Somo la 12: Kumbukumbu la Torati Katika Agano Jipya

Mathayo 4, Kumbukumbu la Torati 6, 8 & 32, Wagalatia 3, Waebrania 10
Swahili
Year: 
2021
Quarter: 
4
Lesson Number: 
12

Somo la 12: Kumbukumbu la Torati Katika Agano Jipya

(Mathayo 4, Kumbukumbu la Torati 6, 8 & 32, Wagalatia 3, Waebrania 10)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Juma lililopita tulijifunza juu ya kunukuliwa. Kwa mahsusi, kunukuliwa pale kitabu cha Kumbukumbu la Torati kiliponukuliwa katika maeneo mengine kwenye Agano la Kale. Tulihitimisha kwamba nukuu hizo zilionyesha umuhimu wa kitabu cha Kumbukumbu la Torati. Juma hili tunaendelea na mada ile ile ya kunukuu, isipokuwa tu safari hii tunaangalia jinsi kitabu cha Kumbukumbu la Torati kinavyonukuliwa katika Agano Jipya. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tujifunze zaidi!

  1.    Pambano Nyikani – Sehemu ya I
    1.    Soma Mathayo 4:1. Katika sura iliyotangulia, Yesu ametoka kubatizwa. Kwa nini Roho Mtakatifu amwongoze Yesu majaribuni? Nilidhani Roho Mtakatifu yuko hapa ili kutukinga dhidi ya majaribu?
      1.    Soma sehemu hii ya Sala ya Bwana katika Mathayo 6:13 na usome Yakobo 1:13. Sala ya Bwana inaonekana kuashiria kuwa hilo linaweza kutokea. Unaelewaje suala la Mungu kutujaribu? Kwani hiyo si kazi ya Shetani?
    1.    Soma Mathayo 4:2-3. Kuna jambo gani hatarishi katika jaribu hili?
      1.    Unadhani Shetani amekuwa akipangilia jambo hili kwa muda mrefu sana? Unadhani alifanya mikutano kadhaa miongoni mwa pepo wa ngazi za juu ili kujadili majaribu bora kabisa ya kuletwa dhidi ya Yesu?
      1.    Ikiwa umejibu kuwa mustakabali wa dunia na ulimwengu ulikuwa hatarini, ikiwa ulidhani kuwa Shetani ataleta majaribu yake bora kabisa dhidi ya Yesu, je, jaribu hili halionekani kuwa la kishamba kidogo? (Nadhani kuwa Roho Mtakatifu alimharakisha Yesu kwenye pambano hili kabla Shetani hajalitarajia. Roho Mtakatifu alilipeleka pambano kwa Shetani, hakuwa akimsaidia Shetani kumjaribu Yesu, bali kinyume chake.)
    1.    Soma Mathayo 4:4. Unadhani Yesu alimaanisha nini kwa kauli hii? Je, badala yake Yesu atakula maneno ya Mungu?
    1.    Soma Kumbukumbu la Torati 8:1-3. Tunaweza kuona kwamba Yesu ananukuu Kumbukumbu la Torati 8:3. Maneno haya yanamaanisha nini katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati? Muktadha unatusaidiaje kuelewa jambo hili vizuri zaidi? (Kinachomaanishwa katika Kumbukumbu la Torati ni kwamba tunapaswa kumtumaini Mungu kwa mahitaji yetu muhimu. Mungu aliwalisha kwa namna isiyotarajiwa kabisa. Alikuwa suluhisho la njaa yao.)
      1.    Kwa kuwa sasa umeshauangalia muktadha, “unatafsirije” jibu la Yesu kwa Shetani? (“Hapana, nashukuru. Nadhani nitamtumaini tu Mungu kushughulikia njaa yangu.”)
  1.   Pambano Nyikani – Sehemu ya II
    1.    Soma Mathayo 4:5-7. Una maoni gani juu ya usasa/ustaarabu wa jaribu hili? (Linaonekana kutofautiana na jaribu la kwanza, lakini ni baya zaidi. Bado Shetani anatia changamoto suala la Uungu wa Yesu, lakini kwa namna inayoonekana kuwa na mvuto mdogo zaidi kuliko jaribu la kwanza. Ningependa kushibisha njaa yangu, lakini nisingependa kujirusha kutoka kwenye jengo refu!)
    1.    Soma Kumbukumbu la Torati 6:16. Je, muktadha huu unakusaidia kulielewa vizuri zaidi jaribu hili?
      1.    Unadhani sababu ya rejea ya “Masa” ni ipi?
    1.    Soma Kutoka 17:1 na 3-4, na Kutoka 17:5-7. Kwa kuwa sasa umeshasoma muktadha wa kweli, suala halisi ni lipi katika kiini cha jaribu hili? (Kwa mara nyingine, ni kumtumaini Mungu. Lakini, limepindishwa kidogo. Hatupaswi kumfedhehesha Mungu kwa kushindwa kumtumaini yeye. Watu walipaswa kumtumaini Mungu ili kupata maji. Badala yake, “walimjaribu” kwa kumfedhehesha kwa upungufu wao wa imani.)
      1.    Kwa kuwa sasa umeshauangalia muktadha, “unatafsirije” jibu la Yesu kwa Shetani? (“Hapana, asante, hiyo itafanya ionekane kana kwamba simwamini Baba wa mbinguni.”)
  1. Pambano Nyikani – Sehemu ya III
    1.    Soma Mathayo 4:8-9. Hapa jaribu ni lipi? (Yesu anaweza kuupata ulimwengu bila haja ya kufa kifo cha uchungu msalabani.)
      1.    Unatathminije usasa wa jaribu hili? (Hili ni jaribu la kikatili. Ni sawa na mtesaji kusema “Sitakudhuru kama utanipa fedha zako.” Hii inalifanya jaribu la kwanza lionekane la kisasa kwa sababu kwa jaribu hilo ungeweza kujadili kama kutengeneza mkate ni jambo baya.)
    1.    Soma Mathayo 4:10, Kumbukumbu la Torati 6:13, na Kumbukumbu la Torati 5:7. Sidhani kama jibu la Yesu linahitaji kutafsiriwa – Yesu anajibuje jaribu hili? (Yesu ananukuu kitabu cha Kumbukumbu la Torati kwa kauli ya kwamba Mungu pekee ndiye anayepaswa kuabudiwa.)
      1.    Majaribu haya yanalinganishwaje na yale yanayokujia? Je, majaribu yako mengi ni yale ambayo unajua kuwa ni mabaya na unatakiwa kutomtii Mungu? Au, majaribu mengi yanayokujia ni yale yenye kuibua mjadala – huna uhakika ni lipi lililo sahihi kulitenda?
    1.    Soma Mathayo 4:11. Malaika walijuaje ili kuja kumsaidia Yesu? (Walikuwa wanatazama jambo hili kwanza katika mfululizo wa mapambano ya ulimwengu!)
  1.   Kuangikwa Juu ya Mti
    1.    Soma Wagalatia 3:10-11. Inamaanisha nini “kuyategemea matendo ya sheria?” (Kifungu cha 11 kinatuambia kuwa hii inahusiana na “kuhesabiwa haki mbele za Mungu.”)
      1.    Je, unayazingatia “mambo yote yaliyoandikwa katika Kitabu cha Torati?” (Kama jibu ni, “Hapana,” na hilo ndilo jibu pekee sahihi hapa, basi umelaaniwa.)
    1.    Soma Wagalatia 3:12-14. Tunakombolewaje katika laana ya kutoishika torati? (Yesu alitukomboa kutoka kwenye laana hiyo.)
      1.    Yesu alitendaje hilo? (Aliangikwa juu ya mti “kwa ajili yetu.”)
    1.    Soma Kumbukumbu la Torati 27:26 na Kumbukumbu la Torati 21:22-23. Torati inasema kuwa adhabu sahihi kwa kutoishika torati ni ipi? (Kulaaniwa na kuangikwa juu ya mti.)
      1.    Hebu niambie, kwa nini Yesu afanye hivyo kwa ajili yetu?
      1.    Hebu niambie, unadhani mjibizo wetu unapaswa kuwaje kwa kile ambacho Yesu ametutendea? (Shukrani kwa Yesu isiyo na kikomo. Lakini, pia kutambua kuwa torati ni ya muhimu kwa Mungu (na kwetu). Kama torati isingekuwa na maana, Mungu angeifutilia mbali tu na kumuepusha Yesu na mateso makubwa na fedheha.)
    1.    Soma Waebrania 10:28-29. Mwandishi wa kitabu cha Waebrania anasema kuwa mjibizo wetu kwa kile Yesu alichotutendea unapaswa kuwaje? (Kama kifo kingekuwa adhabu ya kuikiuka sheria, ni tatizo kubwa kiasi gani kupuuzia kafara ya Yesu iliyotukomboa kutoka kwenye adhabu ya kifo? Tunapaswa kuwa na shukurani kwa kile ambacho Yesu ametutendea.)
    1.    Soma Waebrania 10:30-31. Kitabu cha Waebrania hakizungumzii juu ya mjibizo wetu kwa kile alichokifanya Yesu. Badala yake, vifungu hivi vinahusu mjibizo wa Mungu kwa jinsi tunavyokiendea kifo cha Yesu kwa ajili yetu. Mungu anaonyesha mjibizo gani kwetu kwa kuikataa kafara ya Yesu? Hii inaendanaje na Mungu wa upendo? (Mungu wa upendo alijitoa kafara yeye mwenyewe kwa ajili yetu! Hii inaonekana kuhalalisha kitendo kiovu cha ukatili kabisa kwa niaba yake.)
      1.    Je, unakubaliana kwamba Mungu “analipiza kisasi?” (Vifungu vinasema “Kupatiliza kisasi ni juu yangu,” lakini mpangilio wa kawaida wa matukio unaonyesha kuwa dhambi inatuua. Anachokifanya mwandishi wa Kitabu cha Waebrania ni kujenga hoja madhubuti dhidi ya kupuuzia kafara ya Yesu. Huo ndio ujumbe wake wa msingi.)
    1.    Soma Kumbukumbu la Torati 32:28-31. Mungu anatuambia kuwa atatupatia nini? (Atakuwa pamoja nasi. Hatupo katika jambo hili peke yetu isipokuwa tu kama tutachagua kufanya hivyo. Mungu analeta utofauti katika mapambano ya maisha, kwa namna chanya na hasi. Ukimkataa Mungu, basi askari wako elfu kumi wanaweza kushindwa na watu wawili!)
    1.    Soma Kumbukumbu la Torati 32:36. Mungu ana mtazamo gani kwa watu wake? (Anawahurumia.)
    1.    Soma Kumbukumbu la Torati 32:46-47. Maneno haya katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati ni ya muhimu kiasi gani? Maonyo na ahadi ni ya muhimu kiasi gani? (Hakuna kilicho cha muhimu zaidi. Hayo ni “maisha yetu” na maisha ya watoto wetu.)
    1.    Marafiki, kifungu hiki cha mwisho kinazungumzia kwa ufupi umuhimu wa kweli wa kitabu cha Kumbukumbu la Torati. Sio tu kwamba ni cha muhimu vya kutosha kiasi cha kunukuliwa kwingineko kwenye Biblia, bali pia maelekezo ya Mungu yaliyomo katika kitabu hicho ndio maisha yetu halisi! Je, utadhamiria, kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, kutembea katika njia hiyo ya uzima?
  1.    Juma lijalo: Ufufuo wa Musa.