Somo la 6: Tena Liko Taifa Gani Kubwa?

Kumbukumbu la Torati 4, Hesabu 22-25, Mathayo 15
Swahili
Year: 
2021
Quarter: 
4
Lesson Number: 
6

Somo la 6: Tena Liko Taifa Gani Kubwa?

(Kumbukumbu la Torati 4, Hesabu 22-25, Mathayo 15)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Je, kuna mafundisho magumu kwenye Biblia? Je, nyakati nyingine tunapata changamoto ya kumwona Yesu katika “Mungu wa Agano la Kale?” Jibu ni “ndiyo.” Juma hili tunalo fundisho gumu. Lakini, badala ya kugeuza macho yetu, tunatakiwa kujifunza mafunzo magumu ili kubaini kile ambacho Mungu anataka kutufundisha. Hebu tuzame kwenye somo letu la Kumbukumbu la Torati 4 na tujifunze zaidi!

  1.    Kupunguza Neno
    1.    Soma Kumbukumbu la Torati 4:2. Katika somo lililopita tuliangalia kilichomaanishwa tunaposema kuongezea neno katika neno la Mungu. Tutafanya hivyo tena baadaye katika somo hili. Hebu tuangalie kupunguza neno katika neno la Mungu. Unadhani inamaanisha nini “kupunguza neno katika [amri za Mungu]?” (Kuwaambia kuwa amri za Mungu hazijalishi.)
    1.    Soma Kumbukumbu la Torati 4:3. Mungu anazielekeza wapi akili za watu kwa ajili ya ufafanuzi wa hili suala la “kupunguza neno” katika amri za Mungu? (Jambo lililotokea kule Baal-peori.)
  1.   Baal-peori
    1.    Soma Hesabu 22:1-3. Watu wa Moabu wanaonyesha hisia gani (mjibizo) kwa watu wa Mungu wanaoikaribia Kaanani? (“Wanajawa hofu.” Wana wasiwasi kwamba Israeli itawaangamiza.)
    1.    Soma Hesabu 22:4-6. Mfalme wa Moabu anabuni mpango gani ili kulilinda taifa lake? (Anaamua kujihusisha kwenye pambano la kiroho dhidi ya watu wa Mungu. Anafanya uamuzi kwamba vita vya asili vitasababisha maafa kwa watu wa Moabu na Midiani.)
    1.    Mfalme Balaki wa Moabu anatoa fedha kwa nabii Balaamu ili ailaani Israeli. Hebu tuone jinsi jambo hilo linavyofanya kazi. Soma Hesabu 23:23-26. Balaamu anaishia kufanya nini? (Kuwabariki watu wa Mungu. Anasema Israeli itateketeza mawindo yake na kunywa damu ya waliouawa.)
      1.    Mfalme Balaki anatoa ombi gani la mwisho kabisa katika kuonyesha hisia zake kwenye baraka hii? (Anaacha kuomba kwamba watu hawa walaaniwe, na kumwomba Balaamu angalao basi aache kuwabariki.)
    1.    Tumeruka sehemu kubwa ya utangulizi huu, lakini kwa ufupi ni kwamba Balaamu aliibariki Israeli mara tatu wakati alitakiwa kuilaani. Kwa utangulizi huu, soma Hesabu 25:1-2. Moabu imegundua mkakati gani mpya wa kuishambulia Israeli? (Yumkini si mkakati mpya sana – hili ni shambulizi la kiroho la aina tofauti.)
      1.    Je, Shetani ataendelea kutafuta njia mpya za kujaribu kutushambulia?
    1.    Soma Hesabu 25:3. Watu wa Mungu wamevunja amri gani? (Amri ya kwanza na ya pili (dhidi ya kuabudu miungu mingine), na amri ya saba (dhidi ya uzinifu).)
      1.    Mungu anaonyesha hisia gani kwenye kitendo hiki cha “kupunguza neno” katika amri zake? (Amekasirika.)
        1.    Unadhani kwa nini Mungu amekasirika? Je, ni kutokana na kufedheheshwa? Au, amekasirika kwa sababu watu wake wanatenda mambo ya kipumbavu yatakayowanyima baraka alizowapatia?
    1.    Soma Hesabu 25:4-5. Viongozi wa Israeli wanashughulikiwaje? (Viongozi wa wafuasi “waliojiungamanisha” na Baali wanauawa. Viongozi wanadhihirishwa hadharani kama mifano ya watenda mabaya.)
    1.    Soma Hesabu 25:6. Watu wengi wanaonyesha hisia gani kwenye jambo hili? (Wanalia.)
      1.    Kilio hiki kinatofautianaje na mtu anayemleta mwanamke wa Mimidiani “katika familia yake?” (Tofauti ni kubwa. Watu wengi wanalia kuhusiana na hili. Mtu huyu anaendelea na dhambi yake kwa ujasiri – hajali kama watu wote wanamwona.)
    1.    Soma Hesabu 25:7-9. Hii iaashiria kuwa viongozi wa dini walioidhinishwa wanapaswa kufanya nini kuhusu dhambi ya wazi mbele za watu? (Kuchukua uamuzi madhubuti dhidi ya dhambi hiyo.)
    1.    Hebu tuzungumzie kuhusu kisa hiki “kigumu.” Watu wa Mungu walikuwa kwenye uhatarishi kiasi gani kwenye mashambulizi ya asili ya kijeshi? (Hawakuwa katika hali hatarishi.)
      1.    Je, Shetani aliweza kuiba baraka zao bila ridhaa yao? (Hapana! Balaamu aliweza tu kuwabariki.)
      1.    Shetani alitakiwa kutumia mkakati gani ili kuwashinda? (Alilazimika kuwashawishi watu wa Mungu kuzikataa amri za Mungu. Alilazimika kuwashawishi watu wa Mungu kujidhuru wenyewe.)
      1.    Kuna fundisho gani kwenye kisa hiki kwa Wakristo wa leo? (Shetani hawezi kuwashinda moja kwa moja wale wanaobarikiwa na Mungu. Badala yake, lazima Shetani apate kibali ili baraka zetu ziweze kuondolewa. Lazima turidhie ili tudhuriwe.)
      1.    Je, umewahi kumsikia mtu akisema kuwa Shetani anamshambulia? Jibu sahihi kwa swali hilo ni lipi? (Shetani anaweza tu kutudhuru kama tukiiacha njia ya Mungu.)
      1.    Vipi kuhusu kisa cha Ayubu? Kamwe hakuiacha njia ya Mungu kabla hajashambuliwa na Shetani? (Soma Ayubu 2:3-6. Hii inatuonesha kuwa kauli yangu kwamba “tunaweza kudhuriwa tu” ikiwa tutaiacha njia si kauli sahihi. Tunaweza tu kudhuriwa kwa uamuzi wetu na ruhusa dhahiri ya Mungu.)
  1. Ambatana
    1.    Soma Kumbukumbu la Torati 4:4. Kisa hiki kinafuatia mara tu baada ya rejea ya kisa cha Baal-peori. Mungu anatutaka tuchukue fundisho gani kutoka kwenye kisa hicho? (Mungu hasemi kuwa, “usinikasirishe.” Badala yake, Mungu anaoyesha baraka za kuwa hai. Watu wa Moabu walidhamiria kuwaua.)
    1.    Soma Kumbukumbu la Torati 4:5-6. Watu wataonyesha hisia gani kwako kama unamtii Mungu? (Watakuita mtu mwenye “hekima na akili.”)
      1.    Je, ungelipendelea jambo hilo?
      1.    Je, hivyo ndivyo watu wanavyokuita sasa?
  1.   Kuabudu Bure
    1.    Soma Mathayo 15:8-9. Sasa tunageukia kwenye “kuongezea neno” kwenye kile anachokiamuru Mungu. Mungu analiitaje tatizo la kubadilisha “amri za wanadamu” kuwa amri za Mungu? (Kuabudu bure.)
      1.    Nini maana ya kuabudu bure? (Inamaanisha kuwa kuabudu huko hakuna manufaa kwako.)    
    1.    Soma Mathayo 15:10-11. Je, unamfahamu mtu yeyote anayeshindwa kulielewa hili?
    1.    Soma Mathayo 15:12. Baadhi ya watu wataitikiaje kile alichokisema Yesu kuhusu asili halisi ya kutiwa unajisi? (Wanachukizwa.)
    1.    Soma Mathayo 15:13-14. Walimu hawa wa uongo wamechukizwa. Tunapaswa kuwachukuliaje? (Tuachane nao. Tuwapuuzie tu.)
      1.    Soma Warumi 14:1-4. Je, fundisho la Warumi linaendana na alichokisema Yesu katika Mathayo 15? (Hapa tunahitaji utambuzi. Warumi 14 ni mjadala wa kanuni zinazoleta mashaka (“maoni”). Yesu anabainisha kuwa wale wanaoongezea neno kwenye amri za Mungu wanaweza kusababisha madhara makubwa.)
    1.    Soma Mathayo 15:15-20. Suala mahsusi ni kula bila kunawa mikono kwanza. Maelezo ya Yesu kwa Petro yanaenda mbali zaidi ya unawaji mikono. Unaweza kusema kuwa maelezo ya Yesu yanakwenda mbali kiasi gani?
      1.    Je, maelezo hayo yanahusika kwenye chochote kile ukilacho? (Nadhani suala la msingi kwetu ni kutofautisha kati ya mawazo mazuri na amri za Mungu. Unapaswa kuyatia alama “mawazo yako mazuri” kwa muktadha huo huo tu, bila kutoa madai kwamba ndicho anachokitaka Mungu. Endapo sikubaliani, ninapaswa tu kupuuzia madai yako ya kuwa na mawazo mazuri.)
    1.    Angalia tena Mathayo 15:19-20. Je, kanisa lako limejikita zaidi kwenye “mawazo mazuri” au hizi dhambi kubwa?
      1.    Vipi kuhusu wewe? Umejikita wapi? (Yesu anasema katika Mathayo 15:14 kwamba kama msisitizo wetu hauko sahihi, basi sisi ni “viongozi vipofu” tutakaowasababishia watu wengine kutumbukia shimoni – shimo lile lile tulilomo.)
    1.    Rafiki, kama unataka baraka ambazo Mungu ameziahidi, unatakiwa kufuata amri zake. Tunatakiwa kukaa mbali na eneo hatarishi la kutokutii. Wakati huo huo, tunatakiwa kuwa makini kuchora msitari wa dhahiri kati ya amri za Mungu na mawazo mazuri ya wanadamu ili kuepuka kukiuka amri za Mungu. Je, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, utakuwa makini katika kufuata njia za baraka?
  1.    Juma lijalo: Sheria na Neema.