Somo la 1: Barua kwa Waebrania na Kwetu

Waebrania 1, 2, 3, 10 & 11
Swahili
Year: 
2022
Quarter: 
1
Lesson Number: 
1

Somo la 1: Barua kwa Waebrania na Kwetu

(Waebrania 1, 2, 3, 10 & 11)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Je, umewahi kuwa na tukio au wimbo uliokufanya ujisikie kumtukuza Mungu? Ninakumbuka kuwa na hisia hizo nilipokuwa chuoni na nilikuwa ninaimba katika kanisa la Pioneer Memorial Church. Kinanda na sauti vilinivuta kwenye huku kumsifu Mungu kwa pekee. Hivi karibuni kabisa, jambo hilo hilo lilitokea kwenye huduma ya kumsifu Mungu katika Chuo Kikuu cha Regent. Muziki hunivuta kwenye furaha hii ya kumsifu Mungu. Na kisha ninarejea kwenye dunia halisi. Somo la leo la Waebrania linafanana hivyo. Linaanza kwa kusifu na kisha linaingia kwenye jambo madhubuti la kuishi wakati bado tuking’ang’ania kwenye tumaini linalohamasisha kusifu kwetu. Hebu tuzame kwenye somo letu jipya katika Waebrania na tujifunze zaidi!

  1.    Kusifu
    1.    Soma Waebrania 1:1-2. Wanafunzi wengi wa Biblia wanaamini kuwa kitabu cha Waebrania kiliandikwa na Paulo. Je, utangulizi wa kitabu cha Waebrania unaanza vile vile kama vitabu vingine vya Paulo, kwa mfano, Waefeso? (Soma Waefeso 1:1-2. Kitabu cha Waebrania hakina salaam au utambulisho wa mwandishi au hadhira.)
    1.    Soma Waebrania 1:3-4 na Mathayo 6:9. Unaona mfanano gani kati ya mwanzo wa Waebrania na mwanzo wa sala ya Bwana? (Vyote vinaanza kwa kumaifu Mungu.)
      1.    Kwa nini unabashiri kwamba mwandishi wa kitabu cha Waebrania anaanza kwa kumsifu Yesu? (Alijawa sifa! Alihemewa hisia za kuelezea upendo wake na kujitoa kwake kiibada kwa Yesu.)
  1.   Kuanza kwa Usahihi kwa Uzingativu
    1.    Soma Waebrania 2:1. Ninawasikia wazungumzaji wakiniambia kusikiliza kwa makini kabla hawajasema jambo fulani, bali siwasikii wakiniambia kuzingatia kwa umakini baada ya wao kuzungumza. Je, unakubaliana kwamba kifungu hiki kinatutaka tuwe wazingativu baada ya hotuba?
      1.    Kama unakubaliana nami, hii inamaanisha nini? (Baada ya kuanza kwa kusifu katika Waebrania 1, mwandishi anaingia kwenye matatizo halisi ya watu ambao kwanza walikuwa wanaizingatia injili, lakini sasa wamepoteza dira.)
      1.    Kuna hatari gani ya kupoteza dira kwa kile tulichofundishwa kama Wakristo? (Kwamba tutapoteza mvuto na “kutanga mbali.”)
    1.    Soma Waebrania 2:2. Hoja ni ipi ya kuendelea kujikita na kuizingatia injili? (Ni ya kuaminika na mambo mabaya yatatokea kama ukiacha kutii.)
      1.    Hiyo inamaanisha nini? Kifungu kinaporejelea “ujira wa haki,” je, hiyo inamaanisha kuwa Mungu anakupiga kofi pale unapoacha kutii? (Nadhani hii inaelezea matokeo ya asili yanayotokana na kutokutii. Hiyo ndio sababu tuliambiwa kuwa ujumbe “unaaminika.” Imethibitika kuwa njia salama ya kuepuka kuingia kwenye matatizo.)
    1.    Soma Waebrania 2:3-4. Kwa nini tuuchukulie ujumbe wa injili kuwa wa kuaminika? (Hii inaorodhesha sababu kadhaa. Kwanza, Mungu ndiye chanzo cha ujumbe. Pili, uzoefu wa kibinadamu unauthibitisha. Tatu, matukio yasiyo ya kawaida yapitayo akili zetu yanaushuhudia.)
      1.    Mwisho wa kifungu cha 4 una kauli ya kufurahisha. Kinarejelea “na kwa magawanyo ya Roho Mtakatifu, kama alivyopenda mwenyewe.” Hiyo inathibitishaje kuwa ujumbe wa injili ni wa kuaminika? (Ushirika kati ya wanadamu na Roho Mtakatifu katika mfumo wa karama za roho ni uthibitisho zaidi kwamba injili ni jambo la kweli.)
  1.        Kuishi Maisha Yako Bora?
    1.    Soma Waebrania 2:18. Tuchukulie kwamba hujapoteza uzingativu wako kwenye ujumbe wa injili. Unajisikiaje pale unapojaribiwa kutenda dhambi?
      1.    Kifungu hiki kinarejelea “mateso” kama mjibizo wa majaribu. Je, hivyo ndivyo unavyokichukulia?
      1.    “Mwenyewe” ni nani anayerejelewa kwenye kifungu hiki? (Ukiuangalia muktadha, huyu ni Yesu.)
      1.    Kamwe Yesu hakushindwa majaribu. Je, hiyo inaongeza mateso yake, ikilinganishwa na wewe?
    1.    Soma Waebrania 3:12. Je, unapambana na kutokuamini, kutilia shaka kama Mungu yupo, au kama yupo, basi anajali mambo yako na hali yako?
    1.    Soma Waebrania 3:13. Kitu gani kitakusaidia na aina hii ya upambanaji? (Kutiwa moyo na waumini wenzio.)
      1.    Kitu gani kinaweza kutokea tukishindwa kuwatia moyo wengine? (Wanakomaa kwenye dhambi yao. Wanadanganywa na dhambi yao.)
      1.    Kumbuka Utangulizi wa somo hili na uzoefu wangu wa kumsifu Mungu miongoni mwa kundi la watu wengine wakiimba nyimbo za sifa. Kama umepitia uzoefu wa jambo kama hili, je, uzoefu huo unakutia moyo katika imani yako?
        1.    Fikiria maisha yako yangekuwa ya umasikini kiasi gani kama ungekuwa hujawahi kupitia uzoefu wa jambo kama hilo?
    1.    Soma Waebrania 10:32-33. Hii inaonekana kuonyesha taswira ya watu wanaokabiliana na majaribu lakini hawashindwi nayo. Matokeo yake yanaweza kuwa ni yepi? (Kwamba unapata mateso. Watu wanaweza kukudhihaki na kukupatia wakati mgumu.)
    1.    Soma Waebrania 10:34-35. Sidhani kama hii inahusu huduma ya megerezani, bali ni rejea ya wasomaji kutupwa gerezani na mali yao kuibwa au kuharibiwa. Utajisikiaje kuhusiana na hilo?
      1.    Hii inaashiria kuwa unapokea upotevu wa mali yako kwa furaha. Hilo linawezekanaje? (Una vitu vingine vizuri zaidi ambavyo haviwezi kuondolewa kwako.)
        1.    Ni kitu gani hicho? (Mbingu!)
    1.    Angalia Waebrania 10:32 na usome Waebrania 10:24-25. Je, matukio haya yanaelezwa kwa kuzingaia muda yanayotokea moja baada ya jingine? (Hapana. Kifungu cha 32 kinawaambia wakumbuke siku walizoteseka. Hivyo, Waebrania 10:24-25 inafuatiza muda wa mateso. Ndio maana nimegeuza mpangilio wa usomaji.)
      1.    Tunawezaje kujiweka kwenye nafasi ya kutiwa moyo? (Kwa kukutana pamoja na waumini wengine. Na, kwa kuwatia moyo wengine.)
      1.    Je, kukusanyika pamoja na wengine ili kumsifu Mungu ni sehemu ya kutia moyo huku? (Naam, hiyo ni sehemu yake. Hii ni sehemu ya kurejea kwenye sehemu bora ya maisha.)
      1.    Tunapokaribia mwisho wa nyakati, je, kukaa pamoja na waumini wengine ni muhimu zaidi au hakuna umuhimu? (Kifungu cha 25 kinaashiria kuwa ni muhimu zaidi.)
  1.   Imani kwa Ajili ya Siku Zijazo
    1.    Soma Waebrania 11:1. Inamaanisha nini kuwa na imani? (Kuamini katika mambo yatarajiwayo, na yale mambo ambayo hatujayaona.)
    1.    Waebrania 11:2-12 inaelezea habari za mashujaa wengi wa Biblia waliokuwa na imani na hawakushuhudia thawabu kamili za imani hiyo. Soma Waebrania 11:13-16. Umuhimu wa kushikilia imani yetu ni upi? (Kwamba “twaitamani nchi iliyo bora.”)
      1.    Hiyo nchi bora ni ipi? “Mji” ambao Mungu ametuandalia ni upi? (Nchi bora ni mbingu na mji ni Yerusalemu Mpya.)
    1.    Soma Waebrania 11:39-40. Waebrania 11 inawabainisha mashujaa wa zamani. Kwa nini kifungu cha 40 kinasema “ili wao wasikamilishwe pasipo sisi?” (Sote tuko pamoja katika hili. Mashujaa wa Agano la Kale waliutazamia ushindi wa Yesu dhidi ya dhambi. Tunauangalia ushindi huo. Sisi sote, pamoja, tunayatazamia makao yetu ya milele mbinguni yakiwezeshwa na kile alichotutendea Yesu kwa ajili yetu!)
    1.    Rafiki, tunamtumikia Mungu mkuu! Hata hivyo, maisha yanaweza kuwa na changamoto. Tunatiwa changamoto pale tunapokuwa si watiifu. Na tunatiwa changamoto pale tunapokuwa watiifu na kushambuliwa na wapagani. Sehemu ya muhimu ni kushikilia imani yetu kwa Mungu na mustakabali ambao ametupangia. Mungu apewe sifa!
  1.    Juma lijalo: Ujumbe wa Waebrania.