Somo la 7: Yesu, Nanga ya Roho

Waebrania 6
Swahili
Year: 
2022
Quarter: 
1
Lesson Number: 
7

Somo la 7: Yesu, Nanga ya Roho

(Waebrania 6)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2020, Bruce N. Cameron, J.D. Kwa wanaotumia lugha ya Kiingereza, marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya ESV® (Biblia Takatifu, English Standard Version®) copyright © by Crossway, wachapishaji wa “Good News Publishers.” Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya ESV® inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na likakupotea kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza na lugha nyinginezo kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Je, kuna nyakati maisha yanaishia kuwa kwenye ratiba ya uchoshi (boring)? Je, matatizo na changamoto zinatufanya tujikite kwayo badala ya kumzingatia Mungu? Je, mafanikio na mali vinatufanya tugeuke na kuacha kumtegemea Mungu? Je, kuna nyakati unashawishika kuuacha nyuma Ukristo? Tunatakiwa kujifunga kwa Yesu ili kwamba isitokee hali yoyote kati ya hizo ikatuteka na kutuelekeza kuiacha imani yetu kwa Yesu. Waebrania 6 inalizungumzia tatizo hili. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia na tujifunze zaidi!

 1.    Maendeleo ya Imani
  1.    Soma Waebrania 6:1-2. Tunaambiwa “kuacha kunena mafundisho ya kwanza ya Kristo, tukaze mwendo ili tuufikie utimilifu.” Je, “kuacha” kunamaanisha “kupuuzia” au “kusahau?” (Hapana, haimaanishi vyote hivyo viwili. Hii inatuambia tukomae katika uelewa wetu wa mapenzi ya Mungu. Ni sawa na kutuambia kuacha shule ya msingi na kuendelea na ngazi inayofuata ya kujifunza.)
   1.    Utaona kuwa tunaambiwa tuachane na “msingi wa kuzitubia kazi zisizo na uhai.” Kuzitubia kazi zisizo na uhai inamaanisha nini? (Unatubu dhidi ya kuyategemea matendo yako kwa ajili ya wokovu.)
    1.    Kwa nini tuachane na kuhesabiwa haki kwa imani? Ni kwa jinsi gani hili ni tatizo? (Ninamkumbuka mchungaji aliyehubiri kwa kubadilikabadilika kwenye mada ya kuhesabiwa haki kwa imani katika kila hubiri. Mwandishi wa kitabu cha Waebrania anatutaka tujifunze somo hilo na tusonge mbele katika uzoefu wetu wa Kikristo.)
   1.    Kama unayasoma masomo haya mara kwa mara, basi unafahamu kuwa ninazungumzia kwa kurudiarudia kuhusu kuhesabiwa haki kwa imani tu. Je, mwandishi wa kitabu cha Waebrania ananiambia niache huu urudiaji wa mara kwa mara? (Natumaini jibu ni hapana. Katika Maisha yangu mwenyewe ninahitaji kusonga mbele kwenye uelewa wangu wa mapenzi ya Mungu kwangu. Lakini, kufundisha kunahusisha wanafunzi walio katika ngazi tofauti, na baadhi yao kamwe hawajawahi kujifunza au kuielewa neema vizuri. Sidhani kama huu ni ushauri kwa walimu.)
   1.    Je, ni ushauri kwa mchungaji niliyembainisha ambaye alihubiri mada ya kuhesabiwa haki kwa imani tu? (Inawezekana ushauri unawahusu wachungaji wanaonena na kundi la watu wale wale kila juma. Ninadhani sio wengi walio na kusanyiko lile lile la watu lisilobadilika.)
  1.    Soma Waebrania 6:3. “Mungu akijalia?” Kwa nini Mungu asijalie kusonga mbele kwa ukomavu wa Kikristo? (Hili ni jibu la ziada kwa maswali niliyoyauliza hivi punde kuhusu matumizi ya maelekezo haya. Roho Mtakatifu atatusaidia kuelewa wakati gani tunahitajika kusonga mbele.)
 1.   Kuiacha Imani
  1.    Soma Waebrania 6:4-6. Ninakumbuka kusoma vifungu hivi siku za nyuma na kufikia uamuzi kwamba ni suala la kupoteza muda kujaribu kuwarejesha washiriki wa kanisa walioliacha kanisa. Mara wanapoliacha kanisa, “haitawezekana” kwa wao kurejea. Je, huo ndio uelewa sahihi wa vifungu hivi?
   1.    Soma Mathayo 10:14-15. Je, huu ni ujumbe ule ule wa “unatakiwa kujaribu mara moja tu?” Kama wasikilizaji wakiamua kulikataa kanisa, waache na uamuzi wao?
  1.    Hebu tuangalie kwa ukaribu zaidi Waebrania 6:4-5. Je, hii inawaelezea watu walioisikia injili mara moja pekee? (Hapana. Inaorodhesha vigezo vitano vinavyowaelezea wale wanaopotea kama wakiondoka. Mtu “anapewa nuru,” “ameonja kipawa cha mbinguni,” amekuwa akiongozwa na Roho Mtakatifu, na “kulionja neno zuri la Mungu,” na “nguvu za zamani zijazo.”)
   1.    Hebu tujadili kila mojawapo ya vigezo hivi. Unadhani inamaanisha nini “kupewa nuru?” (Kuielewa injili.)
   1.    Inamaanisha nini “kukionja kipawa cha mbinguni?” (Kupata uzoefu wa wema na uzuri wa Mungu.)
   1.    Inamaanisha nini “kufanywa washirika wa Roho Mtakatifu”? (Hii sio tu “ladha,” bali huyu ni mtu aliyepitia uzoefu wa Roho Mtakatifu na kushiriki uzoefu huo na watu wengine.)
   1.    Inamaanisha nini “kulionja neno zuri la Mungu?” (Umepitia uzoefu wa manufaa ya kuyafuata mapenzi ya Mungu.)
   1.    Inamaanisha nini kuonja “nguvu za zamani zijazo?” (Tunatarajia (angalia Yoeli 2:28-30) kwamba katika siku za mwisho patakuwepo na udhihirishaji wa pekee wa nguvu za Roho Mtakatifu. Mtu huyu “amelionja” hilo.)
   1.    Aina gani ya Mkristo anafikia vigezo vyote hivi vitano?
  1.    Soma Ufunuo 2:2-5. Hawa ni watu wanaoweza kutubu. Unawatofautishaje na watu wa vigezo vitano walioelezewa katika Waebrania 6:4-6?
  1.    Soma tena Waebrania 6:6. Hii inatoa sababu ya watu wa vigezo vitano kupotea mara wanapoondoka. Tabia gani “inamsulubisha” Yesu na “kumfedhehi?” (Wale waliomsulubisha Yesu walikuwa na uhasama naye. Walimdhihaki Yesu. Hiyo ndio tabia inayoelezewa hapa.)
   1.    Katika sheria ya Marekani kuna nyakati tunazijinaisha tabia za “kizembe” juu ya kile ambacho ni cha “kudhamiria.” Unadhani watu wa vigezo vitano wanaweza kupotea kutokana na tabia ya kizembe pekee?
   1.    Utaona kwamba kifungu cha sita pia kinasema kuwa kitendo hiki cha kumgeuka Yesu matokeo yake ni “madhara” kwa watu wa vigezo vitano. Unadhani madhara ya gani yanahusika? (Kwa dhahiri, ni madhara ya kupotea. Lakini, nadhani hili ni onyo halisi kivitendo. Ulidhani maisha yako yatakuwa mazuri zaidi kama utageuka na kumwacha Yesu, lakini kinyume chake Maisha yanakuwa mabaya Zaidi.)
  1.    Soma Marko 3:28-29. Mojawapo ya vigezo vitano ilikuwa ni “kufanywa washirika na Roho Mtakatifu.” Je, kifungu hiki katika kitabu cha Marko kinaongezea chochote kwenye uelewa wetu wa kigezo hicho?
   1.    Muktadha ni wa muhimu sana hapa. Soma Marko 3:22-24. Muktadha unaashiria kuwa “kumkufuru” Roho Mtakatifu ni kufanyaje? (Kumhusisha Shetani kwenye matendo ya Roho Mtakatifu.)
   1.    Je, hii inaongezea uelewa wa ziada kwenye kigezo hiki? (Hii inaongezea kwenye uelewa wetu wa kumsulubisha Yesu. Mtu huyu anauhusisha uovu kwenye matendo ya Roho Mtakatifu.)
  1.    Soma Waebrania 10:26-27. Je, umetenda dhambi kwa makusudi? (Sote tumefanya hivyo.)
   1.    Kama sote tumefanya hivyo, tunapaswa kukielewaje kifungu hiki? Je, kila mtu amepotea? (Ninadhani mjadala wetu wa vigezo vitano unatusaidia kulifafanua hili. “Tukifanya dhambi kusudi” lazima ielezee kuachana na Yesu kwa mtu aliyekuwa na uhusiano naye wa dhati hapo kabla.)
 1. Tumaini kwa Ajili ya Siku Zijazo
  1.    Soma Waebrania 6:9. Tumekuwa tukijadili maonyo ya kutisha kiasi! Tunapaswa kuyatazamaje maonyo haya? (Mwandishi wa kitabu cha Waebrania anatuambia kuwa tutazamie mambo mazuri. “Kusadiki mambo yaliyo mazuri zaidi.”)
  1.    Soma Waebrania 6:10. Je, matendo yetu na upendo wetu vinatupatia sifa kwa Mungu? (Sidhani kama hili limekusudiwa kukinzana na neema. Badala yake, hii inatuambia kuwa Mungu ni mwenye haki katika yote ayafanyayo. Kabla Mungu hajatuchukulia kama wapotevu, anazingatia kile tunachomtendea.)
  1.    Soma Waebrania 6:11-12. Ni njia gani iliyo chanya zaidi katika kuangalia maonyo haya? (Yanatusaidia kuwa na ari na bidii na sio kuwa wavivu. Yanavuta uzingativu ili kuhamasisha uzingativu mkubwa kwa Mungu.)
  1.    Soma Waebrania 6:17-18. Badala ya kumgeuka Yesu, lengo la Mungu kwetu ni lipi? (Anataka kututia moyo tung’ang’anie katika tumaini letu.
  1.    Soma Waebrania 6:19-20. Je, unaweza kutumia nanga kwa ajili ya roho yako? Ikiwa ndivyo, Yesu anasema kuwa ahadi zake kwa siku zijazo, na kile anachotutendea sasa hivi kama Kuhani wetu Mkuu, vinapaswa kutupatia utiwaji moyo wa msingi.)
  1.    Rafiki, Yesu anatutaka tujikite upya umakinifu wetu kwake. Haonyi tu katika suala la kuanguka, bali anatuhakikishia kuwa lengo lake ni kututia moyo, kutegemeza tumaini letu kwake. Uwe na moyo mkuu. Yesu anataka kutupatia tumaini!
 1.   Juma lijalo: Yesu, Mpatanishi wa Agano Jipya