Yesu mara kwa mara huwa anarejea hukumu inayotegemea matendo ilhali Paulo ana kaulimbiu madhubuti ya wokovu kwa njia ya neema. Je, tunaweza kuhusianisha hayo mawazo mawili pamoja? Kama hivyo ndivyo, je, ni kwa manma gani tutafanya hivyo? Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tuweze kuona kile tunachoweza kujifunza!
- Hukumu
- Soma Mathayo 12:36-37 na Mathayo 16:27. Je, Bwana wetu anasema kuwa kiwango cha hukumu ni kipi? (Maneno yetu na matendo yetu!)
- Soma 2 Wakorintho 5:10. Aaaah la! Huyu ni Paulo. Je, Paulo anasema kuwa msingi wa hukumu ni upi? (Matendo yatendwayo “katika mwili.”)
- Je, kitu gani kinaendelea hapa? Ni majuma machache tu yaliyopita tulijifunza kwenye kitabu cha Wagalatia kuwa tunaokolewa kwa neema. Hebu tulichukulie suala hili katika hali ya mtu binafsi kuhusu hukumu inayotokana na matendo. Je, unataka watu wengine wasimamishwe na kuandikiwa kulipa faini kwa kuendesha kwa mwendo wa kasi barabarani? (Ndiyo! Hususan pale wanapoendesha kwa mwendo wa kasi kwenye maeneo yetu tunapoishi.)
- Vipi kuhusu wewe – je, unataka polisi akuandikie kulipa faini kwa kuendesha kwa mwendo wa kasi? (Hii inathibitisha taswira pana zaidi, tunataka hukumu kutegemeana na matendo ya watu wengine, sio kwa ajili yetu wenyewe.)
- Je, tunadhani kuwa watu wengine wanastahili hukumu kutokana na matendo yao, lakini sisi (walao mimi) tuwe na uwezo wa kuepuka hukumu? (Tunaweza kuona kwamba somo hili ni gumu kidogo kwa sababu tuna upendeleo wa asili dhidi ya hukumu zetu. Hatutaki kupata kile tunachostahili, lakini tungependa watu wengine wakipate kitu hicho hicho.)
- Nyoka Jangwani
- Hebu tuone kama tunaweza kulichukulia suala hili ukiachilia mbali upendeleo wetu. Soma Yohana 3:14-18. Je, Yesu anajichanganya? Yesu anawezaje kusema hapa kuwa imani katika yeye ndio msingi wa uzima wa milele, lakini hapo awali alisema kuwa matendo ndio yalikuwa msingi wa hukumu? (Utabaini kuwa Yesu alikuwa anarejea mtu “anayeshutumiwa” badala ya kuhukumiwa.)
- Juma lililopita tulijadili huduma ya patakatifu. Mdhambi alipokuja hekaluni na kafara, je, mdhambi alikuwa na hatia? (Ndiyo. Tunahukumiwa kwa matendo yetu – aidha tuna hatia ama hatuna hatia. Na bila kuingia kwa undani zaidi, mara zote huwa tuna hatia kwa sababu ya asili yetu ya dhambi. Mdhambi alipokuja na mwana-kondoo, hakuwa “asiye na hatia,” badala yake hakuhumiwa kwa sababu kafara ililipa adhabu kwa niaba yake.)
- Je, bado hatuna tatizo na maneno ya Paulo (2 Wakorintho 5:10) kwamba tutahukumiwa kutokana na mambo “mazuri”? Vipi kuhusu Yesu anaposema (Mathayo 5:10) kuwa tutahukumiwa kutokana na mambo “mazuri?” Vipi kuhusu Yesu anaposema (Mathayo 12:37) kuwa maneno yetu yanaweza “kututendea vizuri/vyema?”
- Hebu tuendelee kusoma katika Yohana 3 ili tuone kama tunaweza kuona kidokezo chochote. Soma Yohana 3:19-21. Sasa tuna kitu kipya, “nuru!” Je, nuru ina nini cha kujihusisha na wokovu wetu? (Tukiupenda mwanga tunaokolewa, tukilipenda giza hatuokolewi.)
- Tuna mambo mengi sana yasiyo sawia hapa. Tuna matendo, tuna imani na tuna nuru. Je, unaweza kuunganisha haya mambo yasiyo sawia ili kuleta nadharia yenye mantiki? Au, je, mawazo yote haya ni mkanganyiko tu?
- Hebu turejee kwenye kisa cha awali (cha asili). Soma Hesabu 21:6-9. Nini kilichosababisha watu wafe? (Nyoka. Hata hivyo, ukiangalia muktadha huo, nyoka walipelekwa pale kama hukumu kwa ajili ya dhambi.)
- Je, kwa nini Mungu alimwambia Musa awaambie watizame kiwakilishi cha kile kilichowafanya wafe? (Kwa muda mrefu sana nimekuwa nikifikiria kwamba hiki kisa cha kutisha kinatufundisha kuwa lazima tuziangalie (tuzichukulie kwa dhati, tuzitubu, nk.) dhambi zetu. Hatua ya kwanza ya kuuelekea wokovu ni kuziangalia na kutubu dhambi zetu, na matendo yetu mabaya.)
- Hebu tusome tena Yohana 3:14-15 na Yohana 3:19-20. Je, ni kwa jinsi gani kisa cha nyoka na kuipenda/kuichukia nuru sasa kinalenta mantiki? (Kwamba kama tukiipenda sana dhambi yetu sana kiasi cha kushindwa kuja nuruni, basi sisi tu kama wale waliokataa kuitazama nyoka. Yesu alileta nuru ya injili. Kuikubali nuru ya injili kimsingi hakuendani na kujificha (kusalia) dhambini. Aidha tutachagua kuzikabili dhambi zetu na kuokolewa kwa neema, au tutapendelea kusalia dhambini na kumkataa Yesu.)
- Je, mazungumzo yote haya kuhusiana na “matendo” na hukumu sasa yanaleta mantiki? (Kwa mtazamo mwingine, wokovu unahusika sana na matendo yetu. Tukiamua kusalia dhambini, hatutaitafuta neema. Lakini, tukizikabili dhambi zetu na kuzitambua, basi tunao uchaguzi mmoja tu – neema!)
- Jielekeze zaidi kwenye Yohana 3:21. Je, hii inamaanisha nini: “kile alichokitenda kimetendwa katika Mungu?” (Neema ni kazi ya Mungu. Kama tulivyojifunza kwenye somo letu la Wagalatia, hatuwezi kujipatia wokovu, Yesu tayari amekwishafanya hivyo kwa ajili yetu. Lakini, tunachagua kama “tutaiangalia nyoka,” kama “tutakuja nuruni,” kama tutatubu dhambi zetu na kuepuka hukumu kwa damu ya Mwana-kondoo.)
- Hebu tuone kama tunaweza kulichukulia suala hili ukiachilia mbali upendeleo wetu. Soma Yohana 3:14-18. Je, Yesu anajichanganya? Yesu anawezaje kusema hapa kuwa imani katika yeye ndio msingi wa uzima wa milele, lakini hapo awali alisema kuwa matendo ndio yalikuwa msingi wa hukumu? (Utabaini kuwa Yesu alikuwa anarejea mtu “anayeshutumiwa” badala ya kuhukumiwa.)
- . Mfano wa Nuhu
- Hebu angalia mfano wa jambo hili. Soma Mwanzo 6:5-7. Je, Mungu anafikiri kuwa suluhisho la huu uovu wote ni lipi? (Hukumu!)
- Soma Mwanzo 6:13, Mwanzo 7:6-10, na 2 Petro 2:5. Je, ilikuwa ni vigumu kiasi gani kwa waovu kuingia kwenye safina? (Walionywa. 2 Petro 2:5 inapendekeza kuwa Nuhu aliwahubiria. Wakati ambapo Nuhu alikuwa akiendelea na juhudi za kujenga safina, mtu mwingine yeyote angeweza kuendelea pia. Waovu walipendelea maisha yao ya sasa (giza), na hawakutaka kuungana na Nuhu (kuja nuruni.))
- Hukumu ya Siku ya Mwisho
- Soma Ufunuo 14:6-7. Je, ujumbe kwa wale wanaoishi katika siku za mwisho ni upi? (Kwamba hukumu ya Mungi i juu yao.)
- Je, mkabiliono wetu sahihi tunapoikaribia hukumu ni upi? (Utabaini kuwa, haisemi kuwa, “usiache kutenda dhambi,” inasema kuwa kwenye mahusiano sahihi na Mungu. Tunahitajika kumtii (kumcha) Mungu, tunahitajika kumpatia utukufu, na tunahitajika kukiri uwezo wake kama Muumba wa vyote.)
- Soma Ufunuo 14:8. Je, ni ukweli gani wa muhimu kuhusu hukumu tunaohitajika kuujua? (Kwamba Mungu ameushinda uovu. Wale wasio waaminifu kwa Mungu wanaelekea chini kabisa kwenye kushindwa.)
- Soma Ufunuo 14:9-11. Je, fungu linasema kuwa wale wanaojihusisha kwenye matendo maovu watahimili nguvu ya hasira ya Mungu? (Hapana. Linasema kuwa wale wanaokataa kumwabudu Mungu, na kumwabudu adui wa Mungu watateseka na hukumu. Kiwango cha hukumu ni utii. Wale wanaokuja nuruni dhidi ya wale wanaosalia gizani.)
- Soma Ufunuo 14:12. Kwa mujibu wa hii hukumu inayokaribia, je, tunaitwa kufanya kitu gani? (“Malaika” wanaelezewa kuwa kama wale “wanaosalia kuwa waaminifu kwa Yesu.” Imani katika Yesu ni haki kwa imani!)
- Vipi kuhusu sehemu ya “kutii amri za Mungu?” (Hii inaelezea mjadala wetu wa awali. Tukiyapenda matendo yetu maovu, tutakaa gizani na hatutakuja kwenye nuru ya neema ya Yesu. Lakini, tukiipenda nuru, basi tutataka kuyafanya mapenzi ya Yesu. Tutataka kumtii.)
- Tafakari mafungu katika Ufunuo 14 ambayo tumeyasoma hivi punde. Je, tofauti ya msingi kati ya wenye haki na wasio na haki? (Wenye haki wanamwabudu na kumtukuza Mungu Muumba wao. Waovu wanaawabudu na kuwatii waovu. Hiki ndicho kinachomaanishwa kwa chapa katika kipaji cha uso (akili) na mkono (matendo). Utajwaji wa kuabudu, uumbaji na amri unapendekeza umuhimu mkubwa wa Sabato ya kila juma, kwani ni muda wa kuabudu, muda wa kumpa Mungu utukufu, na muda wa kusherehekea Uumbaji (“Ikumbuke siku ya Sabato …. maana kwa siku sita [Mungu aliumba].”))
- Rafiki, hukumu inakuja. Hukumu itategemeana na matendo yetu. Kwa kiwango hicho, hakuna hata mmoja wetu anayeweza kuepuka hukumu. Hata hivyo, Yesu anatupatia njia ya kuepuka ya kuhukumiwa kutokana na matendo yetu maovu. Yeye ni Mwana-kondoo wa Mungu aliyekufa kwa ajili ya dhambi zetu. Tukizikabili dhambi zetu kwa kuzikiri na kuzitubu, basi atazifunika dhambi zetu kwa damu yake. Je, hii ni ofa unayoweza kuikataa? Kama sivyo, kwa nini usiikubali hii leo? Kabiliana na nyoka wa maisha yako ya kidhambi, na utoke kwenye giza na uingie nuruni!
- Soma Ufunuo 14:6-7. Je, ujumbe kwa wale wanaoishi katika siku za mwisho ni upi? (Kwamba hukumu ya Mungi i juu yao.)
- Juma lijalo: Utakatifu wa Mungu.