Somo la 4: Gharama ya Pumziko
Somo la 4: Gharama ya Pumziko
(2 Samweli 11-12, Zaburi 51)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Juma lililopita tuliangalia baadhi ya Matunda ya Roho. Mojawapo ya tunda tulilolibainisha ni “amani,” ambalo ni tunda la tatu. Angalia Wagalatia 5:22. Je, amani inahusiana kivyovyote vile na pumziko? Ninadhani inahusiana. Inaonekana ni vigumu kupata pumziko ikiwa huna amani. Je, utakubaliana kwamba kuachana na vitendo “vinavyokuibia amani yako” ni “gharama” ya pumziko? Kwa mfano, ikiwa unakubaliana kwamba kuwahi kazini kwa wakati ni muhimu ili kuendelea kuwa kwenye ajira yako, basi kuachana na usingizi kitandani ni gharama, “gharama” moja ya kuendelea kuwa na ajira. Yote haya yanaashiria kuwa maisha yanayoongozwa na Roho Mtakatifu ni kigezo kwa ajili ya kuwa na pumziko la kweli. Hebu tuzame kwenye somo letu tuone kama Biblia inakubaliana na dhana hii.
- Mtazamo
-
- Soma 2 Samweli 11:1. Je, unatarajia Mfalme aliongoze jeshi? (Daudi alikuwa mpiganaji, hivyo ingekuwa kawaida kumtarajia awe na jeshi lake.)
-
-
- Je, ungekuwa na amani na pumziko kama ungekuwa vitani? (La hasha.)
-
-
-
- Je, ungejisikia hatia kama ungedhani kuwa hukuwa ukifanya kazi yako vizuri?
-
-
- Soma 2 Samweli 11:2. Je, Daudi yuko mahali penye amani?
-
-
- Unadhani Daudi ana uchoshi (bored)? (Huenda ana amani kubwa kupita kiasi.)
-
-
- Hebu tujikite kwenye sehemu ya pili ya 2 Samweli 11:2. Unapokuwa unaoga, je, huwa uko makini kuzingatia kama watu wanaweza kukuona? Zingatia kifungu kinasema kuwa huu ulikuwa “wakati wa jioni.” Huu ni wakati ya kutwa.
-
-
- Kama wewe ni mwanamke mrembo, je, ungependa watu wakuone na kupendezewa nawe?
-
-
-
- Au, unadhani kuna uwezekano kwamba mwanamke huyu hakuwa na habari kuwa anaweza kuonekana?
-
-
- Soma 2 Samweli 11:3. Je, kuna ubaya wowote kwa Daudi kuulizia habari za mwanamke huyu mzuri?
-
-
- Je, jibu hili linamhabarisha Daudi juu ya kila anachohitaji kukifahamu? (Anatambua kuwa mwanamke huyu ameolewa.)
-
- Dhambi
-
- Soma 2 Samweli 11:4. Je, kuna ubaya wowote kwa Daudi kutaka kukutana na mke wa Uria Mhiti?
-
-
- Je, unapenda kukutana na kutumia muda wako na watu wa jinsia tofauti walio warembo au wenye nguvu na ushawishi mkubwa?
-
-
-
- Kabla hawajakutana unadhani kuwa Daudi na Bathsheba walifanya uamuzi ikiwa wako radhi kufanya ngono? Au, kuna uwezekano mkubwa kwamba kitendo cha ngono kilitokea tu kama ajali?
-
-
-
- Walipofanya ngono, kwa dhahiri walivuka msitari wa dhambi. Biblia haisemi chochote kama Bathsheba alilazimishwa. Wasomi wa Biblia wanaashiria kuwa hakulazimishwa. Tuchukulie kwamba hakulazimishwa, kitu gani kilimhamasisha kufanya ngono na Daudi?
-
-
-
-
- Kitu gani kilimhamasisha Daudi kufanya naye ngono kinyume na mapenzi ya Mungu? (Sidhani kama “ashiki,” au “tamaa” vinatoa maelezo ya kutosha. Unaweza kuwa na ashiki na tamaa bila kufanya ngono. Mzizi wa dhambi ulikuwa ni ubinafsi. Daudi alijipenda zaidi kuliko kulipenda neno la Mungu.)
-
-
-
-
- Unadhani baada ya kufanya ngono, Daudi na Bathsheba walikuwa na amani?
-
- Matokeo
-
- Soma 2 Samweli 11:5. Je, sasa wana amani?
-
-
- Kichwa cha habari cha somo letu kinasema “Gharama ya Pumziko.” Gharama ya pumziko ni ipi hapa? (“Gharama” ya amani (ambayo ni muhimu kwa ajili ya pumziko) ni kujizuia kufanya ngono na mtu asiye mke wako. Usiwe mbinafsi.)
-
-
- Soma 2 Samweli 11:7-9. Hii inatuambia nini kuhusu Uria? (Kwa dhahiri si mbinafsi.)
-
- Soma 2 Samweli 11:11-13. Uria yuko radhi kula na kunywa na Daudi (tofauti na mke wake), kwa nini Daudi anataka kumlevya Uria? (Ingawa kitendo hicho hakikufanya kazi kwa upande wa Uria, hii inatufundisha kwamba ni vigumu zaidi kuwa mwaminifu kwa Mungu tunapokuwa tumelewa.)
-
-
- Je, Bathsheba na Daudi wana amani mbele ya Uria kwa kitendo chake cha kutokuwa mbinafsi?
-
-
- Soma 2 Samweli 11:15 na 2 Samweli 11:23-25. Je, unadhani kuwa sasa Bathsheba na Daudi wana amani? (Bado dhambi yao ni ya siri, lakini amempoteza mumewe na Daudi amesababisha kifo cha askari zaidi ya mmoja.)
-
- Soma 2 Samweli 11:26-27, 2 Samweli 12:1, na 2 Samweli 12:7-9. Unahimizwa kusoma kisa chote anachokielezea Nathani ili kumtia hatiani Daudi kutokana na dhambi yake ya kikatili na kufedhehesha. Kama Mungu hafurahishwi nawe, je, anaacha tu mambo yapite hivi hivi bila kuchukua hatua?
-
-
- Unayaweka katika mizania gani malalamiko ya Mungu dhidi ya Daudi? Je, ni kwa kuwa tu alifanya uzinzi? (Malalamiko ya Mungu ni kwamba Daudi hana shukrani. Mungu amembariki Daudi, kwa nini anamtaka mke wa Uria? Kwa nini anahitaji kuua?
-
-
-
- Ungejibu nini kama ungekuwa Daudi? (Nadhani nia ya Daudi kuua ilikuwa ni kuepuka fedheha. Uzinzi ulikuwa ni dhambi iliyostahili adhabu ya kifo. Kiuhalisia hakuna aliyekuwa anamuua Mfalme, lakini ingekuwa kashfa.)
-
-
- Soma 2 Samweli 12:11-13. Una maoni gani kwamba Mungu amemsamehe Daudi papo hapo kutokana na dhambi yake, lakini Mungu ametangaza adhabu iliyoongeza fedheha ambayo Daudi atataabika na kuteseka nayo kutokana na dhambi hii?
-
-
- Ninawasikia watu wakisema kuwa Mungu anasamehe dhambi zetu, lakini haondoi matokeo ya dhambi. Ninadhani wanazungumzia matokeo ya asili, si matokeo anayoyaamuru Mungu. Je, Mungu anatenda haki? Je, analipiza kisasi?
-
-
-
- Tafakari matokeo mabaya aliyoyapitia Mungu kutokana na dhambi ya Daudi. Ni matokeo gani hayo? (Kiongozi wa Mungu, mtu ambaye Mungu amembariki, anaidharau sheria ya Mungu. Anamfedhehesha Mungu na kuhimiza uvunjaji wa sheria.)
-
-
-
- Kwa kuwa sasa tumeliangalia hili kupitia jicho la Mungu, unaizungumziaje haki ya Mungu? (Daudi anasimama kama mfano wa matokeo ya kuidharau sheria ya Mungu. Hakuna mtu mwenye kutumia akili ya kawaida atakayesema “Daudi alipona dhambi yake, hivyo nami niko huru kufanya kile alichokifanya.”)
-
-
-
- Je, umewahi kudhani kuwa unaweza kutenda dhambi na mambo yakawa sawa kwa kuwa Mungu atakusamehe?
-
-
-
- Kwa nini Mungu hakumsaidia Daudi kufanya mambo yote haya kuwa siri kubwa? Hii ingeepusha fedheha kwa wote wawili. (Utaona katika 2 Samweli 12:11-12 kwamba mara mbili Mungu anabainisha kuwa atatenda mambo “mbele ya jua.” Soma Yohana 12:46 na Luka 8:17. Mungu ni nuru, analeta nuru na halisaidii giza.)
-
- Gharama ya Pumziko
-
- Soma Zaburi 51:3-4. Daudi anajihukumuje na kuichukuliaje haki ya Mungu? (Anasema kuwa Mungu ni “safi atoapo hukumu [Yake].”)
-
- Soma Zaburi 51:7-8. Daudi anatafuta nini? Je, hii inaendana na amani na pumziko?
-
- Soma Zaburi 51:10-12. Kitu gani kitampatia Daudi pumziko?
-
- Soma Zaburi 51:13. Hii inaelezeaje suala la dhambi ya Daudi kuwahamasisha watu wengine kutenda dhambi? (Daudi anasema kuwa anataka kuwa na ushawishi mzuri, badala ya kuwa na ushawishi mbaya.)
-
- Rafiki, je, unataka pumziko? Maisha yanayoendana na mapenzi ya Mungu huleta amani. Amani hiyo hukupatia pumziko. Kwa nini usimwombe Roho Mtakatifu, sasa hivi, akuumbie moyo safi na kuifanya upya roho iliyotulia ndani yako?
- Juma lijalo: “‘Njoni Kwangu... ’”