Somo la 6: Kupata Pumziko Katika Uhusiano wa Kifamilia

Mwanzo 37, 39, 41 & 50; Waefeso 6
Swahili
Year: 
2021
Quarter: 
3
Lesson Number: 
6

Somo la 6: Kupata Pumziko Katika Uhusiano wa Kifamilia

(Mwanzo 37, 39, 41 & 50; Waefeso 6)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Mojawapo ya baraka kubwa kabisa kwangu ni kwamba nina uhusiano mzuri sana na familia yangu. Uhusiano wako na familia yako ukoje? Katika Somo la 3 tulijadili alichokisema Yesu katika Mathayo 10 kuhusu kuleta mgawanyiko kwenye familia. Je, dhana iliyopo kwenye kichwa cha somo si sahihi? Je, hali yangu ya uhusiano wa kifamilia ni jambo la nadra? Kama inawezekana kupata pumziko katika uhusiano wa kifamilia, tunalifikiaje pumziko hilo? Huenda, inaweza kuwa na ufanisi zaidi kujifunza kile tunachopaswa kuepuka kukitenda. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tujifunze zaidi!

 1.    Kusababisha Purukushani
  1.    Soma Mwanzo 37:3. Yusufu ni mwana anayependwa zaidi, ingawa ni wa pili kutoka mwisho kwa kuzaliwa! Kwa nini anapendwa zaidi na Israeli (Yakobo)? (Kifungu kinasema ni kwa sababu Yusufu alizaliwa wakati baba yake akiwa mzee. Baba yake alikuwa mzee zaidi wakati Benyamini alipozaliwa. Angalia Mwanzo 42:4,13.)
   1.    Je, nia ya Yakobo inaleta mantiki yoyote kwako?
  1.    Soma Mwanzo 37:4. Je, kimsingi ni kwamba Yakobo anamnufaisha Yusufu? (Ndugu zake wanamchukia kiasi kwamba hawaongei naye kwa amani.)
   1.    Je, Yakobo ni mjinga? Unadhani ana upofu kwa kile alichokifanya? Unadhani matokeo ya kumpatia Yusufu kanzu maalum ilikuwa ni jambo lisiloweza kuonekana?
    1.    Unadhani Yakobo anajali? (Ninachukulia kwamba Yakobo si mjinga. Bali, hajali kama wanaye wengine hawapendi kile alichokifanya kumheshimisha Yusufu.)
   1.    Tunajifunza nini katika jambo hili kwa wazazi wa leo? (Usionyeshe upendeleo! Fikiria mambo kwa kina na kwa umakini mkubwa. Kama utakuwa na mtoto umpendaye zaidi, ni vizuri zaidi sababu za kumpenda zikawa bayana kwa kila mtu – hadi kwa watoto wasiopendelewa.)
  1.    Soma Mwanzo 37:5-8. Je, Yusufu ni mjinga? Unadhani ana upofu kwa kile alichokifanya?
   1.    Unadhani Yusufu anajali kuhusu kile wanachokifikiria ndugu zake?
   1.    Taarifa ya Yusufu juu ya ndoto yake inatuambia nini kuhusu endapo ni mjinga, asiyejali, au jambo lolote jingine?
   1.    Tunajifunza nini katika jambo hili kwa watoto wanaopendwa zaidi katika zama za leo? (Kuonyesha hali yako ya kupendelewa mbele ya ndugu zako ni jambo baya. Inaonekana si Yakobo wala Yusufu aliyetafakari kwa kina tatizo hili. Hakuna hata mmoja kati yao aliyeonyesha umahiri wa kutawala hisia (emotional intelligence).)
 1.   Malipo
  1.    Soma Mwanzo 37:12-14. Kazi hii ya kutumwa inachukuliwaje na ndugu zake Yusufu? (Baba yake amemtuma kijana mdogo kuchunguza kazi ya kaka zake wakubwa!)
   1.    Je, ungekasirika juu ya jambo hili endapo ungekuwa kaka mkubwa na mwenye ukomavu zaidi?
  1.    Soma Mwanzo 37:18-20. Iliwachukua muda gani kufanya uamuzi wa kumwua Yusufu?
   1.    Je, hii njama ya kufanya mauaji imejengwa juu ya mtazamo wa Yusufu dhidi yao? (Ndiyo. Wanaifungamanisha moja kwa moja na taarifa ya ndoto ya Yusufu.)
   1.    Je, ndugu hawa ni watu waovu kweli kweli?  Au, je, njama hii ya mauaji ina sababu za msingi?
    1.    Kama umejibu kuwa kweli ni watu waovu, una maoni gani kwamba wanakuwa wakuu wa makabila kumi na mawili ya Israeli?
  1.    Soma Mwanzo 37:21-22 na Mwanzo 37:25-28. Reubeni alipaswa kutenda jambo gani kwa namna nyingine tofauti?
   1.    Kwa nini Mungu anaruhusu jambo hili? Je, hili ni kosa la Yakobo na Yusufu?
   1.    Je, wale ndugu waovu (isipokuwa Reubeni) wanawajibika kwa matendo yao licha ya makosa ya kijinga ya Yakobo na Yusufu?
    1.    Natumai tunakubaliana kwamba kamwe mauaji hayahalalishwi. Hata hivyo, katika kushughulika na wanafamilia, je, tunapaswa kufanya marekebisho kwa ajili ya dhambi? Je, tunapaswa kujaribu kuridhia mitazamo ya dhambi bila kuiidhinisha?
 1. Kumtumaini Mungu
  1.    Soma Mwanzo 39:1-3. Jiweke kwenye nafasi ya Yusufu. Mungu anabariki kila unachokifanya. Unapatanishaje suala la kuuzwa utumwani na wakati huo kuo kubarikiwa?
  1.    Soma Mwanzo 39:6-9. Kwa nini Yusufu anaashiria kuwa kufanya ngono na mke wa bwana wake ni dhambi dhidi ya Mungu badala ya bwana wake? (Hii inaturejesha nyuma kwenye somo letu majuma mawili yaliyopita kuhusu Mfalme Daudi. Anasema kuwa dhambi yake ilikuwa dhidi ya Mungu pekee (Zaburi 51:4), na malalamiko ya msingi ya Mungu dhidi ya Daudi ni kwamba alifanya hivi mbele ya baraka kubwa ya Mungu kwake. 2 Samweli 12:8-9. Mtazamo wa Yusufu unafanana na ule wa Daudi kwa kuzingatia aina ya dhambi, tofauti ni kwamba Yusufu anakiri na kutambua baraka zake na anamtii Mungu.)
   1.    Tafakari tofauti zilizopo kwa namna ambavyo Daudi na Yusufu walikuwa wamebarikiwa hadi kufikia hapa.
  1.    Soma Mwanzo 39:20-21. Hakuna jambo jema lisiloadhibiwa, sawa? Kwa kuwa Yusufu alikuwa mwaminifu, anatupwa gerezani. Hadhi yake katika jamii inaendelea kudorora na kudorora. Jiweke tena kwenye nafasi ya Yusufu. Utapatanishaje jambo hili na kauli ya kwamba Mungu anamwonesha “fadhili?”
  1.    Soma Mwanzo 41:10-12 na Mwanzo 41:14-15. Je, ilikuwa muhimu kwa Yusufu kuwekwa gerezani kwa tukio hili kujitokeza?
  1.    Yusufu anamtukuza Mungu na kutafsiri ndoto ya Farao, ndoto ikitafsiri njaa katika siku zijazo. Soma Mwanzo 41:39-41. Tafakari kama Mungu angeweza kutoa mwongozo huu kwa Farao (au mtu yeyote mwenye mamlaka makubwa) kuwaokoa watu dhidi ya njaa kwa namna ambayo ingekuwa na madhara madogo kwa Yusufu?
   1.    Kwa kawaida maisha ya Yusufu hufananishwa na maisha ya Yesu. Je, Mungu angeweza kuwaokoa wanadamu kwa namna ambayo ingekuwa na madhara madogo kwa Yesu?
  1.    Soma Mwanzo 50:19-21. Hili ni jibu la Yusufu kwa swali la kwa nini Mungu aliruhusu auzwe utumwani. Je, unakubaliana na Yusufu?
   1.    Kama kuna jambo lisiloenda vizuri katika familia yako, je, hii ndio sababu? Je,Mungu analeta jambo zuri kutokana na jambo hilo?
   1.    Yusufu anasema kuwa ndugu zake “walikusudia mabaya” dhidi yake. Je, baadhi ya wanafamilia wako wanakusudia mabaya kwako au kwa wanafamilia wengine?
    1.    Au, je, wewe ndiye “uliyekusudia mabaya?”
 1.   Zitafakari Njia Zako
  1.    Soma Mwanzo 50:24. Yusufu aliona nini juu ya mustakabali wa watu wake? (Kwamba watarejea Kaanani.)
  1.    Soma Kutoka 1:8-10 na Kutoka 1:13. Kwa nini Mungu aliruhusu jambo hili?
   1.    Kwa nini watu wa Mungu hawakuondoka Misri Yusufu alipofariki?
   1.    Kwa nini watu wa Mungu hawakuondoka Misri na kurejea kwenye nchi ya ahadi njaa alipokwisha?
   1.    Je, utumwa wa uzao wa ndugu wa Yusufu ni matokeo ya haki kwa kitendo chao cha kumuuza Yusufu utumwani?
  1.    Soma Waefeso 6:1-3. Kama wewe ni mtu mzima kiasi cha kutosha kuweza kushuhudia uhusiano wa kifamilia ukikua kwa muda mrefu, je, unaona mwelekeo huo huo hapa? Wale waliowatendea wengine mabaya wanajikuta wakitendewa mabaya?
  1.    Inaonekana kuwa mataifa yote kwa wakati fulani yaliruhusu utumwa. Hii ilikuwa sifa ya ulimwengu wa Kikristo na Kiislamu. Nimesoma mahali kwamba hivi leo kuna watumwa wengi zaidi duniani kuliko wale waliohusika katika biashara ya utumwa ya Atlantiki. Je, mwelekeo huu wa malipo bado upo?
   1.    Kama malipo yapo, nani anayepaswa kupata mateso ya malipo?
   1.    Katika suala la Yusufu malipo yalikuja dhidi ya uzao wa ndugu zake waliomuuza utumwani, na si kwa wale waliomnunua.
   1.    Au, je, kuangamizwa kwa jeshi la Misri na mateso yanayofanana na hayo yaliyosababishwa na mapigo ndio malipo yenyewe? Angalia Kutoka 7-15.
  1.    Soma Waefeso 6:5-9. Yusufu alidhihirisha mtazamo gani kuhusu utumwa wake? Biblia inasema tuwe na mtazamo gani kuhusu utumwa? (Yusufu anaonekana kushikilia mtazamo chanya. Waefeso inatuambia kuwa tukitenda mema, hata katika mazingira magumu, Mungu atatulipa mema hayo. Waefeso pia inawaonya mabwana wa watumwa kuhusu malipo.)
   1.    Unapatanishaje mtazamo wa Yusufu na Biblia na mamia ya miaka ya utumwa waliyoteseka wana wa ndugu za Yusufu?
  1.    Rafiki, tunaona kwenye somo letu kwamba uamuzi wa kijinga wa familia uliendelea kuongeza matatizo ya kutisha. Je, utamwomba Roho Mtakatifu akupatie hekima kwenye uhusiano wa kifamilia?
 1.    Juma lijalo: Pumziko, Uhusiano, na Uponyaji.